Kwanza kabisa ngoja niseme jambo kuhusu blogu ya Mongi. Mongi ni kati ya wanablogu Tanzania wanaoblogu kwa kiingereza. Baadhi ya watu wanadhani kuwa wanablogu wa kiswahili tuna ubaya na kiingereza. Kiingereza kama zilivyo lugha nyingine duniani kina nafasi na umuhimu wake. Mongi yuko kwenye mtandao wa wataalamu wa kilimo duniani. Blogu yake ni sehemu ya mtandao wa wataalamu hawa wa kupeana taarifa. Katika blogu zote za Watanzania, blogu ya Mongi ndio blogu ya kwanza ya kifani. Blogu zetu nyingi tunaandika jambo lolote tunaloona linafaa kuandikwa. Mongi yeye anaandika kuhusu kilimo kwa ajili ya mtandao alionao na wenzake na pia watu wengine wenye kufuatilia mambo haya. Kwahiyo tunaona kuwa blogu zinaweza kutumiwa kujenga mtandao na kuwa kisima cha maarifa, taarifa, na habari kwa manufaa ya fani au taaluma fulani. Bonyeza hapa uende kwenye blogu ya Mongi. Nadhani mtu mwingine ambaye anakuja na blogu ya kifani ni Paul Kihwelo, mkuu wa kitivo cha sheria Chuo Kikuu Huria Tanzania na msimamizi wa mradi wa Creative Commons Tanzania. Paul yeye atakuwa anaandika kuhusu sheria. (bonyeza hapo chini umalize kusoma habari hii.)

Sasa niseme jambo hasa nililotaka kusema. Majuzi niliandika kuhusu kuhamia kwenye programu huria ya Wordpress toka kwenye programu ambayo wengi tunatumia ya Blogger. Soma hapa niliyoandika. Baada ya kuandika hayo, Mongi aliingia kwenye blogu na kutoa maoni yake ambapo aliuliza maswali ya msingi katika suala zima la Wordpress na Blogger. Haya ndio aliyoandika:

Nimekuwa naijaribu wordpress kwa nia ya kujiunga. Ni huduma nzuri na yenye mvuto. Hata hivyo huduma hii inatupunja watu ambao ni vigumu kulipia. Huduma hii hairuhusu mwenye blogu asiyelipia kuona na kuhariri template yake kama ilivyo kwa blogger. Ni lazima kununua domain ili kupata ruhusa hiyo. Sijui kama niko sahihi, lakini ndilo nililogundua.

Uamuzi wangu wa kujiunga na Wordpress ulikuwa mgumu sana. Toka nilipoanza kublogu mwaka 2004 nilikuwa natumia Blogger hadi nilipohama hivi majuzi. Karibu wanablogu wote wa Tanzania wanatumia Blogger. Blogger kwangu ilikuwa sio tu chombo ninachotumia kublogu bali ilikuwa ni kama jumuiya. Kwakuwa tumekuwa tukitumia programu moja imekuwa ni rahisi mara kwa mara kuulizana maswali kunapokuwa na tatizo au kupeana ushauri. Utashangaa kuwa uamuzi wa kuhama nimekuwa nikiuahirisha karibu mwaka. Mwishoni mwa mwaka jana nilihamia Typepad kwa dakika chache kisha nikarudi Blogger. Kama uliwahi kuja kwenye blogu yangu ya zamani, hii hapa, ukakuta maruweruwe, basi ndio wakati huo nilikuwa nahamisha. Nikarudi. Nilijisikia kama vile ninawakimbia ndugu zangu. Nikahisi upweke fulani hivi.

Sasa kwanini hivi sasa nimeamua kuhama? Ili kujibu swali hili itabidi nijibu swali la Mongi na mengine ambayo hayajaulizwa. Mongi amesema jambo moja ambalo ni kweli. Kama utatumia Wordpress ile ambayo ni ya bure, hutakuwa na uwezo wa kuingia ndani ya templeti yako kama ambavyo unaweza kufanya ndani ya Blogger. Lakini ukiwa na Wordpress ya kulipia unaweza kufanya hilo. Mongi hujakosea.

