January 2006
Monthly Archive
Sun 22 Jan 2006
Na admin, Maudhui:
bloguToa Maoni
Nimeamka asubuhi hii na kwenda moja kwa moja kwenye ukumbi pepe wa mjadala kuhusu neno muafaka la Kiswahili la teknolojia hii ya blogu. Nikasoma mawazo mazuri sana ya wachangiaji, nami nikaweka neno langu. Napenda uende pale ili ujue mjadala umefikia wapi. Kuna masuala fulani ya kinadharia kuhusu lugha na kuhusu blogu ambayo yamejitokeza. Ila pia mjadala huu umetuletea Spika. Unajua Liberia wamepata rais mwanamke. Ujeremani wamepata Kansela mwanamke. Chile wamepata raisi mwanamke. Tanzania imepata waziri wa fedha mwanamke. Kuna jambo linatokea duniani hivi sasa. Nasi tumepata spika mwanamke. Ukitaka kumjua nenda kwenye ukumbi pepe wa majadiliano ya neno blogu. Spika huyu tumekuwa tukimwita Mheshimiwa ila napendekeza tumwite ndugu. Naona neno ndugu lina maana nzuri zaidi ya mheshimiwa. Watwawala wetu wanaitwa waheshimiwa…si ndio?
Haya, bonyeza hapa.
Fri 20 Jan 2006
Furaha niliyonayo sijui nifanye nini. Au niseme nini.
Ngoja nianzie mwaka jana mwezi wa sita: mwezi wa sita mwaka jana nilikwenda jiji la Egoli/Jozi (au Johannersburg, kama hujui), Afrika Kusini, kwenye mkutano wa
Commons-Sense kwenye
chuo kikuu cha Wits. Mkutano huu ulikuwa ni wa ufunguzi wa tawi la shirika la Creative Commons nchini Afrika Kusini.
Bonyeza hapa usome hisia nilizopata nilipotembelea hapo kwa Madiba.Creative Commons in vuguvugu linaloendeleza mfumo wa hatimiliki mbadala (kwa kiingereza: “copyleft” badala ya “copyright”). Kwahiyo badala ya kazi zilizoko chini ya hatimiliki kusema “Haki Zote Zimehifadhiwa” kama ambavyo mfumo wa hatimiliki uliozoeleka ulivyo, Creative Commons inatoa nafasi kwa wamiliki wa kazi mbalimbali kuweza kusema, “Baadhi ya Haki Zimehifadhiwa,” au “Hakuna Haki Zilizohifadhiwa.” Kimsingi, mfumo huu, tofauti na mfumo wa hatimiliki uliozoeleka ambao una kila chembe za falsafa za kibepari, umejengwa juu ya falsafa kama vile Ujamaa au Ubuntu. Msingi wa Ubuntu ni huu: mtu sio mtu bila watu. (
bonyeza hapa kusoma kwa kifupi kuhusu ubuntu). Kwahiyo sio vigumu sana kwa Waafrika kuelewa mantiki ya vuguvugu kama Creative Commons. Afrika Kusini ndio nchi ya kwanza Afrika kuwa na tawi.Vuguvugu la Creative Commons nimekuwa nikilifuatilia kwa muda mrefu. Nilipokwenda mkutano wa Afrika Kusini na kukutana na wanaharakati wengine wa vuguvugu hili na pia “baba” wa Creative Commons,
Larry Lessig (
bofya hapa kuna blogu yake) mwili mzima ulinisisimka. Kabla ya hapo nilikuwa nimewagusia marafiki zangu kadhaa Tanzania juu ya vuguvugu hili ila hakuna aliyeonekana kujali. Walinisikiliza tu. Nikawaacha. Sasa mwezi Septemba nikiwa njiani kwenda Helsinki, Ufini (ambapo ndipo nilikutana na
Michuzi na blogu yake kabambe ilipozaliwa…blogu yake ina uraia wa Ufini!), nikiwa uwanja wa ndege Uholanzi nikakutana na Paul Kihwelo, ambaye zaidi ya kuwa mshikaji wangu, ni mkuu wa kitivo cha sheria, Chuo Kikuu Huria Tanzania. Tukaongea kidogo nikamgusia kuhusu Creative Commons na umuhimu wa kujenga vuguvugu lake Tanzania. Hatukuwa na muda wa kutosha. Tukakubaliana kuandikiana. Basi kukutana kwetu pale uwanja wa ndege kumezaa matunda. Na ndio furaha yangu niliyonayo. Paul ni kati ya watu ambao akikwambia kuwa atafanya jambo, ujue kuwa atafanya.
Ombi letu kwa ofisi inayoshughulikia uanzishwaji wa matawi ya Creative Commons katika nchi mbalimbali kutaka kuanzisha Creative Commons Tanzania limekubaliwa. Kwahiyo shughuli rasmi ya kujenga tawi la Creative Commons na kuwezesha wasanii, watunzi, shule, vyuo, wanasayansi, n.k. kutoa kazi zao kupitia Creative Commons imeanza. Paul Kihwelo ndio mwanasheria muongozaji wa zoezi zima la kuanzisha tawi lake nchini Tanzania. Zoezi hili litakuwa chini ya kitivo cha sheria, chuo kikuu huria (moja ya masharti ya kuanzisha tawi ni kuwa lazima kuwe na taasisi ambayo ndio itasimamia). Jumapili tutawasiliana na Paul kuhusu ujenzi wa tovuti maana katika masharti ya mradi huu ni kwamba lazima kuwepo na tovuti. Tayari kuna mashirika mawili ambayo yako tayari kutoa nafasi ya bure ya kuhifadhi tovuti yetu. Kesho ninakutana na Chris Blow wa shirika la NonProfit Design, ambaye yuko tayari sio tu kuhifadhi tovuti hiyo bali pia kuiunda.
Ukibonyeza hapa utaona jina la Tanzania tayari limeingizwa katika nchi ambazo ziko mbioni kuunda Creative Commons (Tazama upande wa chini sehemu isemayo: Upcoming Project Jurisdictions).
