Sun 18 Feb 2007
Nilipomaliza Kuandika Makala Hii Nilipiga Ngumi Ukutani!
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: siasa , tanzania , demokrasia , makalaNilipopiga ngumi ukutani, nilijiumiza mwenyewe…soma makala ambayo imetoka jumapili ya wiki hii katika safu yangu ya Gumzo La Wiki kwenye gazeti la Mwananchi. Makala hiyo ina kichwa hikii: KABLA YA KUBADILI NCHI, BADILI MTAANI KWENU. Ni makala inayokutana inayokutaka kuanza kujifunza mbinu rahisi za kuleta mabadiliko ya kudumu nchini. Kati ya mambo niliyosema katika makala hiyo ni:
Nchi ya Kauli Mbiu Na Mapambio:
Nchi ya kauli mbiu na mapambio. Mapambio ya chama twawala. Twawala nanyi mwalala. Mapambio: vyombo vya habari ni sauti ya pili, wananchi sauti ya nne. Wakereketwa sauti ya kwanza. Wakoloni wapya kwa jina la washauri, Benki ya Dunia (eti benki ya dunia), shirika la fedha duniani, n.k., ni wapiga ala. Wanatuambia kwenye ripoti zao kuwa serikali yetu inaendesha uchumi kwa ufanisi na imepiga hatua mbele kwenye vita dhidi ya rushwa.
Eti nini? Rushwa? Niambie, toka uzaliwe, umemsikia nani kati ya akina nani hii amefikishwa mahakamani kwa rushwa kisha akaenda jela? Niambie ni kesi ngapi unazifahamu za rushwa ya mamilioni? Ukisikia mtu kakamatwa kwa rushwa, utasikia elfu 50 au laki moja. Wote hawa ni dagaa tu. Samaki wakubwa mahakamani hawafikishwi, jela hawaioni. Kwanza walioko kwenye tume ya rushwa ni dagaa, watathubutu kuwaendea samaki wakubwa? Wamezwe?
Kuhusu Dege la Rais Na Hadhi Yake:
Hivi nani kasema kuwa Rais ni mtu mwenye hadhi ya juu kuliko Watanzania wote? Ofisi yake ina majukumu makubwa, ndio. Lakini hii hadhi tunayoambiwa ambayo inahitaji dege la kifahari sijui imetoka wapi. Hivi huyu si mtumishi wetu? Watu tuna mawazo tofauti, achilia mbali suala la ndege. Mimi binafsi sioni sababu yoyote ya Rais eti kufunguliwa mlango wa gari. Kama anaumwa, sawa. Mfungulie mlango, na hata mbebeni kabisa. Kisha mpelekeni hospitali (tena hospitali ambayo wananchi wengine wanakwenda, sio sijui Ulaya, mara Afrika Kusini). Ila kama ni mzima wa afya hakuna sababu yoyote ya kuwapa binadamu wengine kazi za kitumwa na wengine vyeo vya kimungumungu hapa duniani.
Kumfungulia binadamu mwenzako mlango wakati ana afya njema ni aina ya utumwa unaomfanya yule anayefunguliwa mlango kukwezwa kwenye daraja linalokaribia kuabudiwa. Ndio ibada hizo tulizoambiwa na mchora vikaragosi wa Kenya. Ibada za vyombo vya habari Tanzania kumlamba miguu. Kama anashindwa kufungua mlango wa gari, basi hata kuvaa nguo avalishwe, tuajiri mtu wa kumsaidia kupiga mswaki. Mtu wa kumlisha. Tusimnunulie ndege tu, bali meli na helikopta pia. Tunaweza pia kumnunulia visiwa vyetu vilivyoko bahari ya hindi iwapo Waarabu na Wahindi hawajavinunua vyote.
Anzisha Mabadiliko Mtaani Kwenu Kwanza…
Mjadala huu lazima tuuanze hivi sasa. Ni vipi wananchi, ambao ndio wengi kuliko viongozi walaghai, tutakuwa na uwezo, njia, na mfumo imara wa kuhakikisha kuwa hatuibiwi kama watoto wadogo? Kuna wakati niliandika kuhusu mbinu za kuleta mabadiliko kwenye jamii. Nilisema kuwa iwapo hujaweza kumwajibisha mwenyekiti wa serikali za mtaani kwenu, ni vipi utaweza kumwajibisha raisi, mbunge, au waziri? Kama hujaweza kuunda vuguvugu mtaani kwenu kuhakikisha kuwa mnaondoa wezi, mnajenga utamaduni wa kutupa takataka sehemu zinazohusika, mna utaratibu wa kusafisha mtaa wenu, n.k., ni vipi utaweza kuongelea suala la utunzaji wa mazingira kitaifa au kampeni ya kukamata majambazi kitaifa?
Utakapoweza kuleta mabadiliko mtaani kwenu kwa kushirikiana na wenzako, hapo utakuwa umeanza safari ya kuleta mabadiliko kitaifa. Utajifunza mbinu na kanuni muhimu za harakati za kijamii na kisiasa. Utakuwa na uzoefu ambao utakusaidia kuweza kuleta mabadiliko makubwa ya kitaifa. Anza mtaani kwenu kisha panda juu. Unaweza hata kuanza kwa balozi. Makundi haya madogo madogo yanaendesha vuguvugu la kuleta mabadiliko katika mitaa na vitongoji, ndio haya haya yanakuja kuungana na kutumia mbinu na mshikamano unaotokana na uzoefu wa kuleta mabadiliko madogo madogo ili kuleta mabadiliko makubwa.
Hii ndio changamoto tuliyonayo. Je tunaweza kuhakikisha kuwa wilaya zetu zinatumia fedha zake sawasawa? Je bajeti ya shule anayokwenda mwanao unaijua? Je inatumiwa ipasavyo? Je unajua manispaa yako ina bajeti gani? Inatumia vipi fedha hizo? Je unajua ripoti ya mkaguzi wa mahesabu wa manispaa yako au wilaya yako inasema nini? Je kituo cha polisi unapoishi kina askari wa kutosha? Je ni waadilifu? Kama jibu ni hapana, unafanya nini? Unamsubiri nani?
Haya, soma makala nzima iliyonifanya kupiga ukuta ngumi kwa kubonyeza hapa.
WordPress database error: [Table 'wp_comments' is marked as crashed and last (automatic?) repair failed]
SELECT * FROM wp_comments WHERE comment_post_ID = '1391' AND comment_approved = '1' ORDER BY comment_date