Moja ya nyanja ambazo zinapata changamoto kubwa kutokana na mabadiliko ya kasi ya teknolojia ni nyanja ya sheria. Teknolojia zinabadilika na kuimarika kila siku na katika kufanya hivyo zinabadili nyanja za uchumi, siasa, habari, elimu, burudani, na utamaduni. Ni jinsi gani ambavyo watunga sheria wataweza kuhakikisha kuwa kunakuwapo na sheria ambazo zinakidhi mahitaji ya wakati?

Kesi iliyoihusu kampuni ya Yahoo! (bonyeza hapa na hapa) ni moja ya vielelezo vya changamoto ninayozungumzia.

Hata hivyo, pamoja na mabadiliko ya kasi ya teknolojia, misingi ya sheria nyingi bado iko pale pale. Kwa mfano, sheria ya hakimiliki. Bado ni kosa kisheria na pia sio ustaarabu kuiba kazi za mtu mwingine (iwe ni maandishi, picha, filamu, muziki, n.k.) bila idhini ya mtu huyo. Hata kama kazi hizo ziko ndani ya blogu. Ndio, hata kama kazi hizo ziko ndani ya blogu. (bonyeza hapo chini umalize kusoma habari hii).

Inawezekana baadhi yetu tunadhani kuwa sheria za hatimiki na pia kanuni na maadili ya uandishi havitulindi wanablogu. Yaani mambo tunayoandika ndani ya blogu zetu ni sawa kabisa akitokea mtu yeyote akaamua kuyatumia (iwe ni picha, mashairi, hadithi, makala) bila kutuomba ruhusu na wala kusema ametoa wapi. Wako watu wanaodhani hivi. Na pengine wako watu wanaojua kuwa ni kosa kufanya hivyo ila wanaamua tu kwa “kibri” kufanya hivyo. Hatutakubali jambo hili litokee.

Limetokea tukio ambalo limenifanya kukaa chini ili kuweka masuala haya ya hatimiliki wazi ili tujue tumesimama wapi na wale wote wanaotaka kufanya kama vile blogu hazilindwi na sheria za hatimiliki wajue kuwa hawako sahihi. Wanaodhani kuwa blogu ni kisima cha kubeba makala na picha na kuweka kwenye magazeti au tovuti zao bila idhini yetu, wajue kuwa ni kosa na pia sio ustaarabu. Hivi majuzi, jamaa wa DarHotwire wameweka makala ya mapishi iliyoandikwa na mwanablogu mwenzetu, Miriam, bila ruhusa yake. Wametumia pia na picha aliyoipiga yeye bila ruhusa yake wala kuwa na ustaarabu wa kusema chanzo cha picha hiyo. Wala hawakuweka anuani ya blogu yake au tovuti yake. Bonyeza hapa uione kazi hiyo waliyoitumia bila idhini.

Kosa hili, kwa wale walioko kwenye nyanja ya habari, sio kosa linalotokana na kutojua sheria. Suala la kuonyesha chanzo cha picha, chanzo cha habari, na kuomba ruhusa ya mwenye habari hiyo ni suala la msingi sana katika nyanja ya habari. Pengine, nasemea pengine, walidhani kuwa wanablogu ni jamaa wasio na muda wanaoamua kucheza na kompyuta hivyo hawana sababu za kupoteza muda kuomba idhini. Hapana, wanablogu ni watu ambao tunajali kazi zetu. Na sio tunazijali tu, bali tunataka kazi zetu ziheshimike na tuko tayari kuzilinda kazi zetu kwa sheria za hakimiliki zilizopo na maadili ya nyanya ya habari.

Ushahidi wa kuwa tunalinda kazi zetu utaona ukitembelea blogu mbalimbali, ukasoma chini kabisa ya blogu hizo utakuta maneno ya “Haki zote zimehifadhiwa” na wakati mwingine yataambatana na alama ya ©”. Maneno hayo na alama hiyo hayajawekwa pale bila sababu zote za msingi. Maneno haya sio mapambo. Maneno hayo yanaashiria nia ya dhati ya wenye blogu kulinda kazi zao kwa kufuata sheria za kitaifa na kimataifa za hakimiliki.

Ukitembelea blogu ya Issa Michuzi utaona maneno hayo. Huwezi kuanza kunyofoa picha zilizoko pale ukazitumia bila kuomba idhini yake. Haina maana kuwa hataki watu wazitumie, ila lazima upate idhini yake. Lazima ajue kuwa picha hizo unazitumia kwa shughuli gani. Asipolinda picha zake, wanaweza wakatokea watu wakaanza kuzitumia kwa nia mbaya, au kwasababu za kibiashara juu ya mgongo wake. Kama utazitumia kibiashara, basi Michuzi ana haki ya kupata malipo fulani ya kazi zake. Blogu ya mapishi ya Miriam nayo inasema wazi kuwa kilichoko ndani ya blogu yake ni mali yake Miriam, hivyo huwezi kutumia chochote bila idhini yake. Maneno aliyotumia ni haya: © Copyright 2006 mirecipe.com Tanzanian Recipes. All rights reserved.

Ni vyema ikaeleweka kuwa humu bloguni kuna watu wana kazi zao ambazo wana mipango nayo ya mbeleni. Kuna washairi na watunzi wa riwaya ambao wanaandika kwa nia ya kuja kuchapa vitabu baadaye. Wanablogu hawa wanataka kazi zao ziwe ni kazi zao. Kama mtu mwingine anataka kutumia, basi atumie taratibu zinazoeleweka za kutumia kazi ya mtu.

