Iwapo wewe ni mwandishi wa habari, unaweza kujaribu bahati yako kwa kutuma maombi ya skolashipu zifuatazo: Dag Hammarskjold Distinguished Journalist ni skolashipu ambayo ukiipata utagharamiwa ili kuweza kuhudhuria mkutano wa 61 wa Umoja wa Mataifa (gharama zote juu yao). Nenda hapa upate maelezo kamili. Skolashipu nyingine ni ile ya Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini Mwa Afrika (MISA). Tazama hapa. Na ya mwisho ni skolashipu ya uandishi wa kimataifa ya Kurt Schork. Habari zake zisome hapa. Skolashipu zote hizi nadhani kuna waandishi Tanzania ambao wana sifa za kutosha kuweza kuzipata. Kazi kwako, usije ukasema hukuwa na habari. Shukrani zimwendee Subi aliyenitumia viungo vya habari hii.
March 2006
Thu 30 Mar 2006
Skolashipu kwa waandishi wa habari
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: skolashipu , waandishi wa habariToa Maoni [1]
Thu 30 Mar 2006
Kwaya za mapambio kwa jina la vyombo vya “habari”
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: Wapi tunakwenda? , vyombo vya habari/uongoToa Maoni [6]
Majuzi niliandika kuhusu hatari ya vyombo vya uongo kulazimisha wananchi kupenda jambo fulani au mtu fulani (hata kama hawawezi kuorodhesha sababu za msingi za kupenda jambo hilo au mtu huyo). Nikasema kuwa vyombo hivi huzalisha “makubaliano.” Vinaweza kufanya wananchi katika nchi fulani kuamini kuwa wana mtazamo sawa kuhusu jambo fulani au “makubaliano” kuwa mtwawala fulani ni ni kiboko.
Maliza kusoma habari hii kwa kubonyeza hapa: (more…)
Wed 29 Mar 2006
Kaybees 2006: Tuzo ya Blogu Za Kenya
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: blogu , wanablogu , kenyaToa Maoni [3]
Jumuiya ya wanablogu wa Kenya imeandaa tuzo ya blogu za Kenya, Kaybees, ambayo itatolewa tarehe 17 mwezi ujao. Tuzo hiyo itatolewa kwa blogu katika makundi 13. Mtu yeyote anaruhusiwa kupendekeza blogu si zaidi ya tatu katika kila kundi. Mapendekezo yatafanywa kwa kutumia barua pepe. Baada ya kupata blogu zilizoingia fainali, wanachama wa jumuiya ya blogu za Kenya watapiga kura kuchagua blogu bora. Bonyeza hapa usome kuhusu tuzo hiyo. Nenda hapa nyumbani kwa blogu za Wakenya.
Jumuiya ya wanablogu wa Kenya ni kati ya jumuiya za wanablogu duniani ambazo zinashamiri na kukua kwa kasi. Majuzi gazeti la Daily Nation lilitoa makala ndefu na nzuri kuhusu wanablogu wa Kenya. Bonyeza hapa uisome. (lazima ujiandikishe kwanza kabla ya kuweza kusoma habari hii). Tayari ninajua blogu nitakazochagua (”mshikaji” unajua lazima nikuchague…sentensi hii atailewa mtu mmoja tu duniani!). Na labda, ingawa mimi sio Mkenya, nitaruhusiwa kupiga kura maana ni mwanachama wa blogu za Kenya (mambo ya jumuiya ya afrika mashariki..si ndio?).
Sun 26 Mar 2006
Blogu za Kiswahili za Wakenya: hii ni ishara njema?
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: wanablogu , lughaToa Maoni [3]
Baada ya ndugu yetu, Maitha, toka Kenya kuanza kublogu kwa Kiswahili toka Novemba 2004, wanablogu wa Kenya wamekuwa wakiongezeka kwa kasi. Ila lugha yao kuu ni kiingereza. Hivi sasa kapata mwenziye kwa jina la Mtandawazi (ndugu David). Imechukua muda mrefu sana kwa wenzetu wa Kenya kufanya kama alivyosema Shaban Robert kuhusu titi la mama…..hata kama la mbwa. Naamini wataibuka wengine wengi maana hata sisi ilianza polepole. Kwa jinsi alivyoanza inaelekea kuwa atatia sana changamoto lile vuguvugu la kusafisha akili, kuelimisha, na kuburudisha. Bonyeza hapa. Mwanablogu David anatumia programu ya Wordpress kama afanyavyo mwanablogu mwingine mpya wa Tanzania, Kabendera. Muone hapa.
Thu 23 Mar 2006
Kikwete ameandikwa kwenye kurani na biblia?