Wordpress na Blogger zote zina faida zake na pia zina kasoro zake. Uamuzi wa kutumia programu ipi ni uamuzi wa binafsi ambao inabidi uufanye baada ya kutazama tofauti na ulinganifu uliopo kati ya programu hizi mbili. Hatua ya mwanzo unayoweza kufanya ili kuweza kutoa uamuzi sahihi ni kufanya majaribio ya kuhamia Wordpress kama alivyofanya Idya wa Pambazuko. Ukihamisha mambo yako toka Blogger kwenda Wordpress, hutapoteza blogu yako ya zamani. Bonyeza hapa utaona blogu ya Idya iliyoko Blogger na bofya hapa uone blogu yake iliyoko Wordpress.

Majaribio haya yatakuwezesha kuingia ndani ya Wordpress kuona ilivyo na inavyofanya kazi. Unaweza kusoma mwongozo nilioandika wa jinsi ya kuhamisha mambo yako toka Blogger (bila kuiua blogu yako hiyo) kwenda Wordpress. Bonyeza hapa. Kwa kifupi nitachambua tofauti zilizoko kati ya Blogger na Wordpress. Tofauti hizi hasa ndizo zilizonifanya kuhama.

Kwanza kabisa ni suala la upangaji wa mambo uliyoandika katika makundi ya kimaudhui. Kwa mtu anayepanga kublogu kwa muda mrefu suala hili ni la muhimu sana. Kwa mfano kukawa na mwanafunzi anafanya utafiti kuhusu masuala ya utamaduni. Akaja kwenye blogu yako, tusema mwaka 2010, ni vipi ataweza kujua yaliko mambo uliyoandika kuhusu utamaduni? Au msomaji akawa kwenye blogu ya Mwandani akataka kusoma habari alizoandika kuhusu ubaguzi wa rangi, tuseme miaka mitatu toka sasa. Ni vipi ataweza kujua habari kuhusu ubaguzi wa rangi, ambazo Nambiza huwa anaziandika vizuri sana, ziko wapi? Itabidi atafute habari kwa kubahatisha, kwa kubonyeza miezi kwenye kisehemu cha nyaraka. Zaidi ya Wordpress kukupa uwezo wa kupanga mambo kimaudhui, kuna kisanduku cha kusaka habari ambazo umeandika. Kwa mfano, ukiwa unataka kutafuta habari nilizowahi kuandika kuhusu Mwalimu Nyerere, unachofanya ni kuandika jina lake kwenye hicho kisanduku na kuzisaka habari zote nilizoandika kuhusu Nyerere. Hebu fikiria uwe na kitabu cha kurasa maelfu ambacho hakina ukurasa wa “Yaliyomo.”

Tuangalie blogu ya Michuzi. Ukiwa unaandika habari kuhusu kampeni za uchaguzi, ukataka kutumia picha toka kwa Michuzi. Ukienda kwenye blogu yake utajuaje ziliko picha zinazohusu kampeni za uchaguzi? Au ukataka picha za viongozi wa Afrika, utajuaje ziliko picha hizo? Labda uwe unakumbuka siku na mwezi na mwaka ambao aliziweka picha hizo kwenye blogu yake. Njia pekee ya kuweza kupanga picha hizo kwa nia ambayo wasomaji, watafiti, n.k. wataweza kuzipata ni kuziweka katika makundi ya kimaudhui. Michuzi hana namna…tunamjengea blogu itakayompa uwezo wa kupanga picha zake katika maudhui. Blogu ya Michuzi ni kumbukumbu/historia ya taifa kwa picha. Watoto wa vitukuu vyetu watakuja kuitumia kujua historia yao. Wakati huo blogu itakuwa kama vile yale madaftari yenye “tebo” ukurasa wa nyuma, yaani itakuwa ni kitu cha kawaida.

