Nenda sehemu yenye makala zangu (pembeni mkono wa kuume) kisha ukongoli kwenye makala mpya niliyoiweka leo. Hii makala niliandika siku za nyuma. Inaitwa UMEDANGANYWA.
August 2004
Sun 29 Aug 2004
Sun 29 Aug 2004
Barua za watu wanaowasiliana nami zinaonyesha kuwa watu wengi bado wanatawaliwa na hofu ambayo imekuwa ikitumiwa na wanasiasa na dini kutupumbaza na kutufanya watumwa. Usiogope kuhoji lolote lile. Wewe kama biandamu una haki ambayo haitoki kwa mtu yeyote (awe rais, hakimu, polisi, kasisi au shehe) ya kuhoji kila kitu. Hoji. Pinga. Iwe ni serikali. Iwe ni dini. Uwe ni mfumo wa elimu. Iwe ni sheria. Iwe ni desturi. Una haki hiyo na hakuna kiumbe ambaye ataweza kukuzuia ukikataa kuwa kondoo.
Watatokea watu watakwambia kuwa ukihoji serikali utafungwa. Anayekwambia hivyo ndiye anapaswa kufungwa. Hoji serikali. Kama serikali uliyoichagua au iliyochaguliwa na wengi (kwa mujibu wa tume yao ya uchaguzi) haiwakilishi matakwa yako, kuna jambo moja la kufanya. IONDOE MADARAKANI. Iangushe. Ipindue. Chukua madaraka. Jiongozeni wenyewe!
Wengine watakwambia kuwa ukihoji mambo ya dini au Mungu utakuwa kichaa. Au utakwenda motoni. Wanaokwambia hivi tayari wanaungua. Muhoji hata Mungu. Anapenda sana kuhojiwa. Utawasikia wakisema, “Tafuteni nanyi mtaona,” “Watu wangu wataangamia kwa kukosa maarifa.” Laiti wangejua maana ya maneno haya.
Ndugu yangu, hoji usiogope. Kuhoji ni mwanzo wa uhuru.
Sun 29 Aug 2004
Madaktari huko Ujerumani wameweza “kuotesha” taya mgongoni mwa Mjerumani mmoja aliyekuwa amepoteza taya lake kutokana na ugonjwa wa kansa. Mgonjwa huyo ameweza kula chakula kwa mara ya kwanza baada ya miaka 9. Soma undani wa habari hiyo kwa kubonyeza hapa.
Sun 29 Aug 2004
Ujumbe wa leo ni kipande kifupi toka kwenye shairi langu liitwalo TAFAKARI:
Mahakimu wanahukumu
Wala rushwa,
Lakini nao rushwa wanashiriki,
Wao nani atawahukumu?
Nani!
Sun 29 Aug 2004
Tukifungua mdomo kusema
Wako watakaochukia
Na kununa,
Kutukamata
Kutufunga
Kutunyang’anya uraia,
Lakini usishangae,
Hawa ndio waliomsulubu masihi
Huku wanadai kumwamini.
- ndesanjo©
DSM, 2002.
Fri 27 Aug 2004
Kufuatia mfululizo wa makala nilizotoa katika gazeti la Mwananchi juu ya imani na falsafa ya Urasta, watu wengi wameniuliza wanapoweza kupata vitabu juu ya Urasta. Ukiwa Tanzania, kitabu ambacho kinaweza kupatikana kwa urahisi ni RASTA AND RESISTANCE: From Marcus Garvey To Walter Rodney. Kitabu hiki kiliandikwa na Profesa Horace Campbell wakati akiishi na kufundisha nchini Tanzania na kuchapwa na Tanzania Publishinga House. Nadhani unaweza kukipata katika duka la TPH lililoko mtaa wa Samora, jijini Dar Es Salaam. Kwa walioko ughaibuni, tafuteni kitabu kiitwacho RASTAFARI: Healing of the Nations. Hiki nadhani ni kiboko katika vitabu vyote nilivyosoma juu ya Urasta. Kimeandikwa na Rasta mwanasosholojia, Dennis Forsythe.
Baadhi ya Marasta hawapendi kitabu cha Horace Campbell kutokana na madai kuwa Profesa Campbell ni mfuasi wa itikadi ya Ki-Marx. Marx aliandika kuwa dini ni aina ya ulevi wa kupumbaza masikini ili waweze kutawaliwa. Marx hakuwa akiamini uwepo wa Mungu. Kwahiyo Rasta hao wanaona kuwa mtu kama huyo hawezi kuandika kwa usahihi juu ya imani ya Kirasta.