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: tanzania , demokrasia , vyombo vya habari/uongoToa Maoni [9]
Kuna wakati huwa ninaviita vyombo vya habari “vyombo vya uongo.” Kuna ukweli fulani kwenye jina hili. Siwezi kuelezea jinsi gani ilivyo muhimu kwa wananchi kuwa na mtazamo wa kutilia shaka vombo vya habari badala ya kumeza kila kinachoandikwa. Mtazamo na tabia zetu, mara nyingi bila kujijua, huwa vinaathiriwa sana na vyombo hivi. Kati ya sababu kubwa ni mtazamo, ambao ulijengeka toka ilipogunduliwa teknolojia ya kuchapisha, kuwa kitu kikiandikwa ni kweli. Ndio maana katika mabishano kati ya akina Mazinge na wakristo, utasikia Mazinge akiwauliza wakristo, “Nipe aya. Imeandikwa wapi?” Au atasema, “Yahaya, mpe aya huyo.” Hii ni kutokana na imani kuwa kama jambo ni la kweli basi lazima liwe na ushahidi wa maandishi. Huruhusiwi kusema kuwa jambo ni kweli kutokana na hisia zako, fikra zako, au kama ambavyo umewahi kusikia toka kwenye simulizi za mababu. (Bonyeza hapo chini umaliza kusoma habari hii).
Wed 22 Mar 2006
Hadi sasa kwenye blogu zetu kuna washairi, wachambuzi wa masuala ya kisiasa, kitamaduni, kiuchumi, n.k., wana riwaya, wafuatiliaji wa masuala ya michezo, wapiga picha, n.k. Sasa kumekuja blogu ambayo inafungua ukurasa mpya. Blogu hii ni ya katuni/vikaragosi. Sijaelewa itakuwa vipi. Hii ndio shauku yangu kubwa. Karibu mwanakwetu. Tunasubiri uanze kushusha nondo na mitaimbo. Bonyeza hapa umtazame.
Wed 22 Mar 2006
Mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Benin, Yayi Boni, (ambaye ni mgombea huru [kwa habari nilizonazo] ni mwanablogu! Anatumia huduma ya kublogu Typepad, ambayo ni ya kulipia. Bonyeza hapa umsome (iwapo unajua kifaransa zaidi ya neno “bonjour”). Mgombea urais wa Chadema, Freeman Mbowe, ana blogu ila haikuitumia wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu Tanzania.
Wed 22 Mar 2006
Ukibadili Dini Utauwa…halafu kazi Wyclef huko Haiti
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: dini , MengineyoToa Maoni
Huwezi kuamini kuwa dunia ya leo ina nchi zenye sheria zinazokataza binadamu kubadili dini yake. Yaani sheria za nchi zinalazimisha watu wote kwenye nchi kuwa na dini moja. Ukivunja sheria hiyo hukumu yake ni kifo, Ajabu ni kuwa hukumu hii ni kinyume na moja ya amri kumi za huyo mungu wanayedai kumwamini na kutaka kulazimisha kila mtu amwamini. Mungu huyo anasema, kwenye vitabu vyao, usiue. Nadhani ningezaliwa nchi hii ningeshatiwa kitanzi zamani sana. Bonyeza hapa usome mwenyewe.
Halafu kuna habari hii kuhusu mwanamuziki ninayemzimia sana, Jean Wyclef, ambaye kamwe hasahau alikotoka. Kazi zake za kuendeleza watu wake, hasa vijana, katika nchi yake ya Haiti zinaelezewa kuwa moja ya mifano ambayo inaweza kuigwa na watu wengine waliohama toka nchi fukara kwenda nchi zinazoaminika kuwa zina ustawi. Soma hapa anayofanya kupitia vuguvugu la Yéle Haiti. Yéle ni neno limaanishalo yowe au kilio.
Mon 20 Mar 2006
Mbona utamu unaongezeka? Ndugu yetu, Miruko, ametutaarifu kuhusu mwanablogu mpya, Omega Ngole. Bonyeza hapa umtembelee. Taarifa hizi za wanablogu wapya ni muhimu sana kama ilivyo muhimu kutembelea wanablogu wapya na kuwakaribisha na kuwasaidia kwa lolote lile. Ngole karibu. Uwapo na tatizo unaweza kuuliza mwanablogu yeyote yule. Pia unaweza kutazama Mwongozo wa Wanablogu kwa kubinya hapa.
Sun 19 Mar 2006
Inafurahisha sana unapokutana na viungo vya miziki ya kwetu ambayo inakukumbusha utotoni na kukuonyesha jinsi ambavyo Afrika Mashariki tumewahi kuwa na bendi matata za muziki-maarufu wa dansi. Ingawa “kizazi kipya” cha “dot.com” kinakuja na miziki ya kuimba kwa midundo iliyotengenezwa na tarakilishi bila kuwa na wazee wa kudonoa nyuzi bin nyuzi kama marehemu Kasheba au mzee wa Kasimbangu “tunakula muziki….kaabuka,” au safu ya wapiga matarumbeta kama wale wa Sikinde, n.k., muziki wa dansi una nafasi yake na utamu wake. Huwezi kubadili utamu wa msondo na kitu chochote kile.
