November 2004
Monthly Archive
Tue 30 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Nimekumbuka jeshini! Da! Historia ile sitakaa nisahau. Nakumbuka siku naondoka na Nickson Malisa kuelekea tusikokujua. Kwanza tulipangwa kwenda kule Mgambo, Tanga. Mwanzoni tulitaka kujipeleka…ile kambi ya Arusha inaitwaje tena? Nimeisahau jina. Hata hivyo tukaamua kuelekea Tanga. Lakini tukiwa ndani ya basi tukaamua kwenda Maramba badala ya Mgambo. Tulisikia habari za kutisha kuhusu Mgambo na habari njema kuhusu Maramba. Basi hao tukamua kuchagua kambi wenyewe. Wakati huo tayari tumeshachelewa kuripoti. Tarehe zilishapita siku nyingi. Tukaingia Maramba jioni jioni hivi na vibegi vyetu na makubazi. Nakumbuka tulikuwa tunapenda sana kuvaa soksi za bluu na yale makubazi. Tulipoingia Maramba tuliamua kuwa hakuna haja ya kuripoti. Kuripoti kosa. Soo. Tulikuwa tunatumia mbinu za juu kabisa za kikachero. Ukifika mahali, kaa chini. Tafuta wajuaji. Ongea nao. Chunguza, “Kilitoka wapi, kikaishia wapi.” Hii ilikuwa ndio mbinu yetu ya kwanza.
Na wajuaji ndio akina nani? Wajuaji si wengine bali ni wale wanaolipia siku. Wale ambao hawajaruhusiwa kwenda nyumbani na wenzao kutokana na makosa kama utoro. Hawa ndio tuliwatafuta giza lilipoingia. Tuliingia bweni hadi bweni tukiwatafuta na kuongea nao. Nakumbuka, kama kumbukumbu hainihadai, kuna bwana mmoja ambaye hivi sasa anaishi Kinondoni. Nadhani ni fundi wa elektroniki. Alisoma Chuo cha Ufundi Mbeya. Basi huyu alikuwa ni mmoja wa jamaa waliotupa “picha” halisi. Jamaa poa sana. Usiku huo baada ya kuongea na watu kadhaa, tukaenda pembeni (mimi na Nickson Malisa) na kuanza kuchambua taarifa tulizokusanya. Kabla jimbi hajawika tulishaamua kuwa Maramba sio kambi yetu. Tutakaa hadi kesho yake usiku, kisha tutatoroka.
Sasa swali likaja, kwakuwa tunatoroka na hatutaki kujiandikisha, tutafanya nini siku nzima ili tusishtukiwe?
Wazo hili sijui nani alikuja nalo kati yangu na Nickson. Kesho yake asubuhi wakati jamaa wengine wanaelekea kwenye “kazi za ujenzi wa taifa” sisi tulielekea nje ya ofisi ya mkuu wa kambi! Tulijua kuwa watu wanaongopa sana eneo lile. Afande yeyote akituona pale hawezi kutubugudhi. Lazima atajua kuwa tumeamriwa kusubiri mtu hapo. Basi tulikaa pale hadi saa ya kula. Tukaenda kula. Wakati tunachukua chakula tukashtukiwa. “Sura ngeni hizi.” Tukajitetea ni wageni na tumetakiwa tuonane na mkuu wa kituo na anavyotuona hivyo tukimaliza chakula tunaenda ofisini kwake. Tukala, kisha hao tukarudi kwenye “ofisi” yetu. Tukasimama nje ya ofisi ya mkuu wa kituo tukipiga gumzo na kubishana. Tulikuwa tunapenda kubishana sana enzi zile. Kubishana na kucheka. Na kuzidi watu akili! Hakuna kitu kilichotufurahisha kama kuzidi watu akili. Hasa watu kama maafande.
ITAENDELEA
***************************************++*****************************************
Nabakisha uhondo kwa ajili ya siku nyingine. Njoo nitaendelea. Nitakupa pia na kisa cha kambi ya Ruvu nilipokutana na bwana Obey Nkya amekusanya watu anahubiri ukombozi…Obey, mpaka leo sikumalizi. Sitakaa nisahau pale Ruvu. Mimi na Nickson tulikutazama kisha tukatazamana na kusema, “Huyu jamaa ni nani? Lazima tujuane naye.”
