October 2005
Monthly Archive
Sun 30 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Hivi sasa kila alhamisi, kutakuwa na makala fupi kuhusu yazungumzwayo katika baadhi ya blogu za Watanzania/Kiswahili katika blogu ya Sauti za Dunia (Global Voices).
Bonyeza hapa usome makala ya wiki iliyopita. Bonyeza hapa usome ya wiki ile nyingine.
Sun 30 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Kuna nafasi za kuhudhuria warsha kuhusu matumizi ya programu huria za kompyuta kwa wanaharakati wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya wanawake. Barua pepe iliyonitaarifu kuhusu warsha hii sikuifungua mapema. Washiriki wa warsha hii (hasa wanawake) watagharimiwa kila kitu. Tarehe ya mwisho kuomba kushiriki ni tarehe kwanza/mosi mwezi wa 11 (Novemba). Ingawa siku zimebaki chache, fomu yenyewe inauliza maswali machache sana.
Kama uko kwenye shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na masuala ya wanawake au unafahamu mtu yeyote, tafadhali chukua hatua ya kuomba au kutaarifu wanaohusika. Muda ni kidogo hivyo fanya hima.
Au nenda kwenye anuanni hii:
Sun 30 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Sikujua kuwa naweza kwenda mwendo wa kinyumenyume nikiwa nimevaa viatu vya juujuu. Mmoja wa waanzilishi wa mradi wa Sauti za Dunia (Global Voices) , Ethan Zuckerman, ndivyo anavyosema. Ethan ambaye tulikuwa naye kwenye mkutano wa teknolojia wa Pop!Tech ameandika juu yangu. Pambazuko ndio kanikumbusha juu ya makala hiyo. Bonyeza hapa uisome.
Sun 30 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Mradi wa
The Hole in the Wall ndio unachofanya. Hawa jamaa wanachukua kompyuta, wanakwenda maeneo ambayo watu hawajui na hawajawahi kuona kompyuta, kisha wanawapa watoto kompyuta bila kuwapa mafunzo yoyote. Swali ni kuwa ukimpa, kwa mfano, mtoto wa kijijini kompyuta, ataifanyia nini?
Bonyeza hapa uone yanayotokea unapowapa watoto kompyuta bila kuwaambia cha kufanya.
Sat 29 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Fide Tungaraza anasema kuwa alidhani kizazi cha Watanganyika (ambao pia huitwa Wadanyanyika) walibeba maiti ya Dakta Livingstone toka Kigoma hadi Bwagamoyo kwa miguu kilikwisha. Kwanini anasema hivyo? Soma waraka wake hapo chini:
Mimi nilifikiri kizazi cha wale Watanganyika waliombeba Dr Livingstone tena akiwa kafa kilikwisha! La hasha! Kumbe wajukuu zao bado tupo na tunaendeleza waliyoyafanya! Nilipokuwa Chuo cha Sanaa Bagamoyo nilikuwa nikienda kanisani na kutazama pale mahala waliposimama wale Watanganyika waliombeba mfu Dr Livingstone na kuwaambia wazungu wenziye kwamba “..Bwana amefariki..” Nilikuwa sipati majibu kwamba: Wale Watanganyika walikuwa na utu sana? Au walifanya vile kwa sababu walikuwa wanataka walipwe mishahara, marupurupu, mafao na pensheni zao kwa kukileta kidhibiti cha maiti? Au walimpenda sana Hayati Dr Livingstone? Au walikuwa wafanyakazi watiifu na waaminifu kwa mwajiri wao? Au walikuwa kama Waswahili wasemavyo mafala? Au walikuwa wapumbavu kupindukia? Au kama uchawi upo walikuwa wamelogwa?
