JIBINI = CHEESE
January 2005
Sun 30 Jan 2005
Sun 30 Jan 2005
Binadamu tuna tabia za aina mbalimbali kuhusiana na vyakula. Kuna watu wasiokula nyama kutokana na sababu mbalimbali kama za dini au afya. Hawali chochote kinachotembea ardhini, ruka juu ya nchi, kuogelea baharini (samaki). Hawa wanaitwa ni wala majani, mbegu, na matunda, kwa kiingereza “vegetarians.” Kuna wengine wasiokula sio tu nyama bali chochote kile kinachotokana na wanyama. Hawa kwa kiingereza (bado natafuta jina la kiswahili) wanaitwa vegans. Tofauti ya “vegetarians” na “vegans” ni kuwa “vegetarians” huwa wanakula mayai, jibini, kunywa maziwa, n.k. Wakati “vegans” hawagusi hivyo vitu na wengine wala hawavai nguo, mikanda, viatu, au kubeba mikoba iliyotengenezwa kutokana na ngozi za wanyama. Nenda hapa na hapa kupata undani wa “veganism.”
Halafu kuna wengine ambao ndio funga kazi. Hawa ni wala vyakula vibichi. Kwa kimombo wanaitwa “raw foodist.” Hawa hawapiki chakula hata siku moja. Kwa maana hiyo hawahitaji kuwa na jiko majumbani mwao! Inaaminika kuwa hakuna njia inayoharibu virutubisho vilivyomo ndani ya chakula kama kupika. Watu wengi hawafahamu kuwa binadamu walitembea juu ya dunia hii kwa miaka mingi sana kabla moto haujagunduliwa. Kwahiyo wanachofanya ma-raw foodist sio jambo geni. Wanadamu walikuwa wakila vyakula vibichi kwa miaka mingi sana. Na wako wanaoendelea hadi leo. Wasome hapa.
Kuna kundi pia la wanaoishi kwa kula matunda tu. Wala matunda wanaitwa “fructarians.” Wasome hapa.
Kuna watu wengine wanaitwa “freegans” ambao wao chakula wanachokula ni kile ambacho kimeachwa, kusazwa, au kutupwa na watu wengine. Wasome hapa.
Kuna watu wengine ambao wanachukulia vegans na makundi mengine kuwa kama makundi madogo ndani ya mfumo mzima wa vegetarianism (ulaji wa mboga, mbegu, na matunda). Uchambuzi wangu wa makundi haya naweza kusema kuwa ni wa rahisi na juujuu kuliko ilivyo hasa. Tembelea hapa usome zaidi juu ya “vegetarianism” na mahusiano ya mfumo huu wa maisha na dini mbalimbali.
Sun 30 Jan 2005
Kuanzia sasa nitakuwa ninatumia teknolojia ya blogu ya sauti (audioblog) pamoja na hii ya maandishi. Kwahiyo hata nikiwa safarini, porini, milimani, vijijini, chooni, n.k. naweza kutumia simu ya mkono kuwasiliana nanyi ndugu zangu.
Sun 30 Jan 2005
Sun 30 Jan 2005
Sat 29 Jan 2005
Hatimaye yule mwandishi wa BBC, Ivan Noble, ameweka nukta ya mwisho katika kitabu chake cha kumbukumbu kilichokuwa mtandaoni kikionyesha maisha yake baada ya kupatikana na kansa ya ubongo. Ameweka nukta ya mwisho baada ya hali yake kuzidi kuwa mbaya. Msome.
Kitabu chake cha kumbukumbu kilikuwa kikisomwa na watu 100,000 kwa siku.