Sheria za hakimiliki zinatoa upenyo wa watu kuweza kutumia kazi za watu wengine iwapo sehemu ndogo ya kazi hiyo itatumika na sio kazi nzima. Kwa mfano, naweza kutumia mistari kumi toka katika kitabu cha mwandishi (na nikasema mistari hiyo nimetoa wapi) katika kuelezea jambo. Ila sio kutumia kazi yake yote na pia sio kutumia mistari hiyo bila kusema chanzo chake. Iwapo nitataka kutumia kazi yote ya mtu mwingine basi hapo nitatakiwa kupata idhini yake. Nikitumia mistari 20 toka katika kitabu cha kurasa 300 sitatakiwa kuomba idhini (ila nitatakiwa kueleza wazi chanzo chake).

Haya, hoja yangu ni kuwa ni vyema watu wote wanaotembelea blogu zetu wakaelewa kuwa kazi zetu ni kama vile kazi za vitabu, muziki, sinema, n.k. zinalindwa na sheria za hakimiliki na tunaamini kuwa kila mtu ataheshimu kazi zetu hizi. Anapotokea mtu yeyote, iwe ni gazeti, tovuti, au mtu binafsi akataka kutumia kazi zilizoko kwenye blogu zetu NI LAZIMA APATE IDHINI TOKA KWETU. Tena iwapo kazi hiyo itatumika katika tovuti kama ya DarHotwire ambayo inalipisha watangazaji malipo ya kuweka matangazo kwenye tovuti yao, lazima mwenye kazi hiyo atoe idhini. Ina maana ni kazi kama za mwanablogu huyo zinazoleta wasomaji kwenye tovuti hiyo, na kuwepo kwa wasomaji ndio kunaleta watangazaji ambao wanalipa hela ambazo hakuna njururu inayokwenda kwa mwanablogu ambaye kazi yake imetumiwa.

Mtu anaweza kutokea na kuuliza “Mwanablogu Miriam yuko Marekani na DarHotwire wako Tanzania, je watakuwaje wamevunja sheria?” Jibu ni kuwa sheria za hakimiliki zinavuka mipaka! Iwapo mwanablogu yuko Tanzania, akatokea mtu anayeishi Afrika Kusini akatumia kazi za mwanablogu huyo wa Tanzania bila idhini yake, ingawa hawako nchi moja bado anakuwa amevunja sheria. Kabla ya kuwepo kwa mkataba unaosimamia masuala ya hatimiliki kimataifa, Mkataba wa Berne, nguvu za sheria za hakimiliki ilikuwa ni ndani ya nchi aliyemo yule mwenye haki hizo. Yaani kama mwenye haki hiyo yuko Malawi, basi anaweza kudai kuwa haki zake zimevunjwa na mtu mwingine aliyeko ndani ya Malawi na sio nje ya Malawi. Lakini baada ya Mkataba wa Berne, nguvu za hakimili zinavuka mipaka.

Wizi au utumiaji wa kazi za wanablogu bila idhini yao sio jambo geni. Huko nyuma wanablogu wa Kenya walimdaka mwandishi wa habari aliyekuwa akitumia kazi za wanablogu na kuzipa jina lake, kama vile yeye ndio kaziandika. Hii ni tofauti kidogo na waliyofanya Dar Hotwire. Bonyeza hapa uone mfano wa kazi ya mwanablogu wa Kenya iliyonyofolewa.

Ningependa wanablogu wanaojali suala hili la hakimiliki za kazi zetu na wasomaji wanaojali na kupenda kazi zetu kuwaandikia jamaa wa DarHotwire na kuwataka wafanye mawili:

1. Waondoe kazi waliyochukua toka kwa mwanablogu mwenzetu, Miriam, bila idhini yake na kuomba msamaha.

2. Waombe msamaha na kumuomba mwanablogu huyo ruhusa ya kutumia kazi yake (na wakipewa ruhusa hiyo waeleze wazi chanzo cha kazi hiyo na waweke anuani ya blogu.

Hizi ni anuani zao:

Mhariri wa Habari: Ray John: ray@infocomtechnologies.com

Mtengeneza Tovuti (na rafiki yangu): Robert Shija: shija@infocomtechnologies.com

Tumia dakika chache kuwaandikia waraka mfupi na kuwataka waheshimu sheria za hakimiliki na kazi za wanablogu.

Hatua hii ni moja ya njia ya kulinda kazi zetu, hasa zile za riwaya au picha, dhidi ya watu ambao wanaweza kutaka kutumia bila idhini yetu. Hii ni njia mojawapo pia ya kuuambia umma wa Tanzania na dunia kuwa BLOGU ZINALINDWA NA SHERIA ZA HAKIMILI. Na kuwa maneno “All Rights Reserved” yaliyoko kwenye baadhi ya blogu zetu sio mapambo. Niongeze: kisheria, hataka kama maneno “All Rights Reserved” hayako bado mwenye blogu atakuwa na haki zote!

Tuwaandikie barua za kistaarabu, bila vitisho wala dharau. Huenda walipitiwa, huenda hawakujua kuwa blogu ni nini, huenda walifanya hivyo bila kujali, lakini lazima wafanye kati ya mambo mawili niliyoandika hapo juu. Hakuna njia ya mkato.

Kwa faida ya kila mtu. Mambo ya kuzingatia kuhusu kazi zilizoko ndani ya blogu:

  1. Usitumie kazi yoyote ndani ya blogu, iwe ni picha au makala, bila idhini ya mwenye blogu
  2. Elezea chanzo cha habari au picha uliyotumia toka kwenye blogu na weka kiungo cha blogu yenyewe

DarHotwire, tafadhalini sana, fanyeni mambo mawili niliyoorodhesha hapo juu. Mapema.