Siku zilizopita nilikarahishwa na habari kama hii kwenye gazeti la Dar Leo
(http://www.bsctimes.com/). Habari hiyo ilikuwa na kichwa cha habari ASKARI WA KIINGEREZA WAUA CHANGUDOA. Habari hiyo niliituma kwa baadhi yetu na kwa Mheshimiwa Waziri Omar Mapuri na Balozi Abdulkadir Shareef ili kwamba ichukuliwe hatua. Sijui kama kuna hatua iliyochukuliwa. Leo nimekumbana tena na habari za kabila hiyo hiyo yenye kichwa cha habari MCHINA AMTWANGA ‘HEDI’ MBANTU NA KUZIRAI. Kuna tusi limenijia lakini nalihifadhi, hivi ingekuwa MBANTU KAMPIGA ‘HEDI’ MCHINA NA KUZIRAI ndani ya mitaa ya Beijing huyo Mbantu angekuwa hai mpaka saa hizi? Leo imenipasa kusema kwamba wajukuu wa wale Watanganyika bado tupo baada ya kukumbana na taarifa hii kwenye gazeti la Nipashe (
Sat 29 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Bwana mmoja kanitumia makala moja kiboko. Anazungumzia hadithi ambayo Watanzania tumekuwa tukipigiwa na wezi wa kalamu. Wezi wa kalamu ni watawala. Fela Kuti ana wimbo anasema kuwa wezi wanaotumia silaha wasitutishe kama wezi wa kalamu. Unajua mwizi wa silaha anaweza akaenda dukani kwa Mangi akaiba na kuua watu wawili. Wezi wa kalamu walioko madarakani wizi wao unaua taifa zima.
Basi makala hiyo inazungumzia hadithi ya toka mwaka 1973 ya kuhamia “makao makuu” Dodoma. Makala hiyo itatoka kwenye blogu mojawapo za Kiswahili karibuni kwahiyo sitaizungumzia. Nilichotaka kusema ni kuwa ndani ya makala hiyo huyu bwana hataki kuita wakoloni wapya “wawekezaji.” Anawaita “waekezaji.” Anasema kuwa kazi yao wakoloni hawa, wanaoshirikiana na akina Mangungo wa Msovero wa siku hizi ambao wanaishi kwenye jengo lenye kuta nene kuliko gereza la Ukonga, ni kuezeka kwani Watanzania tayari tumejenga. Kwahiyo jina lao ni waekezaji.
Makala hii imezungumzia suala la Watanzania kutopenda vitu vyao. Hii inanikumbusha jambo moja linalokera sana. Utasikia wakati fulani Rais Mkapa akiwataka Watanzania kujenga tabia ya kununua bidhaa za Tanzania. Ajabu ni kuwa wakati Mkapa anasema hivyo kila kitu mwilini mwake kuanzia anjifu/leso, tai, viatu hadi nguo ya ndani (kinasa) vimetoka kwenye nchi za viongozi anaopenda sana kupiga nao picha. Ukienda pale ikulu huoni vitu vya Tanzania, hata mapambo…sasa anapotuambia tununue vya Tanzania anakuwa anatutania au? Sio Mkapa tu anayefanya hivyo, hotuba za kuwataka Watanzania wanunue bidhaa zao hutolewa mara kwa mara na watu mbalimbali.
Huenda watawala hawa wanaohubiri wasichofanya wanaiga kwa wahubiri wa kidini wanaosema, “Fuata ninayohubiri sio ninayotenda.” Unafiki wa-hedi!
Wed 26 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni

Baada ya siku kadhaa za pilikapilika za mkutano katika mji huu mdogo (pichani) wa Camden, ninapumua. Mji huu wa ajabu sana. Siku ya mwisho ya mkutano wa
Pop!Tech (ambao hufanyika kila mwaka, kwa miaka tisa sasa), hoteli, migahawa, lojingi, n.k. hufungwa. Mimi na rafiki yangu, Denver Hopkins wa
ThoughtFarm, tulikwenda kula chakula cha mchana hoteli moja siku ya mwisho wa mkutano. Tunafika pale tunakuta wenye hoteli na wafanyakazi wanajichana. Wakatukaribisha na kutuambia kuwa siku hiyo ni mwisho wa biashara hadi baada ya miezi sita kipindi cha baridi kitakapomalizika. Ninapokaa mimi na anapokaa Denver napo wanatia kufuli. Hoteli nyingine walitia kufuli toka asubuhi. Mji huu hasa ni wa jamaa wenye nazo wanaokuja kupumzika kipindi cha majira ya joto. Jamaa mmoja wa Google ambaye nyumbani kwake kila jioni kulikuwa na tafrija ya kukata na shoka, yeye hukaa kwenye nyumba yake hiyo mwezi mmoja kwa mwaka. Camden ni ile miji Marekani ambayo imejaa watu wenye siasa za mrengo wa kulia, wenye pesa, wenye kupenda kuchangia pesa zao kwenye miradi ya maendeleo. Ni miji ile isiyo na uhalifu…sikuona polisi hata siku moja. Ni miji ambayo iko kama vile kisiwa, ukikaa hapo unaweza kudhani kuwa Marekani ni mbinguni…toka kidogo uone.
