Kasri ametushtua kuwa tumelala. Mjadala umepoteza mwelekeo. Anasema zile jitihada za kubunga bongo kupata neno muafala la Kiswahili la blogu ni vyema zifikie mwisho. Jitihada hizi hadi sasa zimetuletea maneno haya: DURU, KASIRI, LIPULI,VUGA, DONDOO, LIPULI, VUGA, UWANJA WA FIKRA KOMAVU, GAZETI TANDO, NGWANGA, BAWAZI, TANDO PEPE na DIMBA. Bonyeza hapa uende uliko mjadala huo. Aliyoandika Kasri yasome kwa kubofya hapa. Pia soma maoni ya wasomaji wake. (bonyeza hapo chini umalize kusoma habari hii.)
February 2006
Tue 21 Feb 2006
Mjadala wa neno muafaka la blogu: je blogu ni gazeti?
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: teknolojia , bloguToa Maoni [22]
Sun 19 Feb 2006
Waraka toka kwa Mari-Djata Amadi kwaa Atsiaya
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: utamaduni , lughaToa Maoni [5]
Kuna wakati wasomaji fulani wanaandika mambo ambayo sio sawa mtu mmoja kuyasoma mwenyewe. Mari-Djata ni msomaji toka Kenya. Pamoja na mambo mengine anajihusisha na shirika la Drama Tool. Nilipoamua kuwa nataka kutoa maoni yake bloguni niliamua kumuuliza kwanza kama ana pingamizi. Alisema kuwa hana pingamizi lolote. Nikamshauri aanze kublogu. Akajibu kuwa ataanzisha blogu ili aweze “kutapika kigunzi…” Soma alivyosema mwenyewe:
Ninaahidi kwamba nitaanzisha blogu yangu mwenyewe hivi karibuni ili niweze kukitapika hiki kigunzi kilichonisakama. Pengine, kama yule mhubiri wa jangwani tunayeambiwa kwenye biblia, itasadifu kwamba angalau vichwa kadha viziandae sumaku na koleo zao kuyanyaka machache na vile vile kuongezea rutuba ya akili zetu sisi wenyewe.
Haya, waraka wa Mari-Djata ambao nimependa muusome wote huu hapa:
Kaka Macha,
Mimi ni Mkenya, na ninapenda na kujivunia sana lugha zetu na hasa, lugha ya Kiswahili ambayo inatuunganisha sisi kama Waafrika; ikiwa yenyewe ni lugha yetu.
Nilikumbana na makala yako kwa mara ya kwanza katika gazeti fulani la Tanzania. Nafikiri ni gazeti la Mwananchi. Nilifurahishwa mno na maoni yako kuhusu matukio ya ulimwnguni, hasa kuhusu kuhusika kwa dini na viongozi wake katika vita ulimwenguni. Baadaye, nilitafuta kwenye mtandao na nika’vumbua’ (samahani kwa kukumbusha msamiati pendwa wa wakoloni kwani waliwavumbua hata Wahehe) blogu lako ambako nimekuwa nikifaidi uhondo tele.
Majina yangu ni Mari-Djata Amadi kwaa Atsiaya. Nilipozaliwa, nilipewa jina kubwa na zito la Kiyahudi. Baadaye, nilighadhabika nilipoona kwamba hakuna mtu aliyekuwa na hasira tosha kuhusu yale ambayo tumetendewa tangu mababu zetu hadi leo. Niliamua kufarakana na minyororo ya jina zito ambalo kumbukumbu ya torati ilimtwika yule aliyenitangulia, ambaye alidanganywa kufumba macho na kutoa raslimali yangu kwa aliyenikandamiza na kusema amen! Basi watu wamekuwa wakiniuliza : Na jina lako la Kizungu ni nani? Nashangaa ni tangu lini ikawa lazima kwa Mwafrika kuwa na jina la Kizungu. Wengine nao wanauliza: Na jina lako la Kikristo ni nani? Nashangaa ni kuanzia lini dini ya Kikristo ikawa ni dini yetu kwa kawaida? Wengine wanataka kujua kama mimi ni Amadi Muislamu, na swali langu ni lilo hilo.
Nilichangamka mno niliposoma makala yako kuhusu majina na dini. Ni kama tulikaa nawe kilingeni mahali na kula njama kutoa jibu hilo!
Kwa ufupi ni kwamba, ninatoka katika jamii ambayo imekengeuka mno. Mkenya ni shabiki mkereketwa katika kuukubali na kuusherehekea ukoloni na viambata vyake. Nakumbuka nikienda chuo kikuu na kukataa kujifunza masomo mengine na kuchagua Kiswahili. Wengi walicheka sana na kuniona duni kwani kwao, Kiswahili ni lugha ya vitongojini, miongoni mwa wauza kashata na kaimati. Si lugha ya wasomi, si lugha ambayo inaweza kujadili falsafa na mambo ya kina kama vile asili na mstakabali wa mwanadamu. Usidhani mawazo yanayosheheniwa na misahafu, ambayo ni falsafa ya kina. Usijali ushairi mzito kama vile Rasil’Ghuli, Al-Ghuli na kadhalika. Usijali mtiririko wa mawazo ambao tulionyeshwa mfano mzuri na Mwalimu Nyerere….
Kaka, siwezi kulitoa jasho la moyo wangu lote na likaisha lote leo. Tuendelee kutekerenyana.
Mimiwako.
Amadi.
Huo ndio waraka wa Mari-Djata. Makala kuhusu majina anayoizungumzia niliiandika huko nyuma. Unaweza kuisoma kwa kubonyeza hapa.
Sat 18 Feb 2006
Ili uelewe ninazungumzia nini, inakupasa usome kwenza mambo niliyoandika hapo chini kwenye kichwa cha habari: Ipi bora kati ya Blogger na Wordpress? Unaweza kushuka hapo chini ili usome au unaweza kubonyeza hapa. Ninayoandika sasa ni muendelezo wa mada hiyo.
Mwanablogu anayeandika kwa Gikuyu, Gatua wa Mbugwa ameniuliza swali kuhusu kiasi cha malipo ya kutumia Wordpress. Huduma ya Wordpress inapatikana na bure na pia kwa kulipia. Huduma ya bure kama ilivyo Blogger unaipata kwa kubonyeza hapa. Huduma ya kulipia gharama zake zitategemea unatumia kampuni gani kuhifadhi blogu yako. Wordpress wana orodha ya huduma ambazo kwa mawazo yao wanaamini kuwa ni nzuri. Bonyeza hapa uone huduma hizo. Huduma hiyo ya kulipia taarifa zake bonyeza hapa. Kumbuka kuwa kama una nia ya kutumia Wordpress ya kulipia sio lazima utumie kampuni zilizoorodheshwa na Wordpress. Moja ya faida ya kutumia huduma za kulipia ni kuwa utaweza kupata anuani unayotaka ambayo haina neno “wordpress.” Inaweza kuwa www.sinadinizakuja.com. Au chochote kile.
Jambo jingine muhimu ambalo sikulifafanua vizuri ni kuhusu Wordpress kuwa ni programu huria. Kwakuwa ni programu huria, ina maana kuwa kuna watu maelfu wanaoikarabati na kuijenga programu hii kwa kujitolea. Programu kama ya Blogger ambayo inalindwa na hatimiliki ni vigumu kwa watumiaji kuifanyia mabadiliko. Mabadiliko yoyote lazima yapitie kwenye mkono wa wafanyakazi wa wanaoimiliki. Kwakuwa Wordpress ni programu huria inakuwa rahisi kwa mwanateknolojia kama Chris aliyeamua kujiunga nasi kujenga toleo la Wordpress la kiswahili. Soma aliyoandika Chris kuhusu mradi huo kwa kubonyeza hapa. Tukitaka toleo la kiswahili la Blogger hatuwezi kufanya chochote hadi wenye kampuni waamue kuwa wanatengeneza toleo la kiswahili. Nimewahi kuwaandikia mara nyingi kuhusu toleo la kiswahili lakini wala hawakujibu. Nikakutana na bwana anayeendesha mradi wa Google Eearth nikamgusia akasema atawaambia lakini wapi. Kwenye Wordpress hatuhitaji ruhusu ya mtoto wa mtu kufanya hivyo. Ndio maana ninawaambieni kuwa kifalsafa programu huria ninazipenda sana.
Halafu ningependa kujilinda kwa kusema haya: teknolojia mpya za habari, maarifa, na mawasiliano zinabadilika haraka mno. Niliyoandika hapa leo huenda kesho yakawa yamebadilika. Kwahivyo kasoro nilizotoa hapo chini za Wordpress au Blogger usishangae iwapo kesho utakuwa zimerekebishwa. Niliyosema ni hali iliyopo siku ya leo ninapoandika haya.
