Unakumbuka wimbo wa “Mesenja kaleta balaa nyumbani kwa meneja”?

Ule mkutano nilioutangaza siku za nyuma (bonyeza hapa) uitwao “Digital Citizen Indaba” ulio chini ya mkutano wa kila mwaka wa Highway Africa umezua kasheshe katika ulimwengu wa blogu. Hii “indaba” ni indaba kweli au ni indaba babaisha? Ndio wanauliza baadhi ya wanablogu na watoa maoni. Mwanablogu Bullets and Honey alianza kuhoji mkutano huu kama ni wanablogu wa Afrika au ni indaba ya wazungu na waafrika wachache. Akaandika makala aliyoiita: (White?) African Blogger Conference in a Week. Isome hapa utazame na mjadala mkali kwenye sehemu ya maoni. Kisha Vincent Maher, mmoja wa waandaaji akajibu. Akasema kuwa alichoandika Bullets and Honey ni ubaguzi wa rangi. Msome hapa. Bullets and Honey anamwita Vincent Maher, Vincent “Madiba” Maher. Hiyo ni kejeli na sio kumsifia.(bonyeza hapo chini umalize kusoma habari hii).

Mwanablogu Cool Breeze naye akaingia katika mjadala huu. Bonyeza hapa umsome. Bullets and Honey hakuishia hapo, akaandika makala nyingine tena. Hii ikiwa inaitwa: Is the Digital Indaba the Internet Berlin Conference of 2006? Bonyeza hapa uisome na pia soma mjadala sehemu ya maoni. Kenyan Pundit naye akaandika kifupi kuhusu kuwasili kwake Grahamstown ambako ndipo unapofanyika mkutano huo. Naye akarusha dongo la kichinichini. Anasema tumwamshe siku Waafrika “halisi” watakuwa na mkutano wao! Msome hapa.

Jambo moja ambalo limenishangaza binafsi ni kitendo cha “indaba” ya wanablogu wa Afrika, kama tovuti ya mkutano inavyosema, kufanyika bila kuwepo wanablogu kwa lugha namba moja ya Kiafrika katika ulimwengu wa blogu, yaani Kiswahili. Wako wanablogu wengi mahiri wa Kiswahili wanaoishi Tanzania na wachache nchini Kenya. Tanzania au Kenya sio mbali na Afrika Kusini. Kama waandaaji wameweza kusafirisha watu toka nje ya bara la Afrika, sijui kwanini wameshindwa kutoa skolashipu kwa wanablogu wa Kiswahili walioko Tanzania. Unaweza kusema, “Labda hawakutuma maombi.” Najua baadhi ya wanablogu wa Kiswahili walioko Tanzania walituma maombi yao.

Kwanini indaba ya “waafrika” isionyeshe heshima angalau kidogo kwa lugha za Kiafrika? Iwapo unazungumzia mapinduzi haya ya blogu Afrika bila kuzungumzia au kuonyesha umuhimu wa Waafrika kuendeleza lugha zao kwa kutumia teknolojia hii, kwa kuwashirikisha wanablogu wanaonyonya titi la mama ingawa la mbwa katika dunia hii ya ubeberu wa kiingereza….Sijui.

——

Fuatilia mkutano huu kwa kusoma blogu maalum ya mkutano na pia umsome rafiki yangu Ethan Zuckerman ambaye anahudhuria na pia Kenyan Pundit.