Nimerudia kukisoma tena kitabu cha Mwembechai Killings and the Political Future of Tanzania kilichoandikwa na Hamza Mustapha Njozi na kupigwa marufuku na kiranja mkuu mtawala wa Tanzania Benjamin Mkapa. Sielewi hata kidogo sababu ya siri-kali ya Tanzania kukipiga marufuku. Hebu nawe kipitie kwa kubonyeza hapa.
October 2004
Sun 31 Oct 2004
Sun 31 Oct 2004
Kuna mjadala mtamu sana unaendelea juu ya ununuzi wa ndege ya Rais wa Tanzania. Nadhani ili watu wengi wafaidike na mjadala wenyewe, nitaweka maoni ya watu mbalimbali waliochangia na wanaoendelea kuchangia ndani ya blogu hii. Mjadala ni moja ya nguzo za demokrasia: Kujadili, kushawishiana, kukubaliana, kukataa kukubaliana, n.k.
Sijachangia lolote katika mjadala huu. Nina swali dogo ambalo ninatafuta jibu lake kabla sijaingia rasmi mjadalani. Hivi kwanini wachawi wa Tanzania wasisaidie taifa letu kwa kumpatia Rais ungo wa kusafiria?
Sun 31 Oct 2004
Rais mwizi wa kura, Joji Kichaka, anaandamwa na wapinzani wake kwa tuhuma kuwa hana kitu kichwani. Wanadai huyu jamaa shuleni mambo yalikuwa hayapandi hata kidogo. Moja ya vielelezo vya kuwa yeye ni mbumbumbu ni madai kuwa katika mjadala wa Urais alikuwa amevaa kidude cha mtandao usiwaya (wireless) ili awasiliane na mshauri wake Karl Rove, ambaye alikuwa akimnong’onezea majibu!
Wanadai pia kuwa ingawa Kiingereza ni lugha pekee anayoijua, lugha hii inampa tabu sana. Katika mjadala wake wa mwisho wa mwongo mwenzake wa chama cha Democratic, John Kerry, Bush alisema “internets” wakati ambapo neno internet halina wingi kwahiyo huna haja ya kuongeza “s” kama alivyofundishwa akiwa mtoto!
Ukitaka kuona picha ya kidude cha mtandao usiwaya alichovaa Joji Kichaka, kongoli hapa.
Sat 30 Oct 2004
Nimeweka makala mpya mbili kwenye kona ya makala zangu ambayo iko mkono wa kuume chini ya picha yangu. Makala hizi ni Dini na Utu (sehemu ya kwanza na ya pili). Kwahiyo ni vyema ukaanza kusoma namba moja kisha namba mbili. Makala hizi niliziandika kwa ajili ya safu yangu kwenye gazeti la Mwananchi, Gumzo la Wiki, kila jumapili. Karibu uzisome.
Sat 30 Oct 2004
JE WAJUA?
KWA MUJIBU WA UTAFITI ULIOFANYWA NA ASASI MOJA ISIYO YA KISERIKALI (NGO), IJULIKANAYO KAMA MKAKA FOUNDATION UMEGUNDUA YAFUATAYO:
1. ZAIDI YA ASILIMIA 89.76 YA MA BARMAIDS HAPA DAR ES SALAAM NI WENYEJI WA MKOA WA TANGA,YAANI WAZIGUA,WABONDEI,WASAMBAA NA WADIGO! TANGA KUNANI PALEEEE?
2. ZAIDI YA ASILIMIA 92 YA MA HOUSE GIRLS HAPA DAR ES SALAAM NI WENYEJI WA MKOA WA IRINGA YAANI WAHEHE. NYIKA VIPI HII KITU, MNOGEGE MNOFWELA?
3. ZAIDI YA ASILIMIA 78 YA WAUZA KAHAWA NA MAJI KWENYE MIKOKOTENI NI WENYEJI WA MKOA WA DODOMA YAANI WAGOGO. BABA MALECELA CIGWEMISI NI AJE?