Sat 18 Feb 2006
Kwanza kabisa ngoja niseme jambo kuhusu blogu ya Mongi. Mongi ni kati ya wanablogu Tanzania wanaoblogu kwa kiingereza. Baadhi ya watu wanadhani kuwa wanablogu wa kiswahili tuna ubaya na kiingereza. Kiingereza kama zilivyo lugha nyingine duniani kina nafasi na umuhimu wake. Mongi yuko kwenye mtandao wa wataalamu wa kilimo duniani. Blogu yake ni sehemu ya mtandao wa wataalamu hawa wa kupeana taarifa. Katika blogu zote za Watanzania, blogu ya Mongi ndio blogu ya kwanza ya kifani. Blogu zetu nyingi tunaandika jambo lolote tunaloona linafaa kuandikwa. Mongi yeye anaandika kuhusu kilimo kwa ajili ya mtandao alionao na wenzake na pia watu wengine wenye kufuatilia mambo haya. Kwahiyo tunaona kuwa blogu zinaweza kutumiwa kujenga mtandao na kuwa kisima cha maarifa, taarifa, na habari kwa manufaa ya fani au taaluma fulani. Bonyeza hapa uende kwenye blogu ya Mongi. Nadhani mtu mwingine ambaye anakuja na blogu ya kifani ni Paul Kihwelo, mkuu wa kitivo cha sheria Chuo Kikuu Huria Tanzania na msimamizi wa mradi wa Creative Commons Tanzania. Paul yeye atakuwa anaandika kuhusu sheria. (bonyeza hapo chini umalize kusoma habari hii.)
Sasa niseme jambo hasa nililotaka kusema. Majuzi niliandika kuhusu kuhamia kwenye programu huria ya Wordpress toka kwenye programu ambayo wengi tunatumia ya Blogger. Soma hapa niliyoandika. Baada ya kuandika hayo, Mongi aliingia kwenye blogu na kutoa maoni yake ambapo aliuliza maswali ya msingi katika suala zima la Wordpress na Blogger. Haya ndio aliyoandika:
Nimekuwa naijaribu wordpress kwa nia ya kujiunga. Ni huduma nzuri na yenye mvuto. Hata hivyo huduma hii inatupunja watu ambao ni vigumu kulipia. Huduma hii hairuhusu mwenye blogu asiyelipia kuona na kuhariri template yake kama ilivyo kwa blogger. Ni lazima kununua domain ili kupata ruhusa hiyo. Sijui kama niko sahihi, lakini ndilo nililogundua.
Uamuzi wangu wa kujiunga na Wordpress ulikuwa mgumu sana. Toka nilipoanza kublogu mwaka 2004 nilikuwa natumia Blogger hadi nilipohama hivi majuzi. Karibu wanablogu wote wa Tanzania wanatumia Blogger. Blogger kwangu ilikuwa sio tu chombo ninachotumia kublogu bali ilikuwa ni kama jumuiya. Kwakuwa tumekuwa tukitumia programu moja imekuwa ni rahisi mara kwa mara kuulizana maswali kunapokuwa na tatizo au kupeana ushauri. Utashangaa kuwa uamuzi wa kuhama nimekuwa nikiuahirisha karibu mwaka. Mwishoni mwa mwaka jana nilihamia Typepad kwa dakika chache kisha nikarudi Blogger. Kama uliwahi kuja kwenye blogu yangu ya zamani, hii hapa, ukakuta maruweruwe, basi ndio wakati huo nilikuwa nahamisha. Nikarudi. Nilijisikia kama vile ninawakimbia ndugu zangu. Nikahisi upweke fulani hivi.
Sasa kwanini hivi sasa nimeamua kuhama? Ili kujibu swali hili itabidi nijibu swali la Mongi na mengine ambayo hayajaulizwa. Mongi amesema jambo moja ambalo ni kweli. Kama utatumia Wordpress ile ambayo ni ya bure, hutakuwa na uwezo wa kuingia ndani ya templeti yako kama ambavyo unaweza kufanya ndani ya Blogger. Lakini ukiwa na Wordpress ya kulipia unaweza kufanya hilo. Mongi hujakosea.
Wordpress na Blogger zote zina faida zake na pia zina kasoro zake. Uamuzi wa kutumia programu ipi ni uamuzi wa binafsi ambao inabidi uufanye baada ya kutazama tofauti na ulinganifu uliopo kati ya programu hizi mbili. Hatua ya mwanzo unayoweza kufanya ili kuweza kutoa uamuzi sahihi ni kufanya majaribio ya kuhamia Wordpress kama alivyofanya Idya wa Pambazuko. Ukihamisha mambo yako toka Blogger kwenda Wordpress, hutapoteza blogu yako ya zamani. Bonyeza hapa utaona blogu ya Idya iliyoko Blogger na bofya hapa uone blogu yake iliyoko Wordpress.
Majaribio haya yatakuwezesha kuingia ndani ya Wordpress kuona ilivyo na inavyofanya kazi. Unaweza kusoma mwongozo nilioandika wa jinsi ya kuhamisha mambo yako toka Blogger (bila kuiua blogu yako hiyo) kwenda Wordpress. Bonyeza hapa. Kwa kifupi nitachambua tofauti zilizoko kati ya Blogger na Wordpress. Tofauti hizi hasa ndizo zilizonifanya kuhama.
Kwanza kabisa ni suala la upangaji wa mambo uliyoandika katika makundi ya kimaudhui. Kwa mtu anayepanga kublogu kwa muda mrefu suala hili ni la muhimu sana. Kwa mfano kukawa na mwanafunzi anafanya utafiti kuhusu masuala ya utamaduni. Akaja kwenye blogu yako, tusema mwaka 2010, ni vipi ataweza kujua yaliko mambo uliyoandika kuhusu utamaduni? Au msomaji akawa kwenye blogu ya Mwandani akataka kusoma habari alizoandika kuhusu ubaguzi wa rangi, tuseme miaka mitatu toka sasa. Ni vipi ataweza kujua habari kuhusu ubaguzi wa rangi, ambazo Nambiza huwa anaziandika vizuri sana, ziko wapi? Itabidi atafute habari kwa kubahatisha, kwa kubonyeza miezi kwenye kisehemu cha nyaraka. Zaidi ya Wordpress kukupa uwezo wa kupanga mambo kimaudhui, kuna kisanduku cha kusaka habari ambazo umeandika. Kwa mfano, ukiwa unataka kutafuta habari nilizowahi kuandika kuhusu Mwalimu Nyerere, unachofanya ni kuandika jina lake kwenye hicho kisanduku na kuzisaka habari zote nilizoandika kuhusu Nyerere. Hebu fikiria uwe na kitabu cha kurasa maelfu ambacho hakina ukurasa wa “Yaliyomo.”
Tuangalie blogu ya Michuzi. Ukiwa unaandika habari kuhusu kampeni za uchaguzi, ukataka kutumia picha toka kwa Michuzi. Ukienda kwenye blogu yake utajuaje ziliko picha zinazohusu kampeni za uchaguzi? Au ukataka picha za viongozi wa Afrika, utajuaje ziliko picha hizo? Labda uwe unakumbuka siku na mwezi na mwaka ambao aliziweka picha hizo kwenye blogu yake. Njia pekee ya kuweza kupanga picha hizo kwa nia ambayo wasomaji, watafiti, n.k. wataweza kuzipata ni kuziweka katika makundi ya kimaudhui. Michuzi hana namna…tunamjengea blogu itakayompa uwezo wa kupanga picha zake katika maudhui. Blogu ya Michuzi ni kumbukumbu/historia ya taifa kwa picha. Watoto wa vitukuu vyetu watakuja kuitumia kujua historia yao. Wakati huo blogu itakuwa kama vile yale madaftari yenye “tebo” ukurasa wa nyuma, yaani itakuwa ni kitu cha kawaida.
Ingawa ni kweli kuwa ukitumia Wordpress ya bure huwezi kuingia ndani ya templeti yako, mambo mengi ambayo unayafanya kwenye Blogger kwa kuingia kwenye templeti yako unaweza kuyafanya kwenye Wordpress bila kuingia kwenye templeti yako. Kwa mfano, mambo kama viuongo, maudhui, taarifa juu yako, anuani yako, n.k. unaweza kuvifanya ingawa huingii kwenye templeti. Faida mojawapo ni kuwa huna haja ya kujua HTML au CSS, lugha zinazotumika kuunda tovuti. Kwenye blogger, kwakuwa unaingia kwenye templeti ambayo iko katika lugha ya HTML na CSS, unahitaji uwe na utaalamu fulani wa masuala hayo. Lakini sio vigumu kujifunza.
Kwenye Blogger kuna kitu kinaitwa “recover post” ambacho kinakusaidia kuweza kupata mambo uliyoandika yakafutika kwa bahati mbaya. Huwezi kufanya hivyo kwenye Wordpress. Kwenye Wordpress kuna urahisi wa kupata anuani ya habari mtu aliyoandika. Kwa mfano, kama unataka kupata kiungo cha habari hii unayosoma hivi sasa, bonyeza juu ya kichwa cha habari hii hapo juu utapelekwa kwenye ukurasa wenye anuani ya habari hii. Huwezi kufanya hivi kwenye Blogger. Hii inafanya mara nyingi watu wanapozungumzia habari fulani badala ya kuweka kiungo cha habari yenyewe wanaweka kiungo cha blogu nzima ambapo ukifika hapo inakupasa uanze kutafuta habari wanayoizungumzia iko wapi. Na kama hakuna mpangilio wa kimaudhui, unaweza kukesha.
