July 2005
Monthly Archive
Sat 16 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Napumzika. Mwili na akili huwa vinahitaji kupumzika. Toka nirudi toka kwenye ule “mchezo wa kuigiza” wa wakuu wa makuhani wa ubepari (mkutano wa genge la wanaume nane, G8) sijaandika chochote hapa. Nimekuwa navuta pumzi,
natafakuri,
nanyoosha viungo,
na kutembea milimani.
Nadhani nitarudi rasmi kwenye blogu leo usiku au kesho. Au kesho kutwa. Nausikiliza mwili.
Ukisema neno, miye natii. Nawe usiwe unasahau kupumzisha mwili na akili.
Mon 11 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Ndio tumerudi mtaa wa Simba Mweupe, zilipo ofisi za Panos. Tayari tumemaliza mahojiano na kipindi cha BBC cha Go Digital.
Nilikuwa na John Kamau.
Pia tumefanya mahojiano mafupi kuhusu masuala ya Afrika na mkutano wa wakuu wa makuhani wa ubepari, yaani G8, na Mariam Omar wa idhaa ya Kiswahili ya BBC.
Na kesho alfajiri saa kumi na moja na nusu (au ni kumi na moja kamili?…nitahakikisha) nitazungumzia masuala ya uandishi, blogu, na G8 katika kipindi cha BBC Network Africa.
Kisha baada ya hapo nitaelekea uwanja wa ndege…chai sijui nitakunywa wapi. Mimi bila chai akili itaacha kufanya kazi! Kamau yeye ataongea na BBC Focus on Africa saa mbili asubuhi.
Mon 11 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Baadhi yetu wanaondoka leo. Wengine, nikiwemo mimi, tunaondoka kesho. Nadhani niko tayari kuondoka. Bado jiji lina huzuni huzuni hivi. Siwezi kuficha kuwa asubuhi tulipopanda basi kuja hapa nilikuwa na hofui kidogo.
Dakika 20 zijazo mimi na John tutaondoka kwenda Bush House kwa ajili ya mahojiano ya kipindi cha BBC kiitwacho Go Digital. Ninapitia msururu wa barua pepe zilizojaa kashani.
Sat 9 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Tumewasili London. Kumekaa kihuzuni huzuni hivi. Ugaidi ni kitu kingine kabisa. Tumechoka, tumekwisha kabisa. Akili hata kufikiria ni vigumu. Kuna waliouliza makala za Padri Karugendo. Hizo mpaka nirudi kwa Joji.
Uhuru!
Fri 8 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Ni saa tisa usiku. Nilikaa Gleneagles hadi saa sita usiku. Nilikuwa kati ya watu wa mwisho kuondoka maana nilijua nikija nyumbani nikiona kitanda nitalala, kama ambavyo nitafanya nikishamaliza kuandika hapa. Wakati naondoka kuelekea kwenye basi nilitazama kila upande bila kuamini kuwa sehemu iliyokuwa imejaa askari na watu wenye kamera, beji zinazoning’inia shingoni (kila mtu ilikuwa lazima awe na beji), makaratasi, kalamu, kompyuta za mapajani, wahudumu, n.k. ghafla imekuwa mahame. Askari walikuwa wameyeyuka. Wanaharakati wametoweka. Waandishi wamebaki wachache, nao ndio wanaondoka. Helikopta hazipo tena angani.
Natembea polepole na begi langu nikijiuliza, “hivi nilikuja kufanya nini hapa?”
Nilijiona kama mtu anayetoka ndani ya chumba cha maigizo akirudi kwenye dunia halisi. Kuna mwanafalsafa mmoja, sikumbuki ni nani, alisema kuwa dunia hivi sasa imekuwa kitu alichokiita, “media spectacle.” Yaani maisha ni kama vile kioja kwa ajili ya vyombo vya uongo (vyombo vya habari). Na hivyo ndivyo ilivyokuwa pale Gleneagles. Mchezo wa kuigiza unaofanyika kila mwaka kwa jina la G8 Summit. Mchezo huu utaendelea mwaka ujao kule Urusi.