Napumua.
Sat 22 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Siku imamelizika hapa katika mkutano wa Pop!Tech. Kilichobaki sasa ni kwenda kwenye tafrija. Tafrija hiyo inafanyika hapa. Ninachofurahi ni kuwa leo hawajaleta ule mchezo wa kutuambia eti tuvae suti nyeusi.
Sat 22 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Zaidi ya asilimia 70 ya Wamarekani wanaamini kuwa Saddam Hussein na Osama bin Laden wana uhusiano wa damu! Anayesema hayo ni Robert Trivers. Anasema kuwa binadamu wanapenda sana kudanganywa na kujidanganya.
Sat 22 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni [1]
Watu wametoka kwenye pumziko. Sasa tunapata dozi ya falsafa toka kwa mwanafalsafa na mwanahesabu,
Nassim Taleb. Sijui kama nitaweza kusikiliza vyema. Kuna mengi yanaendelea. Ninatazama teknolojia ya kufundishia mtandaoni toka kwa mwalimu mmoja hapa pembeni yangu. Bonyeza
hapa uone shirika analofanya kazi. Anaandaa kompyuta yake ili aniingize kwenye darasa lake (liliko mtandaoni). Nimekuwa namuona kila dakika yuko bize akiandika. Nikamuuliza, mbona? Nilidhani ni mwanablogu kumbe mwenzangu tuko wote hapa lakini wakati huo huo anafundisha wanafunzi waliotapakaa sehemu mbalimbali duniani! Mwanablogu wa Kenya,
Ory (Kenyan Pundit) yuko mbele yangu upande wa kulia akihojiwa na Renee Blodget (ambaye ameishi Tanzania na hata kulala lupango!). Anamuhoji Ory kwa ajili ya
blogu yake hii hapa. . Kesho asubuhi Waafrika wote 12 tulioko hapa tutakuwa kwenye kiti moto kwa ajili ya kipindi cha luninga
kituo cha PBS. Tulikuwa na mkutano kabla ya chakula cha mchana kujadili jinsi ambavyo kiti moto kitakavyoendeshwa. Mwendeshaji wa kiti moto atakuwa ni David Kirkpatrick ambaye ni mhariri wa masuala ya intaneti wa jarida la
Fortune. David ni kati ya wazungu wachache ambao wameweza kutamla jina langu inavyopaswa bila kuketishwa chini na kufundishwa kwa kiboko. Labda ni kwakuwa aliwahi kuishi Afrika (Nigeria) na ametembelea nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania.
Huyu mwanafalsafa naona anawaacha wengi nje…wanaoanza kusinzia ni wengi. Wapiga miayo nao wamo…wanafalsafa wakati mwingine…anakuwa kama anaongea mwenyewe.
Baadaye.
Sat 22 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Anaongea sasa
Susan Blackmore:-Dhana ya “memetic” imezungumziwa katika kitabu cha
The Selfish Gene cha Richard Dwarkin
-tafsiri ni kuwa meme ni kitu ambacho kinaigwa, kinajirudia, kinaambukiza…
- inaweza kuwa ni nyimbo, teknolojia, hadithi, mitindo, tabia, nembo
-ni kitu gani kinafanya vitu au mawazo au tabia fulani kuigwa zaidi ya nyingine?