4. ZAIDI YA ASILIMIA 96 YA WAVUNJA MAWE NA KOKOTO HUKO KUNDUCHI, TEGETA NI WENYEJI WA MKOA WA KIGOMA YAANI WAHA, HE BURAZA K NI AJE?
5.ZAIDI YA ASILIMIA 70 YA POMBE YA CHIBUKU INAYOZALISHWA KIWANDANI HUNYWEWA NA MAKABILA YA WANDAMBA,WARUGURU,WAPOGORO NA WANGONI WAISHIO MAENEO YA KIGOGO,MSIMBAZI MISSION, MBURAHATI NA TANDALE UWANJA WA FISI!
6.ZAIDI YA ASILIMIA 70 YA WASAMBAZAJI WA MAYAI YA KUKU WA KISASA HAPA DAR ES SALAAM NI WENYEJI WA MKOA WA MARA, WA KABILA LA WAKURYA, WAISHIO HUKO KIPUNGUNI NA GONGO LA MBOTO!
Sat 30 Oct 2004
Nimepata habari hii toka kwenye blogu mpya ya Mtanzania iitwayo Furahia Maisha Yako. Anasema kuwa orodha hii ni ya majina ya walioingia raundi ya pili katika mchuano wa wenye majina yasiyo ya kawaida. Kweli kuna majina hata mimi ninayetetea umuhimu wa kuwa na majina ya asili yamenitoa jasho nene. Orodha hii hapa:
1. Ndugu TAMPERA NGUNAMABWOKO-Muhitimu wa kidato cha sita shule ya sekondari ya wavulana Tabora mwaka 1992.
2. Ndugu GOGOMOKA MISALABA-Muhitimu wa kidato cha sita shule ya sekondari Minaki mwaka 1998.
3. Ndugu ABDALLAH NYUNDO KICHECHE-Mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Minaki mwaka 2002
4. Ndugu MASANINGA SUMAKU POMBOJOLOWE a.k.a PUMBU-Dereva wa mabasi ya Hood
5. Koplo RUBYENEKO MUGANYIZI BYOMBARIRWA-Mpishi mkuu wa kikosi cha 34 cha Jeshi (34 KJ), Mbeya.
6. Ndugu TAKOTAKO WA PUMBUJE a.k.a AKANANA-Muuza miwa na maji baridi maarufu pale magomeni makutano ya barabara za Rashid Kawawa na Morogoro
7. Mheshimiwa NJENGAFIBILI MWAIKUNGILE-Jaji wa mahakama kuu ya Tanzania
8. Mheshimiwa JOHN POMBE MAGUFULI-Waziri wa Ujenzi Tanzania
9.Ndugu TUNTUFYE MWAIKIMBA a.k.a KIMBA-Fundi majiko maarufu Railway Gerezani Dar es Salaam
10. Ndugu BENADETTA TYETYETYE-Muhitimu wa chuo kikuu cha Dar es Salaam, mwaka 2001 fani ya sayansi ya jamii (BA)
Fri 29 Oct 2004
Desemba mwaka huu wana Hip Hop wa Tanzania watafanya mkutano mkubwa katika ukumbi wa Diamond Jubilee. Kwa habari zaidi tembelea tovuti yao kwa kubonyeza hapa. Nimepata tarifa hizi toka kwenye blogu mpya ya Furahia Maisha Yako.
