Wakati tunaingia katika awamu ya pili ya teknolojia za mawasiliano na habari, yaani Webu 2.0 (au kama wanavyoita: Web 2.0), kuna faida ambazo ni nzuri sana kwa wale tunaotokea katika nchi za Kusini, tukiwemo wale wa bara la Afrika. Hivi sasa kuna teknolojia na zana ambazo mtumiaji anaweza kuzitumia bila kupakua progamu yoyote kwenye tarakilishi/kompyuta. Programu hizi ni zile zilizojikita webuni.

Programu za kujikita webuni zina faida mbalimbali kwa bara kama la Afrika: watu wengi hawana tarakilishi zao nyumbani hivyo wanatumia huduma za migahawa ya Intaneti. Migahawa mingi imefunga tarakilishi zake ili watumiaji wasiweze kupakua programu bila ruhusa yao (kwa ajili ya usalama wa tarakilishi zao na mambo mengine). Hivyo kukiwa na programu ya kumwezesha mwananchi kufanya jambo fulani, programu hiyo ikawa haiwezi kutumika webuni ila mpaka uipakue na kuiweka ndani ya tarakilishi unayotumia, basi mwananchi huyo (anayetumia huduma za migahawa ya Intaneti) anakuwa hana la kufanya. Itabidi asubiri hadi awe na tarakilishi yake mwenyewe.

Hata kama umeenda kwenye mgahawa ambao umefanikiwa kupakua programu fulani, ina maana kuwa ukitaka kuendelea kutumia programu hiyo lazima uende kwenye mgahawa huo huo na utumie tarakilishi ile ile uliyoweka hiyo programu. Ukifika hapo kwenye mgahawa ukakuta mtu mwingine anatumia tarakilishi hiyo itakubidi usubiri hadi amalize. Ikiwa umesafiri ukaenda mkoa mwingine, mji mwingine, kitongoji kingine au hata nchi nyingine, hutaweza kuendelea kufanya kazi uliyokuwa ukifanya katika ile programu (maana utakuwa umeihifadhi ndani ya ile tarakilishi katika mgahawa wa Intaneti). Unachoweza kufanya labda ni kupakua tena programu hiyo katika tarakilishi nyingine katika mji uliotembelea. Huu ni usumbufu na upotezaji wa muda, hasa ukichukulia kuwa kwenye migahawa hii tunalipia.

Sasa programu za webuni ndio zinakuwa na faida katika mazingira kama haya. Na hizi ndizo hasa ninazitazama kwa undani siku hizi na kuzitangaza. Programu hizi zinakuwezesha kufanya mambo karibu yote ambayo yanafanywa na tarakilishi bila kupakua programu yoyote. Na pia zinakuwezesha kufanya kazi hiyo bila kuhitaji kufanya hivyo katika tarakilishi moja tu. Ukiwa popote pale penye Intaneti utaweza kuendelea kufanya kazi zako. Utafanya kazi, iwe ni kazi ambayo kawaida inatumia programu za kuandika kama tulizozoea za Microsoft Word, au lahajedwali (spreadsheet), na nyinginezo, bila kujali unatumia tarakilishi gani au kama mwenye tarakilishi hiyo anakuruhusu kupakua programu au la. Shughuli zote za kuandika, kutunza picha, kuhariri picha, kutunza video, kuhariri video, kujenga tovuti, kujenga blogu, kuhifadhi tovuti muhimu n.k. unaweza kuzifanya webuni bila kuweka chochote kipya kwenye tarakilishi na pia bila kuwa na haja ya kuwa na diski ya kuhifadhia kazi zako.

Mara nyingi tumekuwa tukikumbwa na tatizo la kuhifadhi kazi kwenye diski ambapo baadaye, kutokana na hali ya hewa na mambo mengine, diski hiyo inaharibika. Unajikuta umepoteza kazi muhimu sana. Lakini pia kuna suala la kupoteza diski au diski kuibiwa. Au kusahau diski kwenye mgahawa wa Intaneti…unarudi kesho yake unakuta haipo. Huduma za webuni zinakusaidia kuhifadhi kazi zako webuni. Unaweza kuweka kwenye diski au chombo kingine lakini kazi zako zinakuwepo webuni ambapo ukiwa kwenye tarakilishi yoyote unaweza kutumia. Huduma hii inaweza kukusaidia kuondokana na hofu ya diski kuharibika na pia gharama za kununua diski zenye nafasi kubwa ya kuhifadhi kazi iwapo wewe unahifadhi kazi kama za picha au video ambazo zinachukua nafasi kubwa sana.

Nilipoandika juu ya Wetpaint, baada ya kukutana na waanzilishi wake Boston, mwanablogu Marazzmatazz, ametukumbusha juu ya huduma kama Dreamweaver. Dreamweaver nayo kama Wetpaint inawezesha mtu yeyote kujenga tovuti bila kujua lugha ya HTML. Lakini tofauti inayokuja kati ya huduma hizi ni kuwa Wetpaint ni huduma ambayo huhitaji kupakua programu yoyote ndani ya tarakilishi. Kama huna tarakilishi yako mwenyewe inaweza kuwa vigumu kujenga tovuti kwa kutumia Dreamweaver. Wengi wetu hatuna tarakilishi zetu. Wetpaint inakuwezesha kujenga tovuti iwapo una uwezo wa kuingia kwenye Intaneti. Lakini pia unapojenga tovuti kupitia Dreamweaver lazima uwe na mahali pa kuhifadhi tovuti yako, hapa linakuja suala la gharama ambalo ni muhimu sana kwetu Waafrika. Kwa huduma kama ya Wetpaint, huna haja ya kuingia gharama ya za kuhifadhi tovuti yako.

Haya yote niliyoandika hapa nimeyaandika kwa kutazama watu ambao bado, kwasababu mbalimbali, uwezo wao kiuchumi na kiteknolojia ni mdogo. Hawa huduma za webuni ni muhimu sana.

Kwahiyo watu hawa badala ya kutumia Microsoft Word, wanaweza kutumia huduma ya Writely (huduma hii naitumia na ninaipenda) au wanaweza kupata huduma pana zaidi kwa kupitia Think Free. Wakiwa wanahitaji kufanya kazi za lahajedwali, wanaweza kutumia huduma za Google, bonyeza hapa. Badala ya kuhifadhi tovuti wazipendazo katika tarakilishi(ambayo sio yao), wanaweza kuziweka webuni kwa kutumia del.icio.us.