** Anaonyesha mfano wa zile barua (zamani zilikuwa barua za posta siku hizi ni barua pepe) tunazotumiwa inayokwambia kuwa unatakiwa kutuma kwa watu wengine 10 au 20 ili upate bahati na usipofanya hivyo utakumbwa na balaa
- anaelezea sababu inayofanya barua hizi kufanikiwa na kuzunguka dunia mara nyingi: authority, ahadi za mambo mazuri, kuna vitisho kwenye barua hizo (mfano, usipoituma majanga yatakukumba), n.k.
** Anachekesha kidogo:
- nimetafiti Kurani nikakuta kuwa wanaume wanaokufa wakitetea uislamu wanapewa mabikira mbinguni. Lakini sikuona zawadi wanayopewa wanawake. Mimi binafsi nisingependa kupata wanaume mabikira. Nataka wanaume wanaojua majamboz!
- Mto Ganges unaaminiwa kuwa unatakasa waumini wa dini ya Kihindu. Tatizo ni kuwa mto huu ni kati ya mito michafu kuliko yote duniani. Ila waumini wanaamini kuwa nafsi zao zinatakaswa
**Siwezi kumsikiliza huyu mama hadi mwisho. Nakwenda kuongea na bwana mmoja ambaye anaondoka hapa Camden muda sio mrefu hivyo lazima tuongee sasa.
Sat 22 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
- dunia imejaa imani ambazo hazikubaliani
- dini kuu zimetokana na vitabu vilivyoandikwa na watu
- nitaongea mambo kadhaa ambayo yanaweza kukera baadhi ya watu
- najua kuwa watu asilimia 90 wanamwamini mungu, asilimia 93 wanaamini kuwa Yesu alifufuka, kwahiyo lazima nitaudhi baadhi ya watu maana nitaongea mambo makali sana dhidi ya dini na imani
- asilimia 22 ya Wamarekani wanaamini kuwa Yesu atashuka toka mawinguni na kuokoa dunia hii hivi karibuni
- Wamarekani wanaamini kuwa Israeli ni nchi iliyotengwa na mungu kwa ajili ya waisraeli
- asilimia zaidi ya asilimia 50 wanaamini kuwa binadamu wanaamini kuwa ni kweli kabisa kuwa tuliumbwa toka kwenye udongo, wanaamini kisa cha nyoka kuongea na kumshawishi Hawa kula tunda
- chukua mfano huu: eti matumizi ya kondomu ni kinyume na mapenzi ya mungu. Nenda Afrika katika vijiji ambavyo mamilioni wanakufa, nenda huko ukasambaze imani hii. Huu ni ujinga na kosa la jinai
- ninachosema ni kuwa lazima fikra na imani potofu zipewe changamoto. Sitaki kukataza watu kuwa na imani hizo au kupitisha sheria dhidi ya imani hizi. Ninachotaka ni watu kuhoji imani na fikra hizo
- tatizo la dini ni kuwa dini hazitaki hoja au ushahidi
- ndio unaona tofauti ya sayansi na dini, kwenye sayansi lazima kuwe na ushahidi. Unaona wakristo wenye siasa kali Marekani wanasema kuwa shambulio la Septemba 11 linatokana na ghadhabu ya mungu kutokana na Marekani kuwa na mashoga na kuruhusu utoaji mimba
- hivi wako wapi magaidi wa kujitoa mhanga wa Kibudha? Unatakiwa kufanya kazi kubwa sana kupata watu wa kujitoa mhanga katika imani ya Kibudha
- nashindwa kuelewa kwanini watu wenye siasa za kushoto hawataki kukubali kuwa uislamu una itikadi inayofanya rahisi kwa waumini wake kujitoa mhanga na kuua wasio na hatia
- kwenye uislamu kuna imani kuwa wanaojitoa mhanga wanapata maisha ya raha ya milele
- vitabu vya dini havifundishi uvumilivu wa dini na imani tofauti na yako. Vinafundisha ukereketwa na siasa kali. Hakuna kitabu cha dini kinachosema dini zote zina haki sawa
- wakristo waliokuwa wakichoma watu moto
- “Mtakatifu” Aquinas alisema kuwa wanaopinga ukristo hawana budi kuuawa. “Mtakatifu” Augustine alisema kuwa wateswe vikali sana
Maswali:
Anaulizwa anafikiria nini kuhusu “intuition”
- anajibu na kusema kuwa tunazungumzia “intuition” pale tunaposhindwa kuelezea hisia fulani
Anaulizwa swali kuhusu maendeleo ya binadamu na imani ya dini
- anajibu kwa kusema kuwa ukitazama ripoti ya Umoja ya Mataifa ya Maendeleo inayotolewa kila mwaka inaonyesha kuwa nchi ambazo zina maisha bora zaidi (kwa vipimo kama afya, elimu, vitendo vya uhalifu, vifo vya watoto, usawa wa jinsi, n.k) ni zile ambazo zina watu wengi wasio waumini wa dini (Mawazo yangu: huenda huyu bwana kasoma makala zangu maana hii ni hoja yangu!)
