Thu 24 Jan 2008
Webu 2.0 Katika Vyuo Vikuu Afrika: Chuo Kikuu Cha Namibia
Na Ndesanjo Macha, Maudhui: teknolojia , blogu , webu 2.0 , tekno-elimuKwa muda mrefu nimekuwa nikiongea na walimu mbalimbali wa vyuo vikuu Afrika kuhusu matumizi ya zana kama blogu, podikasti, video-blogu, n.k., kama nyenzo za kufundishia na kujenga mahusiano na ushirikiano kati ya walimu katika idara au kitivo. Wengi wamekuwa wagumu kujaribu kuzitumia. Nimewahi kuandikia hata walimu wa vyuo vikuu Tanzania na hata kuwaahidi kutoa semina za bure ili waelewe jinsi ya kutumia zana hizi. Mara nyingi hata barua huwa hawajibu. Sijui wanasubiri hadi atokee mzungu mwenye cheo cha “consultant” ndio wamsikilize?
Sasa majuzi hapa nimekutana na mwalimu wa kwanza ambaye mambo haya wala huna haya ya kumhubiria. Anayaelewa na amekuwa akifiria jinsi ya kutumia hizi zana. Huyu ni Profesa Kingo Mchombu, toka Tanzania, ambaye hivi sasa ni mkuu wa Kitivo cha Sayansi Jamii katika Chuo Kikuu cha Namibia (UNAM). Yeye mwenyewe tayari ni mwanablogu katika blogu ya The Giraffe.
Profesa Mchombu ameamua kuwa kitivo chake kitakuwa mstari wa mbele katika matumizi ya zana kama blogu. Wataanza na blogu ya kitivo na baadaye wataingilia mambo mengine ya Webu 2.0. Basi hatua ya mwanzo ilikuwa ni leo. Asubuhi saa tatu hadi saa saba mchana nilikuwa natoa mafunzo kwa walimu wenzake. Tulianza kuzungumzia masuala ya nadharia ya mapinduzi haya ya Web 2.0 kisha baadaye tukaingilia masuala ya blogu ambapo walijifunza jinsi ya kufungua blogu na kufanya mambo mbalimbali ndani ya blogu zao. Kesho kutakuwa na darasa la mwisho.
Mtazamo wa Profesa Mchombu kuhusu haya masuala unatia moyo sana. Sana. Walimu na vyuo vingi Afrika bado viko nyuma sana kwenye masuala haya ingawa zana nyingi muhimu hazina gharama yoyote. Vyuo vya Ulaya na Marekani ndio hasa vinatimua vumbi kwenye masuala haya. Lakini naamini kuwa kitivo hiki cha Sayansi ya Jamii cha Chuo Kikuu cha Namibia hapa Windhoek kitakuja kuwa mfano wa kuigwa kwenye matumizi ya teknolojia madarasani na kwenye idara zake kama zana za kufundishia na kushirikiana kikazi baina ya walimu.
Tazama blogu zilizofunguliwa leo na walimu hapa (wengine bado hawajaandika kitu):
Ruacana: UNAM’s Hub for Spatial Analysis, Kalomo’s Weblog: Developmental Social Work, Promoting the University throughusic, Saschcapone’s Weblog, Carola Beyer na Elisha Chiware’s Weblog.
WordPress database error: [Table 'wp_comments' is marked as crashed and last (automatic?) repair failed]
SELECT * FROM wp_comments WHERE comment_post_ID = '1622' AND comment_approved = '1' ORDER BY comment_date