Kupitia blogu ya Steve nimekutana na zilipendwa ambapo nitakuwa na roho mbaya nisipowapeni nanyi mburudike. Kwanza bofya hapa usikilize Shauri Yako wa Super Mazembe, sikiliza Nyako Konya wa Les Mangelepa (wajamaa walikuwa wakipiga magitaa enzi zile acheni tu) kwa kubofya hapa, nenda hapa usikize Shilingi Maua wa Simba Wanyika.
Sat 18 Mar 2006
Maitha aliwahi kutupasha kuhusu makala aliyoandika mwandishi wa riwaya na mwanazuoni Taban Lo Liyong akimchamba Profesa Ali Mazrui. Kama hukumsoma Maitha wakati huo, msome kwa kubinya hapa. Sasa leo wakati napitia habari mbalimbali za kisanga cha mamluki nchini Kenya, nakutana na makala ya Profesa William Ochieng akichamba Ali Mazrui. Isome hapa. Ali Mazrui ni Mkurugenzi wa Institute of Global Cultural Studies katika chuo kikuu cha Binghamton, nchini Marekani kwa mwizi wa kura Joji Kichaka.
Sijui kama Ali atawajibu akinaTaban na William.
Fri 17 Mar 2006
Hivi ni kweli kuwa kuna Watanzania wanahusika katika kisanga kinachoendelea nchini Kenya cha mamluki kushiriki kuvamia gazeti la The Standard la Kenya?
Kisanga hiki ukikifuatilia unaweza kudhani unasoma riwaya za Elvis Musiba kama Kufa na Kupona (Jafeti (sio Japhet!), unakumbuka niliingia mtini na kitabu chako?), Njama, na Hujuma. Bonyeza hapa uone ujvamizi huu ulivyojadiliwa na wanablogu wa Kenya.
Inadaiwa kuwa kati ya watu ambao walikuwa wakila “chabo” katika gazeti hilo walikuwepo Watanzania. Soma hapa. “Utamu” wa kisa hiki unaongezeka kila asubuhi huku serikali ya Kenya ikiwa haitaki kusema lolote la maana. Uraia wa jamaa wanaodaiwa kuongoza uvamizi huo umejaa utata kama ilivyo katika habari hii hapa. Na jana mmoja wao karibu atolewe ngeu na wanawake barabarani jijini Nairobi. Kama serikali zetu zimefikia hatua ya kutumia mamluki kwenye michezo yao michafu kuna kazi kubwa mbele yetu.
Wed 15 Mar 2006
Ninapoongelea masuala ya teknolojia ya blogu kwa bara la Afrika na nchi kama Tanzania, baadhi ya watu huniambia kuwa teknolojia hii haina nafasi au umuhimu kwakuwa watu wengi hawana uwezo wa kupata au kutumia tarakilishi. Ni kweli kabisa kuwa bado Afrika ina safari ndefu katika kueneza sio tu teknolojia mpya bali pia mahitaji ya msingi kwa wananchi wake. Lakini kama mtu anafuatilia kwa karibu masuala ya teknolojia mpya za mawasiliano na habari atajua kuwa hivi sasa ili uweze kuwa na blogu au kuingia kwenye mtandao wa tarakilishi (Intaneti) sio lazima uwe na tarakilishi kwani hata ukiwa na simu za mkono unaweza kuingia kwenye mtandao wa tarakilishi kutafuta au kusoma habari, unaweza kutuma barua barua pepe na pia kusoma ulizotumiwa, unaweza kusoma blogu na hata kuwa na blogu yako mwenyewe, n.k. (bonyeza hapo chini umalize kusoma habari hii.)
Mon 13 Mar 2006
Tumkaribishe kwenye jumuiya yetu, mwanablogu Frank Geofrey. Bonyeza hapa umtembelee.
Sun 12 Mar 2006
Kamusi elezo huria na uandishi wa kijamaa
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: kamusi elezo ya kiswahili , lugha , wikipediaToa Maoni [9]
Moja ya mfano mzuri wa programu au teknolojia zinazowezesha jamii kushirikiana kijamaa ni kamusi huru ya “wikipedia.” Mradi wa Wikipedia ni mradi unaowezesha watu wenye ujuzi, elimu, na maarifa mbalimbali kushirikiana kuandika kamusi elezo kwa lugha yoyote ile. Hivi sasa mradi huu una kamusi elezo za lugha mbalimbali kama kiingereza, kiswahili, kiafrikana, kilangala, kitagalogu, kiyorùbá, n.k. (bonyeza hapo chini umalize kusoma habari hii.)