Tue 30 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Kuna nasaha nyingine za Rehema Nchimbi: SHIME TUSHIKAMANE. Kongoli hapa ujisomee.
Pia kuna barua toka Amsterdam ambayo nimeifuta kimakosa. Barua hii ni toka kwa bwana Chumi. Nitamuomba atume tena.
Tue 30 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Makala niliyoahidi tayari nimeiweka hapa ndani. Nenda pale kwenye kona za makala zangu. Kumbuka ni chini ya picha yangu, upande wa kulia, chini ya maneno haya: KONGOLI USOME MAKALA ZANGU. Makala yenyewe inaitwa: Mapinduzi ya Umma Dhidi ya Dhuluma.
Tue 30 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Yule mshairi mahiri wa hapa Marekani, Gil Scott-Heron, ana shairi liitwalo The Revolution Will Not Be Televised (kongoli hapa ulisome). Sasa sisi wanablogu tunakuja na yetu. Tunasema kuwa MAPINDUZI YATATOKEA BLOGUNI (The revolution Will be Blogged!). Tazama jamaa wa Kona Yangu anavyochanja mbuga na kutimulia vumbi wabunge, wana si-hasa, na wahariri wenye mikono inayotetemeka. Halafu kuna jirani yetu wa Mawazo na Mawaidha. Anakwenda mwendo wa Kimombasa, ambako meli hupita barabarani na nyumba zina gorofa ndani kwa ndani. Yeye tayari ameshamlima “Baba” Moi. Eti “Baba.” Ilibaki kidogo tu wangemwita mungu! Unakumbuka kila taarifa ya habari Kenya ilikuwa lazima ianze na habari za “Baba.” Mara kakohoa. Mara kalala mchana. Kila jumapili lazima tuambiwe eti kaenda kanisani. Hivi alikuwa anatumia mdomo huo huo kudanganya wananchi kwa kuombea mola au alikuwa ana mdomo mwingine?
Haya, kuna ndugu yetu Mponji wa Furahia Maisha. Anauliza, “Ulaya kunani?” Kaahidi mambo yako jikoni. Epua upesi!
Kuna yule dada yetu Ory Okolloh wa Kenyan Pundit. Anaambaa kwa blogu ya ung’eng’e toka Harvard. Katundika hadharani furaha yake kwa kuona wanablogu wa Kiswahili wanavamia uwanja. Ndio, tumeingia na baraka za mizimu ya mababu. Jamani, mnakumbuka wimbo wa marehemu Kalikawe wa Mizimu? Katika nyimbo alizoandika ule wimbo. Halafu kuna wanablogu Waafrika wengine kama akina Mshairi, Uaridi, Beginsathome, na kadhalika.
Tue 30 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Siku mpenda ugomvi Rumsfield alipomtembelea Saddam Hussein mjini Baghdad na kushikana mkono wa urafiki. Tazama mikono yenye damu ikisalimiana. Bonyeza hapa.
Mon 29 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Nimeng’ang’aniwa. Kono la beberu kooni. Buti lake mgongoni. Nahema kwa masikio! Nikiuliza naambiwa, “Ndio ‘American Dream’ ati! Ulidhani picha za kwenye gazeti la Ebony ndio maisha halisi ya kiwanja cha Joji Dabliyuu Kichaka? Utashaa…”
Basi wakati napambana na beberu, bwanyeye, mchuna nafsi, ngozi, na utu nakushauri kongoli/bonyeza hapa.
Sun 28 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Siku hizi najisikia kama vile naishi nchi ya kipolisi. Licha ya kuwa kuna vimulimuli vya polisi na ving’ora kila mahali, sasa hivi madereva wanabanwa kila kona. Barabarani manjagu wamejaa, halafu kuna kamera zinazochukua picha ukivunja sheria ambapo unatumiwa tiketi nyumbani kwa njia ya posta pamoja na uthibitisho wa picha ya gari lako (namba zake) na saa. Zaidi ya hilo hapa Toledo wameanza kutumia helikopta. Jamani! Ukiendesha unakuwa kama vile kuku aliyemwagiwa maji. Kama utatazama kila upande kutafuta askari ujue una kazi ya kuendesha huku ukitazama angani kutafuta iliko helikopta.
Tuache hilo, wanadai wanaimarisha usalama.