Watu wengi ukiongea nao kuhusu masuala ya faida ya kuwa na hatimiliki ya “baadhi ya haki zimehifadhiwa” au “hakuna haki zilizohifadhiwa” badala ya mfumo wa “hazi ZOTE zimehifadhiwa,” mawazo yao yanakuwa yanakwenda tu kwenye masuala kama ya muziki. Vuguvugu kama la Creative Commons linagusa maeneo mengi sana kwenye jamii. Hasa maeneo yanayohusu maarifa na elimu. Mfumo wa hatimiliki uliopo hivi sasa unapendelea watu wahodhi maarifa na elimu wakati ambapo Creative Commons inataka kuachilia huru maarifa na elimu. Kutokana na Creative Commons, kuna vitabu ambavyo unaweza kuvipata bure. Bila hata sumni. Kwa mfano, bonyeza hapa upate kitabu kimojawapo.
Lakini pia Creative Commons inaachilia huru maarifa ya vyuo vikuu kwa ajili ya faida ya watu wote hata kama sio wanafunzi waliolipa ada wa chuo chenyewe. Kwa mfano, chuo cha MIT kimeweka masomo yake wazi mtandaoni kwa watu wote wanaotaka kufaidi bure. Bonyeza hapa.
Hata chuo kikuu cha Rice nacho kinaunga mkono vuguvugu hili. Bonyeza hapa. Blogu yangu iko chini ya Creative Commons. Huenda umewahi kuona nembo ya Creative Commons ukashindwa kujua inafanya nini hapa. Ni kwamba kazi zilizoko hapa haziko chini ya mfumo wa “haki zote zimehifadhiwa.” Ina maana kuwa kama unataka kuzitumia (iwe ni picha, makala, kisa, shairi, n.k.) sio lazima uiombe ruhusu au unilipe.
Bonyeza hapa ukitaka kusoma zaidi juu ya Creative Commons (kwa kiinglishi).
Wed 18 Jan 2006
Na admin, Maudhui:
wanabloguToa Maoni
Mwanablogu mpya, Kimanzichana, bado nimnacheki kinamna. Sijui wewe. Mtembelee kwa kubofya hapa. Je ni mtu wa kejeli, dhihaka, sanifu, ucheshi, n.k.?
Wed 18 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Ni kweli kuwa bado blogu za Kiswahili ni chache ukilinganisha, kwa mfano, na blogu za Kiingereza za Wakenya. Ni kweli kuwa ni Watanzania wachache hivi sasa wenye uwezo, nafasi, na ujuzi wa kutumia tarakilishi na mtandao wa tarakilishi. Ninafurahi kuwa ukweli huu hauzuii wenye nia ya kublogu kufanya hivyo. Ukitazama historia ya magazeti, kwa mfano, nchini Tanzania utakuta kuwa kuna wakati kulikuwa na gazeti moja. Kuna wakati magazeti yalikuwa machache mno na tena hayakuwa yakisambazwa nchi nzima. Na tena yalikuwa yakisomwa na watu wachache sana. Na tena kulikuwa na watu wengi wasiojua kusoma. Lakini mambo yamekwenda hadi tumefika wakati ambapo huwezi kusoma magazeti yote yanayotolewa kwa siku. Na magazeti hayo yanafikia watu wengi zaidi. Blogu nazo kuna siku tutakaa na kusema, “unakumbuka enzi zile watu walikuwa hawajui blogu ni nini?” Utafika wakati huo. Jitihada zinafanyika. Kwa mfano, blogu zetu siku si nyingi zitaanza kusomwa asubuhi redioni na kwenye luninga kwenye vipindi vile wanavyosoma magazeti ya siku. Yaani kama wanavyosoma magazeti ya siku ndivyo watakuwa wanasoma blogu zetu, jambo ambalo litasaidia tunayoandika kufikia watu wengi zaidi. Tunajua kuwa redio ndio chombo cha habari kinachofikia watu wengi zaidi duniani hivi sasa. Tutaingia kwenye chombo hicho. Kwahiyo upo uwezekano wa kutumia vyombo vya habari vinavyofikia watu wengi kusambaza cheche tunazotoa kwenye blogu zetu.
Tararira yote hiyo nilitaka kumkaribisha mwanablogu mpya, ndugu Bwire (asante sana
Kasri la Mwanazuo kwa kutuletea). Bwire anasema kuwa weka kila kitu kando, fikra ndio mambo yote.
Bonyeza hapa umtembelee.
Mon 16 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Kutokana na maswali ninayopata toka kwa watu wenye nia ya kublogu na hamasa kubwa waliyonayo watu wengi wenye kutaka kutumia teknolojia hii kutoa mawazo yao, kujieleza, na kuelimishana na wengine, nimeamua kujenga blogu maalum ya mwongozo kwa wanaotaka kublogu na pia wale ambao tayari wanablogu. Blogu hii itasaidia watu wa kawaida wanaotaka kublogu, itakuwa na eneo la waandishi wa habari wanaotaka kublogu, kutakuwa na ukurasa kwa ajili ya wanaharakati au wenye mashirika yasiyo ya kiserikali wanaotaka kublogu, ukurasa wa kusaidia wanasiasa wanaotaka kublogu, ukurasa wa kusaidia wanaoblogu jinsi ya kutangaza blogu zao, ukurasa wa maelezo kwa wale wanaotaka kublogu bila kujulikana kuwa wao ni akina nani (kwa mfano, kama unafanya ofisi ya rais na unaona mambo ambayo unadhani ni muhimu umma ukajua lakini hutaki rais ajue kuwa wewe ndiye unayetoboa siri!), n.k. Iwapo kuna suala ambalo ungependa liwe na ukurasa wake, usisite kuniambia. Majina ya kurasa zenyewe yako upande wa kuume wa blogu hiyo, chini ya orodha ya miezi. Blogu hiyo utaiona kwa
kubonyeza hapa.
