Sun 1 Oct 2006
Kikwete kuwa “dumb bitch” na Watanzania kuwa “maimuna”!
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: siasa , lugha , tanzania , kenyaMajuzi kulitokea tukio ambalo limeleta kizazaa fulani kwenye duru za kidiplomasia. Kizazaa hicho kimeonyesha pia sura halisi ya mwanablogu mmoja wa Kenya. Rais wa Tanzania, ndugu Jakaya Kikwete, alipokuwa nchini Marekani, inasemekana kuwa alijadili suala la “hali mbaya ya kisiasa” nchini Kenya na rais wa Marekani, mpenda vita na mwizi wa kura na mwenyekiti wa Marais waongo duniani, Joji Kichaka. Mmoja wa wanablogu wa Kenya mwenye blogu ya My Part of the World aliposikia habari hizo akaandika mambo kadhaa ambayo yalinishtua kidogo. Bonyeza hapa usome aliyoandika. Nina wanablogu wa Kenya wengi ambao ni marafiki zangu, na Wakenya wengine ambao sio wanablogu ambao nao ni marafiki zangu. Sio marafiki zangu tu, bali pia wana utu na ustaarabu. Urafiki wangu na upenzi wa blogu za Wakenya ndio umenifanya kuwa mwanachama wa jumuiya ya wanablogu wa Kenya, Kenya Unlimited. Tena blogu za Wakenya kama vile Kenyan Pundit ndio zilizonichochea nikaanza kublogu. (bonyeza hapo chini umalize makala hii).
Sasa huyu mwanablogu wa My Part of the World anaandika kama vile Wakenya na Watanzania tuna uadui wa kutupa. Amefika hatua ya kutoa kashfa na kutukana. Sasa mimi kama Mtanzania na mwanablogu ninaamini kuwa nina haki ya kuchangia mjadala huu na kujibu hoja zake bila kashfa wala kutukana. Na wengine mnaweza kushiriki kwenye mjadala huu, bila jazba.
Mwanablogu huyu, jina kwenye blogu yake ni Acolyte, amepinga vikali hatua ya Rais wa Tanzania kuijadili Kenya wakati ambapo Kenya ina ubalozi Marekani. Akizungumzia Kikwete (mwanablogu huyu anamwita Kikwete, “Kiwete.”) anasema, “…don’t know where that punk gets off talking about Kenya.” Yaani Kikwete ghafla amekuwa “that punk.” Halafu anaendelea, “That dumb bitch needs to handle his own country’s business and then that’s when he can start talking about us.” Ghafla Rais wa Tanzania amekuwa “that dumb bitch.”
Kwanini Kikwete amekuwa “Kiwete,” “that punk,” “that dumb bitch”? Eti kwakuwa vyombo vya habari vimenukuu maofisa wa serikali ya Marekani wakisema kuwa suala la hali mbaya ya kisiasa Kenya lilijadiliwa Kikwete alipokutana na Joji Kichaka. Tuanze uchambuzi: Tunajua kuwa Kenya ilijadiliwa wakati viongozi hao wawili walipokutana. Ila hatujui Kikwete (au Kiwete kwa mujibu wa ndugu Acolyte) alisema nini. Hatujui mada hiyo alianzisha nani. Ukienda katiba blogu hiyo ya Acolyte utaona katika sehemu ya maoni, bonyeza hapa, baadhi ya mambo yaliyojadiliwa hapo ni suala la jambo gani Kikwete alisema. Acolyete ameulizwa na ninategema atoe jibu: What did Kikwete say about Kenya? Inawezekana Acolyte anajua Kikwete alisema nini ndio maana amekuja juu. Inawezekana alikuwa ukumbini hapo wakati maraia hao wakiongea. Kama hajui Kikwete alisema nini, sijui ni kitu gani kimemfanya aanze kumtukana Rais wa Tanzania. Inawezekana, nasema inawezekana, Kikwete alimwambia Joji, “Kenya hakuna hali mbaya ya kisiasa. Yanayotokea pale ni mambo ya kawaida.” Kama alisema hivyo sijui kama bado ataendelea kuwa “that dumb bitch.” Iwapo hatujui kauli gani hasa zilitoka mdomoni mwa Kikwete sioni sababu yoyote ya kuanza kumlaumu na kumtaka aachane na Kenya.