Nimepitia vyombo kadhaa vya habari kuona maoni ya watu juu ya tamko la makuhani wakuu wa ubepari la kuongeza “msaada” kwa nchi za Afrika. Wako wanaounga mkono na wanaopinga. Watu kama akina Bono na Geldof wakiunga mkono nitawaelewa maana wanataka kutudanganya kuwa kampeni zao kama Live 8 ndio zimefanya wezi hawa wa maliasili za Afrika (wakishirikiana na Waafrika) wakaamua “kuisaidia” Afrika. Akina Bono wanataka kutuambia kuwa akina Kichaka wameguswa na kauli ya walimwengu! Hivi unadhani watu bilioni mbili wakisema jambo, na mabosi watatu wa kampuni la kipebari kama Halliburton wakisema jambo, Joji Kichaka atasikiliza kina nani? Watu bilioni mbili? Thubutu!
Nikiwa ndani ya basi kabla ya kusinzia nilijichekea mwenyewe: baada ya tamko la “kuisaidia” Afrika kwa dola bilioni 50 (sijui nyumba ngapi zitajengwa ufukweni mwa bahari, na akaunti ngapi zitafunguliwa ughaibuni, na suti ngapi na vito vya thamani vitanunuliwa na watawala wa Afrika kwa hela hii) kila mwandishi wa kizungu alikuwa akiona mtu mweusi anataka kumhoji. Nilitamani ningevaa bango kusema, “Sitaki kuhojiwa!” Niliona kuwa hata wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari ya Blair, waandishi weusi walipewa nafasi ya juu kidogo tofauti na ilivyo kawaida katika mikutano mikubwa kama hii. Ghfala ngozi nyeusi ilionekana kama vile sijui ni kitu gani. Nyani wamejua kuvaa nguo?
Nililala sehemu kubwa ya safari ya dakika tisini toka Gleneagles hadi Edinburgh. Kisha teksi hadi Royal Circus namba moja. Ndipo nipo sasa na ninakaribia kwenda kulala.
Kesho asubuhi tunarudi London, jiji nilichukialo kwa mbio zake za kuwahi basi, treni, msongomano wa watu, na habari hizi za ugaidi zimenifanya nisiwe na raha ya kurudi pale.
Pazia limefungwa. Mchezo umeisha. Washeni taa. Twendeni nyumbani.
Fri 8 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Wanaharakati wamekuwa wakitaka nchi za Ulaya na Marekani ziache kutoa ruzuku kwa wakulima wake. Je wakulima wenyewe wanasemaje? Niliongea na viongozi wa chama cha wakulima wa Uskoti.
Fri 8 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Wale wakuu wa makuhani wa nchi zinazoongoza kwa ukandamizaji wametoa tamko. Wako jamaa ambao wameipinga vikali. Wasome hapa, hapa, na hapa.
Fri 8 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Fri 8 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Ungewaambia nini? Kusema kweli sijui ningewaambia kitu gani. Ila Waafrika hawa niliohojiana nao wanafahama watakachowaambia. Nadhani mimi ningeweka vidonge kwenye chai ili walale kisha niwatie pingu!
Fri 8 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Sauti kupitia spika katika hema hili la waandishi wa habari inasema kuwa Bono na Geldoff watakuwa na mkutano na waandishi wa habari muda mfupi toka sasa. Sijui niende? Blair kamaliza mkutano wake. Sikwenda. Nilienda kula kisha nikaja kumalizia habari ninazoandika. Naona kama vile ni usumbufu kutembea hadi kwenye mahema ya mikutano ya waandishi wa habari kusikiliza wapiga hadithi wakati kuna luninga kila kona.
Fri 8 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Makala yangu kwenye gazeti la Metro la Uingereza inaelezea siku ya kwanza nilipotua mguu Gleneagles wanapokutana makuhani wakuu wa ubepari. Isome hapa.