Mon 16 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Leo ni siku ya kitaifa nchini Marekani ya kumkumbuka mpigania haki za watu weusi na binadamu wote, Dakta Martin Luther King. Ninakupa viungo kadhaa vya hotuba zake ambazo zilikuwa zinasisimua mno kutokana na ufundi wake wa kuhubiri.
Bonyeza hapa uone video za hotuba zake.
Hapa kuna video ya mahojiano.
Bofya hapa kwa mkusanyiko wa video mbalimbali.
Kuna hotuba zake mbili muhimu sana kusikiliza: ya kwanza ni ile ya “Nina Ndoto.”
Bonyeza hapa usikilize. Hotuba ya pili ni ile ya “Nimefika Kileleni Mlimani” ambayo utaipata
ukibonyeza hapa.
Sun 15 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Mike Mushi, ambaye ndiye aliyeunda tovuti za
Uchaguzi Tanzania na
KikweteShein, ameunda tovuti inayotoa huduma kwa wanaotaka kuanzisha blogu zao bure. Bado ninaipitiapitia tovuti hii kuitazama inavyofanya kazi ili niweze kuifanyia marejeo.
Bonyeza hapa uitembelee.
Sun 15 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Jamaa wa gazeti la
Washington Post wana habari moja nimeisoma dakika hii kuhusu wapiganaji wa msituni Afrika wanavyotumia zana mpya za mawasiliano (blogu zikiwemo) na pia jinsi ambavyo mtandao wa tarakilishi unavyoweza kusaidia wapinzani wa serikali zenye tabia ya kufungia magazeti na redio. Binafsi nadhani habari hii ni nzuri ila mwandishi hakuifanyia utafiti wa kutosha.
Bonyeza hapa uisome.
Sat 14 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Blogu zitatapakaa nchi nzima. Ingawa itachukua muda, hii isituzuie tusianzishe safari hiyo sasa ya wananchi kuwa waandishi. Edison hataki kupitwa na mapinduzi haya ya zana za kupashana habari. Kwa kutumia blogu yake mpya anasema kuwa “saa ya ukombozi ni sasa, tusingoje kesho.” Isije ikawa huyu ni Mtikila amejipa jina jipya!
Mon 9 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Unakaribishwa kwa mikono miwili na bilauri ya maji na ndugu yetu Semkae Kilonzo. Anakukaribisha kwenye tovuti ya habari iitwayo Mbongo (ambapo utakutana na kona ya
Michuzi). Kilonzo kaniambia jambo moja la msingi sana. Anasema kuwa ni jambo la busara iwapo tutaunganisha nguvu za blogu na tovuti katika kujenga jamii mpya. Nadhani swali moja ambalo ndugu yetu hawaweza kuliepuka toka kwetu ni lugha inayotumika kwenye tovuti ya Mbongo. Kilonzo, mbona?
Mon 9 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni [6]
Bwaya kaniuliza swali swali zuri sana. Anataka kujua kama makala zangu (ambazo baadhi ziko ndani ya blogu hii, upande wa kuume chini ya picha yangu) na za wengine zinasomwa na Watanzania?
Bonyeza hapa usome aliyoandika.
Bofya hapa usome swali lake jingine kuhusu makala zangu.
Sijui nijibu swali lake la makala zinasomwa au la kwa upande gani. Ngoja niseme hivi: historia ya mabadiliko ya jamii duniani inaonyesha kuwa kundi dogo sana huwa ndio linaongoza mabadiliko hayo. Kwahiyo unapotaka kuleta mabadiliko unaweza kuwa umegusa watu wachache sana. Muhimu ni aina ya watu uliowafikia. Kwa mfano, walimu kama wewe. Kitendo cha kuwa wewe utakuja kuwa na kazi ya kutengeneza fikra na akili za vizazi vijavyo kimenifanya nifurahi sana kujua kuwa unasoma makala zangu. Hata kama nchi nzima ni wewe peke yake unazisoma, nitaridhika kabisa maana najua kuwa idadi ya watakaosoma makala zangu kupitia wewe (yaani kutokana na mafunzo na maarifa utakayowapa uliyoyapata kwenye makala zangu) ni wengi. Ninatazama jambo hili kwa misingi hiyo.
Lakini pia makala inaweza kusomwa na watu watatu, ila kwakuwa tunaishi kwenye jamii ambayo bado ina utamaduni wa gumzo mtaani, kwenye mabasi, majumbani,n.k., wako wengi ambao hawajaisoma hiyo makala lakini watapata yaliyoko kwenye makala hiyo kupitia wale watatu waliosoma.
Nakubaliana na Bwaya kuwa watu wetu hawapendi sana kusoma masuala nyeti. Wanataka habari nyepesi nyepesi. Lakini napenda tuwatambue wale wachache wenye moyo wa dhati wa kujisomea masuala mazito. Wapo na wanaongezeka. Wapo na wanawavuta wengine. Wapo na kila siku nasoma barua zao pepe wanazoniandikia wakishukuru, wakitaka ufafanuzi zaidi, wakitoa mapendekezo ya mada wanazotaka niandike, wakinikumbusha mada nilizowahi kusema kuwa nitaziandikia na kadhalika.
Kuna wanafunzi ambao wanasoma makala zangu na kujadili katika vilabu walivyoanzisha viitwavyo Jikomboe. Kuna walimu wanaotumia makala hizo kufundishia. Kuna wazazi wananiambia kuwa wanazijadili na familia zao. Wako vijana wameanzisha vikundi mtaani vya kusoma makala zangu kwa pamoja na kuzichanachana (kuzichambua). Wako ambao pia wameitikia wito ambao nimekuwa nautoa mara kwa mara kwa vijana kuunda makundi ya kujadili masuala nyeti ya katiba, utamaduni, historia, n.k. Kundi moja la vijana hawa limeniandikia hivi karibuni kunikumbusha jambo nililozungumzia katika makala moja niliyoandika miaka mitatu iliyopita!