Fri 10 Mar 2006
Niliwahi kuandika kuhusu jambo linalonikera sana kwenye huduma ya Blogger. Jambo hili ni kutokuwepo kwa uwezo wa kupanga mambo uliyoandika kimaudhui. Kero hii imenikaba kabali jana na leo wakati nikitafuta habari toka kwa Mwandani na Michuzi. Nilipoandika kuhusu huduma za blogger na wordpress, Jeff aliniambia kuwa huenda jamaa wa Blogger wanalishughulikia suala hilo, jambo ambalo nilikubaliana naye. Kama hukusoma niliyoandika wakati huo, bonyeza hapa. Nilimjibu kwa kumwambia kuwa sitashangaa kwani teknolojia hizi zinabadilika haraka mno. Tena nikasema niliyoandika kuhusu huduma hizo mbili huenda baada ya wiki moja yakawa sio sahihi kutokana na kubadilika kwa teknolojia kila siku.
Nimekuwa nikitafuta huku na kule ushauri wa namna ambayo tunaweza kuchaza au kudukiza (hack) huduma ya Blogger ili kuweka maudhui (kama ambavyo tumechaza/dukiza mambo kadhaa yaliyoko kwenye Blogger kama lugha, mpangilio wa mambo, n.k.). Katika tafutatafuta hiyo nimepata blogu ambayo inatoa maelezo ya jinsi unaweza kupanga mambo unayoandika katika Blogger katika maudhui kurahishisha wasomaji kupata habari au mambo uliyoandika. Sijasoma vizuri blogu yenyewe kujua cha kufanya. Nimeona niwape kwa sasa. Nitaitazama baadaye. Itazame hapa.
Thu 9 Mar 2006
Kwanini napenda blogu zetu?
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: blogu , wanablogu , Uandishi wa RaiaToa Maoni [3]
Majuzi niliulizwa ni nini faida ya blogu za Kiswahili kwangu. Nilitaja sababu mbalimbali ila mojawapo ningependa niwaeleze. Huko nyuma vyanzo vyangu vya habari vilikuwa ni tovuti kama za BBC, Democracy Now, na magazeti mbalimbali mtandaoni na pia tovuti kadhaa za habari. Siku hizi nimebadili utaratibu huo. Kitu cha kwanza kabisa ninapoamka asubuhi au hata usiku wa matisa ni kutembelea blogu zote za Kiswahili. Uzuri wa kusoma blogu ni huu: habari za kwenye magazeti mtandaoni au tovuti za habari ni kavu sana. Unasoma habari inasema: Tukio A limetokea mahali B. Kwenye blogu habari zina uhai zaidi. Utapata habari kuhusu tukio A kutokea mahali B kama ilivyo kwenye magazeti. Au kiongozi fulani kafanya upuuzi fulani. Lakini utapata maoni na uchambuzi toka kwa mwanablogu kuhusu tukio au jambo lenyewe. Halafu kwenye maoni utapata mawazo ya wasomaji. Wakati mwingine wasomaji hujazia habari hiyo kwa kutoa viungo vya tovuti vinavyohusiana na jambo lenyewe au kuongeza taarifa wanazozijua.
Katika uchambuzi wanaoutoa wanablogu, utakuta wakati mwingine wanaweka viungo vingi tu kutusaidia kuelewa kwa undani jambo lenyewe. Wakati mwingine wanaweka na picha. Na pia kutupa habari za nyuma au historia inayotusaidia kuelewa tukio lililotokea leo hii kwa mapana yake. Tazama, kwa mfano, aliyoandika Msaki wa Kurunzi kuhusu noma la Mahalu. Kashusha viungo na picha kibao. Katupa taarifa za nyuma ambazo zinatusaidia kuelewa noma yenyewe kwa mapana yake. Bonyeza hapa kama hujamsoma. Au kuna habari ya orodha ya majambazi Tanzania (hii imenikumbusha mzee wa “Nji hii” Mrema wa Kiraracha alipoagiza wananchi kumpelekea ofisini kwake majina ya majambazi) ambayo Jeff wa Harakati kaiandikia. Jeff sio tu ametupa kiungo cha habari hiyo bali ametoa mawazo yake, akauliza na maswali. Kaandika hapa.
Mwandani akachangia kwa kuongeza kiungo cha habari hii hapa. (mwandani, nilishindwa kukipata kiungo vizuri, ila sasa nimefanikiwa).
Habari, mawazo, na viungo vyote ninavyopata toka kwenye blogu vinanisaidia sana maana ninakuwa sina haja ya kutembelea kila tovuti ya habari peke yangu. Inakuwa kama tunasaidiana badala ya mtu mmoja kutafuta habari hizo mwenyewe. Kuna wakati pia napata habari toka vyombo vya habari Tanzania, lakini habari zenyewe zinakuwa zina mapungufu fulani. Mara nyingi blogu zimekuwa zikinisaidia kunipa picha halisi inayojazia mapungufu ya kwenye habari za magazeti. Kwa mfano, nadhani jana, kulikuwa na picha ya jamaa wa Mkono wa Matumaini wakizindua tovuti yao. Hakukuwa na anuani ya tovuti yenyewe. Ninazunguka mtandaoni nikiitafuta bila mafanikio. Kupiga hodi kwa Egidio nakuta ametuwekea anuani yenyewe. Tazama hapa.
