Naona tumewaangusha wasomaji wetu ambao wangependa kufuatilia yanayoendelea kwenye mkutano wa Digital Citizen Indaba na Highway Africa. Mtandao wao, kama ilivyokuwa mwaka jana, umekuwa ukisumbua. Nikafika mahali nikasema, “Potelea mbali. Isiwe tabu.” Hata tarakilishi nikairudisha na leo wala sikuja nayo. Unajua uzee tena, basi nikasema ngoja niwaachie vijana wablogu moja kwa moja. Nikasema kijana Bob Sankofa yuko atakuwa anaandika maana kila saa nilikuwa namuona na tarakilishi yake. Kumbe wapi, naye anakuja kuniambia kuwa alidhani kuwa nilikuwa ninablogu maana kapata tabu kuingia mtandaoni.

Digital Citizen Indaba ilifanyika jana. Na kuanzia leo hadi kesho kutwa ndio unafanyika mkutano wa Highway Africa. Jana niliongea wakati wa ufunguzi. Mada yangu niliita: From Rock Paintings to Mental Acrobatics (Mental Acrobatics in blogu ya Daudi Were, ambaye naye anahudhuria Indaba).

Wazungumzaji wengine waliowakilisha Tanzania “ndani ya nyumba” ni Bob Sankofa na Ansbert Ngurumo.

Kusoma zaidi kuhusu mada hiyo bonyeza hapa na hapa. Habari nyingine zaidi, nenda hapa na hapa.

Halafu soma habari kuhusu aliyozungumza Bob Sankofa hapa. Habari hii imeandikwa na mwanablogu mpya, Furaha Thonya. Furaha yeye amekuwa hapa Afrika Kusini akihudhuria kozi ya kitu kiitwacho, “Digital Journalism.” Na tulifurahi sana kukutana na dada yetu akiwa ndio ameanza “kulewa mvinyo” wa kublogu. Bonyeza hapa uone blogu yake.

Baada ya chakula cha mchana leo, nilizunguka nyuma ya ukumbi tunaoutumia kwa chakula. Chuo Kikuu cha Rhodes kiko juu hivi, ukisimama mahali pasipo na miti mingi unaona mji wa Grahamstown kwa uzuri sana. Basi nikaenda hapo ili nitazame mji wenyewe toka juu. Nikamwita jamaa mmoja nikamuuliza, “Eh bwana, zile nyumba kuleeeee wanakaa akina nani?”
Akaniambia, huku akizinyooshea kidole, kuwa nyumba zile mbaya mbaya ndipo wanapokaa weusi, upande mwingine kuna nyumba nzuri nzuri kiasi ambazo wanaokaa ni Warangirangi (coloreds), na upande mwingine kuna nyumba nzuri na za kifahari hizo wanakaa….alipofika hapo alikunja ngumi halafu akatoa ishara ya mtu mnene na mwenye nguvu na kusema, “Wanakaa matajiri.”

Eti, ubaguzi Afrika Kusini si uliisha au?

Kabla sijakuacha: Miaka 30 iliyopita wiki hii, mtetezi wa masuala ya utu wa mtu mweusi Afrika Kusini, Steve Bantu Biko alituacha. Usimsahau.

The most potent weapon in the hands of the oppressor is the mind of the oppressed.
— “White Racism and Black Consciousness”, in I Write What I Like

Hadi baadaye. Nisije nikachelewa tafrija ya jioni hii.