Wale tunaona kuwa lugha yetu ya Kiswahili ina umuhimu sana katika ujenzi wa taifa na utamaduni wetu, tunashindwa kuelewa kwanini Watanzania wamelewa namna hii huu mvinyo wa utumwa wa kifikra. Wazo la Hip Hop Summit na tovuti yao ni zuri mno. Ninawapongeza. Kutumia muziki na falsafa nzima ya hip hop kama moja ya njia ya kupambana na tatizo la ajira kwa vijana nchini Tanzania ni wazo la kuungwa mkono na kila mtu. Lakini swali langu kila siku ni hili: kama unaanzisha jambo kwa ajili ya Watanzania kwanini unatumia lugha ya watu wengine?? Hili ni swali la msingi. Nimetembelea hii tovuti ya hip hop summit nikajiona kama ninasoma jambo linalohusu Marekani, Canada, au Uingereza. Kumbe ni jambo linalotuhusu Watanzania. MOja ya madhumuni ya hip hop summit ni kuwaunganisha watu wote wanaohusika katika nyanja ya muziki huu, kubadilishana mawazo na kutazama jinsi ambavyo muziki unavyosaidia kuondoa tatizo la ajira na umasikini Tanzania. Kama nia yao ni hii, kwanini webu yao wameandika kwa kiingereza? Kwanini wameita Hip Hop Summit? Hao vijana wanaowazungumzia ambao hawana ajira na masikini wanatumia lugha gani katika maisha yao ya kila siku? Mara nyingi vyama, mashirika huanzishwa kwa ajili ya wafadhili, kutokana na sababu hii utaona majina ya mashirika au vyama hivyo ni ya kiingereza (lugha inayotumiwa na hao wafadhili). Nimetembelea tovuti yao kutafuta kiswahili bila mafanikio. Tukumbuke kuwa wanamuziki ndio watatumia uwezo na ubunifu wao kutuondoa katika utumwa wa fikra. Ukombozi wetu na mapambano dhidi ya umasikini Tanzania mwanzo wake ni kwenye fikra.
Tafadhali nenda kwenye hii webu. Waandikie hawa mabwana. Waombe watumie lugha yetu ya Kiswahili. Hii lugha haina mapungufu yoyote. Ni lugha nzuri. Ni lugha ya maendeleo. Ni lugha inayotumiwa na walalanjaa ambao hip hop summit inataka kuwasaidia. Msaada wao uanze kwenye fikra zetu. Watusaidie tujue kuwa uhai wa taifa uko kwenye utamaduni na historia yake. Tafadhali fanya hivi. TUJIKOMBOE!
Fri 29 Oct 2004
Pamoja na kubanwa na shughuli nyingi, zikiwemo za uchaguzi wa Urais wa hapa Marekani, nimeona ni vyema nichukue nafasi hii kutangaza kuwa kuna Mtanzania mwingine, Dennis Mponji, ambaye ameingia kwenye ulimwengu wa wana blogu. Blogu yake iitwayo FURAHIA MAISHA YAKO inaungana na blogu nyingine mpya ya Mtanzania Simon Mkina iitwayo KONA YANGU. Niliwahi kusema kuwa Wakenya kwa upande wa Afrika Mashariki ndio ambao wako mbele sana katika ku-blogu. Ninafurahi ninapoona Watanzania nao wanaanza kutumia teknolojia hii rahisi na nyepesi kujifunza kuwasiliana, kupeana taarifa, kutoa mawazo yao bila kuwa chini ya uangalizi wa mtu yeyote. Kongoli hapa kuiona blogu ya Furahia Maisha Yako. Bado iko kwenye ujenzi, siku zinavyokwenda itazidi kubadilika. Pia kama hujatembelea blogu ya Kona Yangu ambayo iko kwenye safu ya blogu za Wana Afrika Mashariki upande wa kuume ndani ya blogu hii, kongoli hapa uitembelee.
Iwapo kuna mtu yeyote anayetaka kuwa na blogu au ana maswali yoyote juu ya blogu (yawe ni maswali ya kitaaluma, kitaalamu, au vinginevyo) wasiliana nami nitafanya niwezalo kukusaidia. Niandikie: ughaibuni@yahoo.com au kama uko Marekani unaweza kuongea nami: 419-699-8085.
Tue 26 Oct 2004
Hii ni sehemu ya pili ya habari niliyoiita “Kimulimuli nyuma yangu.” Kama hukusoma sehemu ya kwanza, isome ndipo umalizie kusoma hii. Niliiandika jumapili ya tarehe 18 mwezi huu.