Mwisho***
Sat 22 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni [1]
Tunayemsikiliza sasa ni mtu ambaye ninamuheshimu mno mno. Huyu ni mkurugenzi na mwanzilishi wa chuo cha mguu peku,
Barefoot College, ndugu
Bunker Roy. Msikilize:
- nilipomaliza shule nilijiambia kuwa nataka kuanzisha chuo kwa ajili ya watu masikini, watu wasio na elimu hata kidogo
- alianzisha chuo katika kijiji cha Tilonia ambapo ni jangwa. Kuna wakati hawapati mvua kwa miaka 6
- Sababu ya kuita chuo “barefoot” ni kuwa watu wengi duniani wanaotembea bila viatu wana maarifa na uwezo mkubwa
- chuo hiki ni sehemu ambayo walimu na wanafunzi wanajifunza
- chuo hiki hakikubali watu wenye vyeti vya shule au vyuo lakini zaidi ni kuwa hata wanaohitimu chuo hiki hawapewi vyeti
-** Anatuonyesha nyumba zilizojengwa na mwanafunzi wa chuo hicho ambaye hajui kusoma wala kuandika
- paa la chuo hicho lilijengwa na wanawake kwa kutumia teknolojia ya India ambayo imekuwa ikitumika zaidi ya miaka 100
- kijiji cha Tilonia kimeshaingia karne ya 21: wana teknolojia ya mtandao usiwaya, wanauza bidhaa zao mtandaoni (
http://www.tilonia.com/), n.k.
**anatuonyesha teknolojia ya kukusanya maji ya mvua.
- teknolojia hii inasaidia kuwapatia wanavijiji maji na hivyo kuwapa watoto muda wa kwenda shule (maana hutumia masaa mengi kutafuta maji) na pia kuwapa wazazi wao muda wa kufanya mambo mengine badala ya kutembea mwendo mrefu kutatufa maji. Baada ya kuanza kutumia teknolojia hii katika mashule vijijini, idadi ya watoto wanaokwenda shule iliongezeka!
- wahandishi wa kisasa ni wajinga sana…elimu yao imeshindwa kabisa kutatua matatizo makubwa ya masikini na watu vijijini
- alikwenda kwa waziri wa maji kumwambia kuwa serikali ijihusishe na mradi wa kukusanya maji ya mvua mlimani, waziri akasema: Hutaweza maana mhandishi mkuu amesema haiwezekani. Bunker akamwambia waziri: nipe ruhusu nijaribu. Mradi huo ulifanikiwa na sasa vijiji vingi vinatumia teknolojia hiyo
* Anatuonyesha picha ya vibao vinavyokusanya nishati ya jua. Teknolojia hii iliwekwa na inakarabatiwa na mtu ambaye amehudhuria shule kwa miaka 6 tu maishani mwake.
