June 2005
Monthly Archive
Thu 30 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Jana kutokana na harakaharaka nilikosea nikaweka kwenye blogu hii mambo niliyoandika kwa ajili ya blogu ya kiingereza. Kwa ajili ya rekodi nitaacha kama ilivyo. Tumewasili Uskochi kama saa moja lililopita. Baada ya kuingia mtandaoni ndio nimegundua kosa nililofanya. Lakini hakuna lililoharibika. Kinachofuata ni kutazama ratiba na ramani ya mji ili kupanga jinsi ya kufuatilia matukio yanayotokea hapa Uskochi kabla ya mkutano wa wezi wakuu duniani.
We are living for Edinburgh early tomorrow morning. We are all excited. The first thing I want to do when I get there is to look for anarchists! So when you see anarchists, look carefully you will see me blogging!
Thu 30 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Kesho asubuhi na mapema tunaondoka kwa treni kuelekea Edinburgh, Uskochi. Kule ndiko kuna kivumbi cha wezi wa mataifa nane na wanaharakati wanaopinga mpango wa nchi za kibepari kufanya dunia nzima kama mali yao binafsi kwa kutumia viini macho kama vile Tume ya Afrika inayoongozwa na mzungu!
Thu 30 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Ukienda hapa katika tovuti ya kundi la mataifa yanayoongoza kwa wizi duniani, G8, utakuta viungo kwa ajili ya filamu za propaganda za kuonyesha kuwa “misaada” toka kwa Waingereza inasaidia sana bara la Afrika. Sijui ni lini wataonyesha filamu kuhusu jinsi silaha toka Uingereza “zinavyoisaidia” Afrika.
Thu 30 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Leo tumekutana na Paul Mason wa kipindi cha BBC kiitwacho Newsnight.
Kazungumzia mkutano wetu naye kwenye blogu yake. Pia tumekutana na mwanablogu wa gazeti la The Observer, Rafael Behr. Kwa ujumla leo ilikuwa siku nzuri sana na isitoshe tumeshinda ofisini siku nzima, hakukuwa na harakaharaka za kukimbilia kwenye matreni na mabasi, jambo ambalo tumekuwa tukifanya toka niwasili hapa jumatatu. Baada ya dakika 20 hivi jamaa wa kipindi cha Go Digital cha redio ya BBC atawasili hapa ofisini kufanya mahojiano nami juu ya masuala ya kublogu Afrika na mengine kuhusu teknolojia mpya ya habari na mawasiliano. Muda mfupi uliopita nimetuma makala yangu ya kila wiki katika gazeti la Mwananchi. Makala hiyo, siwezi kuipandisha sasa kutokana na muda kuwa mdogo, nimeipa kichwa hiki: Afrika Itaendelezwa na Waafrika na Kudumazwa na Wazungu.
Wed 29 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Hivi sasa ni saa nne kasoro usiku. Nimechoka kutokana na mizunguko ya leo. Tulikwenda kwenye ofisi za BBC Online na baadaye tukafanya mahojiano mazuri mno na mama Claire Short aliyejiuzulu toka serikali ya Blair kutokana na uvamizi dhidi ya Iraki. Kutokana na uchovu, na kutakiwa kuamka mapema mno kesho, sitaweza kuandika aliyosema mama huyu. Kaongea kweli. Kwa kifupi, kasema Tume ya Afrika na ripoti yake ni upuuzi mtupu! Kesho.
Wed 29 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Jana, mimi na John Kamau wa Sunday Standard (Kenya) tulifanya mahojiano na Cliff Stone, mkurugenzi wa City Water aliyetimuliwa nchini. Mahojiano hayo yalipangwa na taasisi ya Panos London. Dhumuni kuu lilikuwa ni kupata taarifa toka kinywani mwake kuhusu mgogoro wa kampuni aliyokuwa akiiongoza na serikali ya Tanzania. Hatukumaliza mahojiano yenyewe, tutaendelea. Siku haijapangwa.
Katika mambo yote tuliyofanya jana, kubwa ni pale tulipokwenda ukumbi wa New Theatre wa London School of Economics kwenye mhadhara ulioitwa Make the G8 History. Nlifurahi sana kumsikiliza na kukutana na Tariq Ali, mwandishi wa habari, mtunzi, na mhariri wa jarida la New Left Review. Tariq ni mwandishi wa kitabu kiitwacho The Clash of Fundamentalisms. Wengine waliozungumza kwenye mhadhara huo ni mwandishi George Monbiot, na Mark Curtis.
Tariq Ali alizungumzia mada iliyoitwa Power and Resistance. Haya ni baadhi ya mambo aliyosema:
- Afrika haitakaa iondoke kwenye dimbwi la umasikini kwa kutumia misaada toka nchi za Magharibi
- Wanasiasa wa mrengo wa kulia na kushoto wana tofauti ndogo sana. Ukiwachambua kwa undani unakuta lao moja
- Marekani ni kati ya nchi zinazoongoza kwa rushwa duniani!