Kwahiyo makala zangu (na zile za akina Boniphace na Jeff) wanaweza wasisome Watanzania wote, ila kumbuka kuwa wale wanaosoma wanaishi miongoni mwa Watanzania ambao kwa namna moja au nyingine wanakuwa kama wamezisoma kupitia mijadala, mabishano, gumzo, n.k., na wale waliozisoma.
Lakini narudia kusema kuwa watu wachache ndio huleta mabadiliko. Au niseme, watu wachache huongoza mabadiliko. Halafu niseme kuwa kama ninasomwa na mwalimu mtarajiwa Bwalya…ninajisikia kuwa kazi yangu sio bure. Hata wasiponisoma Watanzania wote. Mwalimu mtarajiwa mmoja anatosha kabisa.
Kuhusu utamaduni wa kujisomea, kweli hili ni tatizo kubwa nchini kwetu. Utatuzi wake unahitaji juhudi zetu binafsi kwenye familia, juhudi za watunga sera, taasisi, na serikali. Ukitaka kujenga utamaduni wa kujisomea wa nchi nzima utakata tamaa. Usianze na nchi. Anza na waliokuzunguka. Kama hujaweza kujenga utamaduni wa kujisomea wa watoto jirani zako au ndugu zako, huwezi kuanza kufikiria nchi. Utamaduni wa kujisomea wa nchi unaanza kujengwa majumbani, mitaani, nyumba kumikumi, n.k., kasha unakuja kuwa utamaduni wa taifa. Nakumbuka mimi kaka yangu alinisaidia sana kuwa na ari ya kujisomea. Nikiwa darasa la pili alinipeleka maktaba ya mkoa mjini Moshi akaniandikisha nikawa mwanachama. Toka wakati huo hadi leo nimekuwa “mgonjwa” wa kujisomea. Siku hizi nasoma kitabu zaidi ya kimoja kwa wakati mmoja (sina maana dakika hiyo hiyo).
Basi kitendo cha kaka yangu kunifanya nitambue utamu ulioko ndani ya kurasa za vitabu. Nikatumbukia kwenye kujisomea vitabu hadi ikafika wakati nikawa najifanya kuwa naenda shule kumbe nakwenda maktaba, shule siendi. Maktaba nilikuta vitabu ambavyo vilinigusa sana tofauti na vitabu vya shuleni. Masomo shuleni na vitabu tulivyokuwa tukitumia vilikuwa kama pombe ya mbege iliyotiwa maji. Masomo shuleni yalikuwa hayanipi changamoto. Sisemi kuwa huu ni mfano wa kuigwa ila nataka kuonyesha tu jinsi ambavyo nilijawa na hamasa ya kujisomea baada ya kaka yangu kunifungua macho. Toka wakati huo, ukitaka kunipata nenda maktaba au maduka ya vitabu. Utanikuta kwenye kona nimejikalia sakafuni ninachimba. Mji wowote ninaokwenda. Nchi yoyote ninayokwenda.
Kwahiyo tuna wajibu wa kuanza kubadili wale watu waliotuzunguka. Watoto wa jirani yako, watoto wa kaka yako, ndugu wa kuzaliwa tumbo moja, washikaji zako mtaani, n.k. Nikifanya hivyo, na yule akafanya hivyo, na wale nao, ndivyo tunabadili nchi.
Lakini pia tusidharau kabisa nguvu ya vyombo vya uongo (habari). Kuna nguvu nne duniani ambazo ndizo zinatufanya tuwe kama tulivyo. Nguvu hizi ndio zinatujengea mtazamo tulio nao kuhusu maisha: vyombo vya uongo/habari, dini, utamaduni-maarufu, na mfumo wa elimu.
Nje ya hapo hakuna kitu. Sasa tunaweza pia kutumia nguvu hizo hizo kupindua hali ilivyo na kujenga jamii mpya. Tunaweza kujenga hiyo jamii mpya hata tukifikia asilimia 0.5 ya Watanzania wote. Hasa walimu kama Bwalya. Fikiria mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi wangapi katika uhai wake. Sasa ukifikia mwalimu mmoja ni sawa na kufikia idadi ya wanafunzi atakaowafundisha. Na hao wanafunzi atakaowafundisha kuna ambao watakuwa walimu. Nao watafundisha wanafunzi wangapi? Na kuendelea.
Sun 8 Jan 2006
Na admin, Maudhui:
utamaduniToa Maoni
Nimesoma aliyoandika Chemi akitushauri kupenda urembo wa asili. Amezungumzia pia yale mashindano ya “miss world.” Sijui nitasema nini katika waraka huu ila najisikia kuandika kidogo kuhusu hili suala na mengine yanayohusiana nalo.
Bonyeza hapa usome Chemi aliyoandika Chemi. Chemi amehoji vigezo vinavyotumika kuchagua mwanamke mmoja kuwa ni mrembo kuliko wote duniani.Kitendo tu cha dunia yetu ya leo kutumia muda na fedha ili watu washindane kuwa nani mzuri zaidi kinahitaji kuchambuliwa kwa kina zaidi. Ukiingia ndani sana katika uchambuzi wa suala hili utakuta masuala ya mwili wa mwanamke kufanywa kama chombo cha biashara, burudani (kwa macho na tamaa za mwili za wanamume), na mwili huo kuwa ni matangazo ya biashara. Kuna itikadi inayofanya yote hayo. Katika itikadi hii mwanamke anakuwa ni chombo kinachojumuisha tu mwili (matiti, miguu, macho, nywele, rangi ya ngozi, kucha, tabasamu, mwendo, n.k.). Akili na nafsi havina nafasi. Mfumo wa ubepari ulivyo na uchu wa kufanya kila kitu kuwa bidhaa umehamisha ukandamizaji wa wanawake kwa kuupa sura ya kibiashara ambayo inaficha makucha ya ukandamizaji au kuyapa sura mpya inayofanana na ukombozi. Utaona kuwa mwanamke wa nchi za magharibi anadhani kuwa haki zake keshazipata na kuwa mwanamke anayekandamizwa ni yule aliyeko nchi za Kiislamu au Afrika wakati ambapo mwili wake (mwanamke huyo wa magharibi au yule wa Afrika anayetaka kujifanyakama huyo wa magharibi) umekuwa ni malighafi ya mfumo wa kibepari ambao bado unaongozwa na itikadi ya mfumo dume. Kama jinsi ambavyo mashirika ya umma yanavyobinafsishwa ndivyo mwili wa mwanamke unabinafishwa katika mfumo wa soko. Kinachobakia ni kuwa mwanamke anaonekana katika jamii kutokana na mwili wake na mwanaume anaonekana kutokana na anayofanya na fikra zake. Mtazamo huu unaotokana na kasumba ya mfumo dume ndio unafanya magazeti mengi kutoa safu maalum kwa waandishi au wanasafu wanaume. Na wanawake wachache wanaopewa safu wanatakiwa kuandika tu masuala ya haki za wanawake (ambapo kwa upande mmoja sio jambo baya lakini kunakuwa na mtazamo kuwa wanawake hawawezi kuongelea masuala mengine mazito kwenye jamii zaidi ya haki za wanawake).
