Sat 21 Oct 2006
Mkutano wa Wanablogu wa Afrika 2007
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: blogu , wanablogu , afrika , mikutanoBaada ya kuandika kuhusu mkutano wa wanablogu niliohudhuria wa Converge South 2006 (bonyeza hapa kuhusu mkutano huo), mwanablogu Ras Luihamu aliuliza kwanini wanablogu wa Afrika tusiwe na mkutano wetu? Akaandika:
“Kwanini inkuwa vigumu sisi wanablogu kutoka Africa kuwa na mkutano wetu hapahapa Africa?”
Akaandika zaidi:
“Mzee Ndesanjo nasi tungependa tuwe na mkutano wa wana blogu kutoka Africa hapa hapa Afrika kwa sababu tunaweza kujifunza mambo mengi sana,nadhani hatuhitaji wadhamini kwani lengo letu ni kukutana kisha kuzungumzia kazi zetu.Nemeandika mara kwa mara kuhusu hili jambo lakini naona kimya hakuna anae support.Kwa nini? May be no one cares or its none of i and i business.”
Wazo hili ni zuri sana. Ndio maana nimeamua kuandika haya machache pamoja na kutingwa (natafsiri sinema ya Mtanzania mwenzetu, kuna Watanzania wanachonga vipaji vyao sio mchezo!). Tumewahi kulizungumzia suala la mkutano huko nyuma tukaliacha hewani likidundadunda kama kitenesi. Sidhani kuwa wanablogu wa Afrika hatujali kuwa na mkutano wetu wenyewe. Jambo kubwa ni kujua kuwa hakuna mwingine bali sisi wenyewe ndio tunaweza kuwezesha mkutano huo kufanyika. Na mipango ya kufanya mkutano hiyo ilishatangazwa lakini naona kumekuwa na dalili za kujivuta za kuchangia jinsi ambavyo mkutano huo utakavyofanyika.Baada ya ule mjadala mkali wa Digital Indaba (bonyeza hapa usome muhtasari nilioandika kuhusu mjadala huo), mwanablogu mahiri wa Kenya wa blogu ya Mental Acrobatics, alikuja na wazo. Alisema kuwa badala ya kuzozana kuhusu mkutano ule wa Digital Indaba Afrika Kusini, Waafrika tujiunge na kufanya wetu. Bonyeza hapa usome aliyoandika. Akatangaza kuanzishwa kwa kundi la majadiliano la Google. Bonyeza hapa ujiunge na kundi hilo.
Wazo hili nimelipenda kwa kuwa najua umuhimu wa wanablogu wa Afrika kukutana. Juhudi hizo za kufanikisha mkutano huo ni zetu wote. Hakuna mtu wa kumsubiri. Ni juhudi za kijamaa, ki-harambee harambee. Haba na haba hujaza kibaba. Kidole kimoja hakiui inzi wala sisimizi!
Baada ya Daudi wa Mental Acrobatics kutoa wazo hilo na kuanzisha ukurasa wa Google, nilikubaliana na hoja yake hivyo nami nikaamua kuchangia juhudi hizo kwa kuanzisha ukurasa wa wiki ambao utawezesha mtu yeyote kushiriki katika kupanga mikakati hiyo kwa kuweka taarifa na maelezo mbalimbali muhimu. Bonyeza hapa uone ukurasa huo wa wiki. Unaweza kuchangia hapo kwa kubonyeza palipoandikwa “edit.”
Moja ya mambo makubwa ambayo tunaweza kuanza kujadili hivi sasa ni wapi utafanyika mkutano huo, nini madhumuni ya kukutana, je kuna umuhimu wa kuwa na kamati za kusaidia kuratibu maandalizi?, je mkutano huo utaendeshwa kwa utaratibu gani (warsha, semina, n.k.)?, je kama kuna gharama, ni wapi fedha za kugharamia zitapatikana? Mambo yote haya tunaweza kujadili na kufikia maamuzi kwa kutumia wiki na kundi la majadiliano la Google. Kama tunataka kukutana mwaka ujao, kama alivyopendekeza Daudi, basi tunatakiwa kuanza kujadili masuala haya mapema mapema. Hii ni changamoto kwetu wanablogu. Kama tumezoea kunyooshea wengine vidole, basi sasa dimba limekuja kwetu. Tutaongea tu au tutatimiza? Ila swali kuhusu kwanini tukutane, nini madhumuni ya kukutana pengine ndio litaweza kuchochea ushiriki wa wengi. Lazima kuwe na sababu za msingi za watu kukutana na sio kukutana kwakuwa kukutania ni jambo zuri. Ni jambo zuri ila sababu zenyewe ni zipi? Tunaweza kuanzia hapo kabla hata ya kuanza kujadili tutakutana wapi na kama tunahitaji kamati za kuratibu na masuala ya gharama, n.k. Kwanini tunataka kukutana?
Inawezekana pia, nasema inawezekana, tukaongea tu, tusichukue hatua zozote, kila mtu akawa anamsubiri kila mtu, siku zikapita, miezi, mwaka…mara mwisho wa dunia, jamaa karudi tunamwona mawinguni, parapanda zikalia…(hadithi hii unaijua?).
Kwahiyo ndugu Luihamu, tunaweza kukutana. Tukiamua. Tukashiriki kuwezesha mkutano huu kufanyika bila kusubiri mtu. Kazi kwetu.
WordPress database error: [Table 'wp_comments' is marked as crashed and last (automatic?) repair failed]
SELECT * FROM wp_comments WHERE comment_post_ID = '1294' AND comment_approved = '1' ORDER BY comment_date