Kuanzia sasa kutakuwa na maudhui yaitwayo “zana” ambayo kazi yake ni kutoa taarifa za zana mbalimbali ambazo zinaweza kuwa muhimu kwa wanablogu au kwa mtu yeyote anayefuatilia mabadiliko ya zana za habari na mawasiliano. Kwa mfano, kuna huduma mbalimbali ambazo unaweza kutumia ili kuwezesha wasomaji wako wawe wanapokea habari unazoandika kwa njia ya barua pepe. Bonyeza hapa uzione huduma hizo.
April 2006
Thu 27 Apr 2006
Wed 26 Apr 2006
Kuna wanablogu wawili wa Tanzania wanaoandika kwa kiingereza wameingia ulingoni hivi karibuni. Mmoja wao ana staili yake ya kuchanganya Kiswahili na kiingereza. Bwaya aliandika majuzi kuhusu mwanablogu huyu mpya ambaye anaandika masuala ya Ukimwi. Mtazame hapa. Na Mwandani katuandikia kuhusu huyu mwingine anayechanganya Kiswahili na kiingereza ambaye atakuwa akiandika zaidi masuala ya kiuchumi. Mtazame hapa.
Baada ya kusema hayo napenda kukumbusha wanablogu wapya na pia wale wa zamani wasisahau kuorodhesha blogu zao kwenye ukurasa wa “wiki” wa blogu zetu. Ninaupitia mara kwa mara ila wakati mwingine kuna kutingwa kiasi cha kushindwa kuweka blogu mpya mara zinapojitokeza. Kumbuka kuwa ukurasa huu unatumia teknolojia ya “wiki” hivyo mtu yeyote anaweza kuongeza au kufanya marekebisho kwa kubonyeza panaposema “edit.” Bonyeza “edit” iliyo juu ya kifungu unachotaka kuandika au kurekebisha. Bonyeza hapa kama hufahamu ukurasa huo Ukifanya mabadiliko ndani ya ukurasa huu sio lazima ujiandikishe, ila ni vyema ukifanya hivyo kwa ajili ya rekodi.
Wed 26 Apr 2006
Blogu zinabadili mambo. Mwanazuoni mwenye siasa kali za kihafidhina, David Horowitz, ameandika kitabu kiitwacho The Professors: 101 Dangerous Academics in the US :
Katika orodha hiyo, yumo mwanazuoni toka Kenya, Ali Mazrui. Sijui kama unafahamu kuwa Profesa Mazrui aliwahi kuzuiwa uwanja wa ndege kwa kushukiwa kuwa anaweza kuwa na mahusiano na yule jamaa mwenye madevu anayeishi mapangoni akila tende na kunywa maziwa ya kondoo na ngamia! Bonyeza hapa usome kisa hicho.
Bonyeza hapa usome orodha ya maprofesa hao akiwemo Ali Mazrui.
Tue 25 Apr 2006
Ile sheria mbovu kabisa iliyokuwa na nia ya kuingiza wezi na matajiri madarakani na kuzuia kabisa haki na nafasi ya walalanjaa kupata nafasi za uongozi, takrima, imetupiliwa mbali. Hii ni sheria ambayo chama twawala kilidai kuwa eti inaendana na ukarimu na utamaduni wa Watanzania. Nilikuwa nashangaa sana ukarimu gani huo ambao huwa unajitokeza kila baada ya miaka mitano? Huenda umeisoma habari hiyo ya mahakama kuu kuitupilia mbali. Kama hujaisoma, bonyeza hapa.
Sun 23 Apr 2006
Wiki iliyopita niliandika kuhusu blogu ya Jikomboe kupendekezwa katika tuzo ya Kaybees 2006 kwenye kundi la blogu zisizo za kiingereza. Bonyeza hapa iwapo hukusoma niliyoandika. Matokeo ya tuzo hiyo iliyoandaliwa na jumuiya ya Kenya Unlimited (KuL) yametolewa.
Ingawa nilipata habari hizi toka Ijumaa sikutaka kuandika chochote juu yake maana nilikuwa kwenye mapumziko ya siku mbili. Sikutaka kuvunja ahadi niliyojiwekea ya kutoandika chochote katika kipindi cha mapumziko. Ninachukua nafasi hii kuwashukuru waandaaji wa tuzo hii kwa kuipa blogu hii ya Jikomboe tuzo maalum ya Outstanding Member Award.
