Ukurasa wa Global Voices Online (GV) umebadilika. Mafundi wa ukurasa huu kwa miezi kadhaa walikuwa wakiukarabati ili uendane na wakati. Jumatatu wiki hii ukurasa huu ulizinduliwa rasmi. Mmoja wa waanzilishi wa Global Voices Online, Ethan Zuckerman, ametangaza ukurasa huu mpya kwa maneno haya: Our site is prettier than your site.

KABATI LA HABARI
Mambo kadhaa yamebadilika na mengine kuongezwa ili kuwarahisishia wasomaji uwezo wa kupata habari tunazoandika. Zamani ukurasa huu ulikuwa una wingu la nchi mbalimbali ambazo tunaandika habari zake. Hivi sasa kuna “kabati” ambalo limeficha wingu hilo. Ndani ya kabati hilo unaweza kupata habari kwa kuchagua nchi au maudhui.

RAMANI YA HABARI
Kati ya “viungo” vilivyoongezwa kuupa ukurasa huu ladha ni ramani. Unajua zamani ramani zilikuwa hazina uhai. Zamani ramani ikishatengenezwa huwezi kuongeza chochote. Pia ilikuwa vigumu kuweka habari zote ambazo ungependa ziwepo kwenye ramani kutokana na nafasi. Hata pamoja na kutumia nyenzo kama “ufunguo” bado kuna taarifa nyingi zilikuwa hazipatikani. Kwa mfano, ukiwa na ramani ya Tanzania, ukawa na mlima Kilimanjaro, ni vigumu kuweka taarifa zote kuhusu mlima huo kwenye ramani za vitabuni. Unaweza kuweka taarifa chache kama vile urefu wake, uoto wa asili wa eneo hilo, n.k. Lakini msomaji wa ramani anaweza kuwa anataka kujua watalii wangapi hupanda mlima huo, miezi ipi ni muafaka kuupanda, wakazi wa eneo hilo ni akina nani, idadi yao, shughuli zao za biashara, habari kuhusu theluji mlimani hapo, historia yake, n.k. Ungeweka habari zote hizi pengine ramani hiyo isingesomeka kwa kujaa maandishi na alama.

Sasa teknolojia imebadili namna tulivyokuwa tunaelewa na kutengeneza ramani. Ramani siku hizi unaweza kuweka picha, maandishi, video, sauti, n.k. Unaweza kuzifanya ramani hizo kuwa na uwezo wa kuweka taarifa mpya kila zinapojitokeza. Mfano mmoja unaonijia haraka ni Ramani ya Magereza Tunisia iliyotengenezwa na Sami. Sami ni Mkurugenzi wa Utetezi wa Global Voices.

Narudi kwenye mada. Ukurasa mpya wa GV una ramani ya kumsaidia msomaji. Kwahiyo ukiwa unasoma habari kuhusu nchi fulani, utaona ramani ya nchi hiyo. Ndani ya ramani hiyo utaona taarifa mbalimbali kama vile idadi ya habari na viungo vilivyoko kwenye ukurasa kuhusu hiyo nchi, tarehe ya mwisho ya habari iliyoandikwa kuhusu hiyo nchi, n.k. Ramani hii inakuwezesha pia kupata picha za satelaiti za nchi mbalimbali.

Bonyeza hapa usome tangazo la uzinduzi wa ukurasa huu mpya.

WAYBACK MACHINE
Sijui kama unaifahamu Wayback Machine. Wayback Machine ni mradi wa Internet Archive ambao kazi yake ni kutunza historia ya tovuti. Kwa kutumia Wayback Machine unaweza kuona ukurasa wa zamani wa Global Voices Online. Bonyeza hapa uuone (kama hukuwahi kuuona).

Halafu tazama Yahoo! ilivyokuwa mwaka 1996. Linganisha na ukurasa wake wa sasa. Unaweza pia kutazama jinsi Yahoo! ilivyobadilika hadi kuwa ilivyo hivi sasa kwa kutazama kumbukumbu za tovuti zake hapa.

Wayback Machine imenijia nikasema niichomeke hapa. Kikubwa ni taarifa ya ukurasa mpya wa GV. Bonyeza hapa.