Sat 17 Feb 2007
Simu Za Mkono Na Mabadiliko Chanya Ya Jamii
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: teknolojia , afrika , harakati dijitaliHuenda wewe ni mwanaharakati. Huenda unajihusisha kwa njia moja au nyingine katika harakati za kuleta mabadiliko chanya ya jamii. Je ni vipi unaweza kutumia simu ya mkono ili kuleta mabadiliko? Watembelee MobileActive ujifunze mbinu mbalimbali na usome habari zinazohusu simu za mkono na mabadiliko chanya ya kijamii. Bonyeza hapa. Kwa upande wa siasa, unaweza kusoma ripoti inayohusu matumizi ya simu za mkono kwenye uchaguzi mwaka jana nchini Marekani. Bonyeza hapa. Ingawa ripoti hii inahusu Marekani, utaona kuwa zipo mbinu mbalimbali ambazo hata vyama vya siasa vya nchi kama Tanzania wanaweza kuzitumia.
SMS Ilivyotumiwa Kupindua Serikali:
Mwaka 2001 matumizi ya kisiasa ya ujumbe wa maandishi wa simu za mkono (SMS) yalichangia kumuondoa madarakani rais wa Ufilipino, Joseph Estrada.
Huko huko Ufilipino, jamaa wa Txtpower, walichukua sauti ya rais wa nchi hiyo, Gloria Macapagal Arroyo, akiongea na aliyekuwa kamishna wa tume ya uchaguzi wa nchi hiyo, Virgillo Garcilliano, akitaka kupata uhakika toka kwa kamishna huyo kuwa atashinda uchaguzi kwa kura milioni moja. Txtpower walifanya mazungumzo hayo kuwa ni mlio wa simu za mkono. Hivyo waliotumia sauti hiyo, wakipigwa simu wanachosikia ni sauti ya rais huyo akiongea kuhusu wizi wa kura! Mamilioni ya Wafilipino walitumia mlio huo.
Kwakuwa kuna teknolojia nyingi zinazowezesha mtu yeyote kuunda mlio wa simu za mkono, unaweza kurekodi sauti ya kiongozi wa kisiasa, kisha ukatumia watu waitumie na kuwataka nao watumie watu wengine. Ujumbe huo unaweza kuwa ni wa kiongozi wa chama cha siasa ambao utatumiwa katika simu za wafuasi wake au inaweza kuwa ni sauti ya Kikwete akidanganya umma wa Watanzania. Kuna teknolojia kama vile Xingtone ambayo inakuwezesha kutengeneza milio ya simu za mkono. Milio ya simu za mkono inaweza kutolewa bure au kuuzwa. Mlio wa simu za mkono hivi sasa ni biashara kubwa sana. Wanamuziki wakubwa wanatengeneza mamilioni kwa kuuza miziki yao itumiwe kama milio ya simu za mkono. Nchini Marekani kuna kampuni kama vile Jivjiv ambayo inatoa huduma ya kuwezesha watu wanaotengeneza milio ya simu za mkono kufungua viduka vyao mtandaoni na kuuza kazi zao.
Watanzania Wanavyoweza Kutumia SMS:
Moja ya matumizi ya simu za mkono yanayofaa kuanza kutumika Tanzania ni uandaaji wa maandamano kwa kutumia ujumbe wa maandishi. Wanaoandaa maandamano Tanzania hutumia vyombo vya habari kutangaza siku, saa, na mahali yatakapofanyika maandamano. Mara nyingi serikali huzuia wananchi kutumia haki zao za kikatiba kuandamana. Kwakuwa habari za maandamano ziko wazi wazi kwenye vyombo vya habari, serikali hutuma Askari wa Kuanzisha Fujo (AKF) kupiga wananchi, kuwakamata, wakati mwingine kuua ili kuzuia maandamano. Iwapo kundi linaloandaa maandamano hayo lina orodha ya simu za mkono za wafuasi wake, kinachoweza kufanyika ni kutuma ujumbe wa maandishi kwa simu za mkono kuwaambia siku, saa, na mahali pa kukutana kwa ajili ya maandamano. Ujumbe unaweza kusema, “ijumaa saa nane mchana tukutane na mabango yasemayo ‘ununuzi wa rada ni wizi’ katika viwanja vya jangwani.” Mara ijumaa sasa nane, nchi inashangaa ni akina hawa wamejazana Jangwani na mabango? Hadi “Fanya Fujo Uone” (FFU) wafike, ujumbe tayari umeshafika.
Machi 2005, maandamano ya zaidi ya watu milioni moja huko Beirut, Lebanon, yaliyochangia kuondolewa kwa majeshi ya Syria nchini humo, yaliandaliwa kwa kutumia ujumbe wa maandishi wa simu za mkono.
Mbinu hii ya kutuma ujumbe kuwataka watu wakutane mahali fulani, saa fulanu inatumiwa sana na makundi yaitwayo Flash Mobs.
Mifano Zaidi Toka Nchi Mbalimbali:
Bonyeza hapa uone mifano zaidi ya matumizi ya simu za mkono katika harakati.