Nina masikitiko makubwa maana kuna uwezekano kuwa marais wa Afrika hawataongea na waandishi wa habari. Wamekuja, wamekunywa mvinyo na makuhani wa ubepari na kupiga picha za pamoja, kisha kudanganyana kidogo halafu wanarudi Afrika. Nadhani watapitia kwanza kwenye mabenki kutazama akaunti zao, watacheki afya, “shopping” kidogo kisha warudi Afrika.
Fri 8 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Leo ndio siku ya mwisho ya mkutano wa makuhani wakuu wa ubepari. Ukitazama maandalizi, muda, na fedha zilizotumika kwenye mkutano huu huwezi kuamini kwanini wanakutana kwa siku chache hivyo. Muda si mrefu tutaondoka. Wote hapa tuna hamu ya kukutana na marais toka Afrika walioalikwa kwenye makombo. Meza kuu ina wanaume nane. Jana wala makombo walikuwa ni viongozi wa nchi za Brazili, India, n.k.
Thu 7 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Jamaa anayetuhumiwa kuteka watoto wawili alikuwa ana blogu. Blogu yake aliita “msumari wa tano” kutokana na hadithi kuwa msumari wa tano ulikuwa ndio umalize maisha ya Yesu, ila ulifichwa askari wa Kirumi wasiuone. Hii ndio blogu yake.
Thu 7 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Leo nimekuwa hapa Gleneagles toka asubuhi, usisahau kuwa chakula ni cha bure!! Nimekuwa nikizunguka huku na kule kutafuta Waafrika toka vyama visivyo vya kiserikali na pia waandishi wa habari toka Afrika. Nimemuona mwandishi mmoja toka Tanzania, Ayoub Mzee, ambaye anafanya kazi Sky Channel hapa Uingereza.
Kuna wanaharakati wachache sana toka vyama visivyo vya kiserikali hapa Gleneagles. Jamaa fulani kaniambia kuwa wengi wako Edinburgh, hawakutaka kuja hapa. Eti wanafurahia maisha ya Uskoto. Hapa nimeona wanaharakati wanne tu. Nimewahoji tayari. Habari hiyo nitaiwekea kiungo hapa ikishatoka. Pia nimehoji baadhi ya waandishi wa habari wa Afrika. Nitamaliza kesho. Kati ya maswali ambayo nimekuwa nikiwauliza wanaharakati ni hili: ukipata nafasi ya kunywa kahawa na akina Joji Kichaka utawaambia nini?
Usiniulize mimi swali hili maana sitakubali kutumia muda wangu kunywa chai na Joji. Chai haitashuka.
Kesho ndio ilikuwa tuondoke kurudi London ambako kama mnavyojua kumetoka janga kubwa. Ila kwasababu viongozi wa Afrika watafaongea na waandishi jioni, imebidi tukae hapa hadi jumamosi. Je nikikapa nafasi ya kumuuliza Mkapa swali nimuulize nini?
Thu 7 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Wakati tukijiandaa kuja hapa Gleneagles wanapokutana wakuu wa makuhani wa ubepari, tulipata taarifa za shambulio la kigaidi huko London. Muda mfupi uliopita waziri mkuu wa Uingereza, Tony Balir, ameondoka ghalfa toka kwenye mkutano unaoendelea kwenda London. Tunaambiwa kuwa atarudi. Swali ambalo limekuwa likiulizwa na wengi baada ya shambulio hili ni jinsi ambavyo mkutano huu una hatari ya kupeleka macho kwenye suala la ugaidi zaidi ya suala la Afrika. Mwandishi mmoja kaniambia kuwa viongozi wengi wanapoongea na vyombo vya habari hawazungumzii, kwa mfano, suala la mazingira ambalo liko mezani bali ugaidi. Kwa watu wengi kuna masikitiko kuwa Afrika itawekwa kando na ugaidi kuchukua mstari wa mbele. Mimi binafsi sioni kwanini watu wanasikitika. Nadhani kuna watu wanachukulia kuwa makuhani hawa ni wakombozi wa Afrika wakati ambapo wanachofanya ni kunadi bara letu kwa makampuni yanayomilikiwa na marafiki na jamaa zao. Na makampuni mengi wanamiliki wao wenyewe kwa kupitia hisa. Kuna utani fulani unaendelea hapa. Waa
ndishi wakitaka kwenda kula au bar ambako kila kitu ni bure wanasema, “Ngoja nikafanye umasikini kuwa historia.” Wanasema hivi kukejeli kampeni iliyokuwa ikiungwa mkono na serikali ya hapa iitwayo MAKE POVERTY HISTORY.
