Sun 8 Apr 2007
Simu za Kiganjani, SMS, na Harakati Dijitali Afrika
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: teknolojia , siasa , afrika , harakati dijitaliKama ulipitwa na matokeo ya tuzo za blogu Uganda 2006, bonyeza hapa ujue waliozipokea. Ukisoma habari hiyo utaona kuna habari kuhusu matumizi ya ujumbe wa simu za kiganjani (Jeff Msangi: nimetumia “kiganjani”) kupinga hatua inayonuka rushwa na inayodharau kabisa umuhimu wa misitu duniani ya serikali ya rais anayependwa na wazungu, M7, yaani Yoweri Museveni kuipa kampuni ya kutengeneza sukari, Mehta Group, eneo la msitu huo. Sukari, kwa fikra za wezi hawa, ina faida kuliko msitu.
Baada ya habari za upuuzi huu kutangazwa, wanaharakati wakaamua kutumia ujumbe wa simu za kiganjani (SMS) kupinga uamuzi huo. Ujumbe huo ulikuwa ukihamasisha watu ili wasuse sukari ya kampuni hii ya magabacholi. Bonyeza hapa usome habari hiyo ya harakati dijitali dhidi ya wizi na uharibifu wa mazingira. Wanaharakati hao pia wanatumia Petitiontime.com kukusanya sahihi za watu wanaokemea uchafu huu.
Matumizi ya SMS na simu za kiganjani kwa ujumla kwenye harakati na hata shughuli nyingine za maendeleo kama vile kilimo, masoko, biashara, afya, na elimu yanapanuka siku hadi siku.
Hakuna teknolojia ambayo ni rahisi kupatikana na kutumika kama simu za mkono kwa nchi za Afrika ambazo zina mtandao mdogo sana wa simu za nyumbani. Simu za viganjani ndio zitakuja kuwa chombo kikubwa cha watu wa kawaida kuingia kwenye zama za habari na mawasiliano. Sio kompyuta za mezani au za mapajani. Kompyuta zao zitakuwa ndani ya simu zao.
Simu za viganjani zinabadilika kiasi ambacho wakati mwingine inakuwa kama vile tunakosea tukiziita simu. Simu hizi ni kamera za picha, kamera za video, kaseti ya kupiga muziki, redio, kitabu cha kumbukumbu, luninga, n.k.
Nchini Kenya, simu za viganjani zimekuwa benki kabisa! Ukisikia tunatumia neno “mapinduzi” kuelezea mabadiliko yanayotokea kwenye nyanja ya habari na mawasiliano unadhani tunatania. Bonyeza hapa usome habari kuhusu benki ya kwanza dunia ya simu za kiganjani, M-Pesa.
Nchi kama Iraki, Afghanistani, India, na Pakistani simu za viganjani zimetumika kama silaha za vitani. Zimetumika kufyatulia mabomu yaliyotegwa. Hebu soma habari hii hapa.
Kule Zimbabwe baada ya watumwa wa Mugabe kuanza kunyang’anya wananchi redio, redio ya SW Radio Africa ilitangaza kuwa itatuma habari kwa wasikilizaji wake kwa kutumia SMS. Watumwa wa Mugabe ni askari na viongozi wengine wanaotekeleza amri zake kama vile wamepoteza ubinadamu wao. Askari na wanajeshi mwanamuziki Fela Kuti alikuwa akiwaita “Zombie” (Msukule). Alisema,
Zombie haendi hadi umwambie, Nenda!,
Zombie hasimami hadi umwambie, Simama!
Zombie hageuki hadi umwambie, Geuka!
Tuache maana nikimwingilia Fela habari hii haitamalizika. Turudi kwenye simu za kiganjani na harakati dhidi ya Mugabe. Basi SW Radio Africa ikaja na mbinu ya kutumia SMS ili kuwatumia Wazimbabwe habari hata kama hawana redio. Bonyeza hapa usome habari hiyo.
Dunia ya leo watawala wetu hawa itabidi wakeshe wakibuni mbinu. Dunia nyingine kabisa hii. Watakesha na kukesha.
Wazimbabwe wamekuwa pia wakitumia SMS kutumiana vichekesho vya kisiasa ikiwa ni moja ya mbinu za uhamasishaji wa kisiasa. Vichekesho kama silaha dhidi ya udikteta.
Mifano ya baadhi ya vichekesho hivyo:
Baada ya serikali ya Zimbwabwe kutoa noti ya dola za Zimbabwe 100,000 kichekesho hiki kilitumwa kwa watu mbalimbali kwa SMS:
It is only the government of Zimbabwe that loves its people so much that it has made everyone a millionaire!
Kichekesho hiki hiki kinaonyesha jinsi ambavyo sarafu ya Zimbabwe imepoteza thamani. Sijui kama unajua kuwa noti ya Zimbawe ndio noti pekee duniani ambayo ina tarehe ya mwisho ya kutumika kama juisi ya kopo! Bonyeza hapa usome habari kuhusu noti ya nchi hiyo kuwa na tarehe ya mwisho kutumika. Habari hii ina picha ya noti ya dola 20 ambayo ina maneno haya: “Pay the bearer on demand Twenty Dollars on or before 31st July 2007 for the Reserve Bank of Zimbabwe, Issue date 1st August 2006.”
Kichekesho hicho kuhusu kuanguka kwa thamani ya dola ya Zimbabwe kinakwenda hivi:
American President George Bush had $20 000, he bought himself a posh car. South African President Thabo Mbeki had R20 000, he bought a posh car. President Robert Mugabe had Z$20 000. He wanted Z$40 000 more to buy half a loaf of bread.
Kingine hiki:
Vice-President Joshua Nkomo was 82 when he died. Vice-President Simon Muzenda was also 82 when he died. Mugabe has just turned 82. You never know what good happenings are in store for this nation. It’s just a thought.
Bonyeza hapa usome kwa undani habari kuhusu SMS na vichekesho vya kisiasa Zimbawe.
—-
Zaidi ya asilimia 60 ya Waafrika wanaishi kwenye maeneo ambayo yana huduma za simu za kiganjani na kufikia mwaka 2010 idadi hiyo itaongezeka kufikia asilimia 85. Takwimu hii sio ya mchezo. Iwapo wewe ni mwanasiasa au mwanaharakati ambaye hutumii simu za kiganjani kufikia wanachama wako au walengwa wako, au huna mipango ya kufanya hivyo, amka dakika hii. Bonyeza hapa usome habari ambayo inaweza kupanua uelewa wako kuhusu matumizi ya simu za mkono kwenye harakati au shughuli za kimaendeleo.
WordPress database error: [Table 'wp_comments' is marked as crashed and last (automatic?) repair failed]
SELECT * FROM wp_comments WHERE comment_post_ID = '1442' AND comment_approved = '1' ORDER BY comment_date