Nimeanza kuandika moja ya mradi mkubwa wa JIKOMBOE. Mradi huu umepewa jina: MWAFRIKA AKUTANA NA… Kwahiyo kutakuwa na sehemu mbalimbali kwa mfano: MWAFRIKA AKUTANA NA MUISLAMU, MWAFRIKA AKUTANA NA MKRISTO, n.k. Unaweza kujiuliza, “Kwani muislamu na mkristo sio Waafrika?” Ukiwa na swali hili, jua kuwa JIKOMBOE iko kwa ajili yako. Unaihitaji. Wakati unasubiri jibu lake, uwe ukisikiliza Wimbo wa Ukombozi (Redemption Song) wa Bobu Malya (ndio, Malya…hujui Bobu alikuwa Mchagga ndio maana Wachagga huwaambii kitu kwenye marege??)
Kuna habari nzuri sana kanitumia Nambiza Joseph Tungaraza (mwenzetu anayeishi Australia) kuhusu madhara ya dawa za kujichubua. Nitaipandisha hapa maana iko kwenye misingi ya ukombozi wa fikra. Kuna tatizo kila nikiiweka, lakini nitapatia ufumbuzi karibuni. Nitasonga kwanza ugali kisha nije kujaribu tena. Kwa taarifa yako leo najikata ugali wa nguvu. Ugali na kabichi na karanga. Habari hii ya kujichubua inaendana na dhana ya bwana mmoja toka NIgeria, Chinweizu, anayoiita Negro negrophibia. Yaani chuki ya watu weusi kwao wenyewe (kujichukia kwa watu weusi). Huyu bwana ana kitabu kizuri sana kwa watu wanaofuatilia masuala ya ukombozi wa fikra na elimu ya historia na utamaduni wa Mwafrika. Kinaitwa: THE WEST AND THE REST OF US. Nadhani kinapatikana pale British Council, Dar Es Salaam. Sina uhakika, ninadhani. Lazima ukisome hiki kabla hujaaga dunia!!!!!!
Usisahau kutazama blogu mpya nilizopandisha ikiwemo ile ya mwenzetu toka Kenya ya Mawazo na Mawaidha. Iko hapa. Zile mbili za Watanzania, Kona Yangu na Furahia Maisha, nazo zina mambo mapya. Ninakumbusha kuwa wale wanaotaka kuwa na vyombo vya habari (kuwa na “shihata” yao) kwa njia ya blogu wasisite kuwasiliana nami kama wana maswali. Na pia nimeweka somo la kwanza hapa kwenye blogu kwa wale ambao wanazo na wale ambao wanatengeneza zao kama bwana Kesi kule Kampala. Kesi karibu sana kwenye ulimwengu wa blogu.
Sat 27 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Azimio Magehema kaniandikia kisa cha siafu alichokitoa Mwalimu Nyerere. Ujumbe wa kisa hiki unaendana na dhana ya kujikomboa. Ukombozi wa fikra hautokei siku moja. Polepole, tutafika. Nakumbuka maneno ambayo Nambiza Joseph Tungaraza alipenda kuyasema tukiwa pale Ilboru, Arusa (Arusa, ndio, usidhani nimekosea!). Alipenda kusema: Daima Mbele, Nyuma Mwiko.
Haya ujumbe alioniandikia Azimio (jina zuri sana hili) huu hapa:
Namnukuu Mwalimu Nyerere aliposema, “Sungura alimuuliza siafu unakwenda wapi, Siafu akajibu KUMUUA TEMBO!!! Sungura kwa mshangao akasema lakini Tembo mkubwa sana mtamuweza?? Siafu akajibu TUTAJARIBU TENA TENA TENA NA TENA…”
Sat 27 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Nilikuwa natafuta sehemu ya pili ya makala ya Urasta baada ya Azimio Magehema kunikumbusha. Katika tafutatafuta nikakutana na makala ambayo niliiandika miaka mitatu hivi iliyopita. Makala hii itafaa sana kusomwa na Mtanzania aliyeondoka nchini muda mrefu. Hata walioko Tanzania nao itawafaa. Nimeipandisha bila kuipitia kutazama kama kuna mambo yamepitwa na wakati. Wakati huo huo ninaendelea kutafuta sehemu ya pili ya ile ya Urasta. Nenda kwenye kona ya makala zangu kisha bonyeza kwenye makala hii mpya iitwayo: MAMBO YAMEPARAGANYIKA.