Sasa turudi kwenye dhana kuwa dunia inaweza kumpata mwanamke mrembo duniani. Swali linakuja: mwanamke huyo atapatikanaje wakati ambapo vigezo vya urembo vinatofautiana katika mataifa na tamaduni mbalimbali? Wakati unawaza kuhusu swali hilo utajikuta ukisema kuwa tatizo sio tu vile vigezo vya kimagharibi vinavyochukuliwa kama ndio vigezo vya “dunia.” Utaanza kuhoji pia mantiki ya mwanamke kupita mbele ya wanaume na wanawake na nguo ya kuogelea (tena wakati akiwa haendi kuogelea!). Au kama nilivyosema hapo awali, mantiki nzima ya kushindana eti nani mzuri zaidi duniani. Tunarudi kwenye hoja ya mwanamke kuwa ni chombo. Kuwa bidhaa kama vile mche wa sabuni au gari. Chini ya msukumo wa soko na mfumo wa utamaduni-beberu unaoendesha mashindano kama “miss world” falsafa ya mtazamo kuwa mwanamke ni chombo cha burudani kwa mwanaume na pia ni kama bidhaa sokoni imejificha chini utamaduni-maarufu unaotufanya tuone kuwa mashindano hayo ni sehemu tu ya burudani inayofurahisha na kutufanya tufurahie maisha. Na wakati mwingine anayeshinda au kukaribia kushinda akiwa ni mtu wa kwetu, tunajenga imani nzito kabisa kuwa mashindano hayo ni tukio muhimu sana duniani. Utamaduni huu unafanya sehemu kubwa ya maisha kuwa ni kama vile tamthilia ndani ya luninga, maisha ni aina ya kujirusha katika bahari ya umagharibi. Utamaduni huu unafanya itikadi ya soko na utamaduni-beberu vinakuwa sio rahisi kuonekana.
Katika dunia hii ambayo maisha yanakuwa sawa na tamthilia ya kwenye luninga au kituko fulani, masuala ya maarifa, heshima ya utamaduni mseto, mijadala ya masuala ya msingi kwa wanadamu na jamii endelevu havina nafasi yoyote. Ndio maana inakuwa rahisi kwetu kufuatilia mashindano ya “miss” world kwa karibu zaidi kuliko
Mkutano wa Jamii-Habari uliofanyika Tunisia mwaka jana. Ndio maana ni rahisi kwetu kufuatilia kwa furaha na hamasa iliyokaribia kuwa uendawazimu vituko vya kwenye luninga kama Big Brother au habari za udaku magazetini. Ndio maana ni rahisi zaidi kujua nani kashinda mashindano ya “miss” Tanzania zaidi ya jina la mwanafunzi aliyepata maksi za juu kabisa kwenye mtihani wa kidato cha nne. Ndio maana ni rahisi kufuatilia kwa shauku nani atashinda “miss” world kuliko nani atapata tuzo ya Nobeli ya Amani.Kuna itikadi ndani ya haya yote. Itikadi hii ndio iliyofanya kifo cha Diana (aliyewahi kuwa mke wa mwana wa mfalme wa Uingereza, Charles) kuwa ni tukio kubwa kabisa kwa zaidi ya wiki moja huku kifo cha Mama Tereza (aliyefariki kipindi hicho hicho) kuwa ni habari za ukurasa wa ndani kwenye magazeti na habari za sekunde au dakika kadhaa kwenye luninga zilizokuwa zikirusha matangazo ya Diana asubuhi, mchana, jioni. Ni falsafa hii, tunaporudi kwenye suala la mwanamke, inafanya matangazo mengi ya biashara kuwa yana picha za wanawake maana miili yao ni kama kitega uchumi kwenye mfumo wa soko. Miili yao inaweza kuongeza idadi ya wateja wako, kama wanavyoamini watengeneza matangazo.
Turudi kwenye suala la Chemi la vigezo. Nani kasema kuwa dunia inaweza kufikia makubaliano juu ya uzuri wa mwanamke na hata wa mwanaume? Tafsiri na vigezo vya uzuri vinatokana na utamaduni, mazingira, na wakati. Tamaduni tofauti zina vigezo tofauti. Katika vigezo hivi hakuna kigezo bora zaidi ya kingine. Kwahiyo vigezo vya ulimbwende ni tofauti kati ya jamii na jamii ila sio kuwa kuna bora zaidi ya kingine maana kila kigezo kinakidhi mahitaji ya jamii yake. Vigezo vya jamii moja vinaweza visiwe na maana yoyote ukivihamisha kwenye jamii nyingine. Ila kigezo ni bora kwa yule aliyeko kwenye utamaduni uloizalisha kigezo kinachotumika. Inaweza ikatokea kutokana na sababu za utumwa kitamaduni na kifikra, jamii moja ikadhani kuwa vigezo vyake ni vya ovyo na kutaka kuiga vigezo vya wengine kama tunavyofanya sisi. Huu ni ugonjwa, tena mbaya sana lakini uzuri wake ni kuwa una dawa.