- Ili kuondokana na uchumi tegemezi Afrika iache kukimbilia nchi za Magharibi na ianze kushirikiana na nchi za Amerika ya Kusini
- Waafrika waache kutegemea tabaka la wasomi na matajiri wa Afrika na wanasiasa wa Magharibi
Mark Curtis alisema yafuatayo:
- Nia ya Uingereza katika mpango wake wa Afrika sio kuondoa umasikini bali kutengeneza njia kwa ajili ya makampuni ya Magharibi kuwekeza na kuiba utajiri wa Afrika
- Anashangaa sana waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair, anaonekana kama vile ni mwokozi wa Afrika
- Ni ajabu kuwa Uingereza inajifanya ghafla kuwa inaipenda Afrika wakati ilikaa kimya wakati wa mauaji ya Rwanda, iliunga mkono ubaguzi wa rangi Afrika Kusini kwa miaka 50, ilimuunga mkono dikteta Idd Amin kwa mwaka mmoja na nusu, ina historia chafu sana kutokana na mateso ya Kinazi iliyowafanyia mashujaa wa kundi la Maumau nchini Kenya, na kitendo cha serikali ya Uingereza kukaa kimya wakati makampuni ya mafuta ya Uingereza yananyonya utajiri wa Nigeria na mabenki ya Uingereza yakificha fedha za watawala wala rushwa wan chi hiyo
George Monbiot alisema:
- Mwanamuziki Bob Geldof anashangaza baada ya kuwaambia wanamuziki wanaoshiriki kwenye tamasha la Live 8 kuwa wasimsakame mwizi namba moja duniani ambaye ni raisi wa Marekani, Joji Kichaka
- Wazungu nane (viongozi wa G8) wanajifanya kuwa wana uwezo wa kuondoa matatizo ya dunia nzima
Wed 29 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Jamaa mmoja kanitumia habari hii muda sio mrefu. Imenishangaza. Soma mwenyewe.
Tue 28 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Niko kwenye mgahawa wa Copacabana nje ya hoteli ninayokaa katika mtaa wa Southampton. Ninaandika haraka kidogo maana muda si mrefu tutaondoka na waandishi wengine, ambao wanakunywa chai sasa, kwenda ofisi za Panos.
Niliwasili jana asubuhi hapa kwa Malikia Lizabeti, au kama vijana wa kijiweni wanavyopaita, ‘kwa bibi.’ Nimekutana na waandishi wengine walioko kwenye mpango huu wa shirika la Panos wa G8 Media Fellowship: Kamau, Machrine, na Maura. Salamatu toka Sierra Leone anawasili leo.
Jana tulipelekwa kutambulishwa kwa wafanyakazi wa Panos na baada ya mlo wa mchana tulihudhuria kikao cha wafanyakazi wa shirika hili, ambapo kulikuwa na ripoti kuhusu ushiriki wa Panos katika mkutano wa dunia wa masuala ya jamii-habari (world summit on information society). Baadaye tulikwenda ofisi za bunge kuoana na mbunge wa jiji la York, Hugh Bayley, ambaye ni mwenyekiti wa Africa All Party Parliamentary Group. Alitueleza kwa kifupi juu ya kazi na mafanikio ya kundi hili. Nitatoa maelezo yake kadri siku zinavyokwenda.
Leo tutakuwa na mjadala kuhusu agenda ya kundi la nchi nane (G8) na pia kutazama yaliyomo katika vyombo vya habari vya Afrika na Uingereza kuhusu mkutano wa G8 utakaofanyika mwezi ujao, ambapo moja ya agenda kuu ni suala la maendeleo ya Afrika. Tutakwenda katika ofisi za gazeti la Metro, ambalo liko mbioni kuanzisha blogu. Kuna watu kadhaa ambao kuna uwezekano wa kukutana nao leo, au siku nyingine, kutegemea na ratiba itakavyokuwa: Aubrey Meyer wa Global Commons Institute, John Hilary wa kundi la Chatham House, na waziri wa masuala ya maendeleo ya kimataifa, Hilary Ben.
Mchana nitakwenda kufanya mahojiano na mmoja wa wakurugenzi walitimuliwa nchini Tanzania, Cliff Stone, wa kampuni ya City Water iliyokuwa imepewa jukumu la kusambaza maji jijini Dar Es Salaam. Tutakutana katika ofisi za kampuni mama ya City Water iitwayo BiWater.
Ila tukio kubwa nadhani ni kesho tutakapozindua blogu mpya inatakayoendeshwa na waandishi toka Afrika. Anuani yake siwezi kuianika hapa sasa hadi izinduliwe rasmi.
Mengine baadaye.