Campbell mara ya mwisho nilimwona Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Nadhani ilikuwa ni mwaka 2002 au mwishoni mwa 2001. Yeye kawaida katika mazungumzo yake huwa anatoa heshima kwa Jah Rastafari. Kwa mfano katika hotuba yake pale Mlimani, alimaliza hotuba yake kwa kusema, “Jah!” na waliokuwa wanajua jinsi ya kujibu wakajibu, “Rastafari.” Amekuwa kwa miaka mingi akiandika na kutetea imani ya Kirasta katika duru za kitaaluma. Juu ya imani yake sifahamu. Ila nitafanya mawasiliano naye ili kuweka wazi. Kitabu chake nimekisoma na ninaona ni kitabu ambacho kina uchambuzi wa kina na historia ambayo kila Mwafrika anapaswa kuijua. Kuna mambo ambayo sikubaliani naye, ila kwa ujumla naona kitabu hiki kinafaa kusomwa. Hasa zaidi, watu wanaotafuta ukweli juu ya Rasta kwasababu za kitaaluma na utafiti. Kwa masuala ya kiroho, kitabu cha kusoma ni Rastafari: Healing of the Nations.
Jah! Rastafari!
Thu 26 Aug 2004
Vita ya “ukombozi” wa Iraki ina mshahara wake. Kwa akina Joji Kichaka na wenzake, makampuni yao na yale ambayo wana hisa zake, yanapata tenda na faida za mamilioni ya dola. Ila kwa wazazi ambao wanao, wengine wenye umri wa miaka 18!, wanapigana huko Iraki mshahara wake ni msiba. Watoto wa akina Joji Kichaka na genge lake la watu wanaotaka kuunda “dunia mpya” ambayo itatawaliwa na kundi la watu wachache, watoto wao wako vyuo vikuu wakichukua shahada ili waje kuwa watawala kama wazazi wao. Jana jumatano, mzazi mmoja mlalahoi baada ya kuambiwa kuwa mwanaye kafariki huko Najaf, aliingia ndani ya gereji kuchukua kiberiti na petroli kisha akaingia ndani ya gari la wanajeshi waliomtembelea kumpa taarifa za msiba na kutia gari moto akiwemo ndani. Soma habari yake hapa.
Thu 26 Aug 2004
*************************************************************************************
Mweupe mweupe: “Usimwone hivi jamaa yule.”
Maji ya kunde: “Kwani vipi? Si chizi yule?”
Mweupe mweupe:“Kafika chuo kikuu.”
Maji ya kunde: “Chuo kikuu kaenda lini kila siku yuko mtaani?”
Mweupe mweupe:“Hawa ndio wale waliofukuzwa na Mwinyi.”
Maji ya kunde: “Mwinyi aliwaonyesha dawa yao. Ile mijinafunzi ya jabu sana. Walitaka serikali iwape hela hadi za sigara!”
Mweupe mweupe:“Sasa walipofukuzwa waliambiwa waandike barua za kuomba msamaha. Jamaa unayemwita chizi akakataa.”
Maji ya kunde: “Mbishi huyo. Nenda kacheze naye drafti pale dukani kwa Mangi…hakubali kushindwa. Kila jioni hakosi taarifa za BBC. Akitoka hapo ni kubishana mambo ya siasa mtaa mzima.”
Mweupe mweupe:“Sio siasa tu. Usimuone vile, Kurani imefika na Kiingereza ndio usiseme. Anashusha aya kwa Kiarabu kama vile kaandika Kurani yeye.”
Maji ya kunde: “Kujua Kiarabu na Kiingereza au kukariri Kurani huku huna kitu mfukoni ndio nini sasa? Anaishi kwa nyanya yake hadi leo. Unavyomuona pale kazi hana.”
“Tatizo lake watu wanadai ni laana. Eti kaachiwa radhi na wazazi.”
Thu 26 Aug 2004
Swali:
Utawala bora liende
Wawala
Nanyi mwalala?
Kura twapiga, sadaka twatoa
Kodi twalipa, swala twasali
Walalanjaa
Cha moto bado twakiona,
Kwanini?