Fri 26 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Napenda kutangaza kuwa ulimwengu wa blogu una rafiki mwingine toka Kenya. Naye kama ilivyo JIKOMBOE anasema titi la mama litamu. Anaandika kwa Kiswahili. Anasema kuwa alipata mshawasha wa kuwa na blogu baada ya kutembelea JIKOMBOE. Haya ni maneno toka katika blogu yake:
“Juzi katika pilka pilka zangu za kuchakura mtandao nilikutana na ” blogu ” moja ya kaka kutoka tanzania , amabayo kwa kifupi ilinifurahisha sana kiasi cha kwamba nikaamua kuanzisha yangu piaSasa najua wapiga domo watasema kuwa nimeaanza kuiiga lakini kwa sasa nitawaacha waseme kwani wanamuziki wengi tayari washatuambia kuhusu wenzetu ambao huongea sana jioni tu - watalala .”
Blogu yake inaitwa : MAWAZO NA MAWAIDHA. Mtembelee hapa.
Fri 26 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Ukitaka unaweza kushiriki katika mradi wa chuo kikuu cha Yale wa kuandika kamusi ya Kiswahili. Mradi huu unahusisha watu toka pande nne za dunia (dunia ni kweli ina pande nne??). Mtu yeyote anaweza kuweka neno, kuhariri, kusahihisha, n,k. Ni kamusi ambayo inaandikwa na kila mtu. Kamusi yenyewe iko hapa.
Fri 26 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Mahakama Kuu nchini Kenya imeamua kuwa “Baba” Moi na wenzie (akiwemo mwanaye Philip) lazima watoe ushahidi katika uchunguzi wa kashfa ya Goldenberg. Hukumu hii inafuatia kesi iliyofunguliwa na wanaharakati waliodai kuwa uchunguzi huo lazima usikilize ushahidi toka kwa watu hawa. Mambo kama haya yanapotokea Afrika yananifanya niwe na furaha mwezi mzima. Hii tabia ya kuona kuwa mtu akiwa ameshika cheo cha juu serikalini hatakiwi kuhojiwa, kufikishwa mahakamani au mbele ya tume za uchunguzi inachochea rushwa, wizi, uzembe, na ulaghai. Ni tabia mbovu kabisa isiyohitajika barani kwetu. Tanzania nako lazima tubadili sheria inayozuia, kwa mfano, Rais kufikishwa mahakamani. Ukimpeleka Rais mahakamani unaambiwa, “Huwezi kumshtaki Rais wakati akiwa madarakani.” Ukisubiri hadi atoke madarakani kisha ukampeleka mahakamani utaambia, “Sheria inasema kuwa huwezi kumshtaki Rais kwa makosa aliyofanya wakati akiwa madarakani.” Jamani!
Mtu mwenye wadhifa kama Rais akiwa haogopi nguvu ya sheria (na jela), ni vipi tutanajenga uaminifu na uwajibikaji? Hakuna haki ya raia yeyote Afrika anayepaswa kuwa juu ya sheria (sio Rais wala Rais mstaafu). Soma habari hiyo hapa.
Fri 26 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Nimeweka ukurasa wa wanablogu wapya. Nimeanza na somo la kwanza. Baadhi ya wanablogu na wale wanaotaka kuanza wamekuwa wakiniuliza maswali mbalimbali. Ukurasa wenyewe uko chini ya makala na hadithi za Freddy Macha. Bonyeza palipoandikwa: Somo La Kwanza. Wenye maswali zaidi wanaweza kuniandikia. Naweza nisijibu haraka. Usiwe na wasiwasi, nitakujibu.
Kuna habari njema za wanablogu wa kiswahili wa Tanzania. Yule mwanadada wa Kenya, Ory Okolloh, anayesoma sheria katika chuo kikuu cha Harvard ameziweka blogu mbili mpya za Watanzania, Kona yangu na Furahia Maisha, ndani ya blogu yake ambaye inapendwa na kusomwa na watu wengi.
Mimi nami nimeongeza blogu nilizokuwa nimeweka hapa. Kona niliyoiita: Blogu za Wana Afrika Mashariki nimeibadili na kuiita Blogu za Waafrika. Nimeongeza blogu kadhaa na nitaendelea kuweka nyingine.
