Thu 2 Nov 2006
Shiriki Kupanga Mkutano wa Wanablogu wa Tanzania
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: blogu , wanablogu , tanzania , mikutanoSina neno la kuongeza kuelezea kwanini wanablogu wa Tanzania tunahitaji kukutana. Jeff Msangi ameelezea vizuri na baadhi ya wanablogu tayari wametoa maoni kuunga mkono hoja yake. Namshukuru kwa jitihada zake za kutaka tukutane, mtandaoni kwa hivi sasa, wakati tukisubiri siku ambayo tutakaa meza moja, kula, na kucheka pamoja. Kama hujamsoma Jeff akitoa wazo la mkutano huu, bonyeza hapa.
Sasa ili kufanikisha mkutano wenyewe, kuna mambo mawili tunatakiwa kufanya. Jambo la kwanza ni kukubaliana kuhusu siku na saa. Kutokana na ukweli kuwa tumetapakaa katika nchi mbalimbali na hivyo masaa yanatofautiana, inatupasa kuchagua saa kwa makini sana. Kibinafsi ningependa sana tutilie mkazo hali halisi ya wenzetu walioko nyumbani. Kwa mfano, ni rahisi kwa walio Ughaibuni kushikiri kwenye mkutano huu usiku wa manane au matisa kuliko wenzetu walioko Tanzania. (bonyeza hapo chini umalize kusoma habari hii).
Jeff amependekeza tarehe 18 Novemba, saa 6 mchana kweupe kwa saa za Tanzania. Sasa ili tujue kama wote, au wengi wetu tunaweza kuwa na muda siku gani na tarehe gani, nenda katika tovuti nitakayokupa kiungo chake. Nimeiweka hiyo tarehe 18 Novemba, ambayo nadhani ndio tuipe kipaumbele. Hiyo ni siku ya jumamosi (yaani siku ya kwanza ya juma kwenye Uislamu, siku ya sita kwenye Ukristo (ukitoa Wasabato ambao kwao hii ni siku ya saba). Sijui kama tuna mwanablogu Msabato ambaye anaweza kusema kuwa akishiriki itakuwa ni kinyume na dini yake? Binadamu…acha tu, yaani tumeshindwa hata kukubaliana siku ipi ni ya kwanza, na ipi ya pili, n.k.
Turudi kwenye mada. Lakini pia nimeongeza jumapili ya tarehe 19 Novemba, halafu nikaongeza na jumamosi na jumapili ya wiki inayofuata ili kupanua siku za kuchagua. BADILIKO: Imeonekana kuwa ni vyema tukabaki na siku moja, yaani Novemba 18. Hivyo tupilia mbali siku nyingine utakazoziona kwenye kalenda hii. Unachotakiwa kufanya ni kuwa ukifika kwenye kiungo hicho, ambacho nitakupa (kuwa na subira!), andika jina lako pale panaposema “Your Name.” Kisha weka alama ya vema kwenye kisanduku kilichoko katika tarehe na saa ambazo ni muafaka kwako. Hata kama tarehe zote hizo ni bora kwako, weka vema kote. Jeff alichagua saa sita. Nimeongeza saa nane pia (kwa saa za Tanzania).
Nadhani Jeff anaweza kuratibu shughuli hii kwa kutuambia angependa kutoa muda gani ambao tutatazama siku na saa watu walizochagua na kuamua kimoja siku ya mkutano huo (kuendana na siku na saa iliyopata kura nyingi). Kwahiyo basi bonyeza hapa (teknolojia yenyewe inaitwa Doodle. Unaweza kuitumia katika shughuli unazoshirikiana na wengine, hata kazini kwako, kwa ajili ya kupanga tarehe na siku za mikutano na mambo kama hayo. Ni teknolojia ya bure bila hata sentano).
Tukishakubaliana siku na saa, basi tutakutana mtandaoni kwa kutumia teknolojia nyingine ya bure, IRC @ Work. Uzuri wa teknolojia hii ni kuwa hakuna haja ya kushusha programu yoyote kwenye tarakilishi yako, jambo ambalo lingeweza kuwawia vigumu wanablogu wanaotumia migahawa ya Intaneti (ambapo wanaweza wasiwe na uwezo wa kushusha programu kwenye tarakilishi hizo). Hii ni teknolojia iliyojikita webuni, hivyo ukiwa na Intaneti utaweza kushiriki. Ni moja ya teknolojia zenye sifa zinazojenga msingi wa dhana maarufu siku hizi ya Webu 2.0 (bonyeza hapa usome kwa kifupi kuhusu dhana hii. Soma baada ya kuchagua siku ya kukutana iwapo wewe ni mwanablogu au unapenda tu kushiriki ingawa sio mwanablogu).
Teknolojia hii haitumii sauti bali maneno. Bonyeza hapa uone teknolojia yenyewe. Siku hiyo utakachofanya ni kuandika jina lako kwenye kisanduku kinachosema “Nick Name,” kisha pale panaposema “Channel” andika #blogubongo, pale kwenye “Server” usibadili kitu. Kisha utabonyeza “login.” Hapo utaingia kwenye hiyo mitabendi ya #blogubongo na kukutana na wenzako.
Naamini kuwa aliyoandika Jeff tutayachukulia kwa uzito wake na kujaribu kila tuwezalo ili kuweza kukutana mwezi huu. Vitendo muhimu kuliko maneno. Kwenye blogu zetu, tunanena. Je, ukija wakati wa vitendo tupo?
NYONGEZA: Ningeshauri kila mwanablogu anayeunga mkono wazo hili atangaze huu mkutano kwenye blogu yake. Pia nilisahau suala la umeme Tanzania! Walioko huko ndio wanajua mgao unavyokwenda hivyo wanaweza kutoa ushauri bora zaidi kuhusu siku na saa.
WordPress database error: [Table 'wp_comments' is marked as crashed and last (automatic?) repair failed]
SELECT * FROM wp_comments WHERE comment_post_ID = '1301' AND comment_approved = '1' ORDER BY comment_date