Demokrasia ghasia, mafukara twauziwa
Jehanamu ya moto, masikini twatishiwa
Wa kusema wamesema
Wa kusikia ni viziwi,
Chukua Chako Mapema
Ni azimio la wapi?
Wale wa dini, siasa, enjioo*
Matumbo yamewajaa kwa hadaa
Hawakosi madaha, mzaha
Karaha, zinaa
Unashangaa
Awe yule wa msalaba
Au mwezi na nyota,
Wa bendera ya kijani
Nyeupe au Nyekundu,
Wa ofisi mfukoni
Kutumbulia ufukweni
Dola za wafadhili,
Hao lao moja.
Unafiki wauafiki
Viambaza vya utawala,
Enjioo mtaji poa
Wasomi changamkieni,
Myooshapo kidole kimoja
Vitatu vyawahukumu.
Kanisani, msikitini
Uhaini dhidi ya imani
Isaka, Ismaeli
Mababu wa akina nani?
Nukuu za maandiko
Anguko la kizazi
Dalili zi wazi,
Waza na kuwazua
Kwani kumepambazuka,
Wameasi desturi
Mistari ya manabii,
Kunga za mababu na mabibi
Kwenu tamthiliya ya punguani.
Utamaduni msalabani,
Siasa Babeli Mkuu,
Ijumaa, jumamosi, jumapili
Kwa kanzu na misahafu
Wawarubuni,
Leo katika Bunge
Mchezo wa kuigiza,
Viongozi kuwa “watawala twawala”
Ni aya ipi ya katiba?
Utawala bora liende wawala
Nanyi mwalala,
Ndotoni mkiimba
Amani na utulivu.
Amani na utulivu
Watawala ikulu wadai
Huku wakinywa divai,
Mavazi tai shingoni
Sisi viraka nguoni,
Jasho, kilio, machozi.
Amani, utulivu
Sitaki,
Sihitaji!
- Ndesanjo©, Tanzania/USA (2003)
*enjioo = NGOs (Non-Governmental Organisations)
Thu 26 Aug 2004
Watazame…
Hatia imewaganda
Ndani ya dhamira zao
Watafanya kila wawezalo
Kutimiza madhambi yao
Hawa ndio samaki wakubwa
Walao samaki wadogo.
Kama wewe ni mti mkubwa
Basi sisi ni shoka dogo
Lenye makali na tayari
Kukukatilia mbali
Kwa! Kwa! Kwa!
Thu 26 Aug 2004
Uzeni,
Kila kitu uzeni.
Nasema uzeni,
wala bei msitutajie
Mikataba msituonyeshe
Uzeni,
Hata nafsi zetu wauzieni.
Zama za soko huria
Na utandawazi,
Rais atamka
Hotuba redioni.
Utandawizi
Soko holela
Karl Peters wa leo,
Wamasai kuchunga binadamu
Badala ya ng’ombe,
Bajeti kupelekwa Washington
Kabla ya Dodoma.
Dunia ya leo
Ukoloni mamboleo
Wajishinikiza.
Uzeni,
Nasema
Kila kitu uzeni!
- Ndesanjo Macha©, Mbezi, Dar Es Salaam, Tanzania, 2003.
Wed 25 Aug 2004
Niko mbioni kuweka makala na hadithi za mwandishi, mwanamuziki, na mshairi Freddy Macha. Makala hizi zinatokana na maisha yake Kanada, Uingereza, Brazili, Ujeremani, n.k. Hadithi nitakazoweka ndani ya blogu ni baadhi ya mkusanyiko wa hadithi zake utakaochapwa katika kitabu kitakachoitwa Mpe Maneno Yake.
Tue 24 Aug 2004
Karibu ndani ya blogu yangu! I know you don’t speak Swahili, but since you were recently in Tanzania (although you dont remember the name of the places you visited!!!!), I assume you might recognize a few words!
Sun 22 Aug 2004
Ndio ndugu zanguni,
Nimerudi usiku wa leo. Nina rundo la barua pepe toka kwenu ambazo zitaweza kuzipitia na kujibu. Ninahitaji kupumzika. Ninashukuru walioniandikia. Walioniuliza maswali nitawajibu.
Ndugu Maka Patrick Mwasomola ninashukuru kwa kunikumbusha juu ya Siti Binti Saad (1880-1950). Nitaandika kidogo juu ya mwanamama huyu ambaye watu wanataka kumsahau ila historia inakataa.
