Majuzi niliandika kuhusu hatari ya vyombo vya uongo kulazimisha wananchi kupenda jambo fulani au mtu fulani (hata kama hawawezi kuorodhesha sababu za msingi za kupenda jambo hilo au mtu huyo). Nikasema kuwa vyombo hivi huzalisha “makubaliano.” Vinaweza kufanya wananchi katika nchi fulani kuamini kuwa wana mtazamo sawa kuhusu jambo fulani au “makubaliano” kuwa mtwawala fulani ni ni kiboko.

Maliza kusoma habari hii kwa kubonyeza hapa:

Tazama suala la Kikwete. Vyombo vya uongo Tanzania vinafanya wananchi kuamini kuwa Tanzania sio tu imepata Rais bali imepata mkombozi. Hali hii inafanya watu ambao wana mitazamo tofauti na huo kuweza kudhani kuwa hawana akili timamu. Toka alipotangaza kugombea urais dalili za kuwa magazeti, redio, na vituo vya luninga vitakuwa vinafanya kazi ambayo tumezoea kuona ikifanywa na gazeti la Uhuru zilionekana. Sio vyombo hivi tu, bali pia viongozi wa uongo mwingine uitwao dini (hasa hizi za kuja) walifikia hatua ya kusema kuwa kaletwa na mungu. Na wakawa wakiendesha sala na swala za kumuombea kwa mungu. Kama hukusoma niliyoandika, bonyeza hapa.

Kila siku nasoma habari za kishabiki toka kwenye vyombo vya “habari” vinavyoitwa “huru.” Ukichimbachimba utagundua kuwa vyombo hivi vinamilikiwa na wenzetu ambao huwa wanakutana na watwawala wetu kwenye tafrija za “wakubwa.” Wanacheza pamoja michezo kama gofu. Wanaalikana kusherehekea siku zao za kuzaliwa. Wanaalikana kwenye ubatizo na ubarikio wa watoto wao. Au sherehe za mahafali ya wanao. Wanapigiana simu. Na wakati mwingine watwawala hao wanakuwa na hisa kwenye magazeti, redio, au luninga.


Bonyeza hapa usome habari hii uniambie kama hii sio habari ya kishabiki. Ni viongozi gani hao ambao wamepandwa na presha? Habari hizi za viongozi fulani kuona viti vyao kuwa moto nimekuwa nazisoma toka nilipojifunza kusoma. Maagizo kama yanayozungumziwa kwenye habari hii yamekuwa yakitolewa miaka na miaka.

Habari nyingine ya kishabiki ni ile inayohusu wafanyabiashara waliotimuliwa. Wafanyabiashara hao, pamoja na kutimuliwa, wanamsifu Kikwete…kwa mujibu wa mwandishi. Inawezekana kuwa wako waliomsifu, lakini ni kweli kuwa wafanyabiashara WOTE waliotimuliwa hakuna aliyepinga kitendo hiki? Au mwandishi ameamua kutuandikia yaliyosemwa na wale waliomsifu tu na kuyaacha yale ya waliompinga au kuchukizwa na kitendo hicho? Au labda hizi ni enzi za “zidumu amri…” Bonyeza hapa uisome.

Hata waziri mkuu naye naona kila siku kuna habari za kishabiki juu yake kama vile ameanza kuwa serikalini juzi. Huyu bwana kawepo serikalini muda mrefu. Katumikia moja ya wizara chafu kabisa kwa rushwa, Wizara ya Ardhi. Sasa ghafla vyombo vya uongo vinataka kufanya kuwa naye ni “mkombozi.” Malaika aliyemletea ujumbe wa kutukomboa anaitwa nani? Ni Jibrili? Bonyeza hapa usome habari ya kumshabikia.

Kuna watu wanaamini kuwa nchi huongozwa kwa “wito.” Fulani amewataka fulani wafanye jambo fulani. Fulani katoa wito fulani. Majuzi Mwandani alitukumbusha suala hili la nchi kuongozwa kwa “wito” alipoandika:

Na ninaishiwa nguvu pale ninapokumbuka vichwa vya habari vya magazeti ya zamani zile vilivyokuwa vikienda kwa mtindo huu: watoto wanahitaji madawati – Kingunge” “Rushwa lazima itokomezwe –Mwalimu” “Hakuna nafasi kwa wazembe Tanzania – Rais”

Bonyeza hapa umsome.

Jamaa wengi walioko madarakani wamekuwepo serikalini muda mrefu. Wameshiriki kwenye uchafu uliotufikisha hapa tulipo leo. Ushabiki huu ambao pengine ndio ambao Nkya anauita “mkumbokrasia” unaendelezwa hata hata na watu wanaoitwa “wasomi.” Hivi lakini “msomi” na “si msomi” ni nani na nani? Bonyeza hapa usome habari kuhusu wahandisi waliompa Kikwete tuzo kwa “mchango wake katika fani ya uhandisi.” Ukisoma habari hiyo mwanzo hadi mwisho hupati ukweli wa “mchango” wake ni upi. Je tunaweza kusema kuwa kila mtu na kila sekta inataka kujikomba?

Mwanablogu Da Mija aliwahi kuandika kuhusu kashfa ya watu waliopewa dhamana ya kuongoza nchi yetu kulala kwenye hoteli za kitalii ndani ya nchi yao. Pengine ni watalii…tazama majina yao, dini zao, lugha wanazopenda kutumia, mavazi yao…inawezekana wametoka nyika za mbali! Bonyeza hapa usome aliyoandika Da Mija.

Sasa baada ya kashfa hiyo, vyombo vya uongo vinataka kutuhadaa kwa kusema kuwa Kikwete amejibu na kufafanua kuhusu kulala kwao kwenye hoteli za kitalii. Lakini ukisoma habari yenyewe, Kikwete anachosema ni kuwa sio watwawala wote wanahitaji nyumba za sirikali kwani wako ambao wana nyumba zao. Hii haikuwa hoja ya walalanjaa. Walalanjaa walitaka kujua: kwanini watumishi wetu walale kwenye hoteli za kitalii za gharama kubwa namna hii? Kama swali hili alilijibu, nimeshindwa kupata jibu lake. Ni kweli kuwa baadhi ya “watumishi” wetu wanaishi kwenye nyumba zao. Hawa hatuna neno nao. Gadhabu yetu ni kuhusu wale ambao wanaishi kwenye hoteli za kitalii kama vile wamekuja Tanzania kutembelea mbuga za wanyama. Au wanatuona sisi wenye nchi kama wanyama? Bonyeza hapa usome habari hiyo.

Kiongozi mmoja wa Marekani, Thomas Jefferson, aliwahi kusema kuwa akiambiwa achague kati ya kuwa na serikali bila vyombo huru vya habari au vyombo huru vya habari bila serikali, atachagua vyombo huru vya habari bila serikali. Hivi ndivyo baadhi ya watu wanachukulia uhuru wa vyombo vya habari kwa uzito wa juu. Vyombo vya habari vinapokuwa kwaya za kuimba mapambio ya sifa za watwawala, vinapokuwa kama vile TOT ya Kapteni Komba, huku wananchi wakionekana kutoshtushwa…jazia mwenyewe!