Nilipokwenda India, ukiacha suala la kusafisha macho, nilihudhuria mikutano miwili. Mikutano hii ni ule wa Global Voices Online na wa pili uliitwa Hibiscus Project. Mkutano wa Global Voices ulifanyika kwa siku mbili. Nilijaribu, ingawa mtandao-usiwaya uliniangusha, kuandika yaliyojadiliwa siku ya kwanza ya mkutano huo. Bonyeza hapa usome niliyoandika toka ndani ya mkutano (jua kuwa niliandika bila kupitia na kuna mambo mengi pia ambayo yalinipita sikuyaandika). Siku ya kwanza ilikuwa wazi kwa mtu yeyote ambaye alikuwa amejiandikisha. Mkutano wa siku ya pili ulikuwa ni wa wahusika wakuu wa mradi huu ambapo masuala ya ndani yalijadiliwa.

Ninachotaka kuongelea leo ni Hibiscus Project. Mkutano kuhusu Hibiscus Project ulikuwa ni ndio wa kwanza ambapo jambo kuu lilikuwa ni kubadilishana mawazo. Mradi huu ulianza kwa majadiliano kupitia barua pepe kuhusu uwezekano na umuhimu wa kutumia teknolojia ya blogu ili kujenga daraja la mawasiliano kati ya Waafrika na Wachina na pia kuanzisha mijadala kuhusu mahusiano ya China na Afrika. Kutumia blogu ili wanablogu wa wa China waanze kuongea na wanablogu wa Afrika. China na Afrika zipige gumzo.

China inawekeza kwa kasi sana hivi sasa barani Afrika katika nyanja za mawasiliano, mafuta, madini, teknolojia, n.k. Baadhi ya watu wanasema kuwa uhusiano huu ni ukoloni mpya na kuwa unatazama zaidi maslahi ya China ya kiuchumi na kisiasa (kwa mfano inavyozitaka nchi za Afrika kutoitambua Taiwan na kutaka kura za Afrika kama kwenye Umoja wa Mataifa).

Uhusiano huu ambao unahusisha mabilioni ya malighafi kwenda China unahitaji kueleweka vyema kwa wananchi wa China na wale wa Afrika. Wakati huo huo, uhusiano huu wa kisiasa na kiuchumi unaongeza uhusiano wa moja kwa moja kati ya Waafrika na Wachina, unaleta suala la umuhimu wa Waafrika kujifunza Kichina na Wachina kujifunza lugha zinazotumiwa kwa wingi Afrika. Umuhimu wa Waafrika kujua masuala ya China (utamaduni, historia, tabia zao, n.k.) na wao kujua pia juu yetu. Ukifanya kazi au biashara na watu waliotoka utamaduni tofauti kabisa na wako kama Wachina au Wajapani utagundua umuhimu wa kujua utamaduni wa unayefanya naye biashara. Kwa mfano, watu wengi toka nje ya Afrika huwa hawajui kuwa ukiweka miadi ya kukutana saa nne na mtu, sio lazima mtu huyo aje saa nne juu ya alama. Anaweza kuja saa tano kasoro!

Kutokana na ukweli huu (ambao nimeongelea kijuujuu sana), kumeonekana kuwa kuna umuhimu wa kuanzisha juhudi zitakazosaidia raia wa Afrika na China kufahamiana zaidi na kuwepo kwa ukurasa mtandaoni ambao utakuwa na taarifa na habari muhimu kuhusu uhusiano wa Afrika na China (ukurasa huu utakuwa msaada mkubwa kwa waandishi wa habari, wanablogu, wanafunzi, walimu, watunga sera, n.k).

Baada ya mjadala pale New Delhi ambao ulihusisha wanablogu toka China na Afrika (kama Daudi wa Mental Acrobatics na Imnakoya wa Grandiose Parlor), ilionekana kuwa kuna haja ya kuwa na miradi midogo midogo chini ya kivuli cha Hibiscus Project. Kwahiyo kutakuwa na ukurasa ambao wanablogu toka China na Afrika watakuwa wakiandika masuala ya uhusiano huu. Kutakuwa na mradi ambao utaanzisha ziara za wanablogu toka Afrika kwenda kukaa na wanablogu China, na wanablogu toka China kwenda kukaa na wanablogu wa Afrika. Wanablogu hawa hawatakuwa wakikaa hotelini bali nyumbani kwa wanablogu wenzao, kisha watakuwa wakiandika juu ya uzoefu wao katika utamaduni mpya. Moja ya dhumuni la ziara hizi ni kuondoa fikra potofu ambazo Wachina na Waafrika wanazo baina yao. Kutakuwa na mradi ambao wanablogu watapewa kamera ambazo watakuwa wakipiga picha katika sehemu wanazoishi ambazo zitatumika kama zana za kuelimisha. Zitakuwa kama dirisha la kutazama utamaduni wa mwenzako.

Mradi mwingine utahusisha shughuli za kutafsiri kazi mbalimbali (habari toka magazetini, bloguni, machapisho ya kitaaluma, hotuba za viongozi, n.k.) kutoka lugha ya Kichina kwenda katika lugha mbalimbali zinazozungumzwa kwa wingi Afrika.

Wazo la Hibiscus Project limetoka kwa Akwe Amosu ambaye ni mchambuzi mwandamizi wa sera wa taasisi iitwayo Open Society Institute (OSI)

Unaweza kusoma habari zaidi kuhusu mradi huu kwenye blogu ya Ethan Zuckerman na Imnakoya wa Grandiose Parlor, ambao walihudhuria mkutano huu. Bonyeza hapa na hapa.

Pia kuna wanablogu ambao hawakuhudhuria mkutano wa Hibiscus Project ila wanaelekea kufurahishwa na matarajio ya mradi huu. Wasome hapa na hapa.