Nchini India, kesi ya mauaji ya Jessica Lal ni mfano mzuri wa jinsi ambavyo SMS inaweza kutumiwa kupinga rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu. Bonyeza hapa usome jinsi SMS ilivyotumiwa katika kutafuta haki katika kesi hiyo. Bonyeza hapa usikilize kipindi cha redio ya NPR kuhusu kampeni hiyo nchini India.
Textually.org wanaandika habari nzuri sana kuhusu matumizi ya simu za mkono katika harakati za kisiasa na kijamii katika nchi mbalimbali. Bonyeza hapa usome habari hizo. Moja ya habari hizo inahusu waandishi wa habari wa Zimbabwe wanavyotumia ujumbe wa simu za mkono kutoa habari kwenye nchi ambayo utawala wake umetia kitanzi uhusu wa habari.
Habari nyingine za Textually.org zinahusu matumizi ya simu za mkono katika nchi zinazosemekana kuwa zinaendelea. Kwa mfano, kuna habari kuhusu matumizi ya simu za mkono kupambana na Ukimwi Afrika, wakulima wa Afrika wanavyotumia simu za mkono kutafuta masoko na kuuza bidhaa zao kupitia mradi mpya wa TradeNet (gazeti la The Economist lina habari zaidi kuhusu TradeNet), mradi mwingine, Manobi, nao unatumia simu za mkono kuwezesha wakulima na wavua samaki nchini Afrika Kusini na Senegal kuuza bidhaa zao, n.k. Kumbe teknolojia hizi Rasta Luihamu zinawafaa pia wakulima?
FrontlineSMS Na Mobile4Good:
Kwa yale mashirika yasiyo ya kiserikali, kuna mradi ambao una teknolojia ya bure, FrontlineSMS, ambayo inawezesha shirika lako
kurahisisha kazi mbalimbali. Iwapo jibu lako ni “ndio” katika maswali hayo hapo chini, basi unahitaji kutumia huduma hii ya bure ya FrontlineSMS:
Are you a locally- or internationally-based NGO looking at the potential to use mobile phone text messages to reach specific groups of individuals within a target community? Or to run an awareness raising campaign? Or to run a competition, or carry out a text-based survey? Or to simply keep in touch with your fieldworkers?
Shirika la OneWorld lina mradi uitwao Mobile for Good (M4G) ambao dhumuni lake ni kutumia teknolojia ya simu za mkono kuondoa umasikini na kuboresha maisha katika nchi za Kusini. Mradi huu una tawi nchini Kenya, M4G in Kenya.
Viungo Muhimu:
+ Mkutano kuhusu matumizi ya simu za mkono na mabadiliko ya jamii Afrika: Kwa ushirikiano na Tactical Techology (shirika linalosaidia mashirika yasiyo ya kiserikali kutumia teknolojia mpya kwa ufanisi), shirika la Fahamu linaandaa mkutano huu unaopangwa kufanyika nchini Kenya mwezi Mei mwaka huu. Iwapo unatumia teknolojia hii katika harakati au una nia ya kufanya hivyo, wanakutaka uwasiliane nao. Bonyeza hapa.
+ Mlogik ni kampuni ya Afrika (Mauritius) ambayo inawezesha mashirika au vyombo vya habari kutumia ujumbe wa simu za mkono katika kazi zao.
+ TxtVoter: mradi uliotumia teknolojia ya ujumbe wa simu za mkono kuandikisha wapiga kura nchini Marekani. TxtVoter ni mradi uliobuniwa na Mobile Voter.
+ TxtMob: teknolojia hii ya bure unaweza kuitumia kwenye kampeni au kutuma ujumbe kwa walengwa.
+ Vicito: huduma hii inakusaidia kuweza kutuma ujumbe kwa watu wengi kwa wakati mmoja kwa kutumia simu yako ya mkono. Bado huduma hii haijaanza rasmi ila unaweza kuwatumia anuani yako ili wakutaarifu watakapoanza.
+ Feedlix: teknolojia iliyoanzishwa na Mwafrika toka Ethiopia, Ted Kidane, ambayo inawezesha watu kutuma ujumbe wa maandishi wa simu za mkono kwa lugha za Kihindi, Kichina, na Kiethiopia (Ethiopic), Kiingereza, na Kilatini. Ted Kidane atakuwa mmoja wa watoa mada katika mkutano wa TED Global utakaofanyika Arusha Juni mwaka huu.
SMSTZ.COM: kampuni ya Tanzania
+ Habari ya kampuni hii ya SMSTZ nimeipata punde toka kwa Michuzi ambaye ameweka picha ya mwanzilishi wa kampuni hii ambayo nayo inatoa huduma za kutuma ujumbe wa walengwa kwa kutumia SMS.
*** Habari nyingine zinazohusiana na hii: Filamu ya mapinduzi ya simu za mkono Kenya, blogu za simu za mkono na kadhalika.
WordPress database error: [Table 'wp_comments' is marked as crashed and last (automatic?) repair failed]
SELECT * FROM wp_comments WHERE comment_post_ID = '1383' AND comment_approved = '1' ORDER BY comment_date