Kama mnavyojua, wazungu na waarabu kwenye jamii za mwambao wamekuwa wakitupeleka puta miaka na miaka. Puta hii wamemkuwa wakitumia mbinu na mifumo mbalimbali. Karibu ukitazama kila upande utaona putaputa hii ya wazungu na waarabu. Putaputa ya kutufanya tujisahau, tujione kuwa sisi si kitu, sisi ni washenzi, na wao ni bora na mfano wa kuigwa. Kwahiyo mila na desturi zao zinafaa kuigwa zote bila kujali kama zina faida au la. Dini zao ni za kweli na zetu ni za uongo. Manabii wao ni wa kweli na wa kwetu ni wa uongo.
Juzi nimeweka maoni kwenye picha ya baraza la mawaziri iliyoko kwenye blogu nzuri ya picha ya Michuzi. Katika picha hiyo mawaziri wetu walivyovaa ukikata vichwa vyao ukaulizwa useme mawaziri hao ni wa serikali ya nchi gani huwezi kujua. Hawaonyeshi kabisa kuguswa na hisia za utaifa na azma ya kutangaza na kuheshimu utamaduni wetu kupitia mavazi. Gadaffi, ambaye ni mwarabu, siku hizi anatangaza mavazi yetu zaidi ya sisi wenyewe. Maoni niliyotoa hapo ni haya:
Mavazi ya mawaziri wetu yanasema mengi kuhusu fikra zao, athari za elimu (maana sio unaona kuna madokta na maprofesa?), athari za msukumo wa utamaduni-maarufu wa magharibi na mustakabali wa utamaduni utaifa wetu. Hata waziri wa utamaduni naye pia?? Lakini sijui nashangaa nini wakati jina lake (Seif Khatib) linaonyesha amevaa begani mwake utamaduni wa akina nani
.
Utaona kuwa nilikuwa nashangaa kuwa hata waziri wa kulinda na kuendeleza utamaduni wetu hakuvaa vazi la utamaduni anaotakiwa kuulinda na kuuendeleza. Lakini katika kushangaa huko nikakuta najishangaa mwenyewe kwa kumshangaa waziri huyo kwani hata jina lake mwenyewe halijatoka katika utamaduni anaotakiwa kuulida na kuuendeleza. Kama jina lake tu ni la kuazima kwanini nitegemee avae mavazi ya kutukuza utamaduni usio na jina linalomfaa? Anaitwa Seif Khatib. Yaani waziri wetu wa utamaduni amebeba jina la kiarabu huku akiwa “anaendeleza na kulinda” utamaduni wetu. Ugonjwa huu, uzuri mmoja, unatibika. Tutautibu kwa njia yoyote ile. Bonyeza hapa uone picha hiyo kwa Michuzi.
Tutazame mifano zaidi ya gonjwa hili baya lenye dawa. Mifano: unaweza kwenda Rombo ndani ndani kabisa, ukakuta duka limepewa jina la kiingereza wakati ambapo mwenye duka na wateja wake hawafahamu kiingereza sawasawa. Tazama vikundi vya sanaa za maonyesho. Wakati vikundi hivi kazi yake, kama katiba zao zinavyosema, ni kuendeleza utamaduni wa Mtanzania na Mwafrika, majina yao ni ya kiingereza. Unakutana na Tanzania One Theatre, Muungano Cultural Troupe, OYA Theatre Group, Chemchem Art Group, Albino Revolution Cultural Troupe, Chang’ombe Youth Center, Nyunyusa Dancing Troupe, Roots and Kulture, n.k.
Kitendo cha kudai kuendeleza utamaduni wa Mtanzania au Mwafrika na kushindwa kabisa kupata jina la kundi toka katika utamaduni unaouendeleza ni kielelezo cha jinsi gani ugonjwa unaotokana na ukoloni mamboleo, ukoloni uchwara, na ubeberu wa kitamaduni ulivyotuathiri. Kwahiyo usishangae unapoona eti “miss” Afrika akiwa ni yule mrembo aliyechaguliwa na wazungu na kwa kutumia vigezo toka katika tamaduni zao na msukumo wa soko na itikadi za kibepari. Msukumo huu wa soko unatoka pande nyingi ikiwemo pamoja na makampuni ya nguo, vipodozi, kampuni za madawa, mahospitali (yanayofanya upasuaji wa kupunguza watu unene), makampuni ya matangazo, vyombo vya uongo (habari), n.k. Makampuni yote haya yanafaidika kwa namna moja au nyingine dunia inapokuza vizazi vyake kwa ndoto kuwa mwanamke mwembamba ndiye kilele cha uzuri. Kwa maneno mengine, mfumo wa kibeberu unafaidika sana na ugonjwa tulionao Waafrika. Na kama mnavyojua mfumo huu umekuwa ukitutumia na kutumia rasilimali zetu miaka na miaka huku ukijibadili kutokana na upepo wa wakati. Kulikuwa na wakati wa ukabaila, ubepari, na ubeberu. Mifumo hii ndio ilizalisha utumwa, ukoloni, ukoloni mamboeo, utandawizi (kuna tofauti kati ya utandawazi ambao ni mpana zaidi na utandawizi ambao ni mfumo unaoendeshwa na itikadi inayotaka dunia nzima kutawaliwa na kundi dogo la wanaume wa kizungu wanaoishi Ulaya na Marekani).
Niishie hapa. Siku kama leo ni zile siku ninapoandika bila kujua hasa ninaelekea wapi na nitaishia wapi. Kama nimezurura huku na kule bila kuishika mada sawasawa nisamehe. Huu ulikuwa ni mtiririko wa hisia na fikra. Kumbuka hii ni jumapili jioni na ninamsikiliza Bob Marley kwa sauti ya juu! Uhuru!