Ukiingia kwenye Wordpress utaona kuwa hakuna ukurasa wa msaada ulio mzuri kama ilivyo kwenye Blogger, kupitia: blogger knowledge, blogger help, na FAQ (maswali ya mara ka mara). Hata hivyo watumiaji wa Wordpress ni kama jumuiya, hivyo wengi huwa wako tayari kusaidia wengine. Uzuri ni kuwa watumiaji wengi wa Wordpress ni wataalamu wa masuala ya tarakilishi. Lakini ukurasa wa msaada kwenye Blogger umesaidia sana watu wengi nikiwemo mimi.
Kuna kitu kinaitwa “trackback” na “ping.” Hizi ni teknolojia zinazowezesha mawasiliano kati ya blogu na blogu. Wordpress ina huduma nzuri sana ya “trackback” na “ping.” Tunaweza kusema kuwa “trackback” ni mfumo wa kuzitaarifu blogu kuwa umezitaja kwenye habari au jambo uliloandika. Kwenye Wordpress baada ya kuandika habari yako kuna kisanduku cha kuweka blogu ambazo umezitaja kwenye habari hiyo, blogu hizo zitatumiwa habari kuwa umezitaja. Bonyeza hapa usome kuhusu teknolojia hizi kwa maelezo rahisi.
Online Journalism Review wana jedwali ambalo linaweza kukusaidia kuona tofauti kati ya programu mbalimbali za kublogu zikiwemo Blogger na Wordpress. Bonyeza hapa uone jedwali hilo.
Nimalize kwa kusema kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu kutumia programu gani ni wako mwenyewe kutegemea na malengo na dhumuni lako la kublogu. Malengo yako ndio yatakupa uwezo wa kujua programu gani itakusaidia kuyafikia. Unaweza kushawishika kwa sababu moja au sababu kadhaa kutumia programu fulani. Zinaweza kuwa ni sababu za kiufundi, kisura, kiteknolojia zitakazokusaidia kuamua. Zinaweza pia kuwa sababu za kifalsafa. Mimi, kwa mfano, moja ya sababu zilizonifanya kuhamia Wordpress ni kuwa kifalsafa ninaunga mkono programu huria (programu hizi ziko wazi kwa mtu yeyote kuziendeleza tofauti na programu kama za Microsoft ambazo zimezungushiwa ukuta wa sheria ya hatimiliki). Sababu hii ndio inanifanya siku hizi nitumie Mozila Firefox badala ya Internet Explorer na Wikipedia badala ya Encyclopaedia kama Britannica. Programu huria ni aina fulani ya ujamaa. Hii inaendana sana na falsafa za Kiafrika: ujamaa, utu, ubuntu, n.k. Nategemea Maitha ataweza kutoa maoni yake mawili matatu kuhusu mjadala huu.
Wed 15 Feb 2006
Mapema leo niliandika kuhusu mwongozo ambao nimeuandika wa kusaidia wanablogu wenye nia ya kuhama toka Blogger kuingia Wordpress ambayo ni programu huria na yenye vionjo vingi na bora zaidi ya Blogger. Kama hujasoma niliyoandika, bonyeza hapa. Mwongozo wenyewe wa jinsi ya kuhamia Wordpress unapatikana kwenye blogu maalum ya kutoa elimu, taarifa, na maarifa kwa wanablogu na watu wengine wanaotaka kuwa wanablogu. Bonyeza hapa uusome. Ninachotaka kukwambia hasa ni kuwa safari ya kuhamia Wordpress imeanza tayari. Mwanablogu Idya wa Pambazuko tayari amehamia Wordpress na utaona habari zake zimeanza kupangwa kimaudhui. Suala hili la upangaji wa habari kimaudhui ni la muhimu sana. Ukitembelea utaona kuwa alichofanya sio kuanzisha blogu mpya bali kuhamisha ile ya zamani. Bonyeza hapa.
Wed 15 Feb 2006
Majuzi nilihama rasmi toka huduma ya Blogger na kuanza kutumia huduma ya programu huria ya Wordpress. Wordpress ina utamu wake. Mshairi anasema kuwa Wordpress inafanya shughuli ya kublogu kuwa tamu zaidi. Nakubaliana naye. Nilipokuwa nawakaribisha hapa kwenye blogu yangu mpya (ni mpya lakini mambo niliyoandika nikiwa http://jikomboe.blogspot.com yapo hapa) niliongelea baadhi ya sababu zilizonifanya kuhamia kwenye Wordpress. Blogger ina kero zake na watengenezaji wake wanachukua muda mrefu sana kuipa zana zinazoendana na mabadiliko ya nyanja hii. Kama hukusoma niliyoandika wakati nikiwakaribisheni, bonyeza hapa.
Nimemaliza kupandisha mwongozo wa jinsi ya kuhama toka Blogger kwenda Wordpress kwa kuhamisha mambo yote uliyowahi kuandika kwenye Blogger. Katika mwongozo huo nimegusia sababu kadhaa ambazo zinaweza kukushawishi uingie Wordpress. Ukiwa na swali lolote unaweza kuniuliza. Hutajuta kamwe kuingia Wordpress. Utakapohamisha blogu yako toka Blogger kuingia Wordpress, blogu yako ya zamani bado itakuwepo pale pale kama ilivyo blogu yangu ya zamani. Itaendelea kubaki pale kama historia.
Ukiingia wordpress, anuani yako itamalizikia na maneno: wordpress.com. Ukitaka kuwa na jina la blogu yako na neno .com, bila neno “wordpress,” hapo itakupasa kuwa na huduma ya kulipia. Itabidi usajili anuani yako na pia ulipie kampuni ambayo itakuwa inahifadhi blogu yako. Kama uko Tanzania, inaweza kuwa vigumu maana itakupasa kulipa kwa kutumia kadi kama Visa au Mastercard, ambazo wananchi wengi hawana. Sidhani kama kuna haja kubwa ya kuingia gharama. Kwahiyo kama utapenda au una nia ya kuhama hapo baadaye, soma mwongozo huo kwa kubonyeza hapa.
Tue 14 Feb 2006
Majuzi niliandika kuhusu watwawala wetu kuapa kwa vitabu viwili, kimoja kinaaminika kuwa ni kitakatifu na kingine kitukufu (biblia na kurani). Niliandika kuhoji kitendo hicho cha watu wanaojiita wakristo na waislamu kuapa wakati mungu wao anawakataza. Kama hukusoma niliyoandika, bonyeza hapa usome ili uelewe ninazungumzia nini. Ukishasoma, endelea kusoma ninayoandika leo.
Baada ya kuandika, Egidio, mwanablogu wa Pilikapilika Vyuo Vikuu, alitoa maoni yake kufuatia niliyoandika. Haya ndio aliyosema:
Katika mambo ambayo mimi binafsi nimekuwa nikihoji ni kuhusu haya mambo haya ya dini.Juzi pale chuoni watu baada kuona makala ile watu tulianza kuichambua. Watu wengi tumekuwa waoga kuhoji haya mambo ya dini kwa kuwaogopa hawa makasisi wetu. Katika mjadala ule ilifikia kipindi baada ya kuotoa somo kwa kutumia kitabu kitakatifu wengi walikubali kweli tupelekwa pelekwa tu lakini wanasema wenyewe wanafuata dini walizowakutanazo wazazi wao.
Sentensi ya mwisho ndio hasa nimeamka nayo leo. Egidio anasema kuwa watu wengi wanafuata dini walizonazo kwakuwa ndizo dini za wazazi wao. Najua leo sio mara ya kwanza kwako kusikia kuwa wengi wetu dini zetu tunazo kwakuwa ni za wazazi wetu. Huenda hata wewe uko katika kundi hilo. Kuna watu ambao wanaamini kuwa ukiacha kufuata dini za wazazi wako utakuwa umeasi au kudharau wazazi wako. Mimi nilipoachana na dini ya wazazi wangu, watu wengi wakiwemo makasisi, marafiki, na ndugu waliniuliza kwanini ninaasi wazazi wangu. Kwanini ninaacha dini niliyokuzwa na wazazi wangu. Maswali haya yalinionyesha kuwa watu hao wanachukulia dini kuwa ni kama maumbile vile. Ni sawa na kurithi maumbile au tabia za wazazi wako. Hoja hii ya kufuata dini ya wazazi inafanya maamuzi kuhudu dini kuwa ni suala lisilo chini ya uwezo wetu maana sisi hatuchagui wazazi wetu. Unajikuta umezaliwa na wazazi wako na unakutana wan dini fulani, unachopaswa ni kuifuata.