- tumevipa vijiji zaidi ya 6000 teknolojia ya nishati ya jua
- anatuonyesha picha ya mhandisi wa kwanza wa teknolojia ya nishati ya jua ambaye ni mwanamke wa nchini Afghanistan
- asilimia 60 ya watoto vijijini India hawaendi shule maana wanachunga mifugo. Lakini wana uwezo wa kwenda shule usiku, ila hakuna taa. Sasa tumetengeneza taa zinazotumia nishati ya jua kwahiyo kuna shule vijijini ambazo wanafunzi wanakwenda shule usiku
** anatuonyesha picha ya dakitari wa kijijini.
- huyu bwana mnavyomuona ni mlemavu na hakuwa na elimu hata kidogo. Tulikumta barabarani tukamsimamisha tukamwambia, “Twende chuoni kwetu na baada ya miezi sita utakuwa dakitari!” Hivi sasa anafanya kazi kwenye zahanati vijijini akipima watu damu, choo, anatoa dawa, n.k.
- anaseme kuna kijiji Ethiopia ambapo watoto wanatembea zaidi ya saa moja kwwenda shule wakiwa wamebeba maji kwa matumizi shuleni wakati kwa teknolojia rahisi sana shule hizo zinaweza kukusanya maji ya mvua
- wanafunzi wanaokubaliwa katika chuo chake lazima wawe wametoka vijijini, wachaguliwe na kijiji, na mafunzo wanayopata yanaendana na mahitaji ya kijiji wanachotoka na lazima warudi kijijini kwao
- moja ya sababu inayowafanya chuo hiki wasitoe vyeti ni kuwa ukishampa mtu cheti basi ujue atakimbilia mijini wakati nia ya chuo hiki ni kufunza wahandisi, wanasayansi, na wataalamu mbalimbali kwa ajili ya wakazi vijijini
- alipoanza kuishi kijijni baada ya kumaliza chuo wanakijiji walimuuliza kama amefanya kosa mjini na anawakimbia polisi. Wanakijiji walidhani hivyo maana mfumo wa elimu ya kisasa unawaondoa wasomi vijijini, wanakijiji hao hawakuamini kuwa Bunker amekwenda kijijini hapo kuishi nao. Ameishi hapo kwa miaka 35 sasa
- Anamaliza kwa nukuu toka kwa Mahtma Gandhi: Kwanza wanakudharau, kisha wakucheka, kisha wanapambana nawe, kisha unashinda!
Makofi wa! wa! wa! waaaaaaa
Sat 22 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Tumetoka kwenye chai na mandazi ya kizungu.
Neil Gershenfeld wa
Taasisi ya Teknolojia ya Massachussetts (MIT). Sielewi kabisa anaongelea kitu gani. Ninajisikia kama vile niko darasa la Fikizia la mwalimu Mashingia pale sekondari ya Mawenzi. Mashingia ni yule mwalimu aliyetazama mwandiko wangu siku moja na kusema, “Wewe kijana mwandiko watu tu unaonyesha kuwa hesabu zinakupiga chenga.” Da, hapo ni kidato cha pili. Maneno yake yalikuwa ni kama unabii kwani kwenye mtihani wa kitaifa wa kidato cha pili nilipata 11 kwenye hisabati. Nkya, usicheke!
Haya, Neil anaongea. Labda ili uelewe kwanini sielewi, soma kuhusu utafiti anaofanya pale MIT kwa kiingereza, sitaki wala kujaribu kutafsiri):
“His unique laboratory investigates the relationship between the content of information and its physical representation, from molecular quantum computers to virtuosic musical instruments.”
Labda pia majina ya vitabu alivyoandika vitakupa picha ya tabu ninayopata kumwelewa anazungumzia mdudu gani. Hivi ndio vitabu vyake:
When Things Start to Think, The Physics of Information Technology, na The Nature of Mathematical Modeling (hasa hiki cha mwisho!!!).
Pale MIT anapofanya kazi kuna watu wanafanya utafiti ambao ukielezwa unaweza usiamini. Katika maabara za MIT, wana msemo mmoja. Wanasema kuwa kama jambo linasemekana kuwa haliwezekani, basi jambo hilo ndio watataka kulifanyia utafiti na majaribio.
Sat 22 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Anaongea Cameron Sinclair. Huyu ni mwanzilishi wa shirika la Architecture for Humanity.