Thu 25 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Kabla sijaelekea kwenye mazishi ya bata, napenda kuwauliza kama mnafuatilia mwamko wa umma huko Ukraine. Saa moja na dakika nane zilizopita, Mahakama Kuu nchini humo imemzuia anayedaiwa kuiba kura (kama wanavyofanya watawala wa Tanzania) kuchukua madaraka. Soma habari hiyo hapa. Halafu, makala yangu ya wiki hii katika safu la Gumzo ya Wiki, nchini Tanzania inazungumzia juu ya haki na uwezo wa wananchi kuleta mapinduzi. Nitaiweka makala hiyo iitwayo: MIMI NA WEWE TUNA NGUVU KUSHINDA DOLA mara baada ya kutolewa nchini Tanzania. Yanayotokea huko Ukraine ( na yaliyowahi kutokea Jojia, Ufilipino, Indonesia, n.k. ni moja ya vielelezo vya nguvu walizonazo walalanjaa). Ngoja nielekee kwenye bata maana tumbo limeanza kunguruma kwa ubao.
Thu 25 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Leo Marekani nzima ni siku ya kula bata! Ni sikukuu ya thanksgiving hapa Marekani. Maduka kwa siku kadhaa zilizopita yalikuwa yakiuza bata kwa wingi kwa ajili ya siku ya leo. Sikukuu hii ya kula bata, mahindi, na keki ya maboga iitwayo thanksgiving ilianza kusherehekewa rasmi mwaka 1789. Lakini inaaminika kuwa thanksgiving ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1621. Sikukuu hii kama zilivyo sikukuu nyingine kama krisimasi na pasaka, imejengwa juu ya historia ya uongo. Inadaiwa kuwa siku hii ni siku ambayo wavamizi wa nchi hii ya Marekani (kumbuka hii nchi ni ya “Watu wa Kwanza” kama makabila ya wahindi wa asili wanavyopenda kujiita) walikaa kwa upendo na amani wakala chakula na watu wa asili wa nchi hii. Watu wengi wameanza kufundisha watoto wao ukweli wa sikukuu hii na ukweli wa historia ya mauaji ya halaiki, mikataba ya ulaghai, na wizi uliofanywa na wahamiaji waliokuja toka Uingereza. Rafiki yangu, Malaika, ambaye amenipigia simu dakika chache zilizopita kunikaribisha nikale bata anasema kuwa leo asubuhi alikuwa akimfundisha mwanaye juu ya ukweli wa sikukuu hii.
Kwahiyo kama kuna kiyama ya bata basi ni Novemba 25. Malaika anasema alianza kupika toka jana. Siku hii watu hula siku nzima huku wakitembeleana, kujumuika kifamilia, na wengine (hasa wanaume) kutazama mpira wa “miguu” wa Marekani. Huu mchezo wanauita mpira wa miguu (american football) wakati ambapo asilimia 99.99 ya mchezo huu wanatumia mikono! Nashindwa kuwaelewa. Basi Malaika anasema jikoni kwake kumeshehena chakula: bata, viazi vitamu, keki, mboga za majani, soseji, n.k. Anasema kuwa hofu yake ni kuwa mimi sili nyama na eti nisipokula bata leo sijasherehekea thanksgiving. Jamani, nile bata nisile?
Nimemtaja rafiki yangu Mailaika nikakumbuka makala niliyowahi kuandika juu yake iliyokuwa inauliza kama WamarekaniWeusi ni Waafrika. Nitaitafuta na kuipandisha ndani ya blogu. Haya ngoja nielelekee kwa Malaika ingawa sijaamua kama nitashiriki katika ulaji wa bata wa kitaifa au la.