Kama binadamu tunapaswa kufuata dini za wazazi wetu, wazazi wa wazazi wetu hawakufuata dini za wazazi wao? Kwanini waliziacha na kufuata dini zilizoletwa na waarabu wakiwa na mijeledi, majambia na kurani na wazungu wakiwa na bunduki na biblia? Au huu utamaduni wa “kufuata dini ya wazazi” unatakiwa kufuatwa tu pale dini ya wazazi hao inapokuwa sio ya Kiafrika bali toka kwa Waarabu na wazungu? Sijui kama ninajieleza vizuri. Ninauliza: kama binadamu tunapaswa kufuata dini ya wazazi wetu, na kama kutofuata dini ya wazazi ni uasi na ni jambo lililofaa, je uasi huo si waliufanya wazazi wa wazazi wetu walipoacha kufuata dini za wazazi wao na kufuata dini za wakoloni, wamisionari, na wafanyabiashara ya utumwa?
Nimewaambia kuwa watu huniuliza kwanini nimeasi. Jibu langu ni kuwa sijaasi bali ninarekebisha uasi ambao ulifanywa na mababu zetu. Wao ndio waliasi. Waliasi kwa kuacha kufuata imani, mila, na desturi ambao zinatufanya sisi Waafrika kuwa Waafrika. Waliasi kwa kukubali kuwa utamaduni waliokuwa wakifuata wazazi wao ni wa kishenzi. Manabii wetu ni wa uongo. Maandiko na fasihi simulizi zetu kuhusu dini, uumbaji, mungu, n.k. sio ujumbe toka kwa mungu. Utamaduni wa kuja ndio ustaarabu na manabii na misahafu yao ndio yenye maneno ya mungu. Kawaida ninamaliza mazungumzo na watu hao wanaonishutumu kuasi kwa kuwaambia kuwa wasiniulize mimi kwanini ninaasi bali wawaulize wazazi wetu kwanini waliasi mafundisho na njia walizofuata mababu zetu na kufuata mafundisho ya mababu toka Ulaya na Mashariki ya Kati?
Ngoja nitazame mafundisho na historia kutazama kwa undani hoja hii ya kuwa tunapaswa kufuata dini za wazazi wetu. Ngoja nitumie mafundisho ya dini ambazo wengi wenu mmezibeba: uislamu na ukristo. Hivi Yesu/Isa/Yashua alimaanisha nini aliposema kuwa kila mtu atabeba mzigo wake mwenyewe? Mbona hakusema kuwa tutabeba mizigo ya wazazi wetu? Alisema kuwa siku ya mwisho kila mtu atajibu alivyoishi maisha yake. Kama ulichagua dini ya wazazi wako, na dini hiyo ikawa ni ya uongo (ninatoa tu mfano maana suala la dini ya uongo na kweli ni hoja nyingine ndefu sana), je siku hiyo ya hukumu utasemehewa maana uamuzi wa kuwa katika dini hiyo walikuwa nao wazazi wako na sio wewe mwenyewe?
Kwa maneno mengine, kama unaamini kuhusu hukumu ya moto wa milele, je kwanini watu wahukumiwe kwa kufuata dini walizonazo? Kwa mfano, kama mimi ni mkatoliki kwakuwa wazazi wangu ni wakatoliki, na ukatoliki sio dini ya kweli mbele ya mungu (huu ni mfano tu), je kuna sababu yote ya mungu kuniadhibu kwa kuwa kwenye dini ya uongo? Kwanini aniadhibu wakati nilichofanya ni kufuata dini ya wazazi wangu “kama ambavyo binadamu tunavyopasa kufanya?” Si tunatakiwa kufuata dini za wazazi?
Nikiwapa watu mfano huu wananiambia kuwa mungu ametupa wanadamu uwezo wa kufikiria hivyo atatuadhibu kwakuwa tulishindwa kutumia uwezo huo. Hapo unajikuta uko kwenye hoja inayojenga mduara. Hoja ni hii: unatakiwa kufuata dini ya wazazi, ila kama wazazi wako walichagua dini ya uongo, utaadhibiwa maana mungu kakupa uwezo wa kufikiri!
Kama amenipa uwezo wa kufikiri kwanini uamuzi wangu juu ya imani yangu na mungu wangu utegemee maamuzi ya watu wengine? Ina maana kuwa kwakuwa wazazi wangu ndio walionileta hapa duniani maamuzi yao juu ya imani lazima yatakuwa sahihi? Kwanza maamuzi yao ya kufuata dini hii au ile hayatokani na mantiki na uchambuzi waliofanya kuhusu dini mbalimbali. Uamuzi wao unatokana na mambo mawili makubwa: jiografia na historia.
Mahali wazazi wako au wazazi wao walipotokea (jiografia) na dini za wageni walivamia huko walikotokea (historia) ndio vigezo vikubwa vilivyofanya wazazi wako kuwa na dini walizonazo ambazo nawe unazifuata kwakuwa eti “mtu anapaswa kufuata dini ya wazazi wake.” Sababu hii ndio inafanya kuwa rahisi sana kujua mtu dini yake ni ipi kutokana na mahali alipozaliwa. Tutazame kule mkoa wa Kilimanjaro. Kama wazazi wako wametoka Rombo au Kibosho unajua piga ua watakuwa wakatoliki (wako wachache ambao sio). Kama wametoka Moshi ya Zamani (Old Moshi), watakuwa Waluteri. Sababu ni hiyo niliyosema ya jiografia na historia. Kihistoria wamisionari wa Kijerumani walivamia Moshi ya Zamani na wamisionari walioleta ukatoliki walivamia Rombo na Kibosho. Ukitazama Pwani ya Afrika Mashariki unakuta kuwa waliokuwa wakijihusisha na biashara ya utumwa, yaani Waarabu, walivamia maeneo hayo ndio maana unakuta Waislamu wengi Zanzibar, Dar Es Salaam, n.k.
Iwapo mzazi wako alichagua dini aliyonayo baada ya kufanya utafiti na uchambuzi wa kina ningekuwa na mtazamo tofauti, ila kwakuwa dini yake imetokana na sababu za kijiografia na kihistoria zaidi ya mantiki na uchambuzi binafsi lazima nitake unipe sababu za msingi za kutufanya Waafrika tufuate dini kwakuwa eti ni za wazazi wetu. Ni mstari gani huo unaosema kuwa dini zetu ni zile za wazazi? Aya ya ngapi, mlango wa ngapi? Nabii gani alisema hivyo? Mafunzo hayo yametoka wapi? Kwenye simulizi zipi?
Tabia hii ya kufuata dini kwakuwa ni za wazazi na sio kwakuwa tumezichambua na kuzitafiti na kukubali kwa hiari yetu wenyewe kuwa tunazitaka inafanya dini kuwa kama ni mchezo fulani. Mchezo huo unaonekana pale mwanamke anapoolewa. Mwanamke anaweza kuwa ni shahidi wa yehova. Anaamini kabisa kuwa dini yake hiyo ndio sahihi mbele za mungu wake. Anakuja kupendana na mwanaume ambaye ni msabato. Wanaoana. Ghafla, anaacha dhehebu lake hilo anakuwa msabato. Kisa? Eti “wanawake wanafuata dini za waume zao.” Yaani wewe siku zote umesimama kwenye dini A, ukaamini kuwa hiyo ndio dini sahihi, kitendo cha kumpenda fulani kimefanya dini B (sabato) kuwa ndio sahihi? Maisha yetu utaona yamejaa mambo mengi tunayapeleka kimchezo mchezo tu
Hata mtu ambaye watu wengi wanadai kuwa wafuasi wake, Yesu/Yeshua/Isa, angekuwa na mawazo kuwa tunapaswa “kurithi” dini za wazazi wetu basi asingesema kuwa ukitaka kumfuata itabidi uwaache baba na mama yako ili umfuate. Socrates kule Uyunani aliuawa kwa kosa la kuwafunza vijana mafunzo mapya yaliyokuwa ni tofauti na yale ya wazazi wao. Akahukumiwa kifo kwa sumu. Naona nimalize kwa sasa maana naona dalili ya kutoka nje ya somo.
Wazazi wetu walidanganywa na wageni waliokuja kwa mbinu mbalimbali. Wageni waliokuja na kutuambia kuwa manabii zetu akina Lenana, Pharit, simulizi za akina Mrile, Ng’wanamalundi, n.k. ni ushenzi. Walidanganywa kuwa majina toka Ulaya ni ya kikristo wakati Yesu (ambaye ndiye anaamini kuwa msingi wa Ukristo ingawa yeye mwenyewe hakuwa mkristo) hatoki Ulaya na wala hakuwa anaongea kifaransa, kiingereza, au kilatini. Uongo ule tumeubeba hadi leo. Uongo wa dini, majina, tamaduni, elimu, n.k. Je yapi mengine walidanganywa ambayo tunayabeba hadi leo? Jiulize mwenyewe maana hiyo ndio njia ya kuanza kujikomboe kifikra kama Mwafrika na mwanadamu. Ngoja nikomee hapa kwa sasa.
Sun 12 Feb 2006
Imani hii ni potofu. Eti Wakenya hawajui Kiswahili. Nimekuwa nikisubiri kwa muda mrefu wanablogu wa Kiswahili toka Kenya wajitokeze. Nadhani wakati huo umewadia au unakaribia. Wako ambao wameniandikia wakisema wataanza kublogu. Nawasubiri. Baada ya Maitha kuwa mwanablogu wa Kiswahili pekee toka Kenya kwa muda mrefu, amekuja mwingine anayesema kuwa anataka kuweka wazi uhujumu wa sanaa, tamthilia, na utamaduni wetu Waafrika. Bonyeza hapa uone blogu yake.