Shirika lake lina miradi sehemu mbalimbali duniani. Shirika hili linabuni na kujenga makazi katika maeneo yenye maafa, kwa mfano, wamejenga zahanati zinazomfuata mgonjwa kwa ajili ya wagonjwa wa Ukimwi Kusini mwa Afrika, makazi ya wakimbizi wanaorudi makwao, majengo ya michezo.
Haya ndio anayosema:
- wanajenga uwanja wa mpira wa miguu kwa wanawake nchini Afrika Kusini
- ramani ya uwanja hiyo ilibuniwa na vijana walioshiriki kwenye mashindano ya kuchora ramani ya uwanja huo. Aliyeshinda ni kijana toka Singapore mwenye miaka 20
- sababu kubwa ya kujenga uwanja huo ni kuwa wanawake katika kitongoji cha Somkhele, KwaZulu Natal hawana maeno ya kupumzika na kujishusisha na michezo. Pia idadi ya walioathirika kwa ukimi ni kubwa sana. Ili kuepusha vitendo ambavyo vinaweza kuwaweka kwenye hatari ya kupata ukimwi, wakazi wa kitongoji hicho waliamua kuwa eneo la michezo kwa wanawake ni muhimu
** Anatuonyesha picha na video za miradi yao katika nchi mbalimbali duniani
Anaonyesha picha ya nyumba ambayo inaweza kuangushwa na kisha kujengwa kwa dakika 45! Nyumba hii haiwezi kuteketea kwa moto. Anaonyesha picha nyingine ya shule iliyojengwa kwa fedha zilizotokana na mandazi yaliyouzwa na watoto wa shule. Shule hi imejengwa kwa teknolojia ambayo inakusanya maji ya mvua kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
*** Anaonyesha video: inaanza na kauli toka kwa mtu anayesema kuwa Bush hapendi watu weusi. Video ina wimbo wa rap na picha za maafa ya Katrina. Wimbo huu wa rap ni kuhusu maafa ya Katrina. Sijawahi kuusikia. Una maneno makali sana.
** Anaonyesha picha ya nyumba za bei nafuu ambazo wamezibuni kwa ajili ya wakazi wa New Orleans.
(Bwana anaongea haraka kweli!)
- anasema kuwa mtu mmoja katika saba duniani anaishi kwenye makazi yasiyofaa kabisa kuishi kwa mwanadamu.
Sat 22 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Jina la mwanamuziki huyu sikulikia vizuri. Ni binti mmoja mrembo na nywele zake ndefu. Anaimba mashairi ya mshairi ambaye lazima usome mashairi yake kabla hujaondoka hapa duniani. Mshairi huyo ni Rumi. Bonyeza
hapa umsome. Binti sauti nyororo kabisa ya kutoa nyoka, mapanya, panyabuku, vichakoro, na viumbe wengine walioko mapangoni au darini. Anapiga gitana halafu kuna jamaa anapiga matwali (matwali ni aina ya ngoma zipigwazo nchi za kiarabu). Ukumbi mzima mdomo wazi…acha tu. Matwali haya yananikumbusha sikukuu za idi pale mtaani kwetu (nyumbani kwetu ni dakika mbili kwa miguu toka ulipo msikiti wa dini ya kiarabu, uislamu).
Sat 22 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Asubuhi nyingine.
Ingo Gunther ni msanii ambaye anatumia zana mbalimbali kama vile video, satelaiti, kompyuta, n.k. katika kazi zake. Anasema dhumuni kubwa la kazi zake ni kuonyesha mabadiliko na mambo mbalimbali duniani kama vile mazingira, siasa, utamaduni, n.k.
Bonyeza hapa uone moja ya kazi zake iitwayo “World Processor.” Kazi yake nyingine inaitwa Refugee Republic ambayo
utaiona ukibonyeza hapa. Kazi zake na bahari zake zaidi
bonyeza hapa.
Kabla ya Ingo aliongea
Robert Newirth. Kutokana na kuchelewa kulala nilichelewa kuamka na nikachelewa kufika hapa nikakuta ndio anamaliza kuongea. Bwana huyu anazunguka nchi mbalimbali duniani katika makazi ya masikini katika miji mikubwa.