Wakati mwingine blogu huwa zinasaidia kukufanya utambue kuwa hauko peke yako katika kuwaza mambo fulani fulani. Unaweza kuwaza jambo ukajiuliza kama ni wewe mwenyewe au kuna wengine wanawaza hivyo? Ukihisi kuwa ni wewe mwenyewe wakati mwingine unaweza kujiuliza, “Nimechanganyikiwa nini? Mbona watu wengine hawawazi hivi?” Lakini ninapoingia kwenye blogu zetu ninakutana na watu kibao wenye kuwaza kama mimi. Kwa mfano, leo nimekutana na aliyoandika Jeff Mdogo. Msome hapa.
Ni hayo machache wandugu. Ni furaha na msisimko wa blogu zetu vimenisukuma kuandika haya machache.
Wed 8 Mar 2006
Hii ni sehemu ya pili ya mjadala kuhusu neno la kiswahili la teknolojia ya blogu. Niliamua kuendeleza mjadala huu baada ya Makene kutuamsha kama alivyoandika hapa. Kama hukusoma sehemu ya kwanza, bonyeza hapa uisome.
Leo nimeona njia nzuri ya kuendeleza nilipoishia ni kutazama maoni ya wasomaji waliyoyatoa baada ya kuandika hiyo sehemu ya kwanza. Hatua hii itasaidia kuendeleza mjadala hatua kwa hatua bila kuacha masuala na maswali ya msingi hewani.
Jeff aliandika maoni haya:
Kama unakumbuka ule mfano wangu wa bahari na samaki basi blogu ni gazeti na gazeti ni blogu pia. Tofauti ni katika uhuru wa kuchangia na kumiliki. Unajua mimi naweza kuona picha ya mtu nikasema ni mzee na mwingine akaiona akasema ni binti kigori. Swali litakuwa je wote tumeona?? Jibu rahisi ni ndio. Lakini tumeona kisha tukafanya tafakuri gani. Kasheshe
.
Jibu langu kwa Jeff ni kuwa mfano alioutoa wa picha ya mtu kuonekana kuwa ni mzee au binti kigori ni kuwa watu tunaweza kuona kitu kwa namna mbalimbali, lakini ukweli wa kitu chenyewe unategemea sisi tunavyoona au kitu chenyewe? Kwa mfano, mtu kama ni mzee, mimi nikamuona kuwa ni kijana ina maana kuwa mtu huyo ni kijana? Ukweli wa mtu huyo kuwa ni kijana au mzee unategemea mtazamo wangu au unategemea vipimo vya nini ujana na nini uzee?
Mimi nadhani kuwa suala la blogu kuwa ni gazeti na gazeti ni blogu sio la kila mtu anavyoitazama teknolojia hii. Mtu akiwa ni mzee tukamtazama na kusema kuwa ni mtoto mchanga, hatabadilika kuwa mtoto mchanga. Atabaki kuwa mzee licha ya mtazamo wetu.
Katika kisanduku cha maoni nilimuuliza Jeff swali hili: kama blogu ni gazeti na gazeti ni blogu, je ippmedia.com na mbongo.com au kumekucha.com ni blogu? Kama jibu ni ndio basi tukubaliane kuwa blogu zilianza zamani sana maana magazeti kuwa mtandaoni kama ippmedía.com yameanza kabla hata neno “blog” halijazaliwa. Tukikubaliana kuwa ippmedia.com ni blogu, je itakuwa sahihi tukisema kuwa waandishi wa Nipashe, Alasiri, the Guardian ni wanablogu? Je tunaweza kusema kuwa Business Times au the Express ni blogu?
Mwanablogu Mark aliandika haya:
Wenye hoja naona mmefika mapema maana mjadala huu unawahusu kwelikweli. Sasa kumbukeni kuwa ni ninyi mnaotakiwa kufikia tamati ya hoja hasa Ndesanjo maana yeye anatohoa maana za kiteknolojia ili kututia cheche sisi ambao hatuna taaluma hizi. Huyu Ndesanjo ananikumbusha wimbo wa “Banda wa Malawi kutuvalia ngozi ya Chui kututisha watanzania” Enewei hapa natania lakini maelezo haya ya Ndesanjo hayabadiliki kila mara na yeye hatoi majibu na mapendekezo yake, vipi utatoa mapendekezo lini?
.
Nilimjibu hivi (nilikosea siku nilipotoa maoni hayo nikamwita Boni badala ya Mark ndio maana nimefuta jina la Boni):
Siwezi kuficha
BoniMark, kutohoa neno la blogu imekuwa zoezi gumu sana kwangu. Nimefikiria sana, kila ninalofikiria ninaona lina walakini. Labda ninawaza sana. Ninachagua jina, kisha nalitazama kila upande na kukuta halielezei hasa blogu. Kwahiyo nikajisemea ingawa sina pendekezo, sio vibaya kutoa mawazo yangu juu ya mapendekezo yaliyopo na pia juu ya jinsi ninavyoitazama teknolojia yenyewe. Ingawa umesema kuwa umetania kuhusu kutisha watu, wako wengine wanaweza kudhani kuwa maelezo hayo ni ya kutishia. Ukweli ni kuwa maelezo hayo ni kutusaidia wote na wengine ambao wana nia ya kutumia teknolojia hii. Masuala ya blogu napenda kuyazungumzia sana kiasi ambacho naona kuna watu walio karibu nami wanaanza kugusana nikitaja neno blogu. Kwahiyo mchango wangu kwa sasa, kutokana na kushindwa kabisa kupata neno la kupendekeza, ni kujaribu kuchambua na kutoa maswali ambayo yanaweza kwa namna moja au nyingine kutusaidia kufikia uamuzi sahihi
.