Sun 12 Feb 2006
Kama wewe ni mtengeneza filamu au unafahamu mtengeneza filamu tafadhali mpe taarifa hizi: kuna mashindano ya filamu ya Afrika Mashariki yanayoendesha na waandaaji wa tamasha la kimataifa la filamu la Amakula, Kampala, Uganda. Tarehe 10 mwezi wa tatu ndio mwisho wa kuingia kwenye shindano hili. Matamasha kama haya ni sehemu nzuri sana ya kuitangaza kazi yako iwapo wewe ni mtengeneza filamu.
Sankofa…lazima uingie kwenye shindano. Sawa?
Taarifa za jinsi ya kuingia kwenye shindano hilo zipate kwa kubonyeza hapa. Ukienda hapa ndipo ilipo tovuti ya tamasha hilo la Amakula.
Sat 11 Feb 2006
Hivi sasa nimekalia blogu za Kiswahili. Nilikuwa nazipitia kila siku ila kwa haraka. Sasa nasoma kwa utulivu. Nimetua kwa Kasri la Mwanazuo. Picha na taarifa kibao. Safi. Katika pitapita nimekutana na mgeni. Huyu ni mwanablogu mpya, ndugu MK, ambaye anasema blogu yake ni ya vichekesho. Inaitwa Vijimambo. Itazame hapa. Niache nifaidi mambo bloguni. Nitarudi maana yapo mambo mengi ya kuambiana.
Sat 11 Feb 2006
Nawakaribisheni nyote kwa furaha kubwa ingawa bado humu ndani bado tunapangapanga samani (fenicha) na kusafisha madirisha, sakafu, n.k. Haya ndio makazi yetu mapya. Uzi ni ule ule. Kazi ni ile ile. Nguvu ni ile ile. Nia ni ile ile.
Kuna mambo mapya kadhaa. Kuanzia sasa itakuwa rahisi kwako kusoma habari unazotaka kwa kuchagua maudhui unayotaka. Tazama kipengele cha maudhui upande wa kulia. Kingine ni kuwa utakuwa una uwezo wa kutumiwa habari mpya ninazoandika kwenye anuani yako ya barua pepe. Utaona kisanduku cha chango kwa njia ya barua pepe. Ukiweka anuani yako pale na kubonyeza, umemaliza kazi. Ninayoandika yatakujia. Halafu kuna kisanduku cha kusaka habari. Kisanduku hiki kitakusaidia kutafuta habari nilizoandika huko nyuma. Kwa mfano, kama unatafuta habari kuhusu dini, utakachofanya ni kuandika neno “dini” kwenye kisanduku cha kusaka na kubonyeza. Iwo unataka kutuma kiungo cha habari niliyoandika kwa mtu au unataka kuweka kiungo cha habari hiyo kwenye jambo unaloandika kwenye blogu yako, badala ya kuweka anuani ya blogu yangu nzima, bonyeza juu ya kichwa cha habari yenyewe. Hapo kiungo cha habari hiyo kitatokea. Kinakili na kubandika kwenye habari unayoandika au barua pepe unayotuma.
Kwahiyo naomba mbadili anuani za kiungo cha blogu yangu kuwa http://jikomboe.com
Karibuni sana.
Fri 10 Feb 2006
Mchezo wa kuigiza: Watanzania na Utanzania wetu
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: Wapi tunakwenda?Toa Maoni [3]
Mti Mkubwa (ambaye Michuzi anamuiita Mti Mkubwa Mkavu) ni mwanablogu ingawa sio mwanablogu. Suala la Mti Mkubwa kuwa mwanablogu ingawa sio mwanablogu ni moja ya mifano ambayo mimi huitazama kama ni faida za teknolojia ya blogu. Je ni mara ngapi umeona maoni ya wasomaji kwenye magazeti yamewekwa ukurasa wa mbele? Mti Mkubwa ni msomaji mzuri sana wa blogu na mtoa maoni changamoto. Mara nyingi maoni yake huwa yanakuwa mazito sana kiasi ambacho wanablogu huyaweka ukurasa wa mbele badala ya kuyaacha kwenye kidirisha cha maoni. Hii ni sawa na mhariri wa gazeti kuchukua maoni ya msomaji na kuyaweka kwenye ukurasa wa mbele. Kwahiyo utaona kuwa kutokana na maoni na taarifa mbalimbali anazotoa Mti Mkubwa kuweka ukurasa wa mbele za blogu zetu, unaweza kusema kuwa Mti Mkavu ni mwanablogu (ingawa sio moja kwa moja, kwa maana ya yeye kufungua blogu yake mwenyewe).
Maoni ya Mti Mkavu nimewahi kuyatumia kuandika makala katika safu yangu ya kila jumapili katika gazeti la Mwananchi. Maoni hayo ni yale aliyotoa akihoji mantiki ya kuomba mungu awabariki viongozi wetu (ambao wengi ni wezi, wazembe, waongo, n.k.). Sasa Mti Mkubwa kaja na kitu kingine ambacho nadhani hiki nacho nitamuomba ruhusu kutumia. Ameandika mchezo mfupi wa kuigiza wenye maonyesho manne. Nimeupata mchezo huu toka kwa Da Mija ambaye ameuweka ukurasa wa mbele. Nakuomba uusome kwa makini sana. Ingawa mchezo wenyewe, kwa ujumla, unatia huzuni, zipo sehemu ambazo lazima ucheke. Cheka usiogope, ila pata ujumbe wenyewe anaoutuma. Kisha mpe maoni yako kupitia hapo kwa Da Mija ulipo mchezo huu. Bonyeza hapa usome.
Fri 10 Feb 2006
Sat 4 Feb 2006
Kama mapinduzi ya uandishi pepe unaona kuwa ni utani, fikiria tena. Kasulu nako kuna blogu. Ndugu yetu Njili Mwakoba amekata shauri. Ameanza kublogu. Mtembelee umkaribishe. Bonyeza hapa.
Fri 3 Feb 2006
Je una habari za kuzaliwa kwa blogu hizi? Nitaandika machache kutokana na ujio wa wanablogu hawa wapya (ukiacha blogu ya watoto ambao ni ukurasa wa pili wa Da Mija). Watembeeleeni tafadhali na kuwaunga mkono. Kuna ndugu Lubuva, bonyeza hapa. Halafu Kisima cha Weledi, bonyeza hapa. Kutana na Jungu Kuu (lina ukoko au halina?), bonyeza hapa. Na masuala ya watoto kupitia Da Mija, bonyeza hapa.
Kasri halali akitafuta kila mbinu za kuleta wanablogu wapya. Msome mwenyewe kwa kubonyeza hapa kuhusu juhudi zake hizo na matunda yake.
Fri 3 Feb 2006
Blogu Mpya, Nguvu za Teknolojia Mpya, na Kadhalika
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: teknolojia , blogu , Uandishi wa RaiaToa Maoni [5]
Kasri la Mwanazuo katuletea mwanablogu mpya. Juhudi zake nazipongeza. Mwanablogu huyo ni Mustapha ambaye amekuja na Hotspot. Mkaribishe na uwe unamtembelea. Bonyeza hapa uende nyumbani kwake. Kuja kwa Mustapha kumetokea dakika chache kabla sijakaa chini kuandika kifupi juu ya masuala ya teknolojia na vyombo vya habari. Huwa sichoki “kuhubiri” juu ya masuala haya kwani mapinduzi ya teknolojia ya habari, mawasiliano, na maarifa yananikuna sana. Mapinduzi haya faida zake kwa nchi kama zetu unaweza usizione lakini ukiwa unatazama mbali na una uwezo wa kuona “picha kamili” utajua kuwa mapinduzi haya yatabadili mambo katika nchi zetu kwa kiasi kikubwa. Kama sio sasa, ni hapo baadaye kidogo.
Moja ya mambo ambayo yanabadilika kutokana na teknolojia mpya ni mahusiano kati ya magazeti na wasomaji. Mahusiano kati ya wahariri, waandishi, na wasomaji wao. Kwa miaka mingi magazeti yamekuwa ni chombo cha habari cha mstari mmoja ulioonyooka ambapo habari, maarifa, na elimu vinatoka katika vyombo hivyo na kwenda kwa wasomaji. Mahusiano kati ya magazeti na wasomaji ni mahusiano kati ya mtoaji na mpokeaji. Magazeti yanatoa habari na maarifa, sisi wasomaji tunapoke. Wasomaji ni walaji. Barua za wasomaji tunaweza kusema kuwa ndio njia kuu ya kufanya mahusiano kati ya magazeti na wasomaji kuwa ya nipe nikupe. Magazeti yanatuambia jambo nasi tunapata nafasi ya kujibu, kuhoji, kuuliza, kusahihisha, kupongeza, n.k kupitia barua za wasomaji. Pia tunaweza kuandika kukemea jambo au kumtaka kiongozi afanye au aache kufanya jambo fulani. Zaidi ya hapo wasomaji hatuna sauti. Sisi ni magolikipa.