Thu 20 Apr 2006
Pamoja na kutingwa na kazi kubwa ya kutafsiri leseni za Creative Commons kwa ajili ya tawi la Creative Commons Tanzania, habari njema zikinijia siwezi kujizuia. Kwanza kabisa Boniphace katutaarifu kuhusu kuongezeka kwa waandishi na wanasafu wa gazeti la Mwananchi (ambalo nami ni mwanasafu wake) katika jumuiya ya wanablogu wa Tanzania (Jeff, Tanzania Daima mna kazi kubwa!). Anatuambia kuwa Midraji Ibrahim amekata shauri. Mtazame hapa.
Wakati huo huo ndugu Lucassano anasema kuwa tumemsahau kwani ameanza kublogu siku nyingi na blogu yake inazungumzia masuala ya soka. Bonyeza hapa umsome. Lakini lazima niseme kuwa nimeingiwa na furaha isiyo na kifani baada ya mwanasafu ambaye naweza kusema jumuiya ya blogu ilikuwa ikimsubiri kuamua kukata shauri baada ya kusoma makala kuhusu blogu. Huyu ni mwanasafu maarufu wa makala za kejeli, ndugu Chesi Mpilipili. Mkaribishe kwa kubonyeza hapa.
Wed 19 Apr 2006
Makala kuhusu teknolojia ya blogu nilizozungumzia jana (bonyeza hapa kama hukusoma niliyoandika jana) ninaziweka hapa ili zisomwe na wale ambao walipitwa na gazeti la Mwananchi au ambao wako Ughaibuni. Makala hizi, ziko katika sehemu tatu, niliandika kwa ajili ya safu yangu ya kila jumapili katika gazeti hilo. Kwa wanablogu, mambo mengi niliyoandika mnayafahamu. Tumekuwa tukiyazungumza mara kwa mara. Sikuandika kwa ajili ya watu ambao tayari ni wanablogu maana ingekuwa ni sawa na “kuhubiria wanakwaya.” Niliandika kwa ajili ya watu ambao hawajui teknolojia hii au ambao wanaisikiasikia. Haya, hizi hapa (bonyeza juu ya vichwa vya habari uzisome): Ndesanjo, Hivi Blogu ni Nini? – 1, Ndesanjo, Hivi Blogu Ni Nini? – 2, Ndesanjo, Hivi Blogu Ni Nini? - 3
Tue 18 Apr 2006
Ni furaha kubwa kuona kuwa tuzo ya blogu ya Kaybees 2006 imetambua mchango wa blogu ambazo sio za kiingereza. Tuzo hii iliyoandaliwa na jumuiya ya wanablogu wa Kenya, Kenya Unlimited (ambayo mimi ni mwanachama…mambo ya jumuiya ya Afrika Mashariki haya!) ingeweza kuhusisha blogu za kiingereza tu kwakuwa blogu karibu zote katika jumuiya hii ni za kiingereza. Katika blogu ambazo zimependekezwa katika kundi la blogu zisizo za kiingereza (kura zitapigwa ili kupata blogu moja katika blogu 7 zilizopendekezwa) zipo blogu za Kiswahili, Sheng, na Gikuyu. Moja ya blogu hizo ni hii ya Jikomboe, jambo ambalo nachukulia kuwa ni heshima kwa blogu zote za Kiswahili. Orodha ya blogu zilizopendekezwa utaisoma ukibonyeza hapa.
Tue 18 Apr 2006
Mwanablogu mpya Severini na makala kuhusu blogu
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: blogu , wanabloguToa Maoni [7]
Kwa wiki tatu mfululizo nimekuwa nikiandika makala kuhusu teknolojia ya blogu katika safu yangu ya kila jumapili katika gazeti la Mwananchi. Makala hizo nia yake ilikuwa ni kutoa habari njema kwa Watanzania kuhusu teknolojia hii. Habari njema hizi zimepokelewa kwa msisimko mkubwa kwa wale ambao wameshtuka kumbe wanaweza kuwa wanahabari bila kusubiri wapate mtaji wa kuanzisha chombo cha habari. Msisimko huo umewapata pia wale waliofunguka macho kwa kujua kuwa Watanzania tuko kwenye mtandao na blogu zetu tukiwasiliana, tukitoa maoni, tukielimishana, tukitoa picha, katuni, hadithi, mashairi, n.k.
Mmoja wa wasomaji walioguswa na makala hizo na kuamua kuanzisha blogu zao ni Severini Mushi. Huu ni waraka aliondikia:
Sun 16 Apr 2006
Jeff, Tanzania Daima nanyi naona mnaanza kuja juu. Mwanasafu wa gazeti la Tanzania Daima,
Innocent Kahwa ameanza kublogu. Mtembelee na kumsabahi hapa.