Mwasomola katuma ubeti toka Diwani ya Shaban Robert, Siti Binti Saad, Kitabu cha Tatu:
Siti Binti Saad,ulikuwa mtu lini?
Ulitoka shamba,
na kaniki mbili chini
Kama si sauti ungekula nini?
Ninapumzika kisha nitarudi. Safari imenichosha. Nina mambo kadhaa mapya. Kaa chonjo!
Wed 18 Aug 2004
Ninasafiri leo alfajiri au kesho usiku kuelekea jimbo la Vermont. Nitarudi jumapili. Sina uhakika kama nitakuwa hewani. Ninajaribu kutengeneza blogu hii ili niweze kutuma taarifa kwa simu nawe uweze kunisikiliza kama una spika kwenye tarakilishi (computer) yako. Nimejaribu kwa lisaa limoja sasa lakini bado sijafanikiwa. Ila ninakuachia zawadi ya makala tatu mpya. Ni mpya katika blogu ila ziliandikwa muda kidogo kwa ajili ya safu yangu ya kila jumapili katika gazeti la Mwananchi. Kwa mfano, makala ya Krisimasi bila Yesu niliandika Krisimasi ya mwaka jana. Makala hizo ziko chini ya picha yangu mkono wa kuume. Nenda soma, furahia. Hadithi ya mtoto wa kichagaa na mtoto wa kizungu itaendelea.
Pia niko mbioni kuweka kamera tovuti (webcam) ili ukija kwenye blogu yangu kama niko mtandaoni utaweza kuniona. Au sio? Kwaheri. Uhuru!
Wed 18 Aug 2004
“Mbona huwa unanikodolea macho sana?” Nimeamua kuvulia maji nguo. Kila siku ninasema nitamuuliza. Leo nimeamua.
“Nakukodolea macho?” Ananiuliza huku akipitisha mkono kichwani kurudisha nywele zake ndefu nyuma.
“Ndio. Hakuna ubaya. Ninapenda kujua kwanini.”
Ananitazama. Anatabasamu. Ananitazama tena. Kama ilivyo mazoea yake, anapitisha kichwani vidole vyake vyembamba vyenye kucha zenye matunzo kurudisha nywele nyuma. Yaelekea anapenda nywele zake sana. Jina lake ni Lisa. Mama ni mtaliano. Baba Mmarekani.
“Unataka nikwambie kwanini nakutazama?” Ananiuliza.
“Nataka uniambie ndio maana nimekuuliza.”
“Napenda nywele zako.” Anasema huku anatoa tabasamu la aibu. Kisha anarudisha nywele nyuma. Safari hii hatumii vidole. Anatikisa kichwa kidogo upande mmoja. Nywele zinatii amri.
” Naomba kushika nywele zako”
ITAENDELEA…
*******************************************************************************
Ndugu yangu kisa hiki kitaendelea. Rudi tena hapa ili usipitwe.
Wed 18 Aug 2004
Baada ya kuishi ukimbizini kwa miaka 22, mwandishi na mwanaharakati wa lugha za kiafrika, Ngugi wa Thiong’o amerudi nyumbani Kenya na kukaribishwa na ukweli wa hali halisi ya maisha ya jijini Nairobi, ambayo wengine wanaita Nairobbery. Soma habari za “ukaribisho” huo kwa kubonyeza hapa.
Tue 17 Aug 2004
Kuna mradi wa kuingiza kiswahili katika teknolojia ya tarakilishi unaoendesha na kampuni ya Microsoft na Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam. Mtu yeyote anaweza kushiriki katika mradi huu kwa kubonyeza hapa.
Najua kwa watu wasiounga mkono kampuni za kibeberu kama Microsoft mradi huu hautawafaa. Kuna watu, kama mimi, ambao tunaegemea zaidi katika programu za tarakilishi zilizo chini ya dhana ya “open source” ambapo programu hizi (tofauti na programu za Microsoft ambazo kanuni [code] zake ni siri na zinamilikiwa na kampuni hii) zinamilikiwa na mtu yeyote. Programu za tarakilishi za “open source” hazilindwi na sheria ya hatimiliki ambayo nia yake ni kutengeneza faida kwa wachache. Dhana ya “open source” au “free source” inabadili kabisa hakimiliki toka kuitwa “copyright” na kuitwa “copyleft.” Watu wengine wanasema kuwa ujamaa wa kweli duniani hivi sasa unaonekana katika vuguvugu la “open/free source” (Open/Free Source Movement) ambalo linaichukua dunia kwa kishindo na kutishia Microsoft. Nchi kama Brazil, China, Vietman, n.k. ziko mbioni kuondoa kabisa matumizi ya Microsoft, hasa serikalini, na kuchukua programu za tarakilishi (software) zinazotokana na “open source” (hasa LINUX/GNU).
