Yaani wazungu wakisikia Afrika wanafikiri ni kama Ethiopia miaka ya 80 au Rwanda wakati wa mauaji ya halaiki. Wanadhani kila kukicha tunakatana mapanga au tunagalagala chini tukisubiri kufa kwa njaa kali. Tazama nchi kama Marekani, watu zaidi ya milioni mbili wako jela, watu zaidi ya milioni 40 hawana bima ya afya (hawa ni wale vibogoyo, kwa mfano, maana hawana hela ya kwenda kwa daktari wa meno!), idadi ya watu wasio na makazi ni kubwa kuliko nchi yoyote ya ulimwengu wa kwanza, watoto wanaoishi ghetto wanakula jumatatu hadi ijumaa chakula kingi maana jumamosi na jumapili nyumbani hakuna chakula, kwa mwaka watu zaidi ya 15,000 wanauawa kwa bunduki, watoto zaidi ya 100,000 wanatekwa…huu ni ulimwengu wa kwanza au wa kumi? Ubepari unaficha mengi. Majumba, sinema, magari, barabara nzuri vinaficha umasikini na unyama wa mfumo huu. Ni kama Afrika Kusini. Majengo mazuri, barabara za kisasa lakini Johannersburg, kwa mfano, inajulikana kama “rape capital of the world.” Kila dakika anabakwa mtu! Ukiacha Moscow hakuna jiji lenye uhalifu kama Johannersburg. Lakini tazama mandhari yake.
June 2004
Tue 29 Jun 2004
Tue 29 Jun 2004
Eti Iraki iko “huru” sasa. Katamka Rais, mwizi wa kura, wa hapa Marekani, Bwana Kichaka (Bush). Hii ni sawa na Afrika Kusini ambako watu weusi wanatawala kisiasa ila nguvu za kiuchumi, ambazo ndizo nguvu halisi, ziko mikononi mwa Makaburu ambao wanainunua Tanzania kwa kasi ya mwanga. Uchumi wa Iraki, ninamaanisha mafuta, uko mikononi mwa makampuni ya Amerika. Ni Wamarekani ambao watakuwa wanatoa maamuzi makuu juu ya sera na biashara ya mafuta. Hii dunia ya uongo, tufanyeje? Nyanyuka mlalanjaa!
Sun 27 Jun 2004

Baba Ukweli na Mama Ukweli na rafiki toka kisiwa cha Martinique (alikotokea Frantz Fanon, yule mwandishi wa kitabu cha Waliolaaniwa). 
Sun 27 Jun 2004

Ndesanjo akiwa utelezini barafuni. Toka kuteleza kwa kisigino pale Mpirani, mkoani Kilimanjaro hadi kwenye barafu. Hapa ni nje ya jiji la Seattle, jimbo la Washington 
Sun 27 Jun 2004
Sun 27 Jun 2004

Kila mwaka mji wa Toledo hapa Ohio huwa unasherehekea siku ya Tanzania. Siku hii huandaliwa na shirika la Great Lakes Consortium ambalo hushughulika na miradi mbalimbali ya maendeleo hapo Tanzania. Pia mji wa Toledo ni mji-dada wa mji wa Tanga. Picha hii inaonyesha siku ya Tanzania mwaka juzi, ambapo vinyago na vitu mbalimbali toka Tanzania viliuzwa. 
Sun 27 Jun 2004
Hii ni sehemu ya shairi jingine ambalo ni refu kidogo. Nitakupa beti mbili tu. Linaitwa Utamaduni Msalabani.
Kura twapiga, sadaka twatoa
Kodi twalipa, swala twasali
Walalanjaa
Cha moto, mbona
Bado Twakiona?
Demokrasia ghasia
Mafukara twauziwa,
Jehanamu ya moto
Masikini twatishiwa,
Wa kusema wamesema
Wa kusikia ni viziwi,
Hivi chukua chako mapema
Ni azimio la wapi?