**********************************************************************************
Basi tarehe 18 nikaelekea mahakamani. Kwanza nilifikiri kuwa nilitakiwa niende asubuhi saa nne. Nikampigia rafiki yangu mmoja simu kumuuliza jinsi ya kufika Mahakama ya Manispaa. Mimi huwa sipendelei sana kwenda katikati ya mji. Sifahamu sana barabara za mjini. Kati ya vitu vinavyonifanya nisiwe na tabia ya kwenda katikati ya mji ni jinsi barabara zake zilivyo. Huwa zinanichanganya sana maana nyingi haziruhusu magari kupishana. Ni barabara za magari yanayoelekea upande mmoja. Halafu kingine ni polisi. Mjini pale kila kona kuna gari la polisi. Sipendi kukutanakutana na polisi hata kidogo. Wananiudhi sana na magari yao yenye ving’ora na vimulimuli. Sehemu za kupaki pia ni chache na ghali.
Basi mshikaji wangu Manley akanipa maelekezo ya jinsi ya kufika mahakamani. Kisha akaniuliza, “Unatakiwa saa ngapi?” Nikamwambia, “Nadhani ni saa nne asubuhi.” Akacheka na kuuliza (huwa anapenda kuniita profesa maana aliwahi kuwa mwanafunzi wangu), “Profesa, unadhani au una uhakika?”
Nikaamua niitazame tena tiketi yangu. Kumbe mahakamani nilitakiwa saa saba mchana. Nikaamua kurudi nyumbani nikale na kutazama kituo cha luninga cha C-Span ambacho hakina matangazo hata siku moja. Saa sita na kitu hivi nikaondoka zangu. Nimezunguka mjini kama dakika 20 nikitafuta mahali pa kupaki gari karibu na mahakamani. Mwishoni nikaamua kupaki karibu na maktaba kwenye makutano ya Michigan na Adams. Nikaweka hela za kupaki za saa moja.
Nilishasahau kuwa ninaishi kwenye nchi yenye hofu ya kuvamiwa na jamaa zake yule bwana mwenye madevu anayeishi mapangoni kule Afghanistan. Basi nikakuta kuna mashine za kutazama kama mtu amebeba silaha. Nikaambiwa nitoe kila kitu mfukoni na kuweka ndani ya bakuli la rangi ya kahawia. Baada ya kuonekana kuwa sina chochote cha kutishia usalama nikaruhusiwa kuingia.
“Naelekea mahakama namba nne.” Namweleza binti aliyeko mapokezi. “Mahakama namba nne imehamia namba sita.” Ananiambia. “Chukua lifti hadi gorofa ya nne.” Ananielekeza. Ninapoifika mahakama namba sita nakuta imeshehena watu. Nachungulia kutazama sehemu ya kukaa. Jaji anasema, “Wenye majina yanayoanza na A hadi M wabaki hapa, waliobaki waende gorofa ya pili mahakama namba 2.” Baadhi ya watu wanaondoka. Najivuta na kuketi. Mahakama inaanza shughuli zake. Watu wanaitwa mmoja mmoja. Wanaokuja hapa wote wana makosa ya barabarani. Jaji anakusome shtaka na adhabu yake na kukuuliza kama unakiri. Ukikataa kosa unapewa siku nyingine. Ukikubali unasomewa adhabu. Kama ni faini unaambiwa ulipe. Kama ni kifungo anakuuliza kama unaelewa kuwa ukikubali kosa utafungwa, na kuwa unaweza kufungwa kuanzia siku hiyo.
“Kosa lako la kuendesha bila leseni linaweza kukupeleka jela miezi sita pamoja/au faini ya dola 1000. Una haki ya kutafuta wakili.” Jaji anasema. Wakati huo mimi ninajiuliza nitafikiwa saa ngapi? Nilidhani kuwa nitakaa mahakamani kama saa moja hivi. Matokeo yake nilikwenda kuweka hela zaidi kwenye mita ya nilikopaki gari mara tatu. Toka saa saba niliondoka mahakamani saa kumi jioni. Nilipofikiwa nilikuwa nimechoka hasa.