Mwandani naye akachangia. Akasema hivi:
Blogu ni blogu, na gazeti ni gazeti. Sawa na njiwa ni njiwa na tetere ni tetere. Wanafanana, wote ni ndege wanaoruka lakini njiwa si tetere. Ukiangalia magazeti kama ya Guardian na mail kwenye mtandao kuna kijisehemu ambacho ukitaka kublogu unaweza kujiunga kublogu. Lakini hicho ni kiunganishi ndani ya gazeti la mtandaoni, wakati gazeti limebaki pale pale kuwa gazeti. Na kiunganishi kitakupeleka kwenye kublogu. Basi ukishaingia huko kublogu miye nasema asilani haiwezekani ukawa unahariri gazeti au kutengeneza gazeti mtandaoni. Misingi ya gazeti kama guardian kwenye mtandao au kwenye karatasi inabaki pale pale. Wewe utakuwa unablogu wala hautakuwa unaandika gazeti. Miye naona blogu ni njia au uwanja unaowapa nguvu jamii kufanya harakati, kujitangaza, kujishaua au kuandika wanayotaka iwe kuhusu maua, magari, mapenzi hata siasa. Tafadhali tutenganishe mambo haya. Tusiwasingizie njiwa kwa kuwaita tetere. Japo jina la kupendekeza sijatoa nadhani ni muhimu kuchagua jina linalokaribia dhana ya kublogu wala si vyenginevyo. La muhimu zaidi ni kuwa waasisi wa kublogu kwa kiswahili ndio siye,na tunajua maana yake ni nini. Ikiwa hatutaweza kutoa jina nachelea huko kutakuwa ni kukosa uongozi. Kama kuna kupiga kura, miye kura yangu nishaishika. Nasubiri kuitosa kwenye kasha
.
Jambo analozungumzia Mwandani hapa ni la muhimu sana. Anatema kuwa magazeti yaliyoko mtandaoni, kwa mfano, Mail and Guardian la Afrika Kusini, yana kisehemu cha blogu. Yapo magazeti kama Mail na Guardian ambayo yana blogu katika kurasa zao kwa ajili ya wasomaji, mengine kama Guardian la Uingereza yana blogu za waandishi wake na mengine kama News and Record ambayo yana kisehemu cha blogu za wasomaji, wahariri, na waandishi wake.
Kwahiyo swali ambalo tunaweza kujiuliza hapa ni hili: kama blogu ni gazeti na gazeti ni blogu kwanini tovuti za magazeti haya zina kisehemu kiitwacho “blog”? Itakuwa ni sawa na magazeti haya kuwa na kisehemu kiitwacho “gazeti.” Sijui kama nimefafanua vizuri hoja ya Mwandani.
Jambo jingine analogusia Mwandani ambalo ni la kutazama vizuri ni mfano wake wa njiwa. Tunaweza kusema kuwa ndege huruka, na njiwa anaruka hivyo ni ndege. Lakini sio sahihi kusema kuwa kila ndege anaruka au kila mnyama arukaye ni ndege. Hii itakuwa ni sawa na kusema kwakuwa gazeti ni chombo cha habari cha maandishi (yaani tofauti na redio au luninga) basi blogu ni gazeti kwakuwa ni chombo cha habari cha maandishi. Tatizo tutakalokumbana nalo hapa ni hili: blogu nyingi ni za maandishi lakini zipo blogu za video, picha, na sauti.
Kila mwaka Redio Ujeremani huwa inatoa tuzo ya blogu duniani. Tazama hapa. Tuzo hii huwa haiendi kwa gazeti hata moja kwasababu moja kubwa: hii ni tuzo ya blogu na sio magazeti. Mashindano haya ni kwa ajili ya blogu kama ya Global Voices (ambayo ilipata tuzo mwaka jana) na sio magazeti kama the Christian Science Monitor, au Daily Standard (ambalo hivi majuzi lilivamiwa kininja na serikali ya Kenya).
Mwandani aliendeleza maoni yake. Aliandika hivi:
web - log = weblog = blog.
Web = mtandao
log = nyaraka, diary nk.
Nadhani hii ndio asili ya blog. kama tunataka kutafsiri moja kwa moja, tusianzishe maana tofauti na hiyo ya weblog kama hatutaki kuanzisha chombo tofauti na blogu
.