Kingine ni kuwa iwapo wakati wa mazungumzo yake na Joji Kichaka, suala hilo lilikuja, inawezekana kuwa lilijadiliwa kutokana na ukweli kuwa Tanzania ni mwanachama anayeiwakilisha Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na pia ni mwanachama wa UN Peace Building Commission. Rais wa nchi yenye vyeo hivi, yaani viti katika baraza na tume hiyo, ndugu yangu Acolyte na wengine wenye msimamo kama wako, ana haki ya kujadili masuala mbalimbali ambayo hayahusu nchi yake. Hivyo, kuna uwezekano kuwa majadiliano hayo yalikuwa yakifanyika Kikwete akiwa si kama Rais wa Tanzania bali pia kiongozi wa nchi yenye viti katika baraza na tume hiyo. Kama ilikuwa hivyo, basi hakuna jambo la ajabu kuwa nchi nyingine (sio Tanzania) ilijadiliwa ingawa Kikwete na Kichaka hawatoki Kenya. Na nisisitize: sijaona nukuu yoyote ya mambo aliyosema Kikwete. Na pia sijaona maelezo yoyote ya kuonyesha kuwa ni nani, kati ya Kikwete na Kichaka, alianzisha hiyo mada. Kama Kichaka ndio aliianzisha, Kikwete analaumiwa kwa kosa gani?Sasa baada ya kumwandama Kikwete, mwanablogu huyu akaamua kutumia tukio hilo kuwaweka Watanzania wote kwenye kundi moja kama vile Watanzania wote wana mawazo na fikra zinazofanana. Anasema, “Tanzanians lately have seemed to have some major dislike for Kenya and those statements confirm it.” Inawezekana kuwa kuna Watanzania wanaochukia Wakenya. Katika nchi ya watu milioni zaidi ya 30, haiwezekani hakuna mtu anayechukia Wakenya. Kama vile ambapo sio ajabu kukuta Wakenya wanaochukia Watanzania. Au Wakongo wanaochukia Wamalawi. Au Waganda wanaochukia Wasudani. Ndani ya nchi tu unakuta watu wanachukiana, sembuse nchi na nchi. Tatizo langu ni pale kuzungumzia jambo hilo kama vile Watanzania wote tuna chuki dhidi ya Wakenya. Mimi ni Mtanzania na hakuna Mkenya hata mmoja ninayemchukia. Nina marafiki toka Kenya. Wengine tumekuwa marafiki kupitia blogu na wengine masuala mengine. Ndugu hawa ninawaona kama binadamu na Waafrika kabla ya kuwaona kama Wakenya.
Anaendelea, “Kenyans in Tanzania are routinely hassled and I think the Nation Media Group even had a number of it’s managers deported on a trumped up technicality.” Suala la kufukuzwa kwa waandishi toka Kenya halikuwa suala la viongozi wa Tanzania kukurupuka na kusema, “Tunawachukia Wakenya, ngoja tuwafukuze.” Suala hili waliokuwa wanalifuatilia lilikuwa pana sana. Halikuhusu hisia za Watanzania kuhusu Wakenya. Kulikuwa na mkono wa siasa na mambo mengine ambayo sio dhumuni la makala hii. Ukichukulia idadi ya Wakenya ambao wamewahi kufukuzwa Tanzania na idadi ya Wakenya ambao wako nchini Tanzania hivi sasa wakifanya kazi bila bugudha yoyote, utagundua kuwa madai kuwa Watanzania wanachukia Wakenya na hivyo kuwafukuza ni uongo. Ni madai yasio na utafiti wa kina. Halafu suala la raia kufukuzwa halijatokea tu Tanzania kufukuza Wakenya. Watanzania wengi pia wamewahi kufukuzwa Kenya. Na Wakenya wengi wamewahi kufukuzwa Tanzania. Nikianza kuuliza watu wanaofahamu Watanzania waliowahi kufukuzwa Kenya wanyooshe vidole, tutavihesabu hadi kesho kutwa. Nchi zote hizi zimefukuza raia wa nchi jirani yake mara nyingi.
Anaendelea, “Tanzanians are barely making it in their own country and that is why they still have a far smaller GDP than our political instable asses!” Sasa hapa naona amechukua kofia ya masuala ya uchumi. Sentensi hii ya “Tanzanians are barely making it in their own country” unaweza kuitumia kwa nchi yoyote ya Afrika. Nchi za Afrika zote, ikiwemo Kenya, ni masikini za kutupwa. Nchi nyingi Afrika zina matajiri wachache na masikini wengi wanaoishi kama wanyama kwenye mageto na mitaa mijini iliyojaa ujambazi, uchafu, ukahaba, magonjwa, ombaomba, watoto wa mitaani wanaovuta petroli na “glue,” na wananchi wa vijijini wasio na hili wala lile. Hali hii iko Tanzania. Iko Kenya. Usidanganywe na hiki kitu kinaitwa eti “GDP.” Ndio maana Ufalme wa Bhutan ukaja na kitu wanachokiita GNH, Gross National Happiness. Bonyeza hapa usome habari hiyo. Watu wengine wamekuja na kipimo kiitwacho Genuine Progress Indicator (GPI) ambapo wanatazama kama ukuaji wa uchumi umesaidia kuneemesha maisha ya wananchi. Uchumi unaweza kukua ila kusiwe na mabadiliko makubwa katika ustawi wa jamii. Bonyeza hapa usome kuhusu kipimo hicho.