“Desanyo Maka,” Jaji aliniita. Watu wengi wanashindwa kutamka Ndesanjo na Macha wanadhani inatamkwa Maka. “Nipo.” Nikaitikia na kwenda kizimbani.
“Una kosa la kupita kwenye taa nyekundu na kuendesha bila kuvaa mkanda. Una hatia au huna hatia?” Alinisome shtaka na kuniuliza.
“Nina hatia kwa kosa la kwanza la kupita kwenye taa nyekundu ila sina hatia ya kutokuvaa mkanda.” Askari aliyenikamata alidhani kuwa sikuvaa mkanda maana baada ya kunisimamisha, niliingiza mkono mfukoni ili kutoa leseni ya udereva, nikaweka simu mfukoni na kutoa kamba ya kusikilizia masikioni na kuweka mfukoni, alipoona ninajigusagusa akadhani kuwa ninakazana kufunga mkanda.
Ingawa nimetoka kwenye nchi ambayo watu wengi wanaamini kuwa ukifunga mkanda utashindwa kuruka wakati wa ajali, ninapoingia ndani ya gari jambo la kwanza ni kufunga mkanda. Nimekutana na watu wengi Tanzania wanaosema, “Ukifunga mkanda ni rahisi kufa wakati wa ajali!”
Jaji akaniuliza kama nina bima ya gari. Nikamwonyesha. Akasema, “Una hatia ya kupita kwenye taa nyekundu, unatakiwa ulipe faini ya dola 100. “Utalipa leo au siku nyingine?” Jaji akaniuliza. Nikajibu kwa uchungu, “Leo.” Dola 100! Shenzi taipu!
Tue 26 Oct 2004
Hivi njia ya muongo ni fupi au ndefu? Kongoli hapa.
Fri 22 Oct 2004
Mwanamuziki Ndala Kasheba ameaga dunia. Nimeamua kwa wiki moja sitamsikiliza mwanamuziki yeyote zaidi ya Ndala Kasheba. Kasheba aliingia Tanzania miaka ya 60 akiwa na bendi ya Orchestra Fauvette. Kasheba pamoja na kuwa ndio mwanzilishi wa mtindo ambao bado ninaupenda ile mbaya, Dukuduku Yee!, ni mwanamuziki wa kwanza Tanzania kudonoa gitaa la nyuzi 12. Ni baada ya kuzindua gitaa hili pale viwanja vya Mnazi Mmoja miaka ya 80, marehemu Kasheba alipachikwa jina la Supreme. Siku hiyo alivunja gitaa lake la nyuzi sita na kulivaa gitaa la nyuzi 12 ambalo alikuwa “akilinyanyasa” hadi alipofariki.
Moja ya nyimbo za marehemu ambazo zimewahi kuvuma sana ni ule wa Dezo Dezo alioutunga akiwa na bendi yake ya Zaita Musica. Wimbo huu ulikuja kurekodiwa na Tshala Muana. Katika wimbo huu anasema:
“Ewe mtoto wa kike, acha umbeya, mbeya…nitakusemea…”
“Unapenda dezo dezo…sigara hutaki kuacha…eh bwana we yatakushinda.”
Nyimbo zake nyingine ni Marashi ya Pemba, Chunusi, Marinella, Nimlilie Nani, na Sungura Weba. Santuri yake ya mwisho iliitwa Yellow Card. Hii pia ni santuri yake ya kwanza kutolewa nchini Marekani. Wimbo wa Yellow Card aliuimba kufuatia uvumi kuwa amefariki kwa ukimwi. Katika wimbo huu anasema: “…hata wewe ni marehemu mtarajiwa.”