Kama hujawahi kufanya kwenye magazeti hutajua kuwa ni barua chache sana ambazo wasomaji wanaandika zinapata nafasi ya kusomwa na wahariri na kuchapishwa gazetini. Nyingi huishia kapuni. Na wakati mwingine, “barua za wasomaji” huandikwa na waandishi wa habari wenyewe! Kuna mambo ya ajabu sana ndani ya vyombo vya habari (ndio maana wakati mwingine mimi huviita vyombo vya uongo). Unaweza kusoma habari isemayo, “wananchi wengi waliohojiwa na gazeti hili…” ukaamini kabisa kuwa wananchi wengi waliohojiwa kumbe “wananchi” hao wako kichwani mwa mwandishi. Hajaenda kokote, hajahoji mtu yeyote.
Tofauti na magazeti-jadi ambapo msomaji ni msomaji, mtandao wa tarakilishi (Intaneti) umeleta jambo jipya. Mtandao huu, baadhi ya watu wanauita: soma-andika. Mtandao wa tarakilishi umejengwa kwa namna ambayo inaruhusu mtu kusoma na pia kuandika. Kwa mfano, kama umesoma jambo hapa kwenye blogu ukawa hukubaliani nalo au hukuelewa unaweza kuandika kupinga au kutaka ufafanuzi. Walaji na wazalishaji wanakuwa kitu kimoja. Wasomaji wanakuwa waandishi, waandishi wanakuwa wasomaji (wanasoma yaliyoandikwa na wasomaji wao). Mahusiano ya vyombo vya habari mtandaoni na wasomaji yanabadilika na kuwa ya mistari miwili ya nipe nikupe.
Ngoja nikupe mfano mdogo wa jinsi teknolojia inabadili mambo. Nimekuwa nikiandika magazetini rasmi toka mwaka 1992/93. Toka wakati huo hadi majuzi nilikuwa siwezi kujua wasomaji wangu wanawaza nini, ukiachia mbali wale ambao nilikuwa nakutana nao ana kwa ana. Lakini nilipoanza kuweka anuani yangu kwenye makala zangu nikaanza kuwa na mahusiano ya moja kwa moja na wasomaji wangu. Wasomaji wananiuliza maswali kutaka ufafanuzi, wananipa mapendekezo ya makala za kuandika, wananiunga mkono, wananishushua, wananiponda, wananikumbusha ahadi nilizoweka za kuandika kuhusu jambo fulani, n.k. Nimeandika makala nyingi kutokana na mapendekezo ya wasomaji. Hili ni badiliko kubwa sana.
Blogu zinatuwezesha kwa kiasi kikubwa kufanya mambo ambayo yamekuwa hayawezekani katika magazeti-jadi ya kuuzwa mtaani. Huku bloguni tunaandika. Wasomaji wetu nao wanaandika. Mara yanatokea majadiliano. Sio mtu mmoja tu anawaambia wengine ambao wanasoma bila kuwa na uwezo wa kujibu, kuunga mkono, au kuuliza maswali. Hapana. Blogu inawezesha nyanja ya habari kutoka kwenye zama za wasomaji kuwa kama watu wasio na mawazo, habari, au fikra. Watu wanaopaswa kusoma tu, kupokea bila kutoa. Tunatoka kwenye zama hizo na kuingia kwenye zama ambazo nyanja ya habari inakuwa ni aina fulani ya majadiliano. Mazungumzo. Nipe, nikupe. Mzalishaji ni mlaji na mlaji ni mzalishaji. Kila mtu anakuwa mwanahabari. Hili ndio linafanya blogu kupata umaarufu kwa haraka. Siku hizi zinatolewa hadi skolashipu kwa ajili ya kublogu. Sio mchezo. Bonyeza hapa uione (lazima uwe mwanafunzi wa chuo kilichopo Marekani).
Katika kujaribu kubadili mahusiano kati yake na wasomaji, kwa kutumia teknolojia mpya, magazeti kadhaa yanafanya majaribio ya aina mbalimbali. Kwa mfano, gazeti la Wisconsin State Journal linatumia wasomaji wake kuamua habari zipi ziwekwe ukurasa wa mbele. Wasomaji wanapiga kura. Bonyeza hapa usome kuhusu jaribio hili. Mwaka jana gazeti la Seattle Post-Intelligencer lilianzisha jaribio ambalo tahariri inaandikwa na wahariri wa gazeti hilo na wasomaji wake. Kongoli hapa na hapa kwa undani. Kuna gazeti kama News and Record ambalo limeanzisha ukurasa uitwao Town Square katika tovuti yake ambapo wasomaji wanapewa nafasi ya kuandika habari wenyewe. Bofya hapa uwatazame. Magazeti mengi yanachofanya hivi sasa ni kuwa na waandishi wao ambao wanakuwa na blogu. Blogu hizo zinakuwa ni uwanja wa majadiliano kati ya gazeti na wasomaji wake. Ukiachilia mbali maagazeti hayo, teknolojia mpya zimezalisha miradi mipya kabisa kwenye nyanja ya habari. Kwa mfano, kuna Wikinews, mradi ambao habari zinaandikwa na wasomaji. Zinaandikwa na mtu yeyote. Tazama hapa. Halafu kuna jamaa walioanzisha mradi kabambe wa uandishi wa umma huko Korea ya Kusini, Ohmynews. Ohmynews ina habari ambazo zinaandikwa na wananchi. Wasomaji wakisoma habari wakaipenda wanaweza kumlipa aliyeandika habari hiyo. Bonyeza hapa utazama toleo la kiingereza la Ohmynews.
Kwa ufupi, nilikuwa namkaribisha Mustapha , kumpongeza Kasri kwa kutuletea huyu ndugu, na kusema kuwa tunalofanya kupitia katika blogu zetu hizi ni sehemu ya mapinduzi ambayo yanabadili kabisa mahusiano kati ya watoa habari na wapokeaji.
Fri 3 Feb 2006
Creative Commons, kitabu cha bure, na zoezi la pekee la kuhariri
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: teknolojia , creative commonsToa Maoni
Huu ni mmoja wa mifano ya faida za Creative Commons. Majuzi kimetolewa kitabu cha kufundisha watu wa nchi zinazoitwa “zinazoendelea” juu ya ujenzi wa mtandao usiwaya (wireless network kwa kimombo). Kitabu hiki kimetolewa chini ya nembo ya Creative Commons. Kinapatikana bure. Na kuwakuwa kiko chini ya Creative Commons, mtu yeyote yule anaruhusiwa kukitoa kitabu hiki katika lugha yoyote ile (na hata kuongeza mambo ambayo anaona ni muhimu ila hayako katika kitabu mama). Yote hii unaruhusiwa kufanya bila kuomba ruhusa kwa mtu yeyote kwa masharti kuwa kitabu hicho usikitoe kwa minajili ya kibiashara na pia lazima toleo lako liwe chini ya Creative Commons. Kitabu chenyewe ukibonyeza hapa utakipata. Hapa kuna ukurasawa wa “wiki” wa kitabu hicho.
Kuna mfano mwingine wa mabadiliko makubwa yanayojitokeza kutokana na teknolojia mpya na vuguvugu kama la Creative Commons. Mwaka 1999, Larry Lessig, mwanzilishi wa vuguvugu hili, alitoa kitabu kizuri sana kiitwacho Code and Other Laws of Cyberspace. Hili lilikuwa ni toleo la kwanza. Toleo la pili, yaani Code v. 2, ni muendelezo na upanuaji wa hoja na uchambuzi ulioko katika toleo la kwanza. Kwa staili ya ki-Creative Commons, toleo hili la pili badala ya kuandikwa na Larry Lessig peke yake kama ilivyo kawaida katika nyanja ya vitabu, toleo hili linaandikwa/linahaririwa na watu mbalimbali. Ina maana kuwa hata wewe unaweza kushiriki katika kuandika toleo la pili la kitabu hiki. Bonyeza hapa uone zoezi hili la kipekee.
Fri 3 Feb 2006
Kuapa kwa Biblia na Kurani: Dini tumezibebabeba tu?
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: utamaduni , diniToa Maoni [8]
Wiki iliyopita, kwa ajili ya ukurasa wangu katika gazeti la Mwananchi, niliandika makala kuhusu mawaziri wapya kuapa kwa kutumia kitabu “kitukufu” na “kitakatifu” baada ya kuteuliwa. Soma baadhi ya hoja nilizotoa dhidi ya tendo la kuapa:
Baada ya rais mpya kuteua baraza jipya la mawaziri, kilichofuata kilikuwa ni tendo la kula kiapo. Tukio hili limezungumzwa sana mtaani hasa kutokana na kitendo cha Kingunge Ngombale Mwiru (nitampa zawadi ya jina zuri) kuapa kwa kunyoosha mkono bila kushika kitabu “kitukufu” au “kitakatifu” (kurani au biblia) kama wengine walivyofanya.