Wed 6 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Tumerudi nyumbani toka Gleneagles, mwendo wa kama saa moja na nusu. Mpango uliopo hapa ni kuwa basi linaondoka toka hoteli ya Hilton? Sheraton? (sikumbuki…zote zinafanana) kupeleka waandishi wa habari. Basi tumefika pale tukashuka kwenye gari kisha tukapita sehemu ya kusachiwa, “Weka begi hapa, toa vitu mfukoni, njoo hapa, nyanyua mikono juu, onyesha soli ya viatu vyako…” Hizi ndio amri unazokutana nazo. Lakini kwa ujumla askari ambao nimekutana nao hapa toka nije ni wastaarabu sana. Baada ya kusachiwa tuliingia kwenye basi jingine dogo ambalo lilitupeleka kwenye kituo cha waandishi wa habari. Pale tukakabidhiwa begi. Kila mwandishi anapewa begi hili ambalo ndani yake lina biskuti, chokoleti, magazeti, na wiski aina ya Black Label ambayo imevundikwa kwa miaka 12. Wakati wanatupa nilitaniwa wenzangu, “Wanatuhonga nini?”
Ukiona kiasi cha fedha zilizotumika kwa mkutano huu ambao makuhani wakuu wa ubepari wanakutana kwa masaa sijui mawili kwa siku huwezi kuamini. Kwanza nilipokuwa ndani ya basi baada ya kulala, kuamka, kulala, na kuamka tena, nilijiuliza: Kwanini viongozi waliochaguliwa na watu waje kujificha mbali hivi? Eneo lote limezungushwa waya, juu kuna helikopta zinazunguka, chini askari wamejaa kila upande…kweli hawa ndio makuhani wakuu.
Basi tukaenda kwenye tafrija ya waandishi wa habari ambapo kulikuwa na maakuli ya nguvu ya Kiskoti, mvinyo, wiski, na vitu vingine ambavyo majina yake sijui na sikuthubutu kuuliza nisionekane kuwa nimeshuka mjini leo! Hivi majuzi Rais wa Ufaransa, Chirac, alidai kuwa mapishi ya Uskoti ndio mabaya zaidi Ulaya baada ya mapishi ya Ufini. Waingereza wamechukia na kudai kuwa, “afadhali yetu sisi hatuli konokono na miguu ya chura.” Jamaa ambaye anatuandalia chai asubuhi ni Mfaransa, leo nilimuuliza kama amewahi kula miguu ya chura akacheka karibu akaukie.
Wakati tunajichana tuliambiwa mambo kadhaa kuhusu nchi ya Uskoto: simu, luninga, dawa ya penisilini, vyote viligunduliwa hapa. Mfumo wa kileo wa vyuo vikuu na vitivo ulianzia hapa. Uskoti inaongoza kwa utoaji wa machapisho ya kitaaluma duniani (ukilinganisha machapisho na idadi ya wananchi wake).
