Ili uelewe ninazungumzia nini, inakupasa usome kwenza mambo niliyoandika hapo chini kwenye kichwa cha habari: Ipi bora kati ya Blogger na Wordpress? Unaweza kushuka hapo chini ili usome au unaweza kubonyeza hapa. Ninayoandika sasa ni muendelezo wa mada hiyo.

Mwanablogu anayeandika kwa Gikuyu, Gatua wa Mbugwa ameniuliza swali kuhusu kiasi cha malipo ya kutumia Wordpress. Huduma ya Wordpress inapatikana na bure na pia kwa kulipia. Huduma ya bure kama ilivyo Blogger unaipata kwa kubonyeza hapa. Huduma ya kulipia gharama zake zitategemea unatumia kampuni gani kuhifadhi blogu yako. Wordpress wana orodha ya huduma ambazo kwa mawazo yao wanaamini kuwa ni nzuri. Bonyeza hapa uone huduma hizo. Huduma hiyo ya kulipia taarifa zake bonyeza hapa. Kumbuka kuwa kama una nia ya kutumia Wordpress ya kulipia sio lazima utumie kampuni zilizoorodheshwa na Wordpress. Moja ya faida ya kutumia huduma za kulipia ni kuwa utaweza kupata anuani unayotaka ambayo haina neno “wordpress.” Inaweza kuwa www.sinadinizakuja.com. Au chochote kile.

Jambo jingine muhimu ambalo sikulifafanua vizuri ni kuhusu Wordpress kuwa ni programu huria. Kwakuwa ni programu huria, ina maana kuwa kuna watu maelfu wanaoikarabati na kuijenga programu hii kwa kujitolea. Programu kama ya Blogger ambayo inalindwa na hatimiliki ni vigumu kwa watumiaji kuifanyia mabadiliko. Mabadiliko yoyote lazima yapitie kwenye mkono wa wafanyakazi wa wanaoimiliki. Kwakuwa Wordpress ni programu huria inakuwa rahisi kwa mwanateknolojia kama Chris aliyeamua kujiunga nasi kujenga toleo la Wordpress la kiswahili. Soma aliyoandika Chris kuhusu mradi huo kwa kubonyeza hapa. Tukitaka toleo la kiswahili la Blogger hatuwezi kufanya chochote hadi wenye kampuni waamue kuwa wanatengeneza toleo la kiswahili. Nimewahi kuwaandikia mara nyingi kuhusu toleo la kiswahili lakini wala hawakujibu. Nikakutana na bwana anayeendesha mradi wa Google Eearth nikamgusia akasema atawaambia lakini wapi. Kwenye Wordpress hatuhitaji ruhusu ya mtoto wa mtu kufanya hivyo. Ndio maana ninawaambieni kuwa kifalsafa programu huria ninazipenda sana.

Halafu ningependa kujilinda kwa kusema haya: teknolojia mpya za habari, maarifa, na mawasiliano zinabadilika haraka mno. Niliyoandika hapa leo huenda kesho yakawa yamebadilika. Kwahivyo kasoro nilizotoa hapo chini za Wordpress au Blogger usishangae iwapo kesho utakuwa zimerekebishwa. Niliyosema ni hali iliyopo siku ya leo ninapoandika haya.