Wakati tunahesabu masaa kabla ya ule mkutano wetu wa wanablogu na wapenzi wa blogu wa Tanzania, nimepata habari njema zinazohusu blogu ya mwenzetu. Blogu ya kimombo ya Jeff Msangi imeteuliwa katika kinyang’anyiro cha tuzo za blogu bora nchini Kanada (2006 Canadian Blog Award). Blogu hiyo, African Perpective, iko katika kundi la blogu bora za Kitamaduni (Best Cultural Blog). Bonyeza hapa umpigie kura (shuka chini kwenye orodha ya “best cultural blog). Bonyeza hapa usome blogu yake ya African Perpective.

Haya, mkutano wetu ndio huo. Kuna maelezo ya hatua kwa hatua ya jinsi ya kuingia kwenye chumba cha mkutano. Maelezo hayo yako kwenye ukurasa maalum wa wiki wa mkutano wetu. Bonyeza hapa. Tafadhali sana fuata maelezo hayo hatua kwa hatua, la sivyo utabaki nje ya ukumbi ukipiga soga na wapita njia. Kwa taarifa yako kutakuwa na chai, kalimati, sambusa, vitumbua, kashata na mapochopocho mengine ya Kitanzania kwa hisani ya Miriam! Shauri yako! (bonyeza hapo chini umalize kusoma habari hii)

Muda mfupi ujao ajenda rasmi toka kwa msimamizi wa mkutano, Ramadhani Msangi, zitatangazwa na kubandikwa kwenye ukurasa huu hapa maalum kwa ajili ya mkutano. Tayari ajenda rasmi zimeshatolewa. Bonyeza hapa uzitazame. Kama una maoni kuhusu ajenda hizi, basi jumamosi saa nne asubuhi kwa saa za Tanzania ndio mwisho wa kutoa maoni yako.

Nitabandika maelezo hayo hapo chini. Mambo ya kukumbuka: kile kisanduku kinachosema “NICKNAME,” tafadhali andika jina lako ili washiriki tuweze kufahamiana. Kisanduku kinachosema “SERVER,” tafadhali usibadili chochote hapo. Kisanduku cha tatu kinachosema, “CHANNEL,” andika: #blogubongo (usisahau hii alama ya: # ambayo inapatikana kwenye vidude vyenye tarakimu kwenye kompyuta yako). Chini kabisa ya ukurasa huo ndio kuna kisanduku kirefu chembamba ambacho ndio utatumia kuandika mawazo yako. Ukishaandika unabonyeza “ENTER” ili washiriki wasome ulichoandika.

Maelezo yaliyoko kwenye ukurasa wa mkutano wetu hayo hapo chini (unaweza kuyapata pia kwa kubonyeza hapa):

Mkutano huu utafanyika kupitia teknolojia ya Internet Relay Chat, hivyo utakuwa ni mkutano wa mtandaoni.

Maelezo: Maelezo haya ni muhimu sana maana usipoyafuata hutaweza kushiriki.

1.Nenda kwenye tovuti ya IRC@Work. Bonyeza hapa.

2. Ukifika hapo utakuta kisanduku kina sehemu tatu.

3. Sehemu ya kwanza inasema Nickname. Andika jina lako kwenye kisanduku hicho.

4. Sehemu ya pili inaitwa Server. Usiandike chochote au kubadili chochote hapo

5. Sehemu ya tatu inaitwa Channel, hapo utaandika: #blogubongo

6. Baada ya kufanya hivyo, bonyeza pale panaposema Login

7. Utakuwa umeingia ndani ya ukumbi wa mkutano.

8. Ukishaingia, upande wa juu kulia utaona majina ya watu wengine walioko ukumbini. Ukitazama chini kabisa utaona ufito mwembamba ambao ndio utautumia kuandika mchango wako kwenye mkutano. Ukishaandika unabonyeza Enter kwenye kompyuta yako ili mchango wako usomwe.

Tafadhali fuata vyema maelezo haya.