Fri 14 Apr 2006
Zinapokuja blogu za watengeneza filamu ujue moto umewaka…na Wanjiru naye pia
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: blogu , wanabloguToa Maoni
Amini usiamini, mapinduzi haya ya blogu yatakuja kuwezesha watu wengi. Unajua tuna wanablogu washairi, wana vikaragosi, waandishi wa riwaya, wapiga picha, walimu, wachambuzi wa masuala ya kisiasa, kiuchumi, na kitamaduni, n.k. Sasa wanakuja hata watengeneza filamu. Na aliyeingia kijijini kwetu ni ndugu Sultan Tamba, mwandishi na mtengeneza filamu za Kiswahili nchini Tanzania. Kama ilivyo desturi yetu ya kuwatembelea wanablogu wapya na kuwakaribisha, bonyeza hapa umkaribishe. Karibu sana ndugu Sultan.
Rafiki yangu Wanjiru, mwanadada toka Kenya anayeishi Marekani, ametiwa moyo na blogu zetu za Kiswahili (ingawa anasema Kiswahili chetu kinampa tabu kidogo). Hivyo naye ameanza kublogu (kwa Kiingereza) akisema kuwa uchoyo, tamaa, na ulafi ni tatizo kubwa linalomkabili mwanadamu. Mtazame hapa.
Sun 9 Apr 2006
Mwezi uliopita niliandika habari iliyosema, “Masikini Ali Mazrui.” Niliwapeni makala zilizoandikwa na wanazuoni Prof. Ochieng na Taban Lo Liyong wakimchamba Prof. Ali Mazrui. Nikasema nitakuwa na hamu sana ya kujua majibu ya Ali Mazrui. Bonyeza hapa usome niliyoandika siku hiyo. Sasa Mazrui amewajibu. Liyong alimshambulia Mazrui. Bonyeza hapa. Kisha Mazrui akajibu mapigo. Bonyeza hapa. (asante sana Maitha wa Mawazo na Mawaidha ambaye ametumia kipezatasi (scanner) kutuletea makala hiyo). Makala ya kumshambulia Mazrui toka kwa Prof. Ochieng binya hapa. Na majibu ya Mazrui bonyeza hapa. Utaona Mazrui anamwambia Ochieng watafute siku waende wakajadili ana kwa ana ndani ya chuo kikuu cha Makerere. Sasa sijui akina Ochieng na Liyong watajibu au ndio mchezo umeisha.
Sun 9 Apr 2006
Usisahau Tuzo ya Blogu za Kenya, Kaybees Awards 2006
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: blogu , wanabloguToa Maoni [3]
Msisahau kuwa tarehe 9 mwezi huu ndio mwisho wa kuchagua zile blogu za ndugu zetu wa Kenya ambazo mngependa zipewe tunzo kwenye ile tuzo mpya iitwayo Kaybees Awards 2006. Kama wewe huwa unasoma blogu za Kenya, basi chukua dakika chache uchague zile unazoona zinafaa kutuzwa. Kwa mfano, kuna ndugu yetu wa Mawazo na Mawaidha, ambaye najua mnasoma maana yuko kwenye blogu zetu za Kiswahili. Kuna dada yetu Mshairi (ambaye mimi husoma sana), kuna Kenyan Pundit, ambaye ndiye kati ya watu walionifanya nikaanza kublogu, kuna Akiey, ambaye huwa anatembelea sana blogu zetu. Kuna akina Mental Acrobatics na wengine ambao unaweza kuwapata ukienda hapa. Sijui ninyi huwa mnawasoma akina nani. Basi usisahau kushiriki.
Sun 9 Apr 2006
Hujawahi kuhudhuria onyesho la Rege maisha yako yote kama hujamuona Babu Burning Spear. Ijumaa nilikwenda kwenye onyesho la Babu Burning Spear (jina lake la zamani ni Winston Rodney), ambaye ni mwanablogu mwenzetu (tazama blogu yake hapa). Nimefika kwenye ukumbi wa Ziggy’s kwenye saa tatu usiku nikiwa na mshikaji wangu Mike (ambaye hii ni mara ya nne anamuona Spear). Mlangoni tunachekiwa kama tuna silaha, tunaonyesha tiketi na vitambulisho, kisha tunaingia ukumbini. Ukiingia unapokewa na harufu nzito ya “lile jani.” Ukumbi umeanza kujaa. Weusi, weupe, wahindi, waarabu, wajapani, n.k. Vijana, wazee, wanawake, wanaume. Muda si mrefu ninatambua kuwa ile kanuni ya “puff, puff, pass” inatumika hapa ukumbini. Kama huifahamu kanuni hii basi nenda kwenye onyesho la Burning Spear, utaambiwa. Puff, puff, pass. Hakuna kuruka kijiji. Ushirika. Ujamaa.