Wed 24 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Nawashukuru sana wote wanaoniandikia. Ingawa nina muda kidogo, ninajaribu kuwajibu wote mimi mwenyewe. Situmii mashine kama wengine wanavyodhani. Pamoja na shukrani zangu, nina ombi moja. Sipendi kabisa…narudia, SIPENDI KABISA Watanzania wenzangu wanaponiandikia barua pepe kwa kutumia lugha za watu wengine/wakoloni. Hivi mbona wao hawatumii zetu wanapowasiliana wao kwa wao? Ninaposema “wao” mnajua ninawazungumzia akina nani. Kwa ufupi, mimi lugha ninayoifahamu kwa ufasaha zaidi na kuipenda ni Kiswahili na Kichagga. Hata ndoto huwa napata kwa lugha hizi. Blogu hii iko kwa ajili ya kuendeleza titi la mama yetu: Kiswahili. Iwapo Kiswahili chako ni cha kubabaisha kidogo (kama rafiki zangu wa nchi za jirani ambao huniandikia kwa kiswahili cha hapa na pale na kiingereza…wao nitawasamehe kwa sasa) unaweza kuniandikia kwa hicho kiingereza au lugha yoyote ya kuazima kwa mabeberu ila tafadhali fanya hima, jifunze Kiswahili ili siku za usoni tuwasiliane kwa Kiswahili. Hii ni blogu ya Kiswahili. Mimi nazungumza Kiswahili. Kiingereza nakifahamu kiasi ila sihitaji kukitumia kuwasiliana na watu wangu. Sidhani kuwa kuna ubaya kuzungumza kiingereza. Kwa mfano, ninatumia lugha hii katika shughuli zangu nyingine za kitaaluma. Ninahariri jarida la kiingereza liitwalo Perpectives on Global Development and Technology. Nina blogu ya kiingereza ya masuala ya teknolojia. Sina ugomvi na kiingereza au kifaransa. Mimi mwenyewe ninajilaumu kwanini nilipokuwa shuleni sikusoma kifaransa kwa makini. Pia nina mpango wa kujifunza kiarabu hivi karibuni. Kwahiyo isionekane kuwa mimi ni mtamaduni mwenye siasa kali. Najua tunaishi kwenye dunia ya maingiliano. Watanzania hatutaki kuwa kisiwa. Ila inapokuja katika mawasiliano kati yangu na wewe Mtanzania mwenzangu, hatuhitaji lugha ya kigeni. Nasema haya kwa nia njema ya kujenga na kutunza utu wetu.
Jambo jingine ni kuhusu blogu nyingine mbili za Kiswahili. Ile blogu ya Kona Yangu imeiva kwa habari kuhusu “wawakilishi” wetu (wabunge). Tafadhali ipitie upate undani wa hawa mabwana tunaowapa kura zetu nao wanazifanya kuwa “kula.” Mwandishi wa Kona Yangu, Simon Mkina, alikuwa Dodoma wakati wa kikao cha bunge. Bonyeza hapa kwenda Kona Yangu. Mwandishi wa blogu ya pili, Furahia Maisha Yako, Dennis Mponji, kaniambia kuwa alikuwa na mihangaiko ndio maana amekuwa kimya ila hivi sasa yuko mbioni kuweka mambo mapya. Blogu yake iko hapa.
Wed 24 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Mwanahistoria, mwalimu wa chuo kikuu cha Dar Es Salaama, mzawa mwenzetu, anayesoma pale kwa Kaburu matata iya, Afrika Kusini, Rehema Nchimbi, kaniandika maneno haya ya kutufikirisha. Hivi ndivyo safari ya kujikomboa inavyoanza. Inaanza kwa kubonyeza hapa.
Mon 22 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Makala mpya niliyoahidi kuhusu Joji Dabliyuu Kichaka tayari nimeipandisha bloguni. Nenda kwenye kona ya makala zangu. Inaitwa JOJI KICHAKA NA YESU MNAZARETI. Hii makala iliandikwa kwa ajili ya safu yangu katika gazeti la Mwannanchi, nchini Tanzania.
Sun 21 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Watanzania tutajiheshimu lini?
Ufuatao ni waraka wa Mtanzania anayeishi Helsink, Ufini, Fidelis Tungaraza, kufuatia habari za kuuawa kwa Mtanzania mwenzetu, dada yetu, mwanetu, jirani yetu, binadamu mwenzetu, mlalanjaa mwenzetu, shangazi yetu, binamu yetu….