Tue 28 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Nimewasili hapa Landani (london) jana asubuhi. Wasomaji wangu walioko hapa wanaweza kuwasiliana nami kwenye namba hii: 0207 242-2828. Chumba changu ni nambari: 445.
Sun 26 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Kama nilivyoeleza hapo nyuma, ninakwenda kublogu, pamoja na mambo mengine, mkutano wa nchi zinazoitwa “tajiri” kuliko zote duniani kule Uskochi. Nikiweka kituo sentensi ya mwisho hapa ninabeba begi, huyooo…
Kwahiyo ukisikia tena toka kwangu nitakuwa niko kwa Malikia Lizabeti, itakuwa ni siku ya jumatatu. Kwahiyo fuatilia mkutano huo na mambo mengine kama maandamano ya kupinga wezi hao wa mataifa nane, n.k. katika blogu hii. Mpaka tutakapoonana kesho, uhuru daima!
Sun 26 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni [2]
Kila mara
Ninakaa chini
Nikuandikie shairi
Mahiri
Wangu wa moyoni
Jua la asubuhi
Usiku wa mbalamwezi.
Kila mara ninapokaa
Chini
Nikuandikie shairi
Wangu azizi
Najiuliza
Pasi jibu
Nianze wapi?
Usiku nilikuwaza
Nikatamani
Utamke neno
Nami nijibu.
- Vermont, USA 2005
Sun 26 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Siku ya ijumaa na jumamosi, tarehe kwanza na pili mwezi ujao, Redio ya BBC itatangaza mdahalo uitwao: Je nchi za G8 zinaweza kuinusuru Afrika? Watakaoshirika katika mdahalo huo utakaofanyika katika ukumbi wa Africa Centre, jijini London, ni: Tajudeen Abdul-Raheem, Mkurugenzi wa Justice Africa na katibu mkuu wa Pan African Movement, Rosemary Museminali,balozi wa Rwanda Uingereza, James Shikwati, mwanauchumi toka Kenya, na Lord David Triesman, waziri mtarajiwa wa masuala ya Afrika.
Matangazo ya mdahalo huo yatarushwa siku ya ijumaa tarehe kwanza saa 1900 GMT, 2100 GMT, na 2200 GMT; na siku ya jumamosi tarehe pili saa 1100 GMT.
Sat 25 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Onyesho la kuhamasisha juu ya umasikini barani Afrika, onyesho kubwa kuliko yote yaliyowahi kurushwa kwenye luninga na intaneti. Onyesho hili litapita hata idadi ya watu bilioni 3.9 waliotazama mashindao ya olimpiki kule Athens, Ugiriki.
Fri 24 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Waandishi tunaokwenda nchini Uingereza katika mpango wa shirika la Panos uitwao G8 Media Fellowship, tumefahamishwa kuwa asubuhi ya tarehe 5 mwezi ujao tutakutana na mwandishi na mtangazaji nimpendaye wa siasa za mrengo wa kushoto, George Monbiot. Monbiot huwa anaandika makala za kila wiki katika gazeti la the Guardian la Uingereza. Licha ya kuandika magazetini, Monbiot pia ni mtunzi wa vitabu kama vile The Age of Consent: A Manifesto for a New World Order, Captive State: The Corporate Takeover of Britain, Poisoned Arrows,
na No Man’s Land (alichokiandika kutokana na ukachero alioufanya Kenya na Tanzania). Monbiot, ambaye ameishi na kufanya kazi Indonesia, Brazil, na Afrika ya Mashariki, ni mwalimu wa muda katika chuo kikuu cha Oxford Brookes.
Tembelea tovuti yake kwa habari zaidi juu yake na makala na insha mbalimbali za upembuzi yakinifu.
Fri 24 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Sirikali ya Marekani inayoongozwa na mwizi wa kura, Joji Kichaka, inanichefua kupita kiasi. Wakati wakianza kushawishi dunia bila mafanikio kuhusu uvamizi dhidi ya Iraki, moja ya sababu kuu walizotoa ni kuwa nchi hiyo imekuwa ikizuia wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kukagua maeneo yanayoaminika kuwa yalikuwa yanatengeneza silaha za sumu. Watawala wa nchi hii wakauliza, “Kama Iraki haitengenezi silaha kwanini inakataza wakaguzi wa Umoja wa Mataifa? Kuna nini kinafichwa?”
Sasa kichekesho cha siasa za beberu huyu ni hiki: toka mwaka 2002 (leo ni 2005) Umoja wa Mataifa umekuwa ukiomba ruhusa toka sirikali ya Marekani ili wakaguzi wake waende wakatembelee wafungwa walioko ghuba ya Guatanamo. Hadi dakika hii Marekani haijakubali kuruhusu wakaguzi hao. Ni kitu gani kinafichwa?