Unajua uchumi wa nchi unaweza kukua kwenye tarakimu lakini katika mifuko ya wananchi ikawa haina mapesa na uwezo wao wa kupata huduma muhimu za jamii ukawa mdogo maana unakuta kuna asilimia mbili ambayo ndio inasakatia pato na nchi. Wajanja wachache wa ndani wakishirikiana na wajanja wachache wa kimataifa, yaani wazungu, wanakuwa ndio wanafaidi hizi tarakimu. John Githongo anaweza kukupa moja ya mifano ya kule zinakokwenda njururu za taifa la Kenya. Tarakimu hizi zinapendwa sana na majamaa kama wa Benki ya Wazungu ya Kukopesha Nchi Masikini kama Tanzania na Kenya, (wao wanaiita hiyo benki ya, Benki ya Dunia).
Nikumbushe. Nilikuwa kwenye mada gani vile?….Nimekumbuka. Tanzania na Kenya hakuna kuchekana tukija kwenye ufukara na taratibu mbovu za kuendesha uchumi katika nchi hizi, ubadhirifu, rushwa, umasikini vijijini, ufukara mijini, magenge ya vijana mijini wasio na kazi, n.k.
Ndugu yetu akaendelea na hoja zake akasema kuwa hakumbuki kama kuna wakati Moi aliwahi kuwa na tabia ya kukandia nchi za wengine. “…even at his worst I can’t recall Moi doing so….” Amefanya vizuri kusema kuwa “hakumbuki” badala ya kusema kuwa Moi hajawahi kufanya hivyo. Katika sehemu ya maoni, mwanablogu huyu anakumbushwa kuwa Moi alikuwa na tabia ya kuponda sana nchi za Marekani na Uingereza. Alikuwa akiziponda ile mbaya yake. Na tabia hii ilikuwa ikipendwa sana na baadhi ya watu wasiopenda siasa za nchi hizi za kibeberu. Watu waliokuwa wakitaka kusikia kiongozi akiziambia nchi hizi, “Kitoeni zenu. Ishieni huko na hela zenu.”
Baada ya msomaji kutoa hoja hizo, mwanablogu Acolyte akajibu na kusema kuwa hata kama Moi alifanya hivyo hakuwahi kusema mambo mabaya kuhusu Uganda au Tanzania. Msomaji wake anamuuliza, “Kama kusema nchi za wengine ni jambo baya katika duru za kidiplomasia, basi ni jambo baya bila kujali nchi.” Huwezi kusema eti ni jambo baya kwa Tanzania kuisema Kenya, ila ni sawa kwa Kenya kuisema Marekani. Halafu, kwa wale wanaokumbuka historia, nchi za Tanzania, Kenya, na Uganda zimewahi kusemana. Tanzania ikaisema Kenya, Kenya ikaisema Tanzania, Uganda ikaisema Kenya, Tanzania ikaisema Uganda, n.k. Fuatilia yaliyokuwa yakisemwa kabla ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sisemi kuwa ni sawa, ila yamewahi kutokea.
Katika majibizano sehemu ya maoni, utaona kuna mahali mwanablogu huyu anasema eti Kikwete angetumia muda wake aliokuwa na Joji Kichaka kuomba misaada! Kichefuchefu. Yaani huu mtazamo kuwa unapokutana na ngozi nyeupe unatakiwa kunyoosha mkono na bakuli la ombaomba sijui utaisha lini. Ndugu yetu huyu akaulizwa na msomaji, amejuaje kuwa Kikwete hakuongelea suala la misaada? Je alikuwepo kwenye mazungumzo hayo akasikia kila kitu Kikwete alichosema? Kwanza, sioni sababu yoyote ya kunipa ufahari ya kumtaka Kikwete awe ombaomba mbele ya Joji, na pili, hatujui Kikwete alimwambia nini Joji.
Haya, kwa kumalizia hoja zake, mwanablogu huyu anatuambia Watanzania, “Any Tanzanians online are welcome to defend their leader assuming your English and comp skills allow you to do so.” Kwakuwa Watanzania hatujui kiingereza, kama anavyosema, imebidi nitumie kamusi kutafuta maana ya sentensi hiyo! Ili nisiwasumbue Watanzania wenzagu kuanza kufukuzia kamusi, inabidi niwatafsrie! Eti anatukaribisha kwenye mjadala wa kumtetea kiongozi wetu iwapo uwezo wetu wa kiingereza na utumiaji wa tarakilishi/kompyuta utaturuhusu! Futa jasho. Vuta pumzi. Kunywa maji. Kisha tulia.