Sat 7 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni


Nikifundisha watoto (unajua tena samaki mkunje angali mbichi) maana ya Kwanzaa na umuhimu wake kwa watu wenye asili ya Afrika. Katika picha nyingine hiyo: huyo ni Barry akifungua somo la Kwanzaa kwa ngoma baada ya kutoa tambiko. Barry ni Mmarekani Mweusi ambaye amejifunza kupiga ngoma aina ya Djembe katika nchi ya Guinea, Afrika Magharibi. Mikono yake migumu kama tairi la nyuma la trekta aina ya Kubota (hivi Makubota yaliishiaga wapi?). Juu ya Kwanzaa soma niliyoandika hapo chini na pia
bonyeza hapa.
Bonyeza juu ya picha zenyewe uzione kwa karibu zaidi.
Sat 7 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni [5]

Nadhani baadhi mnafahamu kuwa mimi husherehekea sikukuu ya Kwanzaa. Moja ya mambo yanayofanywa wakati wa kusherehekea sikukuu hii inayoenzi maadili ya Kiafrika ni kuandaa meza ya Kwanzaa inayojumuisha vyakula, mishumaa, kikombe cha umoja, n.k. Unaona mwenye kwenye picha hii. Unaweza kuwa uliwahi kuona kanga hizi zikiuzwa pale Mnazi Mmoja. Meza hii niliandaa kwenye mhadhara ambao nilifundisha watoto weusi juu ya sikukuu hii na umuhimu wake kwao kama watu wenye asili ya Afrika. Baada ya tambiko, mafundisho, na ngoma, tulijumuika katika karamu. Neno karamu (ambalo liko katika wimbo wa Lionel Richie wa All Night Long) ndio hutumika wakati wa sikukuu ya Kwanzaa. Pia wakati wa sikukuu hii wamarekani weusi wanaojali Uafrika wao husalimiana “habari gani.” Kutegemea na maadili ya siku hiyo (yako saba) mtu atajibu. Kama ni siku ya ujima, ukimsalimu atajibu, “Ujima.”
Bonyeza hapa usome zaidi kuhusu Kwanzaa.
Bonyeza juu ya picha ili uzione vizuri zaidi.
Sat 7 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni [3]
Mkutano ndio unafikia mwisho. Umebaki muda wa mvinyo, kujuana zaidi na kubadilisha kadi. Mada tuliyokuwa tukiijadili awali ya matumizi ya podikasiti kufundishia unaweza kuiona kwa kubonyeza hapa. Kiungo nilichotoa hapo chini kinaweza kukupa shida kuipata. Hiki cha sasa kinakupeleka moja kwa moja. Unaweza kuona mfano wa kazi ya watoto wa shule waliyofanya kwa kutumia teknolojia ya podikasiti. Bonyeza hapa.
Kinachofuata sasa ni Jikomboe kupanuka. Kwa sasa Jikomboe, yaani blogu hii, ni kama gazeti pepe langu. Sasa itapanuka kuwa sio gazeti pepe tu bali redio pepe na luninga pepe (podikasiti ya video). Mwambieni Mengi akae chonjo, wanablogu tunaingilia nyanja ya habari kwa ari mpya na nguvu mpya (nakopa maneno yaliyotumika kutufanya tuamini kuwa tunajenga nchi mpya kwa sura zile zile au sura mpya zenye mtazamo kama zile sura za zamani).
Kama tusemavyo kule Moshi ninawaambia, “Watashaa.” Kama hujui maana yake muulize Mtafiti.
Sat 7 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Hivi sasa tunajadili matumizi ya teknolojia ya podikasiti kufundishia wanafunzi. Unaweza kusoma yote tunayojadili katika ukurasa huria wa “wiki” kwa kubonyeza hapa.
Kuna wahudhuriaji zaidi ya mia moja katika mkutano huu kuhusu podikasiti. Unadhani watu weusi tuko wangapi? Huwezi kuamini…Kama zama za mapinduzi ya viwanda zilitupita, tusikubali zama za maarifa na habari zitupite. Haiwezekani.
Sat 7 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Niko ndani ya ukumbi panaponyikia mkutano huu niliouzungumzia jana. Mara naona waraka pepe toka kwa Silvery Duttu akiniambia kuwa blogu yake iko tayari kutangazwa. Usisumbuke na kiingereza alichokiweka hapo, hii itakuwa blogu ya Kiswahili ili kuenzi lugha anayoitumia asubuhi, mchana, jioni. Bonyeza hapa umtembelee kumkaribisha.
Fri 6 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Moja ya sababu kubwa zilizonifanya nianze kublogu kwa Kiswahili ni imani kuwa ili dunia ya leo na kesho (ambayo ni ya zama za habari na maarifa) iwe yetu sote, tunapaswa kutumia teknolojia mpya za habari na mawasiliano kukuza, kuhifadhi, na kuendeleza lugha mbalimbali za wana dunia. Dunia yetu ina lugha kama 6000 hivi lakini ni lugha 12 tu ambazo zinatawala katika mtandao wa tarakilishi. Na katika hizo 12 ni lugha mbili au tatu ambazo hasa ndio zinatumika kueneza habari na maarifa. Wakati huo huo wataalamu wa lugha wanatangaza kila mwaka idadi ya lugha zinazokufa. Lugha inapokufa ni sawa na kuungua kwa moto kwa maktaba kubwa kuliko zote duniani. Unajua lugha, zaidi ya kuwa ni chombo cha mawasiliano, ni hazina au benki ya maarifa, mila, na utamaduni. Maarifa ya jamii huhifadhiwa kwenye lugha. Ili ujue dawa za mitishamba zinazotumiwa na Wa-Kahe, kwa mfano, unapaswa kujua Kikahe. Kikahe kikifa basi na elimu hiyo ya dawa inakufa (nimetumia mfano huu maana ni watu wachache wanajua kuwa Kikahe ni lugha na pia kwakuwa hii ni kati ya lugha ambazo zinapotea). Njia mojawapo ya kuhifadhi lugha ni kuitumia. Lakini ninalopenda kusisitiza hapa ni kuwa unapoitumia lugha au kitu chochote katika teknolojia pepe au elektroniki unakuwa umehifadhi milele na milele. Kublogu ni tofauti na kuchapisha kitabu ambapo kinaweza kuungua, kupotea, kuliwa na mchwa au panya, kuibiwa, n.k. Unapohifadhi mambo kwa njia za elektroniki au pepe unakuwa umehifadhi daima.