Sat 29 Jan 2005
Jana nilipandisha makala moja mpya: Elimu ni Utumwa? Leo nimeweka nyingine tatu ambazo niliziandika nyuma kidogo. Zote hizi tatu zilitoka kwenye safu yangu ya Gumzo la Wiki. Makala ya wiki hii nitaiweka baada ya kutolewa gazetini. Makala za leo ni: 1. WEWE MWENYE RASTA NJOO! 2. NANI ATAWAKAMATA POLISI? 3. YESU/ISA NA WATANZANIA
Sat 29 Jan 2005
Sankofa, habari za masiku? Nitajibu waraka wako ambao umeniandikia muda kidogo. Nimesoma habari ya DJ Spooky nikakukumbuka. DJ Spooky (Paul Miller): anafanya jambo ambalo limenipendeza sana. Ameuganisha u-DJ na utengeneza filamu. Kama jinsi ma-DJ wanavyochanganya muziki (nyimbo, vyombo, vibwagizo, n.k.) ndivyo DJ Spooky anafanya. Ameitengeneza upya ile sinema ya Birth of a Nation, matokeo yake imepatikana filamu ya Rebirth of a Nation.
Pia utaona kazi kwenye tovuti yake mradi wa A Different Utopia ambao ni mchanganyiko wa muziki, insha, teknolojia ya flash katika kuelezea falsafa ya Fela Kuti kupitia makazi yake ambayo aliyaita Jamhuri ya Kalakuta.
Sat 29 Jan 2005
Ninatamani mambo mengi. Mojawapo ni hili: Ninatamani sana siku moja nikutane ana kwa ana na wananchi wanaoitwa, “wananchi wenye hasira kali.” Hawa ni wale ambao wakisikia, “mwizi!” damu inawachemka, wanatafuta mawe, mitaimbo, nyundo, matairi, bisibisi, patasi, petroli, na viberiti ili wamuue mtu ANAYEDAIWA kuwa mwizi.
Ukikuta hawa wananchi wenye hasira kali wanaua binadamu mwenzao, mtafute aliyewasha kiberiti, kisha muulize, “Hivi jamaa kaiba nini?” au, “Kamwibia nani?” Utasikia majibu ya ajabu kweli.
“Ah, jamaa wanasema kaiba mtaa wa pili.” Atakujibu. Anayekujibu hivyo ndiye aliyewasha moto uliomteketeza marehemu. Ukimuuliza akutajie majina ya hao ” jamaa wanaosema” kuwa kaiba mtaa wa pili, atakachoweza ni kuwataja kwa jina la “jamaa.” Atasema, “Jamaa waliomkamata ndio walimuona.”
Jamaa ndio akina nani hao?
Hajui.
Msimamishe yule aliyemwangushia tofali kichwani lililomfanya marehemu atoe damu puani na machoni. Muulize swali, “Kafanya nini marehemu?”
Atakujibu, “Wamezidi hawa!”
Nimesema kuwa ninatamani sana kukutana na “wananchi wenye hasira kali.” Nataka kuwauliza swali hili: Wezi wa kuku mnawapeleka jela. Wezi wa shilingi 1,000 mnawapiga mawe na kuwachoma moto hadi kufa, JE WEZI WA MAMILIONI YA UMMA MNAWAFANYA NINI?
Hizo “hasira kali” zinakuwa wapi wakati nchi ikipigwa mnada??
Natamani sana sana kukutana nao. Ukikutana nao naomba nisaidie kuwauliza swali hilo kisha nitumie majibu.Yesu akauambia umati, “Asiye na dhambi awe wa kwanza kurusha jiwe.” Mara wakaondoka mmoja mmoja na kumwacha na yule mwanamke aliyeshatakiwa kwa uzinzi.
Fri 28 Jan 2005
Nimeweka makala mpya toka kwenye safu yangu ya Gumzo la Wiki katika gazeti la Mwananchi. Makala inaitwa Elimu ni Utumwa? Kama kawaida iko kwenye kona ya makala zangu, upande wa kuume, chini ya picha yangu. Kichwa cha makala hii kilikuwa ni hiki: Elimu ni Ufunguo wa Utegemezi. Nimekibadili kuwa swali: Elimu ni Utumwa? Makala hii ilipaswa kusomwa kama sehemu ya pili ya makala nyingine kuhusu usomi na wasomi. Nimeamua kupeleka mambo kinyume. Nimeanza kukupeni sehemu ya pili kisha niwapeni sehemu ya kwanza!