Mapema leo kulikuwa na mapambano kati ya polisi na waandamanaji. Kulikuwa pia na maandamano yaliyopewa kibali yaliyoongozwa na akina Bono na Geldof. Imeshangaza wengi kuona kuwa serikali ya Uingereza inavyounga mkono akina Bono na pia waandaaji wa Make Poverty History. Unaweza kuamini kuwa waziri wa mambo ya misaada ya kimataifa wa Uingereza, Hilary Ben, alikuwa kwenye maandamano ambayo wengi waliamini kuwa yalikuwa yakipinga ubepari. Maandamano ya kuipinga serikali yanahudhuriwa na mtumishi wa hiyo serikali. Watu sasa wameanza kusema kuwa hawa wakuu wa makuhani wametuzidi kete maana hata maandamano wanaandaa wao kwa kutumia watu wengine.
Sasa nitaandika kifupi juu ya siku ya kwanza kufika pale Gleaneagles kwa ajili ya blogu ya Panos, kisha nikalale maana kesho asubuhi na mapema tunakwenda kule waliko wezi wakuu wahedi! Ratiba inaonyesha kuwa msafara wa rais wa Tanzania utawasili kesho. Nimepewa namba ya kupiga ili kujua kama Mkapa atapatikana kwa ajili ya mahojiano.
Wed 6 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Baada ya mwendo kama wa saa moja na nusu, nimewasili Gleneagles. Hivi sasa tunakunywa mvinyo na kula vyakula vya Kiskoti. “>
Wed 6 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Ninaondoka kwenda kwenye mjadala kwenye kipindi cha redio cha BBC kiitwacho Simon Mayo Show. Mjadala unahusu suala la maandamano na kama huwa yanaleta mabadiliko yoyote. Unaweza kusikiliza kwenye redio au mtandaoni.
Tue 5 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Kuna harakati za wabunge hawa toka nchi mbalimbali duniani za kutaka Benki ya Wezi (benki ya dunia) na shirika ambalo bango moja kwenye maandamano ya jumamosi lilisema kuwa kirefu chake ni International Mother F**** (IMF) yaendeshwe kidemokrasia. Hivi sasa kura za wanachama wa vyombo hivi vya kibaguzi zinategemea uwezo wa kiuchumi wa nchi. Kwahiyo utaoana kuwa Marekani ikitaka kupitisha au kupinga jambo lolote kwenye vyombo hivi watafanikiwa bila kipingamizi chochote. Na jamaa hawa ndio wanasema kuwa wanataka kuifundisha dunia demokrasia.
George Monbiot alisema jambo moja zuri sana jana. Alisema kuwa akina Bono na Geldoff wanashindwa kujua jambo moja muhimu sana: hakuna uwezekano wa kubadili vyombo hivi vya njururu. Vyombo hivi vimeundwa ili kuendeleza matakwa ya nchi tajiri ambazo zinategemea sana umasikini wa nchi za Kusini. Umasikini wa nchi zetu ndio njia pekee ya kuwafanya wao kuwa matajiri. Usitegemee, kwa mfano, Waswisi wataipa Ghana msaada wa kujenga viwanda vya kutengeneza chocolate. Waswisi wanataka kununua cocoa toka Ghana kwa ajili ya viwanda vyao, Ghana ikiwa na uwezo wa kutengeneza chocholate wenye viwanda Uswisi unataka wale polisi?
Monbiot anasema kuwa hakuna njia yoyote ya kuondoa umasikini duniani bila kuhoji, kukabiliana, na kuuondoa mfumo wa ubepari unaowapa viongozi wachache na makampuni ya maswahiba wao au makampuni yenye hisa zao uwezo wa kuamua jambo lolote kwa niaba ya dunia nzima.
Tazama sura halisi ya mfumo huu wa ubepari: makampuni ya Makidonadi na Walt Disney yanatumia fedha za matangazo kwa mwaka mzima ambazo ni zaidi ya bajeti ya elimu na afya ya nchi 18 duniani.
Tue 5 Jul 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Pamoja na kazi niliyonayo ya kuandika habari hii ya City Water kwa ajili ya tovuti ya Panos, siwezi kuacha kuwatangaza wanablogu hawa wapya wa Kiswahili. Yuko huyu mwandishi wa habari, ndugu Ngurumo, na bwana Sagati, ambaye sifahamu anafanya nini.
— Next Page »