Ingawa ni kweli kuwa ukitumia Wordpress ya bure huwezi kuingia ndani ya templeti yako, mambo mengi ambayo unayafanya kwenye Blogger kwa kuingia kwenye templeti yako unaweza kuyafanya kwenye Wordpress bila kuingia kwenye templeti yako. Kwa mfano, mambo kama viuongo, maudhui, taarifa juu yako, anuani yako, n.k. unaweza kuvifanya ingawa huingii kwenye templeti. Faida mojawapo ni kuwa huna haja ya kujua HTML au CSS, lugha zinazotumika kuunda tovuti. Kwenye blogger, kwakuwa unaingia kwenye templeti ambayo iko katika lugha ya HTML na CSS, unahitaji uwe na utaalamu fulani wa masuala hayo. Lakini sio vigumu kujifunza.

Kwenye Blogger kuna kitu kinaitwa “recover post” ambacho kinakusaidia kuweza kupata mambo uliyoandika yakafutika kwa bahati mbaya. Huwezi kufanya hivyo kwenye Wordpress. Kwenye Wordpress kuna urahisi wa kupata anuani ya habari mtu aliyoandika. Kwa mfano, kama unataka kupata kiungo cha habari hii unayosoma hivi sasa, bonyeza juu ya kichwa cha habari hii hapo juu utapelekwa kwenye ukurasa wenye anuani ya habari hii. Huwezi kufanya hivi kwenye Blogger. Hii inafanya mara nyingi watu wanapozungumzia habari fulani badala ya kuweka kiungo cha habari yenyewe wanaweka kiungo cha blogu nzima ambapo ukifika hapo inakupasa uanze kutafuta habari wanayoizungumzia iko wapi. Na kama hakuna mpangilio wa kimaudhui, unaweza kukesha.

Ukiingia kwenye Wordpress utaona kuwa hakuna ukurasa wa msaada ulio mzuri kama ilivyo kwenye Blogger, kupitia: blogger knowledge, blogger help, na FAQ (maswali ya mara ka mara). Hata hivyo watumiaji wa Wordpress ni kama jumuiya, hivyo wengi huwa wako tayari kusaidia wengine. Uzuri ni kuwa watumiaji wengi wa Wordpress ni wataalamu wa masuala ya tarakilishi. Lakini ukurasa wa msaada kwenye Blogger umesaidia sana watu wengi nikiwemo mimi.

Kuna kitu kinaitwa “trackback” na “ping.” Hizi ni teknolojia zinazowezesha mawasiliano kati ya blogu na blogu. Wordpress ina huduma nzuri sana ya “trackback” na “ping.” Tunaweza kusema kuwa “trackback” ni mfumo wa kuzitaarifu blogu kuwa umezitaja kwenye habari au jambo uliloandika. Kwenye Wordpress baada ya kuandika habari yako kuna kisanduku cha kuweka blogu ambazo umezitaja kwenye habari hiyo, blogu hizo zitatumiwa habari kuwa umezitaja. Bonyeza hapa usome kuhusu teknolojia hizi kwa maelezo rahisi.

Online Journalism Review wana jedwali ambalo linaweza kukusaidia kuona tofauti kati ya programu mbalimbali za kublogu zikiwemo Blogger na Wordpress. Bonyeza hapa uone jedwali hilo.

Nimalize kwa kusema kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu kutumia programu gani ni wako mwenyewe kutegemea na malengo na dhumuni lako la kublogu. Malengo yako ndio yatakupa uwezo wa kujua programu gani itakusaidia kuyafikia. Unaweza kushawishika kwa sababu moja au sababu kadhaa kutumia programu fulani. Zinaweza kuwa ni sababu za kiufundi, kisura, kiteknolojia zitakazokusaidia kuamua. Zinaweza pia kuwa sababu za kifalsafa. Mimi, kwa mfano, moja ya sababu zilizonifanya kuhamia Wordpress ni kuwa kifalsafa ninaunga mkono programu huria (programu hizi ziko wazi kwa mtu yeyote kuziendeleza tofauti na programu kama za Microsoft ambazo zimezungushiwa ukuta wa sheria ya hatimiliki). Sababu hii ndio inanifanya siku hizi nitumie Mozila Firefox badala ya Internet Explorer na Wikipedia badala ya Encyclopaedia kama Britannica. Programu huria ni aina fulani ya ujamaa. Hii inaendana sana na falsafa za Kiafrika: ujamaa, utu, ubuntu, n.k. Nategemea Maitha ataweza kutoa maoni yake mawili matatu kuhusu mjadala huu.