Sat 8 Apr 2006
Ewe Mwanablogu: Lifahamu Azimio la Dodoma
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: blogu , wanabloguToa Maoni [7]
Nilitaka kuandika juu ya Burning Spear. Ila habari ya kuwa wanablogu tuna Azimio la Dodoma imeningia hadi kwenye mifupa. Inaonyesha kuwa tunasonga mbele kama jumuiya tukiwa na watu ambao wanapenda kuona jumuiya hii ikiwa na maadili yanayoeleweka. Sijui ninyi. Mimi nimefurahia sana Azimio la Dodoma. Ningependa tuliweke kwenye blogu zetu na pia tulijadili. Shukrani ziwaendee mzee wa Kurunzi, Mark Msaki, Miruko, Hudson, na Martha. Bonyeza hapa ulisome. Na pia soma habari yenyewe toka kwa Miruko na picha zao kwa kubinya hapa.
Fri 7 Apr 2006
No one remembers Old Marcus Garvey….(wimbo wa Burning Spear huo)
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: MuzikiToa Maoni [7]
Nambiza utanionea gere…au unabisha? Ninavyoandika hapa nimekamata tikiti ya onyesho la mzee wetu Burning Spear. Kabla Bob Marley, anayechukuliwa kuwa ndiye baba wa Rege, hajaanza kupiga marege, mzee mzima Burning Spear alikuwa tayari anatangaza injili kwa mujibu wa nabii Marcus Garvey. Sidhani kama kuna mwanamuziki wa rege aliyemwimba Garvey kama Burning Spear. Nikimaliza kuandika hapa ni kuanza safari ya kuelekea ukumbi wa Ziggy’s Rock ambako ndiko atakuwa anamwaga hisia leo. Burning Spear, ambaye jina lake hilo alilichukua toka kwa mzee Jomo Kenyatta, ni kati ya wanamuziki wa rege ambao wamejitahidi kutunza “roots reggae” kimidundo na pia ujumbe. Ingawa ni mzee wa makamo, bado anaendelea kutangaza falsafa ya Urastafari ya amani na upendo.
Burning Spear hayuko nyuma kwenye masuala ya teknolojia, kwani pamoja na tovuti yake hii hapa, yeye ni mwanablogu mahiri! Bonyeza hapa umsome. Naamini hata Bob angekuwepo angekuwa mwanablogu. Lakini nadhani ningekuwa napendelea kusoma blogu ya Peter Tosh zaidi ya blogu ya Bob Marley (utajaza mwenyewe nina maana gani!). Kwa sasa ngoja nikuache na picha ya mzee Burning akiwa na mabinti zake na mjukuu wake, Naillah. Bonyeza hapa. Tunga, ulie tu!
Thu 6 Apr 2006
Nimemtembelea Kasri la Mwanazuo nikakuta habari njema. Magazeti-jadi ya Tanzania (yaani yale ya kuuzwa mtaani) yanayoingia kwenye mtandao wa tarakilishi yanaongezeka. Magazeti ya Mwananchi, Mwanaspoti, na the Citizen yameingia mtandaoni. Nimekuwa nikiyasubiri kwa muda mrefu sana hadi nikasahau kuwa nilikuwa nayasubiri. Ninafurahia, sio tu kwakuwa ninaandikia gazeti la Mwananchi, bali kwakuwa kunapokuwa na vyanzo vingi vya habari inasaidia, wakati mwingine, kupata picha halisi/nzima ya jambo. Ukitembelea tovuti za magazeti haya utaona kuwa bado ujenzi unaendelea. Bonyeza hapa uone gazeti la Mwananchi, na gazeti la the Citizen binya hapa na Mwanaspoti (kwanini hawakuliita Mwanamichezo? Sijui.) ni hapa. Magazeti mengine ya Tanzania ya kuuzwa mtaani yanayopatikana pia mtandaoni ni Majira, Uhuru, Daily News, Arusha Times, the Express, magazeti ya Mengi kwa jina la IPP Media (kama jamaa wa Quality Group watapata bilioni mia moja wanayodai, magazeti haya yataendelea kuwepo?). Lakini utaona magazeti haya bado yako zile enzi za magazeti kutoa habari na sisi wasomaji kupokea. Hakuna mahusiano ya “nipe nikupe” kama inavyoweza kutokea ndani ya blogu zetu. Unatakiwa kusoma magazeti haya kama vile huna sauti au fikra/mawazo yako ya kutoa au kuchangia jambo. Lakini mabadiliko sio lazima yafanyike leo. Kesho ipo, inakuja.