Alichofanya Mwandani katika maoni haya ni kuzungumzia jambo ambalo nitalizungumzia katika sehemu ya tatu. Ni muhimu sana kuipata historia ya blogu. Kama alivyosema Mwandani, neon “blog” linatokana na neno “weblog” (webulogu) ambalo lilifupishwa kuwa “blog.” Neno “log” lilichukuliwa kutokana na mpangilio wa habari katika blogu ambapo habari mpya huwa ziko juu na zile za zamani ziko chini. Pia kuwepo kwa tarehe na saa ya wakati habari au jambo lilipoandikwa na mhusika.
Mkwinda naye hakubaki nyuma. Yeye anashauri tutazame asili ya neno hili kama alivyofanya Mwandani. Lakini pia anasema kuwa pengine ni vyema kubaki na neno lililopo. Soma maoni yake:
Mie binafsi nashindwa kuelewa vipi mjadala huu unavyoendelea kiasi cha watu kuumiza vichwa vyao,Binafsi nadhani tungerudi nyuma kuangalia nini hasa usuli wa neno hili Blog tukipata usuli wake nadhani hakuna utata tena juu ya mjadala huu.
Mara nyingi asili ya neno hunasibishwa na sababu za kuwepo kwa neno hilo,mathalani kuna majina mbalimbali ya makabila ambayo asili yake hunasibishwa na matukio halisi ya jina au neno, Mathalani jina langu mimi la ukoo naitwa Mkwinda, baada ya kufuatilia kwa kina asili ya jina hili kumbe nikaja kugundua kuwa babu yangu alikuwa akipendelea sana kuvaa msuli ambao kwa lugha yetu ya kule Kilwa msuli huitwa KIKWINDA… yaani ukivaa msuli lazima uukunnje na kuufungia mkanda kiunoni ndiyo hasa maana ya Kikwinda, lakini baada ya neno hili kupitia katika vinjwa na lahaja za watu wa aina mbalimbali hatimaye tukajikuta tukiitwa akina Mkwinda.
Nilikuwa najaribu kuweka bayana asili ya maneno mbalimbali kulingana na mazingira ya sehemu. Sasa hebu nirejee katika hii mada ya Blogu, lazima tukubali maneno mengine hayabadiliki kutokana na uasili wake, mathalani leo hii watu tunajaribu kudadavua na kulitohoa neno Kompyuta kwa kulitafutia neno mbadala la kiswahili,huu ni upotoshaji ambao vizazi vijavyo vitashindwa kujua nini asili ya neno hilo kwa kulitafutia neno jingine la lugha ya kiswahili tukiacha asili yake na mengine huwa ni majine ya waanzilishi ya kitu hicho.
Tunapoamua kujadili neno Blogu tuangalie nini maana ya blogu na asili yake kisha ndipo tunaweza kujivunia kwamba tumeanzisha kitu lakini kama kimeanzishwa na mtu asiye kuwa mswahili kwa nini tuendelee kuumiza vichwa kwa vitu ambavyo si asili yetu, tumuache muanzilishi wa blogu ajivunie uasisi wake. Kidogo Mwandani alitaka kuonesha namna ambavyo tunaweza kuanzisha jina ambalo halitofautiani na blogu, tukubali tukatae lazima turejee katika asili ya neno blogu ndipo tutapata neno la kiswahili. Wakatabahu
.
Maitha naye akachangia:
mkwinda na mwandani wameyasema yote , neno blogu latosha kwani tukichukua haja ya kuswahilisha kila neno basi tutajikuta tukiandika kamusi nzima!
.
Hoja ya kuwa tubaki na neno tunalotumia sasa aliwahi kuitoa Mwaipopo huko nyuma. Binafsi nadhani kuwa wakati huu ni mapema sana kunyanyua mikono. Mwaipopo anasema:
Sema wewe Mkwinda, nikisema mimi naonekana nimeathirika na ukoloni. Niliwahi kuyasema haya kwa namna nyingine, tena ya kitaaluma lakini wapi. Nafikiri ilikuwa pale kwa Jeff kabla hata sijaanza kublog.Wajuba wameng’anga’nia pasi na kuwa na hoja ya kitaaluma bali ushabiki na papara. Sasa basi ikiwa leo tumeamua ‘ku-decolonise’ lugha kwa nini tuhangaikie neno lilozuka jusi tu na tusianze na maneno kama ‘rais’ au ‘jamhuri’(haya yalitokana na asili ya kiarau). Hoja si kutafuta jina la kiswahili basi rais mathalani tumwite ‘Kakakuru’, jamhuri tuiite ‘ngelubi’. Si tunang’aka ukoloni mwisho. Lugha itakosa utamu na ladha.Nilisisitiza pale hata Kizungu (King’eng’e) kinatumia maneno lukuki kwa muundo uleule wa lugha asili yake. Kizungu kingali-decolonise leo kingalikuwa lugha masikini sana ya istilahi, pengine kisingalikuwa na matumizi tando (yaliyotanda) kama kilivyo leo hii. Labda tungalikuwa bado tunatumia kirumi, kwacho Kingeleza kimekopa sio mchezo. Lakini wengi wape bwana.