Fri 28 Jan 2005
Kuna mafunzo ya aina mbalimbali kwa njia ya video kwa wale wanaopenda masuala ya teknolojia. Kongoli hapa.
Fri 28 Jan 2005
Terms of reference = Hadidu za rejea
Vinegar = Siki
Furniture = Samani
Kumbuka kuwa Ice ni barafu na snow ni theluji.
Fri 28 Jan 2005
Kumbe hivi karibuni Watanzania tulioko ughaibuni tutaweza kwenda Kigoma na kurudi ughaibuni siku hiyo hiyo. Itakuwa hivyo kama yaliyosemwa kwenye habari hii sio si-hasa bali ukweli.
Fri 28 Jan 2005
Kuta zile zinazojengwa na wa-twawala (yaani watawala au “viongozi”) kuzuia uhuru wa fikra na maoni zinapoanguka lazima tushangilie. Kama ilivyotokea hapa.
Thu 27 Jan 2005
Ndio kunakucha katika ulimwengu wa blogu za Kiswahili. Kuna mwanablogu mpya wa Kiswahili. Huyu ni Innocent Kessy, Mtanzania aliyeko masomoni nchini Uganda. Mtembelee katika blogu yake ya Dira Yangu hapa.
Wed 26 Jan 2005
Kuna mwandishi mmoja wa gazeti la The Christian Science Monitor ambaye ana bloguluninga. Yuko Afrika. Sijaitazama vizuri. Itembelee. Bloguluninga inakuja juu sana hivi sasa. Nimepata habazi zake toka kwa Ethan.
Wed 26 Jan 2005
Kutokana na maombi ya wengi kuhusu makala za uchambuzi na falsafa za Padri Karugendo, ambazo hutoka kila alhamisi katika gazeti la RAI (nguvu ya hoja) nchini Tanzania, ninaweka kona maalum kwa ajili ya makala zake. Hivyo mtaanza kumsoma hivi karibuni.
Ninapenda kutangaza kuwa mwezi ujao, ambao ni mwezi wa historia ya watu weusi hapa Marekani, kutakuwa na mfululizo wa mambo mbalimbali ya kukomboa fikra zetu katika kuenzi historia yetu. Afadhali ukose kuja hapa mwaka mzima ila sio mwezi wa pili!
Tue 25 Jan 2005
Kuna mshairi mwingine ambaye staili yake ninaipenda sana. Napenda wasiomfahamu, wamfahamu. Huyu ni Saul Williams. Ukifika kwenye tovuti yake unaweza kusikiliza baadhi ya mashairi yake. Unaweza pia kusikiliza na hata kuchota CD yake ya hivi karibuni. Pia unaweza kutazama baadhi ya video zake. Nenda hadi mwisho wa ukurasa wa kwanza na ubonyeze panaposema: The Work. Unaweza ukawa umetazama filamu ya Slam ambayo aliicheza.
Tue 25 Jan 2005
Nenda kwenye blogu ya Furahia Maisha Yako. Kuna habari ya Sumaye kushangaa mijinaume inayopenda ngono kiasi ambacho inatoa machozi kabisa, na hata kutumia maelfu kwa ajili ya vitanda katika hoteli za kifahari lakini shilingi 100 ya kondomu hawatoi!
Ukifika hapo usiache kusoma sheria za kuvaa suti. Nimecheka kwa sauti, nadhani majirani wamepata mshtuko. Mwanablogu huyu alinichekesha wakati ule alipoandika sifa za uswahili.
Tue 25 Jan 2005
Sikuwa najua kuwa kuna watu wamekuwa wanablogu safari yao ya kupanda mlima ambao hauko mbali na nilipozaliwa. Blogu ya hao mabwana ni hii na habari yenyewe nimeikuta sebuleni kwa Mawazo na Mawaidha.