Sun 27 Jun 2004
Hili ni sehemu ya moja ya mashairi ambayo yatachapwa karibuni. Linaitwa Amerika:
Hii hapa Amerika
Uliyoililia
Harakaharaka ndio mwendo
Polepole haina baraka
Baridi kali, sheria kali
Utamaduni baridi.
Binadamu wanaongea na mbwa
Wao kwa wananuniana!
Sat 26 Jun 2004
Wakati nikiishi Dar, kila asubuhi na jioni nilisikia sauti ya muezzin (muazini) akiita Waislamu wakasali. Niliishi hatua chache toka msikitini (pale Tabata na Mbagala). Sauti ya “Swalaaaa….,” ilikuwa ikisikika kama vile anayeomba yuko dirishani. Sasa hapa Marekani, kila jioni na asubuhi nasikia sauti ya risasi na ving’ora vya magari ya polisi na magari ya wagonjwa. Hizi risasi sijaweza kujua zinatokea wapi. Ninahisi kuna kambi karibu na hapa ninapoishi, barabara ya Uwanja wa Ndege, nje kidogo ya mji wa Toledo, Ohio. Ule mti niliosema unanitisha, kuwa unaweza kutuangukia chumbani siku moja, bado upo umesimama. Asubuhi ya leo niliutazama weee….
Sat 26 Jun 2004
Wi-fi ni mtando wa mhahalishi (internet) ambao hautumii waya wala mnara. Kama una tarakilishi (kompyuta) ya mkononi unaweza kuingia kwenye webu ukiwa popote pale. Kwa kimombo wanaita wireless, lakini kwa kiswahili inaitwa mtandao usiwaya.
Fri 25 Jun 2004
Kwa sasa watu wanaweza kuwasiliana kwa kutumia
tarakilishi (computer) iliyoungwa kwenye mtandao (network)
kuweza kuvinjari kwenye mdahalisi (internet) ikiwa tu
wanajua anuani ya baruapepe (e-mail) ya wanaemhitaji.
Baruapepe yaweza kuwa kwenye tovuti (website) ambayo
wewe utahitaji kubofya (to surf) tu ili kuipata.
Teknolojia hii imesitisha matumizi ya kinakilishi (fax)
na pia imeongeza kasi ya upatikanaji wa maarifa ya
ujasiliamali (entrepreneurship knowledge) miongoni mwa wafanyabiashara.
Hivi sasa mchakato (process) wa maendeleo duniani unaanza
kuchukua sura tata(complex)kwani kila mahali panatafuta
asasi(resource! ) yake.
Fri 25 Jun 2004
Nimemaliza kufunza wanafunzi kutengeneza blogu zao. Blogu ina umaarufu sana miongoni mwa matineja. Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC asilimia kubwa ya blogu ni za matineja. Soma habari hiyo hapa.
Thu 24 Jun 2004
Bush na wezi wenzie nasikia matumbo yao moto kutokana na filamu ya Michael Moore iitwayo Fahrenheit 911 ambayo pamoja na mambo mengine inaonyesha uhusiano wa familia ya Bush na Osama na pia wauaji wa Kinazi. Bado sijaitazama ila napanga kwenda wikiendi moja na familia. Kuna siku nilisema kuwa Moore ana kitabu kinaitwa Stupid Whitemen! Kumbuka kuwa yeye naye ni mweupe!
Thu 24 Jun 2004
Kuishi ughaibuni kwenye nchi ambayo watu hawapendi mpira wa miguu (soka) ni jambo baya sana. Ukiongelea mpira wa miguu, football kwa kiingereza, wamarekani wanafikiri unazungumzia american football. Huu ni mchezo wa mabavu, unacheza huku ukiwa umevaa machuma usoni! Jambo ambalo sijaweza kupata ufumbuzi wake ni hili. Kwanini wanauita huu mchezo mpira wa miguu wa kimarekani (american football) wakati asilimia 99.99 ya huu mchezo unatumia mikono? Wauite handball!