Mara ya mwisho kumuona akifanya onyesho la hadharani (live) ilikuwa ni mwaka 2002 pale kwenye bustani za Mnazi Mmoja. Alipanda jukwaani na King Kiki na Babu Seya. kati ya mwaka 1994-97 nilikuwa nikihudhuria maonyesho yake ya usiku kule Sinza (nimesahau jina la ile klabu) ambapo tulikuwa tukipeperusha kitambaa cheupe. Onyesho la mwaka 2002 lilinidhihirishia kuwa kwa upigaji wa gitaa Tanzania, marehemu Kasheba hakuwa na mfano. Huyu bwana alikuwa akidonoa nyuzi kama vile anakunywa chai barazani huku akitazama wacheza bao. Tutamkumbuka daima.
Ukitaka kusikiliza baadhi ya nyimbo zake au kununua CD yake (hasa kwa walioko Marekani) kongoli hapa.
Thu 21 Oct 2004
Mfanyakazi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Simon Mkina, ameingia kwenye ulimwengu wa blogu. Hadi hivi sasa Wakenya ndio wako mstari wa mbele katika matumizi ya zana hii mpya ya mawasiliano. Blogu za Wakenya ni za Kiingereza. Siku zinavyokwenda nina imani kuwa Watanzania wengi zaidi wataingia kwenye ulimwengu huu wa blogu ambao tunapashana habari na kuelimishana kwa njia rahisi na haraka. Kongoli hapa uone blogu ya Mkina.
Thu 21 Oct 2004
Nimeweka kona ya blogu za Waafrika Mashariki. Wakenya wako mbele kidogo kwenye ulimwengu wa blogu (blogsphere). Nimeweka blogu nne kwa sasa ila bado ninapandisha nyingine zaidi. Jioni nitaweka moja ya Mtanzania aliyeko Dar. Blogu zenyewe ziko mkono wa kuume chini ya “archives.”
Thu 21 Oct 2004
Nimekuwa na pilikapilika za hapa na pale. Kwa siku mbili hivi sikuwepo hapa ndani ya blogu. Baadaye leo nitaendelea na kile kisa cha kusimamishwa na polisi kwa madai ya kutokutii taa nyekundu na kutokufunga mkanda. Tarehe 18 nilikwenda mahakamani saa saba mchana. Nitakueleza nini kilitokea. Sasa hivi ninakwenda kwenye maandamano dhidi ya mgombea mwenza wa Bush, mwizi na muongo aitwaye Dick Cheney. Kwahiyo tutaonana hapo baadaye.
Sun 17 Oct 2004
Nimemaliza kukata kona ya barabara ya Upton kuingia barabara ya Bancroft. Nadhani ni saa tatu usiku. Nasikiliza zangu muziki wa Fela Kuti. Anaimba wimbo wake uitwao Mwalimu Usinifundishe Upuuzi. Fela! Nashindwa kummaliza…. Basi mara naona gari nyuma yangu yenye kimulimuli. Nafyonza, “Polisi huyo. Nimefanya nini?” Napunguza mwendo, naashiria kuingia upande wa kulia. Ninahamia upande wa kulia kisha nasimamisha gari. Polisi anasimama nyuma yangu. Nabaki ndani ya gari. Inapita kama dakika mbili hivi askari ananijia na kugonga dirishani huku mkono mmoja uko kiunoni penye bastola. Nashusha kioo. “Naomba leseni ya udereva.” Ananiambia. Ninampa. “Una leseni ya jimbo la Washington, una mpango wa kurudi Washington au kuwa hapa?” Namwambia kuwa sina uhakika ila sitakuwepo Ohio kwa muda mrefu. “Kama utaendelea kuishi hapa lazima uombe leseni ya Ohio.” Namwitikia. Anaichukua na kurudi garini kwake.