.
Da Mija naye akaweka neno lake:
Wajameni!..Wajameni!..
Maji tulishayavulia nguo, haitakuwa busara kuyakimbia
.
Baadhi yetu wametoa ushauri kuwa tupige kura. Idya ana mawazo tofauti na suala la kupiga kura. Anasema:
Tatizo la kupiga kura ni lile nililowahi kutamka awali; demokrasia na mkumbokrasia. Semokrasia inasema wengi wape hata kama wamefuata mkumbo. Lakini naamini kwamba sisi si wafuata mkumbo kwa hivyo demokrasia itachukua mkondo wake. Lakini kweli tupige kura sasa hivi? Bado hatijachelewa sana. Mjadala unaweza kuendelea lakini tuache nadharia nyingi mno. Tusifanye mjadala uwe kama nadharia za kitaaluma. Tuendelee kujadili nadhani muafaka haupo mbali
.
Ninakubalina na Idya kuwa muafaka tutaufikia ila ninapingana naye kidogo kwenye suala la nadharia maana ninadhani kuwa bila nadharia hatutaweza kupata nafasi ya kuelewa teknolojia hii kwa undani. Tunaweza kubobea kwenye vitendo, yaani kublogu lakini tukawa hatujatazama masuala fulani ya kinadharia ambayo yanaweza kufungua milango mingi zaidi ya mjadala huu. Nadhani ili tukipe kitu jina lazima tukifahamu, sio kwa kuwa tu tunakitumia (vitendo) bali hata kinadharia. Tazama kwa mfano swali kuhusu blogu kuwa ni chombo/zana au ni mahali. Kuna watu wameita blogu “uwanja” ambapo unaona kuwa wamechukulia blogu kuwa ni mahali. Wengine wametoa majina ambayo yanaonyesha kuwa wanachukulia blogu kuwa ni chombo/zana. Mjadala wa blogu kuwa ni chombo/zana au uwanja, au vyote ni mjadala wa kinadharia. Ninaendelea kutoa hoja ya awali kuwa gazeti sio blogu na blogu sio gazeti.
Itaendelea
Wed 8 Mar 2006
Jabali la muziki Afrika, Ali Farka Touré ametutoka. Kama alivyokuwa marehemu Hukwe Zawose, Ali Farka Touré ni sawa na ule msemo wa “nabii hasifiki kwao.” Afrika haikuwa ikimfahamu na kumthamini kama wapenzi wa muziki wa mataifa mengine. Muziki wa Ali Farka Touré ulipoanza kuingia nchi kama Marekani, wanamuziki na wanahistoria walishtuka sana kutokana na mahusiano ya karibu kati ya muziki wake na muziki uliozaliwa miongoni mwa watu weusi nchini Marekani, Blues. Watafiti ambao wamekuwa wakitafiti chimbuko la muziki wa Blues wamekuwa wakitumia muziki wa Mali, hasa wa Ali Farka Touré, kuonyesha mahusiano kati ya muziki huo wa Blues na muziki wa Afrika. Binafsi huwa nawaweka Hukwe na Ali Farka Toure kwenye kundi moja. “Jamaa” zetu wanapowazungumzia wanamuziki kama akina Mozart na Bach kwa heshima isiyo na kifani, sisi tunaweza kuwazungumzia akina Hukwe na Ali. Lakini kwakuwa huwa hatuna muda wa mambo yetu, wengi wetu Hukwe au Ali huwa tunawasikia kwenye bomba.
Soma historia yake fupi hapa (mwishoni mwa historia hiyo kuna viungo kadhaa). Pia sikiliza mahojiano yake hapa na gitaa lake katika albamu ya Niafunké kwa kubonyeza hapa.
Tue 7 Mar 2006
Samahani wanablogu wote na wasomaji wetu. Nilikumbwa na kisanga kilichonizuia kuweza kuwepo uwanjani. Kutokana na kisanga chenyewe ilikuwa sio ustaarabu kwangu kukaa mbele ya tarakilishi katika kipindi chote hiki. Nilishindwa hata kuandika makala kwa ajili ya safu yangu katika gazeti la Mwananchi.
Nimepitwa na mambo mengi sana. Nitaandika, hasa kuendeleza mjalada wa neno la blogu na mengine. Na zaidi kusoma blogu zote ili kujua yanayoendelea. Najua nimepitwa na mengi: habari, changamoto, mashairi, visa, vichekesho, n.k. Nimegundua kuwa blogu na mtandao wa tarakilishi kwa ujumla ni kama vile ulevi fulani. Kama unga vile. Ilikuwa vigumu mno kukaa nje ya mtandao katika kipindi chote hiki. Nitaandika. Kisha nitawatembelea wanablogu wezangu.