Wakati ambapo kwa watu wengi kuapa bila kutumia kitabu cha dini ilikuwa ni habari kubwa, kwangu mimi kitendo cha wafuasi wa Isa/Yesu kuapa ndio ilikuwa habari kubwa kabisa. Ni habari ya binadamu kuwa na tabia ya kufanya mambo kutokana na mazoea bila kutafiti kwa kina juu ya usahihi wa jambo lenyewe. Ni tabia inayotokana na utamaduni wa kuiga mifumo ya sheria, utawala, na demokrasia ya nchi nyingine tukidharau uwezo wetu wa kuunda mfumo wetu wenyewe.
Tendo la mawaziri kuapa wakitumia kitabu kitakatifu au kitukufu hatujaanzisha sisi. Utamaduni wa mashahidi kuapa mahakamani kwa kutumia vitabu hivyo hatujauanzisha sisi. Tumeiga toka kwa wengine kama ambavyo tumeiga karibu kila kitu.
Kwanini habari kwangu sio Kingunge kuapa mikono mitupu bali Wakristo na Waislamu kuapa? Jibu la swali hili liko katika kitabu cha Matayo, mlango wa 5, aya ya 33 hadi 37. Katika aya ya 34 Yesu/Isa anakataza wafuasi wake (Waislamu na Wakristo ni wafuasi wake) kuwa wasiape kamwe.
Hivi ndivyo asemavyo toka aya ya 33 hadi ya 37: “Tena mmesikia kuwa watu wa kale waliambiwa: `Usivunje kiapo chako, bali ni lazima utimize kiapo chako kwa Bwana. Lakini mimi nawaambieni, msiape kamwe; wala kwa mbingu, maana ni kiti cha enzi cha Mungu; wala kwa dunia, maana ni kiti chake cha kuwekea miguu; wala kwa Yerusalemu, maana ni mji wa Mfalme mkuu. Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kuufanya hata unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi. Ukisema, `Ndiyo`, basi iwe `Ndiyo`; ukisema `Siyo`, basi iwe kweli `Siyo`. Chochote kinachozidi hayo hutoka kwa yule Mwovu.”
Anasema kuwa ingawa huko nyuma kuna manabii waliwaambia wanadamu kuwa wanaweza kuapa, yeye anabadili na kusema kuwa usiape kamwe. Hii haikuwa kwa mara ya kwanza kwa Yesu/Isa kutengua mafundisho ya zamani. Unakumbuka, ingawa iliandikwa “jino kwa jino, jicho kwa jicho,” yeye alikuja na kusema geuza shavu. Mchukie adui yako akabadili kwa kutuambia kuwa tuwapende na tena tuwaombee. Aligeuza sheria ya kupiga mawe hadi kuwaua wanaokamatwa katika uzinzi. Alibadili sheria kuhusu talaka. Alibadili maana ya kuzini kwa kusema kuwa hata ukitamani umeshazini.
Nimetoa mifano hii kukupa picha kidogo ya baadhi ya mambo aliyobadili likiwemo suala la kiapo. Anatuambia kuwa kipimo cha ukweli wa kauli yetu isiwe ni kiapo. Anasema ukisema “ndiyo” iwe “ndiyo” na ukisema “hapana” iwe “hapana.” Ukisema utatii katiba na kutumikia wananchi, basi tii katiba na kutumikia wananchi. Hakuna la kuongeza wala kupunguza. Sema ukweli na simama kwenye hiyo kweli, usianze kuingiza jina la Mungu ili kutufanya tuone kuwa unayosema ni kweli.
Nimekuwa najiuliza kwanini wafuasi wa Mwalimu huyu wamekuwa hawafuati mafundisho yake? Je inawezekana kuwa ufuasi wao ni wa jina tu na sio imani ya dhati na uelewa wa mafundisho yake? Amesema waziwazi usiape. Wewe unaapa, tena kwa kutumia kitabu chenye maneno yake yanayokukataza. Je hili ni tatizo la kufuata tamaduni za wengine bila kuhoji? Au ni tatizo la kuwa wafuasi wa Isa/Yesu bila kusoma mafundisho yake?
Lakini tukiacha hoja hii ya kuwa Isa/Yesu amekataza wafuasi wake kuapa, kuna hoja nyingine ambayo niliwahi kuitoa huko nyuma. Nitairudia kwa kifupi. Haiwezekani kutumia Kurani au Biblia kuapa kuwa utalinda katiba ya nchi ukitegemea kuwa Mungu atakubariki na kukusaidia ili utimize kiapo hicho. Kwa sentensi chache sana nitakueleza ni kwanini kisha nitakuacha ili iwe tafakari yako siku hii ya mungu jua (ndio maana ya jumapili).
Kurani na Biblia zinasema kuwa Mungu ametoa amri kumi. Amri ya kwanza inasema, “Mimi ni Bwana Mungu wako usiwe na miungu wengine ila mimi.” Hili sio ombi. Inaitwa amri. Anasema wazi kuwa anataka umwamini na kumwabudu yeye tu. Yeye Yehova/Allah. Tuje kwenye katiba yetu: katiba yetu inatoa uhuru wa kuabudu. Ina maana kuwa unaweza kuabudu Mungu mmoja au miungu 10, hutakuwa umevunja sheria ya nchi. Sio hivyo tu, unaweza pia kutokuwa na imani yoyote na usiwe umevunja sheria ya nchi.
Kwa maneno mengine, wakati Yehova/Allah anakwambia, “Niabudu mimi” katiba inasema “Abudu chochote kile.” Je Mungu aliyekupa AMRI ya kumwabudu yeye tu, anaweza kukubariki ili uendeleze katiba inayosema abudu chochote kile? Yaani Mungu atakuwa anakubariki ili uendeleze mwongozo ambao unawapa wanadamu ruhusa ya kuvunja amri yake ya kwanza. Tena amri hii sio ya kumi bali ni ya kwanza. Kama katiba ingesema mwamini mungu mmoja ambaye ni Yehova/Allah, basi nisingeshangaa iwapo waumini wa Kikristo na Kiislamu wangekuwa wanamuomba mungu awasaidie kuilinda hiyo katiba. Lakini katiba haisemi hivyo. Inapingana kabisa na mafundisho ya Allha na Yehova. “Usiwe na miungu mingine ila mimi” sio sawa na kusema kila mtu ana haki na uhuru wa kuamini atakacho.
Kwahiyo kitendo cha kutumia kitabu kinachokutaka uwe na Mungu mmoja kuapa kuwa utalinda katiba inayokuruhusu uwe na mungu yoyote, mmoja au miungu wengi, au hata usiwe na imani kabisa, n.k. kinaonyesha kuwa huenda imani zetu tumezibebabeba tu. Au tumebebeshwa.
Fri 3 Feb 2006
Majuzi niliandika kuhusu Tanzania kukubaliwa rasmi kuanzisha tawi la Creative Commons na kuwa Paul Kihwelo, mkuu wa kitivo cha sheria, Chuo Kikuu Huria, ndiye mwongoza mradi upande wa kisheria. Baadaye tunatakiwa kutafuta mwongoza mradi upande wa uhamasishaji. Kama hukusoma niliyoandika siku hiyo, bonyeza hapa. Ukisoma sehemu ya maoni utaona kuwa Mark Msaki ameongelea suala moja ambalo kwa muda mrefu limekuwa lilibishaniwa katika duru za wanazuoni wa masuala ya sheria, sayansi ya jamii, uchumi, na falsafa. Hoja yenyewe ni kuwa sheria ya hatimiliki inachochea ubunifu na ugunduzi. Na kuwa kama kama hakuna faida za kiuchumi/kifedha, watu hawatabuni au kujihusisha na kazi za ugunduzi. Kwahiyo vuguvugu kama la Creative Commons ambalo linachochea watu kuachilia huru kazi zao (iwe ni vitabu, muziki, sinema, n.k.) na kuondoa ukiritimba wa maarifa na elimu, linaweza (vuguvugu hilo) kuondoa msukumo wa kubuni, kutunga, kugundua, n.k.
Hoja hii ina mapengo mengi sana. Mfumo wa hatimiliki una kazi zake. Tunaounga mkono vuguvugu la Creative Commons hatusemi kuwa mfumo wa hatimiliki uondolewe kabisa. Tunasema kuwa mfumo huu unahitaji kufanyiwa mageuzi ili kuendana na upepo wa wakati, teknolojia zilizopo leo hii, na kukidhi matakwa ya umma. Tunachosema ni kuwa tunaweza kutumia itikadi ya ujamaa kwenye kazi ambazo zimekuwa zikifungwa pingu na sheria ya hatimiliki ambayo inakidhi mahitaji ya msukumo wa soko. Msukumo wa soko, kama apendavyo kusema Desmond Tutu, sio mungu. Sio mwanzo na mwisho wa kila kitu.