Katika kujibu maoni ya mmoja wa wasomaji wake, mwanablogu huyu akaendelea na madai yake kuwa Watanzania ni “maimuna” (hatujui kiingereza). Akasema, “I don’t even know why you wasted your time, other than talking smack about Kenyans those Tanzanians need to learn how to speak proper english. Let’s see their slick swahili get them out of the hole they have dug themselves in….”
Kwanza kabisa ningependa kumshauri huyu mwanablogu akasome, au akarudie kukisoma kama alishakisoma, kitabu cha Ngugi wa Thiong’o kiitwacho “Decolonising the Mind.” Yaani huwezi kuamini kuwa katika dunia ya leo, tena katika mwaka 2006 ambao ni Mwaka wa Lugha za Afrika (kwa mujibu wa Umoja wa Afrika), mtu anaweza kutokea akasema kuwa ni kosa kutojua kiingereza. Kwani mtu asipojua kiingereza anakuwa nusu mtu? Utu wake unapungua? Ubinadamu leo hii unapimwa na uwezo wa kuongea kiingereza? Kama utu wangu utapimwa kwa kutazama uwezo wangu wa kuongea lugha za watu wengine, basi niambie kuanzia sasa kuwa mimi ni mnyama. Nitakubali. Afadhali niwe mnyama kwa kushindwa kuongea lugha ya kuazima, lugha ya wengine, kuliko kushindwa kuongea lugha yangu. Hivi unaweza kumtukana Mfaransa kwa kumwambia, “Kwenda huko, kwanza wewe hata Kichina hukijui.” Atakushangaa una maana gani. Wala hatachukia maana kutojua Kichina sio jambo la aibu kwake. Sio tusi. Huwezi kwenda kwa Mswidi au Mchina ukamwabia, “Wewe uko nyuma sana kimaendeleo maana hata kiingereza hukijui sawasawa.” Atajua kuwa unatania tu maana haiwezekani ukawa unamaanisha unachosema.
Sasa kama sio aibu kwa Mfaransa kutojua kiingereza, au Muingereza kutojua Kikuyu, au Mmarekani kutojua Kiswahili, kwanini iwe, kama mwanablogu huyu anavyodhani, kuwa ni kosa kwetu kujua Kiswahili na sio kiingereza? Hakuna ubaya wowote. Hii ni moja ya kati ya vielelezo vingi vya madhara ya kutawaliwa kiasi cha kujifanya tujichukie na kutumia lugha na tamaduni za wengine kama vipimo vya utu, heshima, na maendeleo. Huu ni ugonjwa. Mwandishi wa Nigeria (Mloyi, unamkumbuka), Chinweizu, anaita ugonjwa huu, Negro negrophobia. Ana makala moja iitwayo: On Negrophobia: Psychoneurotic Obstacles to Black Autonomy (or Why I just love Michael Jackson). Majuzi Koigi Wamwere aliandika kuhusu hili suala la kujichukia, ingawa hakuwa anazungumzia lugha, mada yake haina tofauti na mada hii hapa. Isome hapa.
Mimi hata siku moja siwezi kuchukia mtu akiniambia eti sijui lugha za watu wengine. Ila sitakaa kimya. Nitamwelimisha. Kama sizijui, basi sizijui. Muhimu kwanza, kwa maoni yangu, ni kujua lugha ya watu wangu. Kisha mengine yatafuata. Halafu lazima niseme kuwa sio kweli kuwa Watanzania hawajui kiingereza. Unajuwa kuna watu wengine wanaweza kudhani kuwa tunablogu kwa Kiswahili maana hatujui kiingereza. Wanaodhani hivi wamepotea njia. Tuna sababu za kiitikadi, kitamaduni, na kizalendo zinazotufanya tutumie lugha yetu. Tunatumia Kiswahili maana tunaitazama dunia tofauti na mtu ambaye anadhani kuwa ni sifa kujua kiingereza.
Wako Watanzania wanaojua kiingereza na wako wasiojua kiingereza. Wote ubinadamu wao ni sawa. Wako Wakenya wasiojua kiingereza, na wako wanaojua kiingereza. Eti Michuzi, ina maana Daily News na Sunday News mnaandikiwa habari na Waingereza?
Halafu huu mtazamo wa kuwa Watanzania hawajui kiingereza wakati mwingine huenda pamoja na mtazamo potofu kuwa Wakenya hawajui Kiswahili.
—
ITAENDELEA
WordPress database error: [Table 'wp_comments' is marked as crashed and last (automatic?) repair failed]
SELECT * FROM wp_comments WHERE comment_post_ID = '1282' AND comment_approved = '1' ORDER BY comment_date