Fri 21 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Bart Depram anajihusisha na mradi wa kutengeneza zana za kusaidia watu kutumia mtandao wa kompyuta kama sehemu ya kujenga mahusiano. Anasema wafanyabiashara wanataka kufanya webu kuwa ni kama soko moja kubwa. Yeye na wenzake wanataka kufanya webu iwe ni sehemu ya maingiliano, mahusiano, n.k.
Naandika anayosema bila kusahihisha:
(nimetazama pembeni nikapitwa. Ameitaja tovuti hii:
http://secondlife.com/ ila sijui kwanini ameitaja maana sentensi za awali zikuzisikia. Sasa anaonyesha teknolojia wanayotengeneza ambayo inakusanya habari mbalimbali toka kwenye tovuti mbalimbali. Kwa teknolojia hii huna haja ya kwenda kwenye tovuti hizo)
**************
Sasa wazungumzaji wote wameketi jukwaani wanaulizwa maswali. Kiti moto.
Negroponte akijibu swali kuhusu wakazi wa vijijini na watoto wa shule watakavyotunza kompyuta hizo: anasema wamefanya majaribio huko Cambodia na kukuta kuwa watoto wakiona matumizi ya kompyuta hizo watazitunza.
Negroponte anaulizwa je mtu akitokea mtu akitaka kununua kwa dola 300?
Anajibu kuwa kompyuta hizo hazitauzwa kwa kila mtu. Ni kwa ajili ya kusaidia watoto katika nchi zinazoendelea.
(Ninaacha kusikiliza ili nikaongee na jamaa fulani. Wakimaliza tunakwenda kula mlo wa jioni).
Fri 21 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
- ukitaka kubadili maisha ya watu badili mfumo wao wa elimu
- nia yake ni kujenga kompyuta ya mapajani ya dola 100
- asilimia 50 ya bei ya kompyuta za mapajani inakwenda kwenye mambo ambayo hayahusiani na utengenezaji wa kompyuta hizo.
- mwanzoni walitaka badala kuweka kioo kwenye kompyuta hizo ili kupunguza gharama watumie aina ya karatasi ngumu!
- kompyuta hizo zitakuwa pia ni kitabu
- wamekwenda nchi hizi kutangaza mradi wao: China, Brazil, India, Thailand na wanaongea na Afrika Kusini na Nigeria
- watu wengi wanamwambia kuwa yeye ni mwalimu wa chuo kikuu hajui masuala ya uzalishaji wa bidhaa. Anadai kuwa amekuwa kwenye bodi ya kampuni ya Motorola kwa muda mrefu kwahiyo anafahamu kwa kiasi fulani masuala ya uzalishaji wa bidhaa
- Anaweza kuwa wanaweza kushinda kutimiza ndoto yao ila kushindwa kwao hakutamaanisha kuwa kompyuta hizo hazitatengenezwa bali labda watazitengeneza kwa dola 125, kitu kama hicho ila sio kutozitengeneza
- wanaanza kuzitengeneza mwezi wa pili mwakani
(anatuonyesha picha za kompyuta hizo zitakavyokuwa)
- Kompyuta hizo zitakuwa zikitumika kama tunavyotumia kompyuta hivi sasa na pia kama kitabu. Yaani kama unavyoshika kitabu mkononi kukisoma, utaweza kuishika kompyuta hiyo kama kitabu
- wataonyesha kompyuta hizo mwezi ujao kule Tunisia kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Jamii-Habari
** Amemaliza. Maswali baadaye.
Fri 21 Oct 2005
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Hivi sasa tuko kwenye kipindi kiitwacho “Participation Revolution.” Magwiji wawili wataongea. Hawa ni kati ya watu ambao nimekuja kuwasikiliza. Hawa ni
Yochai Benkler ambaye ni mwalimu wa sheria pale Yale. Mwingine atakayekuja nyuma yake ni
Nicholas Negroponte. Negroponte anajihusisha na mradi wa kutengeneza kompyuta za mapajani ambazo zitauzwa kwa dola 100 au chini ya hapo kwa ajili ya nchi zinazoendelea. Tazama kuhusu mradi
huo hapa.
— Next Page »