Mon 3 Apr 2006
Marafiki zangu, Michelle na George, wanaoishi Mexico, waliponitumia toleo la kwanza la mwaka huu la gazeti lao la From the Field nilifurahi sana kukuta moja hadithi iliyoandikwa na Mtanzania Morris Mwavizo. Bonyeza hapa upate toleo hilo. Hadithi ya Mwavizo ni ya pili baada ya makala ya kwanza iliyoandikwa na George. Basi nilipoisoma nikawaandika Michelle na George na kuwaomba wamwandikie Morris ili kumshauri aanze kutumia teknolojia ya blogu kwa ajili ya kazi zake za uandishi. Kwa furaha kubwa napenda kuwaleteeni mwanablogu mpya, Morris Mwavizo, ambaye anafanya kazi kwenye gazeti la Mwananchi. Blogu yake itakuwa hasa ikihusu masuala ya sanaa, filamu, na muziki. Kwa sasa kaandika kwa kiingereza, sijui kama atachanganya kiingereza na Kiswahili au ni kiingereza tupu. Bonyeza hapa umsabahi.
Sun 2 Apr 2006
Kama unadhani kuwa blogu za Kiswahili zitakuwa zikianzishwa na Watanzania pekee utakuwa umekosea. Nilijua kuwa Watanzania wataongoza njia ya kublogu kwa Kiswahili ila wazungumzaji wa Kiswahili wa nchi nyingine, kama Kenya, watafuata, ingawa polepole. Maitha wa Mawazo na Mawaidha tumekuwa naye kwenye blogu zetu za Kiswahili, akiwa mwanablogu pekee wa Kiswahili toka jumuiya ya wanablogu wa Kenya. Halafu baadaye akaja Mhujumu, majuzi akaja ndugu David wa Mtandawazi (ambaye anaelekea atakuwa akiandika mambo yatakayozua mijadala mikali), halafu leo hii tumepata mtoto mpya katika jumuiya ya wanablogu wa Kiswahili wa Kenya. Huyu ni ndugu Jesse ambaye anasema yeye ni Mdadisi. Mtembelee hapa.
Sun 2 Apr 2006
Jumuiya yetu, maadili, kukutana, na kadhalika
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: blogu , wanabloguToa Maoni [18]
Jana niliandika kuhusu wadhalimu fulani fulani duniani ambao wanatishika sana na nguvu za teknolojia ya blogu. Wanafungia huduma za kublogu na pia kutia wanablogu lupango. Iwapo hukusoma niliyoandika, bonyeza hapa usome ndipo uendelee na waraka huu. Baada ya kuandika hayo, Makene amepitia hapo na kutoa mawazo. Amesema jambo moja la msingi. Anasema kuwa wanablogu wa Kiswahili tunaweza tusiwekewe vizingiti na watwawala bali tukajimaliza wenyewe. Anasema:
Ndesanjo, habari hii nilipoisoma niliikimbilia kutaka kujua kuibuka kwa mamluki katika Magazeti Tando ya Kiswahili. Kumekuwa na wachangiaji wanaokatisha tamaa ya kutanuka kwetu. Hawa tukiwaacha watasambaa na kuharibu nia na agenda yetu njem akwa jamii. Hawa niliwahi kuwaandikia makala pale kwangu kulaumu vitendo vyao vya kutoa matusi katika kivuli cha anonimasi. Hawa wanatupaka matope na kutaka kuonyesha kuwa sisi wote hatuna dira na inakuwa vigumu sasa kunadi wazo hili kwa watu muhimu tunaolenga wafanye mabadiliko katika sehemu mbali za maisha yetu. Wakati akina Bush wakifanya kwa upande wao wametambua kuwa kuna watu wana agenda kali na hoja zilizosimama. Sisi kwetu ni hili kundi linalotukana watu na kutoa hoja za kero. Tusipoamka na kupambana na tabia hii na sisi tutajimaliza bila kutumia nguvu za kufungia makampuni kama Blogger au wordpress. Naomba kuwasilisha.
Bonyeza hapa umalize kusoma waraka huu: (more…)