Kwahiyo visa tunavyoandika, mashairi, habari, maoni, n.k. vinachangia kuiweka lugha yetu katika mtandao pepe. Zaidi ya kuwa tunahifadhi tunayoandika na pia kuwezesha wengine kuyasoma wakati wowote, popote pale, tunaongeza idadi za lugha mtandaoni na hivyo kufanya mtandao usiwe tu ni mahali pa wale wenye kuzungumza Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kijapani, Kijerumani, n.k. Jitihada zetu ni moja ya jitihada za kufanya mtandao pepe kuwa wa kidemokrasia na unaojumuisha sauti za tamaduni na lugha mbalimbali. Kama mtandao pepe ni kijiji cha dunia, basi hicho kijiji kisiwe na lugha moja tu bali lugha mbalimbali za wanadunia.
Basi nilipoanza kublogu kwa Kiswahili nilikuwa nikisema jambo moja kwenye kila mahojiano niliyokuwa nikifanya. Wakati ule ilikuwa ni habari nzito. Eti, “kuna jamaa anablogu kwa lugha ya Kiafrika.” Walikuwa wakiniuliza kwanini ninablogu kwa Kiswahili ninawambia kuwa ninaendeleza kazi waliyokuwa wakiifanya akina Ngugi na Chinweizu. Ngugi, kama unakumbuka, aliandika kitabu chake kiitwacho “
Decolonising the African Mind.” na Chinweizu (Mloyi unakumbuka maandiko yake ya Negro negropobia?) aliandika Decolonising African Literature. Katika vitabu hivi walikuwa wakitutaka tuondoe ukoloni mamboleo na ukoloni uchwara katika akili zetu. Walikuwa wakizungumzia hasa fasihi andishi. Wakati ule mapinduzi ya teknolojia za mawasiliano yalikuwa hayajafika katika hatua tuliyoko hivi sasa. Kwahiyo wakati ule ukiongelea fasihi andishi unazungumzia vitabu. Hivi sasa tuna ulimwengu mpya ambao umetuletea maandishi pepe, fasihi pepe, riwaya pepe, n.k. Tuna mtandao pepe. Kinachofanyika hivi sasa ni muendelezo wa kazi za akina Ngugi na Chinweizu. Muendelezo huu, katika mahojiano, nilikuwa nikisema, “I am simply decolonising the Internet.”
Na hiyo ilikuwa ni moja ya sababu zilizonifanya nianza kunyonya titi la mama hata kama la mbwa kwa kutumia teknolojia ya blogu. Sasa sio mimi peke yangu au sisi wenyewe tunaoona umuhimu wa kuwa na lugha mbalimbali katika mtandao pepe.
Shirika la Sayansi, Elimu, na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) limetoa ripoti kuhusu matumizi ya lugha mbalimbali katika mtandao wa tarakilishi. Shirika hili linaamini kuwa dunia itakuwa bora zaidi pale ambapo lugha nyingi zaidi zitaanza kutumika katika mtandao wa tarakilishi. Katika ripoti yake limesema:
UNESCO has been emphasizing the concept of “knowledge societies”, which stresses plurality and diversity instead of a global uniformity in order to bridge the digital divide and to form an inclusive information society. An important theme of this concept is that of multilingualism for cultural diversity and participation for all the languages in cyberspace.
Kusoma ripoti nzima (katika pdf) bonyeza hapa.
Fri 6 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Kesho naenda mkutanoni katika chuo kikuu
hiki hapa. Mikutano haitakaa iishe dunia hii. Unadhani? Naanza mwaka wa Kirumi kwa mikutano. Mkutano huu ni tofauti kidogo na mikutano mingi tuliyoizoea. Kuna aina ya mikutano ambayo siku hizi inayoitwa “mikutano huria” au wakati mwingine wanatumia neno ambalo nimelishindwa kulitafsiri: unconference. Ni kama kusema vile “mkutano usio mkutano”! Mkutano huria ni mkutano ambao hauna watoa mada na wapokea mada. Wahudhuriaji wote ni watoa mada. Kila mmoja ni mshiriki. Kila mmoja anachukuliwa kuwa ni mtalaamu na ana jambo la kusema au kuchangia. Hii ni tofautina mikutano ambayo kunakuwa na wasikilizaji wanaoketi kimya huku “mtaalamu” au “msomi” “akiwaelimisha” juu ya jambo fulani.
Katika mkutano huria, wanaohudhuria ndio wanaoamua nini kijadiliwe au mada zipi ndio muhimu. Na ndivyo mkutano ninaohudhuria kesho ulivyoandaliwa.
Bonyeza hapa usoma kuhusu mikutano huria. Mkutano huria ninaodhudhuria kesho unahusu masuala ya podikasiti. Soma kwa kifupi kuhusu
podikasiti hapa. Mkutano unaitwa Podcastercon 2006.
Bonyeza hapa usome tovuti kuhusu mkutano huo na
hapa usome blogu ya mkutano huo.
Nitaandika zaidi juu ya mkutano huo nikiwa mkutanoni hapo.
Fri 6 Jan 2006
Na , Maudhui: Uncategorized
Toa Maoni
Binyavanga Wainaina ameandika makala moja nzuri sana ambayo inatumia kejeli kutazama jinsi ambavyo watu weupe wanavyolitazama bara la Afrika. Katika makala hii anatoa ushauri wa jinsi ya kuandika habari za Afrika. Lakini, kama nilivyosema hapo awali, ushauri wenyewe ni kejeli fulani hivi.
Bonyeza hapa usome makala yenyewe.
Binyavanga ni mwanzilishi wa jarida la fasihi nchini Kenya liitwalo Kwani?, ambalo unaweza kulisoma kwa
kubofya hapa. Pia unaweza kusoma zaidi juu yake kwa
kubonyeza hapa.
— Next Page »