Nasubiri. Fela bado anaimba wimbo ule ule. Unajua nyimbo za Fela zilivyo ndefu. Wakati fela anarekodi na kampuni kubwa kwa mara ya kwanza, aliambiwa na kampuni hiyo, Polygram, kuwa lazima apunguze urefu wa nyimbo zake. Fela akagoma. Mpaka leo ana nyimbo ambazo ni zaidi ya dakika 30 tofauti na nyimbo nyingi za wanamuziki wengine ambazo huwa ni dakika tatu, nne, au tano. Ninaposikiliza nyimbo za Fela, kama leo hii, ninazidi kuelewa kwanini aligoma kufupisha nyimbo zake. Nyimbo za Fela ukizipiga kwa dakika tano itakuwa ni kama mtu mwenye njaa aliyepewa nusu kijiko cha chakula akipendacho. Nyimbo za Fela ni kama safari ndefu yenye matukio ya kufurahisha, kufikirisha, na kuchangamsha. Mrindimo wa ngoma, magitaa yanayopigwa kwa kurudiarudia kodi moja au mbili, kwaya ya matarumbeta yanayopayuka juu ya kinanda na gitaa la besi linalotembea kwa kuyumbayumba kwa madaha.
Askari amerudi. Ananikabishi leseni yangu na kipande cha karatasi. “Nenda mahakamani tarehe 18 mwezi huu. Umepita kwenye taa nyekundu na hukuwa umefunga mkanda.”
“Sikufunga mkanda? Mbona sikuelewi?”
“Utakapokwenda mahakamani utajitetea. Asante.” Anaondoka.
Kuhusu taa nyekundu sina uhakika kama nilifanya kosa. Ninadhani kama unatokea Upton na taa ni nyekundu, unaweza kuingia Bancroft kama hakuna gari lolote. Tarehe 18 ni wiki ijayo. Tusubiri. Mambo ya kwenda mahakama ya mtu mweupe siyapendi kabisa. Hata hivyo sina la kufanya. Ingekuwa nyumbani tukio hili lingemalizika kwa kuingiza mkono mfukoni.
Binadamu watu wa ajabu sana. Ukitoa rushwa unalalamika kuwa rushwa imekithiri. Ukikutana na mtumishi wa umma anayejali nidhamu ya kazi bado unaudhika!
Nasubiri wiki ijayo nitakueleza.
Sat 16 Oct 2004
Nani anasema kuwa hakuna mtu anayejali tena mila na utamaduni wa Mwafrika? Bonyeza hapa usome harusi ya kimila ya mtunzi Ngugi wa Thiong’o.
Sat 16 Oct 2004
Unakumbuka jinsi michezo ya kuchekesha ya Kenya ilivyokuwa inawamaliza Watanzania? Sasa naona tumerudisha goli kwa bongoflava/hip hop. Kuna habari hii kwenye gazeti la Daily Nation. Iliandikwa mwaka jana, ila kwa taarifa nilizonazo bado muziki wa Tanzania unawazengua Wakenya hadi hivi sasa. Bonyeza hapa usome habari kamili.
Thu 14 Oct 2004
Bonyeza hapa utembelee tovuti hii nzuri sana ya inayohusu muziki wa Afrika. Nimetembelea tovuti nyingi sana. Hii nimeipenda kichizi.
Thu 14 Oct 2004
Kuna ndugu zetu wako India. Walikwenda huko karne nane zilizopita. Wanapenda Kiswahili ambacho wanasema ni lugha ya mababu zao. Unafahamu haya? Nimekumbana na habari yao nilipotembelea blogu ya mwanafunzi Mkenya, Ory Okollah, aliyeko hapa Marekani: Kenyan Pundit (http://blogs.law.harvard.edu/ory/). Bonyeza hapa uisome habari nzima.
Thu 14 Oct 2004
Eti leo ni siku ya kumuenzi Mwalimu Nyerere Tanzania! Watu wanapumzika. Kisha? Kisha kesho wanakwenda kazini hadi mwaka ujao tena! Sijui ni watu wangapi wanamuenzi kwa dhati.
Mwezi wa saba mwaka huu niliandika kipande hiki juu ya Nyerere. Kwa heshima yake nitabandika tena ili ambao hawakupata kusoma wasome. Pia kama unataka kusikiliza hotuba zake, mwisho wa nukuu kuna sehemu ya kubonyeza ili umsikilize.