Mtanzania huyu aliuawa kinyama na askari wawili wenye ngozi isiyo na kemikali muhimu sana ya Melanin. Nawaambia askari hawa, “Mbwa mwizi wa machinjioni!” Soma kwa makini utaelewa kwanini blogu hii nimeiita: Jikomboe. Safari yetu ya kujijua na kuthamini utu wetu ni ndefu ila najua kwa nia moja tutafika. Waraka wenyewe huu hapa chini:
Ndugu mhariri wa gazeti, ndugu viongozi wa serikali, na Watanzania wenzangu wengine, Ninatuma ujumbe huu kwa kustushwa, kusikitishwa, na kukasirishwa kutokana habari ya kuuawa kwa mwanamama wa Kitanzania na askari wahuni wa Kiingereza. Nimestushwa, kusikitishwa, na kukasirishwa kwa unyama na mauaji ya Mtanzania mwenzetu. Pia nimestushwa, kusikitishwa, na kukasirishwa na jinsi gazeti hili ambalo linasomwa na wasomaji wa Kiswahili ulimwenguni kote kupitia kwenye tovuti yao kwa jinsi lilivyoandika juu ya mauaji haya ya kinyama ya Mtanzania mwenzetu, hususani kichwa cha habari cha mauaji haya ya kinyama kama kilivyo hapo chini:
Askari Waingereza wadaiwa kuua changudoa D’Salaam
Ndugu Mhariri wa gazeti na viongozi wa serikali niawaombeni mlichukulie suala hili kwa uzito wa kina kwa upande wa kesi ya mauaji, na pia kwa jinsi gazeti hili lilivyochapisha habari hizi kwa kumuita ‘changudoa’ Mtanzania mwenzetu aliyetendewa ufuska na kuuawa kinyama. Kwa wale wote ambao wamewahi au bado wanaishi nchi za watu weupe tunajua jinsi suala kama hili ambavyo lingekuwa limewekwa katika vyombo vyao vya habari kama ingelikuwa wao ndiyo wametendewa kitendo kama hicho. Suala hili lingelitokea Ulaya, Amerika, Asia, au Uarabuni pengine lingeandikwa ‘Askari wanaharamu, wahuni wa Kiingereza wasemekana kuua raia wetu mwanadada mwananchi maskini mnyonge mpole’ Kuonyesha tu jinsi wanavyojithamini na kuthaminiana. Ndugu zangu wote tunaohusika na suala hili kwa njia moja au nyingine nawaombeni tulifuatilie suala hili.
Tanzania Nakupenda kwa Wote,
Fidelis Tungaraza, Helsinki, Finland.
Kisa chenyewe hiki hapa toka gazeti la Majira:
Askari Waingereza wadaiwakuua changudoa D’Salaam
*Walitoka Iraki vitani kuja kupumzika
*Yadaiwa walifanya mapenzi ufukweni
Na Kulwa Mzee
WANAJESHI wawili wa Uingereza wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka ya mauaji. Wanajeshi hao, Nigel David (23) na Brett Richard (20), walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Bi. Pellagia Khaday. Akisoma mashitaka hayo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Patrick Byatao, alidai kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 10 mwaka huu katika ufukwe wa hoteli ya Silver Sands. Inadaiwa Waingereza hao walimuua Bi. Conjesta Ulikaye. Hata hivyo hawakutakiwa kujibu mashitaka hayo kwa sababu Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi ya mauaji. Habari zilizopatikana mahakamani hapo zinadai kuwa wanajeshi hao walitoka vitani Iraki na walifika nchini kwa ajili ya mapumziko. Inadaiwa wakiwa kwenye ufukwe huo, mmoja wa washitakiwa alifanya mapenzi na changudoa huyo na kumlipa dola 70 (70,000/-) na kumshawishi ili afanye mapenzi pia na mwenzake kwa ahadi ya kumwongezea kitita. Alikubali, lakini haikufahamika walielewana kitu gani na baadaye walionekana washitakiwa wote wawili wanashirikiana kimapenzi na mwanamke huyo. Inadaiwa marehemu alifika katika eneo la tukio kwa ajili ya biashara ya kujiuza akiongozana na mwenzake ambaye alipata Mzungu mwingine. Washitakiwa walirudishwa rumande, upelelezi haujakamilika na kesi itatajwa Novemba 29 mwaka huu.
Sat 20 Nov 2004
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Jana niliizungumzia blogu ya Kona yangu kuwa ilikuwa ni ya kwanza kutupa vipande toka Bungeni Dodoma. Ila nikasema jamaa (Simon Mkina) kawa kimya. Sasa amerudi. Bonyeza hapa usome.
— Next Page »