Zipo faida mbalimbali kwa umma iwapo mfumo wa hatimiliki uliopo (duniani kwa ujumla) utafanyiwa marekebisho. Kwa mfano, tazama suala la dawa za kuongeza maisha ya wenye Ukimwi. Dawa hizi zimegunduliwa (makampuni mengi ya madawa huiba elimu ya jadi ya dawa toka nchi za Kusini) na makampuni ya Magharibi. Dawa zao ni ghali sana kiasi ambacho watu wachache sana wenye ugonjwa huu katika nchi za Kusini wana uwezo wa kuzinunua. Makampuni ya Brazili, India na kwingineko yanatengeneza dawa-chapa kama hizo kwa bei nafuu zaidi. Kutokana na sheria ya hatimikili kitendo cha kampuni hizi kutengeneza dawa hizo bila ruhusa ya makampuni ya Magharibi yaliyozigundua ni kosa. Kitendo cha dawa-chapa hizi kuwa za bei ambayo masikini wengi wanaweza kuimudu kuliko ile ya makampuni ya Kimagharibi hakina nafasi kwenye mjadala. Suala kuu ni hatimiliki na haki ya makampuni haya kufaidi kwanza kwa maiaka kadhaa kabla makampuni mengine hayajaruhusiwa kuzitengeneza. Kwahiyo kumekuwa na kesi mbalimbali ingawa makampuni ya Magharibi yanarudi nyuma kwakuwa yameona kuwa dunia inayaona kama wanyama vile kwa kutaka kuzuia masikini wasio na kipato kupata dawa wanazoweza kununua.
Mfano mzuri wa umuhimu wa vuguvugu la Creative Commons ni huu: Shirika la Habari la BBC linaruhusu Muingereza yoyote kutumia bure chochote BBC walichohifadhi. Kama kuna Muingereza anatengeneza filamu, katika filamu hiyo akawa anahitahi sauti ya simba au tembo au akawa anahitaji video ya mbuga fulani ya wanyama, badala ya kufunga safari kutafuta wanyama hao anaweza kutumia video za BBC. Bure. Kila Muingereza hulipa kodi ya kuendesha BBC. Kwahiyo kila Muingereza ana haki ya kufaidika na kazi za BBC. BBC wakifuata mfumo wa hatimiliki uliopo itabidi wazuie Waingereza ambao ndio hasa wanaoipa uhai BBC kufaidi. Ni sawa na Tanzania. Redio Tanzania inaendeshwa kwa fedha zetu. Je hatimiliki ya kazi zake na rekodi zake zote ni za Watanzania wote? Vuguvugu la Creative Commons linasukuma Redio kama Redio Tanzania kupanua hatimiliki ya kazi zake kuwa ya Watanzania wote ambao kodi yao ndio uhai wa redio hiyo. Bonyeza hapa usome kuhusu BBC kuamua kuweka kazi zao zote chini ya Creative Commons. Unaambiwa kuwa ili umaliza kutazama video walizonazo, unapaswa kutazama video hizo kwa miala 68, usiku na mchana (masaa 24)!
Kuna mtazamo kuwa hatimiliki husaidia sana wagunduzi, watunzi, wanamuziki, n.k. Sio mara zote. Tazama kwenye muziki. Wanamuziki wengi wanapata hela zao sio kwenye kuuza CD bali kwenye maonyesho ya hadharani, matangazo, n.k. Wanaofaidi hasa kazi za wanamuziki ni makampuni ya kurekodi. Utashangaa kuwa makampuni haya ndio huwa yanamikili haki za nyimbo za wanamuziki. Na ndio huchukua sehemu kubwa ya pato linalotokana na kuuza CD. Sasa katika mwelekeo wa ki-Creative Commons, imekuja kampuni inaitwa Magnatune. Kampuni hii inauza CD. Asilimia 50 inakwenda kwa mwanamuziki (hakuna kampuni inayompa mwanamuziki asilimia 50. Hata wanamuziki unaowaona matajiri wanapunjwa wote). Zaidi ya mwanamuziki kupata asilimia 50, mwanamuziki huyo ndiye anayemiliki haki za muziki wake na sio kampuni hiyo. Bonyeza hapa uone kampuni hiyo.
Profesa Kembrew ni mtu wa utani sana. Yeye ni kati ya wanazuoni wanaoandika sana kuhusu mapungufu ya mfumo wa hatimiliki uliopo hivi sasa. Katika kuonyesha mapungufu yake, Profesa Kembrew aliamu kusajili msemo wa kiingereza,”Freedom of Expression.” Baada ya kuusajili msemo huu amepewa haki ya kuweka nembo ya “haki zote zimehifadhiwa”. Yaani hivi: Freedom of Expression©. Kwahiyo hivi sasa yeye ndiye anayemiliki msemo huo. Bonyeza hapa usome kihoja hicho kwa undani.
Fri 3 Feb 2006
Moja ya matatizo ya huduma za kublogu tunazotumia hivi sasa ni lugha. Huduma hizi zimetengenezwa kwa udhanifu kuwa watumiaji ni wazungumzaji wa Kiingereza, Kifaransa, Kichina, Kishirazi, n.k. Kiswahili hakipo. Tatizo jingine ambalo lipo katika huduma kama blogger.com (ambayo wengi tunatumia) ni kukosekana kwa muundo wa kupanga kazi tunazoandika katika makundi ya kimaudhui. Hili ni tatizo kubwa sana hasa kama mtu unapanga kublogu kwa muda mrefu.
Ina maana hapo baaadaye ukitaka kutafuta habari uliyoandika miaka mitatu iliyopita, itakupasa ukumbuke mwezi na tarehe ili uweze kuipata kwa urahisi. Kama hukumbuki uliandika mwezi gani itakubidi utumie muda mrefu kuisaka. Fikiria, je ikiwa imepita miaka saba? Lakini pia kuna suala la wasomaji kuja kwenye blogu yako na kutaka kusoma habari ulizoandika huko nyuma. Kama wanataka kusoma habari ulizoandika kuhusu utamaduni, watazipataje? Au hadithi. Au labda umekwenda kwenye blogu ya Michuzi baada ya miaka miwili, ukawa unatafuta picha ya jiji la Dasalama au ya Mwanza. Utaipataje hiyo picha? Namna rahisi ya kuipata picha hiyo ni kama amehifadhi picha zake kutokana na maudhui. Kwa mfano, maudhui yanaweza kuwa ni: utamaduni, siasa, michezo, uchaguzi, mikoani, Ughaibuni, Rais, Wabunge, Wanawake, Muziki, Historia, Hadithi, n.k.
Nikienda kwenye blogu ya Makene, nikataka kusoma mashairi yake. Bila kujua aliandika lini na mwezi gani itakuwa vigumu sana. Lakini akiwa na uwezo wa kupanga mambo kwenye blogu yake kutokana na maudhui, kila akiandika shairi analiweka kwenye maudhui ya kundi ya ushairi. Hivyo msomaji akienda hapo anabonyeza kwenye maudhui ya ushairi na kuweza kuona mashairi yake yote. Ukija kwangu ukataka kusoma mambo niliyoandika kuhusu utamaduni au kuhusu blogu, utapata tabu sana maana hakuna mpangilio wa kimaudhui. Kunapokuwa na makundi haya yaliyopangwa kimaudhui kunasaidia msomaji kuweza kupata habari ulizoandika huko nyuma kwa urahisi. Inakusaidia hata wewe mwenye blogu kujua mambo uliyoandika yako wapi. Tunapaswa kutatua tatizo hili. Tutalitatua.
Sasa rafiki yangu Chris wa NonProfit Design (bonyeza hapa uone blogu yake) na mimi tunalipatia tatizo la lugha kwenye huduma za kublogu dawa ya kudumu. Kwa kutumia huduma huria ya kublogu ya Wordpress, tunaunda toleo la Kiswahili. Wordpress tayari ina matoleo ya lugha kadhaa. Kiswahili kwa sasa hakimo. Uzuri wa Wordpress ni kuwa ni programu huria hivyo iko wazi kwa mtu yeyote kufanya chochote atakacho (iwapo una ujuzi sahihi).
Mwisho wa wiki Chris alinitembelea tukaa pamoja kwa siku mbili (alikuja na mbwa wake aitwaye IO). Tulitazama kwa undani jinsi ambavyo tunaweza kusaidia wanablogu wote wa Kiswahili kuhama toka walipo hivi sasa na kuweza kuwa na mpangilio wa mambo waliyoandika katika makundi ya kimaudhui na pia hatua za kufuata ili kujenga toleo la Kiswahili la Wordpress. Katikati ya kucheza na kodi za programu mbalimbali za tarakilishi, tulikuwa tukicheza mpira wa meza (ambapo nilimfunga mabao yasiyohesabika. Kama unabisha muulize! Richard Shilangale, unakumbuka kuwa wewe ndiye ulinifundisha kucheza mpira wa meza?). Pia tuliongelea masuala ya Creative Commons maana shirika lake ndilo linalojenga tovuti ya tawi la Creative Commons Tanzania na pia kuihifadhi tovuti hiyo. Bonyeza hapa usome aliyoandika mwenyewe kuhusu toleo la Kiswahili la Wordpress.
**Da Mija: wewe ndio umenikumbusha neno maudhui. Lilinitoka kabisa. Kila nikilitafuta neno linalonijia ni hadhira! hadhira na maudhui wapi na wapi?
?