Taarifa za mateso na unyama uliokithiri unaofanywa na Marekani dhidi ya wafungwa zinatisha. Majuzi tulisikia kuwa badala ya kutumia karatasi maalum za chooni, askari wa Marekani hapo Guantanamo walitumia Kurani. Hivi Marekani imeishiwa kiasi cha kushindwa kununua karatasi za chooni?
Kwanini wakaguzi wa Umoja wa Mataifa hawaruhusiwi? Ukweli ni kuwa wakaguzi hao wakiruhusiwa kuonana na wafungwa, habari za kuteswa kwao tukazisikia, dunia nzima itatambua kuwa sirikali ya Marekani haina tofauti yoyote na sirikali ya Taliban au ya huyo Saddam Hussein waliyemgeuka. Ukitaka kujua ukweli wa serikali hii tazama marafiki zake wakubwa: Saudi Arabia, Israeli, Equatorial Guinea, Pakistani, n.k. Usisahau pia kuwa sirikali za Taliban na Saddam Hussein zilikuwa ni maswahiba wa kufa na kuzikana na Marekani kwa miaka mingi. Ukitaka kumfahamu mtu kwa undani, tazama marafiki zake. Ndivyo hivyo hata kwa sirikali.
Thu 23 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Kama nimekosea naomba nisahihishwe. Katika tafutatafuta nimeona kuwa tafsiri ya Kiswahiliya neno, survey, ni muhtasari.
Tue 21 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Waandishi saba wa Afrika, nikiwemo kati yao, tutakwenda Uingereza, pamoja na mambo mengine, kuhudhuria mkutano wa G8 utakaofanyika tarehe 6-8 mwezi ujao kule Uskochi. Safari yetu itakuwa ya wiki mbili (wiki moja katika jiji la London na wiki nyingine Edinburgh. Tutakuwa katika mpango uitwao G8 Media Fellowship wa shirika lisilo la kiserikali la Panos London. Waandishi wengine watakaoshiriki wametoka Kenya, Uganda, Malawi, Sierra Leone, na Msumbiji. Moja ya madhumuni ya mpango huu ni kuwawezesha waandishi wa habari toka Afrika kuweza kuwa na ufahamu zaidi juu ya masuala ya sera na mikutano ya kimataifa. Pia itawawezesha kuandika habari kuhusu mkutano huo kupitia mtazamo wa Waafrika wenyewe.
Tembelea shirika la Panos kujua zaidi juu ya kazi zake.
*******************************************************************************
Maombi yangu ya visa ya kwenda Uingereza yamekubaliwa leo. Hivyo nitaondoka jumapili kwenda huko kwa Malikia Lizabeta. Nikiwa huko nitablogu hapa Jikomboe juu ya mkutano na matukio mengine yanayohusiana na mkutano wa nchi nane za kibepari. Pia shirika la Panos linatengeneza blogu maalum kwa ajili ya mkutano huo. Nikishapata anuani ya blogu hiyo nitaweka hapa.
Nikiwa ninablogu kwa Kiswahili kupitia Jikomboe,
Mshairi, mwanablogu toka Kenya anayeishi Uingereza amenieleza kuwa ana nia ya kutafsiri (nitakayokuwa naandika kwa Kiswahili) kwa kiingereza kwenye blogu yake. Namshukuru kwa uamuzi wake huo wa kujitolea.
Sun 19 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Mmoja wa wajumbe wa ile Tume ya Afrika ambayo mkuu na mwanzilishi wake ni Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, (sijui Blair alizaliwa kijiji gani Afrika hadi aanzishe tume ya Afrika), ni Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi. Kama tuna mtu kama Zenawi kwenye tume ya kujenga Afrika mpya, hiyo Afrika itakuwa na mito ya damu? Fuata viungo hivi usome unyama wa majeshi ya mjumbe huyu wa tume ya “kuiokoa” Afrika. Kongoli hapa, hapa, na hapa.
Sun 19 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Soma uchambuzi uliofanywa na katibu mkuu wa Pan Africa Movement, Dakta Tajudeen Abdul-Raheem kuhusu juhudi za kuondoa umasikini Afrika bila kushirikisha Waafrika wenyewe. Anachozungumzia ndio hasa mchezo wa kuigiza unaoendelea huku duniani ukipigiwa makofi na vigelegele na viongozi wetu na suti zao wanaozunguka Ulaya na Marekani kunadi nchi zetu.
Sun 19 Jun 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Wanahabari Wasio na Mipaka wametangaza blogu zilizopata tuzo ya kutetea uhusu wa kujieleza. Blogu iliyoshinda toka Afrika ni hii hapa toka Morocco. Na hii ndio orodha ya blogu zote zilizopata ushindi. Wanablogu walioshinda watahojiwa hivi karibuni kupitia ukurasa wa mradi wa Global Voices.
— Next Page »