Kwa taarifa zaidi jinsi ambavyo “open source” inavyosaidia nchi za ulimwengu wa tatu kuondokana na ubeberu mpya kupitia kanuni za programu za tarakilikishi (software codes) bonyeza hapa.
Ukipenda kujua faida za “open source” kwa Afrika (na madhara ya Microsoft) bonyeza hapa.
Ili kujua kwa undani dhana ya “open source” bonyeza hapa.
Tue 17 Aug 2004
Mon 16 Aug 2004
“Soda za bure zimeisha.” Massawe anamjibu huku akijisogeza karibu na dirisha alikojiegemeza. Anaendelea kuomba huku akilegeza macho.
“Soda za bure zimekwisha. Hunisikii?”
“Hizo kwenye friji sio soda? Angekuwa nanihii ungesharuka kumpa duka zima.”
Ni saa mbili mbili asubuhi. Mariamu amejinasua kama kawaida yake. Massawe tamaa kwa Mariamu zimempalia. Lakini leo hataki kutoa soda bure kama afanyavyo kila Mariamu anapokwenda dukani kwake. Amechoka kuwa bwege. Ameanza kuwa “mjanja wa mjini.” Ni miezi sita imepita toka mtoto wa mjomba wake alivyomtoa MOshi na kumleta jijini aje kuuza duka la rejareja lililoko Mbagala Kizuiani.
“Yaani soda nitoe mimi, kufaidi wafaidi wengine.” Anajisemea.
Halafu, “Wewe jana umejifanya kupita kule sio?” Kulikuwa na ahadi ya kukutana jana jioni dukani kwa Massawe kisha waende Mpakani Guest House. Ni mara ya saba hii Mariamu anaacha kutimiza ahadi.
Mariamu anakataa, “Kupita kule wapi?”
“Usijifanye umesahau. Unadhani sikukuona? Ndio bwanako yule?”
“Bwanangu nani?”
“Yule mwendesha mikokoteni hajakupa hela ya kununua soda?”
“Mimi unaona ni mtu wa kununuliwa soda na msukuma mkokoteni?
Massawe anamsogelea Mariamu kama vile anataka kumnusa. Kisha, “Hivi umeoga wewe?”
Leo ni siku ya kumtolea Mariamu uvivu.
“Kwanini nisioge? Labda wewe hapo ndio huogi. Wachagga nyie mnavyopenda hela mnaweza hata mkasahau kuoga.”
“Mbona nasikia harufu ya janaba?”
“Jamani msikieni huyu. Labda wewe ndio unanuka janaba.”
Massawe anaendelea, “Wewe kule ulikolala umeoga?”
“Hebu mwoneni huyu. Kwanini nisioge?”
Massawe anacheka kwa kejeli na hasira iliyojificha, “Yule naye ana bafu? Maji kapata wapi? Bomba lao limekatwa.”
“Wewe ukilala na mwanamke humpi maji?”
“Kama ameyaleta yeye ataoga.”
“He, yaani umchafue tu?!”
“Nani kamchafua nani?”
“Wewe si ndio umemwagia?” Mariamu anasema huku akiondoka. Ameudhika.
“Uchoyo utakuua. Soda moja ya bure ndio imezua yote haya?”
“We unapenda vya bure tu sio?”
Mariamu hajibu. Anaondoka kwa mwendo wa maringo. Massawe anamtazama. Anazidi kumtamani. Donge la hasira na kukata tamaa linamkaba kooni. Kwa miezi miwili amekuwa akitoa soda za bure ila hajafanikiwa. Anashanga: kwanini waendesha mikokoteni, wapiga debe, madereva, makondakta “wanafaidi” ?
Kosa langu nini? Hana jibu. Anaapa kuwa soda za bure hazitoki tena. Kajifunza. Mjini shule, mjini chuo kikuu!
- Mbagala, Dar Es Salaam, Tanzania, 2001



