Baada ya kurudi Afrika na kuzama kwenye shughuli zilizonitoa kidogo nje ya blogu na masuala mengine mtandaoni, nimeibukia Tshwane (jina jipya la Pretoria) nikajisikia kama vile nilikuwa nje ya dunia hii. Pale Tshwane nilishiriki kwenye warsha iliyoitwa Pan African Localisation Workshop. Hii ni warsha iliyokuwa ikiwashirikisha watu mbalimbali toka Ethiopia, Djibouti, Msumbiji, Nigeria, Ghana, Misri, Marekani, Tanzania, Uswisi, Congo (DRC) na Senegal ambao wanajihusisha na masuala ya lugha na teknolojia, hasa masuala ya kuenyejisha (localise) zana/programu za kompyuta na maarifa mtandaoni. Mradi huu umefikisha mwaka wa tatu toka uanze kufadhiliwa na IDRC.

The PanAfrican Localisation project is a three-year effort, funded by IDRC, to build capacity for localisation in African languages including Arabic.

Unaweza kubonyeza hapa kusoma zaidi juu ya mradi huu na agenda ya mkutano wenyewe. Na hawa ndio washiriki na waandaaji wa mkutano. Tofauti kubwa ya warsha hii na nyingine ambazo nimewahi kuhudhuria za masuala ya teknolojia ni kuwa washiriki ni watu ambao wanafanya mambo. Hawasemi kuwa wanapanga kufanya mambo fulani, bali tayari wanafanya na wengine wanafanya kama watu binafsi tu bila malipo yoyote. Kati ya programu wanazozienyejisha ni pamoja na zile za kutambua sauti (ambapo mtu asiyejua kuandika anaweza kuongea kwa lugha ya Kiafrika kisha kompyuta ikaandika anachosema).

Leo imenikuta Egoli/Jozi (Johannesburg). Hapa Jozi tunachokifanya kuendesha
Wikipedia Academy. Wikipedia Academies zimefanyika sehemu nyingine duniani na hasa Ujerumani zimekuwa na mafanikio makubwa ila hapa Afrika hii ni mara ya kwanza. Wikipedia Academy ni tukio ambalo watu wasiofahamu Wikipedia ni nini na jinsi ya kuwa wanawikipedia wanafundishwa. Ingawa hii ni mara ya kwanza haitakuwa mara ya mwisho. Huu ndio mwanzo wa mfululizo wa Wikipedia Academies ambazo zitafanya kwenye nchi mbalimbali za Afrika.

Leo tumekuwa na mkutano wa maandalizi kwenye ofisi za iCommons kwenye kitongoji cha Rosebank. Mkutano umeshirikisha wafanyakazi wa iCommons, Jimmy Wales (mwanzilishi wa Wikipedia), Frank Schulenburg toka Wikipedia ya Kijerumani na wanawikipedia wa Afrika Kusini. Tumekwenda pia kutembelea chuo cha CIDA ambapo ndipo tutaendesha mafunzo kwa wanafunzi 40 chuoni hapo kesho ili waanze kuandika Wikipedia kwa lugha za Kiafrika. Wazo hili la kutumia dhana ya “Wikipedia Academy” kama njia ya kutoa mafunzo kwa Waafrika ili washiriki kupanua au kuanzisha Wikipedia za lugha za Kiafrika naona kama ni moja ya njia sahihi ya kusaidia kukuza lugha na maarifa ya Afrika mtandaoni. Wikipedia Academy ya pili haijajulikana itafanyika wapi ila ninahisi kuwa itafanyika nchini Namibia.

Baada ya kutoa mafunzo pale chuo cha CIDA tutakwenda kwenye onyesho lililoandaliwa na kampuni ya Levi’s liitwalo Rage For the Revolution. Onyesho hili la muziki litafanyika katika sehemu ambayo ni siri hadi sasa. Tiketi za onyesho ni 500 tu na moja ya njia ya kuweza kupata tiketi ni kuwa mtu lazima upime Ukimwi. Nia ya onyesho hili ni kuhamasisha watu kupima umeme. Wenye tiketi wanajua mahali pa kukutani ambako kutakuwa na mabasi ya kuwapeleka watu kwenye onyesho lenyewe.

Haya, nirudi kwenye kazi. Ninaandaa hotuba nitakayoitoa kesho ya kuhamasisha wanafunzi hawa 40 kuona umuhimu wa kuendeleza lugha zetu mtandaoni. Nitaonyesha uhusiano kati ya lugha, teknolojia, maarifa na maendeleo. Halafu nikalale maana kwa siku kadhaa nimekuwa nikilala alfajiri na kuamka alfajiri! Keshokutwa kutakuwa na mkutano mdogo na washiriki wa Wikipedia ya Kiafrikana. Nadhani baada ya mkutano nitajipa masaa kadhaa ya kupitia barua pepe na kujibu.

Je, uko Jozi tukutane?