Wed 23 Jun 2004
Da! Hizi siku mbili tatu huyu mtu mweupe anayekalia hii nchi ya wahindi wa asili (native americans) amenikamata kweli. Unajua tena hii ni nchi ya kodi na bili! Hivyo lazima jasho likutoke. Naona watu wasio na hatia wanaendelea kukatwa vichwa katika aina mpya ya ugaidi.
Mon 21 Jun 2004
Swali: Hivi kwanini unadhani kuwa mbingu au jehanamu utaipata baada ya kufa wkati vyote viko hapa duniani? Usikubali shehe au kasisi akudanganye maisha yako yote. Hoji! Kataa kudanganywa!
Tatizo kubwa ulilonalo ni kudhani kuwa ni kweli kasisi na shehe huwa “wanaongea na mungu.”
Mon 21 Jun 2004
Tume ya kitaifa inayochunguza tukio la kigaida la Septemba 11, 2001, imesema kuwa hakuna ushahidi kuwa Saddam Hussein alihusika na shambulio hilo. Wamesema kuwa Osama alikuwa na uhusiano wa karibu na nchi za Pakistani (ambayo ni rafiki mkuu wa Marekani), Iran, na Saudi Arabia. Kumbuka kuwa Wamarekani waliambiwa, na wengi waliamini, kuwa Iraki lazima ivamiwe maana ilihusika na shambulio la jengo la World Trade Center. Ushahidi hakuna! Bush na makamu wake Cheney hawajui wajifiche wapi. Kila hoja waliyoitoa inapanguliwa. Habari zaidi soma ukurasa huu.
Sun 20 Jun 2004
Mfumo wa uchumi wa kibepari ni kama barabara ya lami mchana wa jua kali. Ukiwa barabarani unaona mbele yako kama vile kuna maji. Kiingereza wanasema hiyo ni mirage. Ndivyo ilivyo hili taifa. Umasikini, hujuma, rushwa, magonjwa ya akili, ukimwi na vitu kama hivyo vimefichika sana. Je unajua kuwa watu milioni 43 hawana bima ya afya? Kama huna bima ya afya katika nchi kama hii wewe ni kama binadamu asiye na uhai!
Ninatazama sinema iitwayo Waco. Unakumbuka lile kundi la dini na Branch Davidians ambalo mwanzo wa miaka ya 1990 lilikuwa na ugomvi na serikali kisha yakatokea mapigano na FBI. Jumba lao liliungua moto. Serikali ilidai kuwa waumini hao waliamua kujiua. Wengine wanadai kuwa serikali iliwaua. Sinema hii inachambua kwa kina tukio hili. Habari zaidi za Branch Davidians nenda hapa
Sat 19 Jun 2004
Kama Adamu na Hawa walikuwa na watoto wa kiume wawili (Kaini na Abeli), je watoto wa Kaini na Abeli walitoka wapi? Jibu ninalo, ila nakupa changamoto kidogo. Na je tunda la katikati ni lipi? Wengine wanadai kuwa ni tendo la ndoa. Mimi napinga. Hawa alikula kwanza mwenyewe hilo tunda kisha ndio akamshawishi Adamu ajaribu. Adamu naye akala mwenyewe. Je ni tendo la ndoa? Kama sio, ni tunda gani? Changamoto nyingine ya jumamosi ya leo ambayo ni siku ya sabato ya wayahudi.
Sat 19 Jun 2004
Aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinto, alilala sebuleni kwenye makochi kwa zaidi ya miezi miwili baada ya kukubali mbele ya mke na mtoto wake kuwa alikuwa na uhusiano wa siri wa kimapenzi na Monica Lewinsky. Kama ingekuwa ni kiongozi wa Tanzania, nadhani mke ndiye angelala sebuleni. Au angerudishwa kwao, pamoja na kuwa mwenye makosa ni mume! Clinto ametoa siri hii ndani ya kitabu chake kipya kiitwacho My Life. Habari zaidi soma hapa.




